KWANZA ninaomba radhi kwa safu hii kuadimika kwa takriban wiki mbili mfululizo. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu.
Pili, ninaomba kutoa angalizo kuwa makala hii, niliiandaa mara baada ya vikao vikuu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko Dodoma ambapo hatimaye chama hicho kilipata mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu. Nimeihariri ili kufidia yaliyojiri kati ya wakati huo na hivi sasa.
Baada ya kugusia hayo, ninaomba kufanya uchambuzi endelevu kuhusu mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa kiti cha urais, wiki mbili zilizopita.
Nitaonekana mwenye chuki binafsi kwa CCM kama sitakipongeza chama hicho tawala kwa kumudu kufikia hatua ya kupata mgombea wake ‘kwa amani.’ Pamoja na kiu kubwa ya Watanzania kufahamu kada gani wa CCM angeibuka kidedea, kwa kiasi kikubwa mchakato wa kupata mgombea wa chama hicho ulikuwa kama ‘referendum’ kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, kuhusu kada maarufu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Swali kubwa lilikuwa, “Je Rais Kikwete ataweza ‘kumtosa’ rafiki yake?” Wengine walilielekeza swali hilo kwa Lowassa na kuwa, “Atakatwa au hakatwi?” hasa kwa kuzingatia kile kilichoonekana kama kada huyo kuungwa mkono na wanaCCM wengi.
Lakini hatimaye, maswali hayo yalipata majibu baada ya Lowassa kutokuwamo katika ‘tano bora.’ Licha ya makada Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kutangaza kutoafikiana na mchakato wa kuchuja ‘wagombea,’ zilipatikana taarifa kuwa kungekuwa na jaribio la kumng’oa Rais Kikwete katika uenyekiti wake na kuivunja Kamati Kuu ya chama hicho, masuala yaliyoishia kuwa porojo tu.
Hatimaye, chama hicho kilimtangaza Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake, ambaye naye alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake, akiandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mgombea mwenza, na iwapo Magufuli akishinda, atakuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania.
Huko nyuma nilifanya ‘ubashiri’ kuhusu makada gani niliodhani walikuwa na nafasi kubwa ya kupita ‘mchujo wa kwanza.’ Wakati si vigumu kuelewa kwa nini Lowassa alikatwa, bado sijaelewa kwa nini kada aliyetarajiwa na wengi kuwa angepitishwa, Jaji Agustino Ramadhani, hakumudu kuingia japo kwenye ‘tano bora.’ Binafsi ninamsikitikia kada huyo kwani kwa namna fulani, ‘kufeli’ kwake kunatia doa wasifu wake ‘wa kupigiwa mstari.’
Pia ‘kufeli’ kwa kada aliyekuwa akitajwa sana, Makongoro Nyerere, kuliwashtua baadhi ya watu lakini yayumkinika kuhisi kuwa msimamo wake mkali wa kutaka kuirekebisha CCM, na kauli yake ya ‘turudishieni CCM yetu’ ilimtengenezea maadui hususan wanaonufaika na ‘sera za ulaji na kulindana’ ndani ya chama hicho.
Nilibashiri kuwa January Makamba angefanya vizuri, na kwa hakika alifanikiwa kuingia kwenye ‘tano bora,’ hatua ambayo yaweza kumtengenezea mazingira mazuri ya kisiasa iwapo ataendelea kuwa na dhamira ya kuiongoza Tanzania huko mbeleni.
Pia nilibashiri mmoja au wawili wa makada wa kike kufanya vizuri katika ‘mchujo wa kwanza,’ na ilikuwa hivyo. Sambamba na hilo, nilibashiri uwezekano wa kuwa na aidha mgombea urais mwanamke au mgombea mwenza/makamu wa rais mwanamke, na hilo limetokea japo nilitarajia angekuwa mmoja wa makada wa kike waliojitokeza kuwania nafasi ya urais.
Kwa upande mwingine, mwathirika mkubwa kabisa wa mchakato huo ni mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye pasipo busara aliamua kujidhihirisha kuwa anamuunga mkono Lowassa. Sidhani kama mzee huyo mwenye uzoefu mkubwa wa kisiasa ana washauri wazuri kwani alipaswa kutambua kuwa laiti ‘mgombea wake’ Lowassa akishindwa basi ‘legacy’ yake nayo itayeyuka. Kwa bahati mbaya kwake, Kingunge atakumbukwa zaidi si kama ‘swahiba wa Baba wa Taifa’ bali ‘mkongwe wa kisiasa aliyeangukia pua kwa kumuunga mkono kada aliyetoswa kwenye kinyang’anyiro cha kusaka urais.’ Waelewa wa mambo wanatahadharisha kuwa kujenga hadhi (reputation) ni kitu kinachochukua muda mrefu na kazi kubwa, lakini kosa dogo tu, linaiondoa hadhi hiyo mara moja. Ni rahisi kubomoa kuliko kujenga.
Kwa upande mmoja kuna hisia kwamba Lowassa anaweza asikubali kupoteza mtaji wake wa kisiasa (political capital) katika kilichoonekana kama kuwa na uungwaji mkono mkubwa ndani na nje ya chama chake, kwa kujiunga Ukawa. Akiwa Ukawa na akagombea urais kuhusu swali kwamba atashinda au la, si rahisi kubashiri kwa sasa.
Lakini kwa upande mwingine, jaribio la kuhama CCM linaweza kumgharimu mno mwanasiasa huyo mzoefu. Moja ya athari za wazi ni uwezekano wa kupoteza stahili kadhaa anazopata kama Waziri Mkuu wa zamani. Kadhalika, akihama CCM, chama hicho tawala kinaweza kutumia kila mbinu ‘kummaliza’ kabisa kisiasa. Kama ana washauri wazuri basi pengine ni vema angekubali tu matokeo na ‘kula pensheni yake’ kama Waziri Mkuu wa zamani, bila kuondoka CCM.
Jingine lililojitokeza katika mchakato huo ni ‘kutoswa’ kwa wasaidizi wakuu wawili wa Rais Kikwete, yaani Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Tafsiri ya haraka ni kuwa katika miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete, tulikuwa na viongozi wakuu wawili wa kitaifa ambao pengine hawakustahili kuwa katika nyadhifa hizo na ndio maana wameshindwa kufaulu katika japo mchujo wa awali. Badala ya kukumbukwa kama Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Gharib na Pinda watakumbukwa zaidi kama wasaidizi wakuu wa Rais ambao walifeli ‘mtihani wa kurithi nafasi ya bosi wao.’
Sasa twende kwa Dk. Magufuli. Kwanza, ni kweli kuwa amekuwa akisifika kama mchapakazi. Lakini pengine hili ni matokeo ya kasumba iliyojengeka miongoni mwa Watanzania kwamba kiongozi akitekeleza wajibu wake ambao analipwa mshahara kutekeleza wajibu huo, anaonekana kama ‘malaika.’
Taifa letu limekuwa na uhaba mkubwa wa wazalendo kiasi kwamba kiongozi akitekeleza wajibu au kukemea rushwa anaonekana kama ametoka sayari nyingine. Binafsi, ninamwona Magufuli kama kiongozi wa ‘kawaida’ tu ambaye mara nyingi alizingatia matakwa na matarajio ya mwajiri wake. Kama tunawaona madaktari wakijitahidi kuokoa maisha ya wagonjwa kila kukicha huko hospitalini, au walimu wanaofika mashuleni kufundisha (wengi wao katika amzingira magumu), iweje tumwone Magufuli tofauti kwa vile tu anatekeleza mengi ya majukumu anayotakiwa kuyatekeleza?
Moja ya ‘madoa’ kuhusu uongozi wa Magufuli ni suala la uuzwaji wa nyumba za serikali, suala ambalo halijapatiwa majibu ya kuridhisha. Jingine ni ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aliyopendekeza hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake kama Waziri wa Ujenzi na Dk. Harrison Mwakyembe (aliyekuwa Naibu Waziri) kutokana na ufisadi unaofikia shilingi bilioni 256. Kama ilivyo kwenye uuzwaji wa nyumba za serikali, suala hili nalo pia halijatolewa maelezo ya kuridhisha.
Lakini pengine ni usahaulifu wa Watanzania wengi, au ni kile Waingereza wanaita ‘settling for less’ (kuridhika na kilicho pungufu), ile picha inayomwonyesha Magufuli akipata ‘tiba ya Babu wa Loliondo’ haionyeshi kuwasumbua wananchi wengi wanaoonekana kuwa na matumaini makubwa kwa kada huyo. Binafsi, pamoja na kuheshimu uamuzi wa Magufuli kutegemea ‘tiba hiyo ya porojo,’ nilitarajia msomi kama yeye, tena mwenye taaluma ya Kemia angejihangaisha kutafiti kidogo tu kuhusu ufanisi wa ‘tiba’ hiyo ya kitapeli. Je hili ninalolitafsiri kama ufyongo wa kimaamuzi halitojitokeza katika urais wake iwapo atashinda hapo Oktoba?
Kubwa zaidi ni uwezekano wa Magufuli kuwa ‘Kikwete mpya.’ Sio siri kuwa Rais Kikwete amekuwa ‘shabiki’ mkubwa wa utendaji kazi wa Magufuli. Hilo si kosa. Lakini pengine ‘ushabiki’ huo umechangia pia katika mafanikio ya kisiasa ya kada huyo, na haihitaji uelewa mkubwa wa siasa kubashiri kuwa huenda Magufuli akawa na ‘deni’ kwa Kikwete. Licha ya hofu yangu kuu kuwa tatizo kubwa la ‘urais wa Magufuli’ ni ukweli kuwa ni kada wa CCM ile ile iliyotufikisha hapa tulipo, wasiwasi wangu mwingine ni huo uwezekano wa kuwa na ‘Rais mstaafu by proxy,’ yaani Kikwete kuwa na ‘influence’ kwa ‘rafiki yake’ aliyepo Ikulu.
Kadhalika, ninadhani wengi hatujasahau ukweli kwamba ukosoaji mkubwa dhidi ya kada January Makamba ilikuwa uamuzi wake wa kubainisha visheni ya ‘urais wake’ aliyoiita ‘Tanzania Mpya.’ Ukosoaji huo uliegemea kwenye hoja kwamba mgombea urais kwa tiketi ya CCM atajinadi kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya chama hicho. Na japo mgombea ana fursa ya kushiriki kuingiza malengo yake, kwa kiasi kikubwa ilani hiyo huandaliwa na chama chenyewe.
Lakini pengine sasa ndio tunatambua umuhimu wa kuwa na visheni kama ‘Tanzania mpya’ ya kada January kwani hatujui lolote kuhusu visheni ya Magufuli zaidi ya kuambiwa ni kuwa ni mchapakazi. Swali la msingi, je, uchapakazi wake utaendana na matakwa ya CCM katika ilani yake ya uchaguzi? Lakini hata kama chama hicho tawala kitamruhusu Magufuli kuandika ilani yake mwenyewe kwa niaba ya chama hicho, je ukada wake (kama ilivyothibitika katika hotuba yake ya kuombea kura huko Dodoma) hautokuwa kikwazo katika kuirejesha CCM kwenye misingi yake ya awali ya kuwatumikia wanyonge badala ya matajiri ilivyo sasa?
Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kuwa moja ya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya nchi yetu ni kutanguliza itikadi ya kisiasa badala ya maslahi ya chama. Kada au mwanae anayefahamika kujihusisha na biashara haramu au ufisadi hachukuliwi hatua kwa vile ‘ni mwenzetu.’ Vyombo vya dola vinashindwa kuchukua hatua kwa kuhofia ‘kuwaudhi vigogo wa kisiasa’ Na CCM imekuwa kimbilio kwa watu wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafisadi kwa vile sio siri kuwa uongozi katika chama hicho ni mithili ya kinga ya uhakika dhidi ya hatua za kisheria
Tanzania yetu sio tu inahitaji Rais ambaye hana deni la fadhila kwa mtu yeyote yule, atakayetumia ipasavyo nguvu anayopewa na Katiba kuiongoza nchi yetu kwa maslahi ya taifa badala ya kuweka mbele maslahi ya chama, na kwa CCM, mwanasiasa anayetambua kuwa chama hicho kimeporwa na wenye fedha –safi na chafu- na kuwatelekeza wanyonge.
Nimalizie makala hii kwa ahadi ya kuendeleza uchambuzi huu katika makala ijayo nikitarajia kuwa muda huo tutakuwa tumeshamfahamu mgombea wa tiketi ya urais kupitia Ukawa. Pia ningependa kuwahimiza Watanzania wenzangu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapigakura .
0 comments:
Post a Comment