28 Aug 2015


KABLA sijaingia kwa undani katika makala hii, ambayo niliahidi katika toleo la wiki iliopita, nitajadili kwa kina kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, ningependa kumpa pole mwanasafu mwenzangu Johnson Mbwambo, kutokana na wingi wa ujumbe mfupi wa maneno (sms) na vitisho kila anapoikosoa Chadema.
Mimi pia nimekuwa mhanga mkubwa wa tabia hiyo ya kukera ambayo imejitokeza mara baada ya mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema/UKAWA kujiunga na chama hicho. Hali kwangu ni mbaya zaidi kutokana na uwepo wangu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Nimeitwa kila aina ya jina na kutukanwa kila aina ya tusi, huku tuhuma kubwa kila ninapoikosoa Chadema au UKAWA ikiwa eti ‘nimenunuliwa na CCM’ au ‘kuahidiwa kitu fulani’.

Kuna ‘wastaarabu’ ambao wananilaumu bila kutumia lugha chafu. Wanadai kuwa mtizamo wa machapisho yangu katika gazeti hili na katika blogu yangu ulikuwa ni kuiunga mkono Chadema na kuikosoa CCM. Sasa wananilaumu kwa vile eti ‘nimewasaliti’ na kwa kuikosoa Chadema au UKAWA, ninaiunga mkono CCM.
Awali suala hili lilinisumbua sana kwa sababu wengi wa watu hawa walikuwa wakiilaumu serikali ya CCM kwa kuja na muswada wa kupambana na uhalifu wa mtandaoni (Cybercrime Bill) na kudai ulilenga kuwanyima uhuru wao wa kujieleza.
Iweje leo watu haohao wafanye kilekile walichokuwa wakiilaumu serikali: kutunyamazisha wenzao wenye mitizamo tofauti nao? Hivi hapa kuna neno sahihi zaidi ya unafiki?
Hatimaye nimefanikiwa kuelewa chanzo cha tatizo hilo ni kipi: kukata tamaa, kuchanganyikiwa, na kukosa mwelekeo.

Chuki kubwa waliyonayo dhidi ya CCM, sambamba na matamanio ya kukiona chama hicho tawala kinaondoka kwa gharama yoyote ile, kumepelekea watu hao kuweka imani isiyo na ukomo kwa mgombea urais kwa tiketi ya chama chao, yaani Lowassa.
Sasa yeyote atakayeongea chochote kile kinachoonekana kupunguza nafasi ya Lowassa kuingia Ikulu anaonekana kama adui wa mabadiliko.
Wakati nimeanza kuzoea matusi na lugha chafu inayoelekezwa kwangu, wasiwasi wangu mkubwa ni hatma (aftermath) ya uchaguzi mkuu katika nafasi ya Rais.
Ninabaki kujiuliza, hivi hawa watu wenye matumaini makubwa kupindukia kuwa mgombea wao ataingia Ikulu, watakuwa katika hali gani iwapo matokeo yatakuwa kinyume?
Je watakubali tu matokeo na kufanya post-mortem kistaarabu au ndio tutajikuta tunarudi katika hali iliyojitokeza huko Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 (Mola aepushe)?
Sasa niingie kwenye mada ya wiki hii. Kama nilivyoeleza katika makala tangulizi, nchi yetu itaingia katika uchaguzi huku kwa kiasi mazingira ya uchaguzi yakiwa yanaipendelea CCM.
Na pengine hili ndilo kosa kubwa wanalofanya wafuasi wa UKAWA; kutarajiwa matokeo tofauti katika uchaguzi unaofanyika katika mazingira yaleyale ‘yaliyowaliza’ katika chaguzi zilizotangulia.

Kwamba watu wengi wamechoshwa na CCM wala si suala la mjadala. Maelfu kwa maelfu ya watu wanaojitokeza kwenye shughuli za kisiasa za Lowassa sio kuashiria cha umaarufu wa mwanasiasa huyo bali hiyo kiu ya kuoina CCM inatoka madarakani. Lakini busara kidogo tu zatosha kutufahamisha kuwa kutaka kitu na kupata kitu ni vitu viwili tofauti.
Watanzania wengi waliochoshwa na CCM, wanataka kuiona inaondoka madarakani hata kesho. Lakini kuwezesha matakwa hayo yatimie si suala rahisi. Naomba nieleweke hapa, Ninasema SI RAHISI lakini sijasema HAIWEZEKANI.
Kudhani kuwa CCM itaondoka kwa kutumia wanasiasa walewale ambao wamechangia kuwafanya Watanzania wengi watake chama hicho kiondoke madarakani ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
Naam, Lowassa anaweza kuwezesha Chadema/UKAWA kuitoa CCM madarakani lakini sababu zilizofanya CCM ichukiwe haziwezi kuondoka.
Kwahiyo faida kubwa iliyonayo CCM ni mfumo wa uchaguzi na kiutawala ambao unakitengenezea mazuri chama chake na yeye binafsi kufanya vizuri katika uchaguzi huo.
Lakini licha ya faida hizo za kimfumo, Magufuli anaingia katika uchaguzi huo akiwa katika CCM ileile iliyoshinda chaguzi zote zilizotangulia, kihalali au la, lakini safari hii inakutana na upinzani ambao Kimsingi umetengenezwa katika mazingira ya ‘zimamoto’.

Jinsi UKAWA ilivyoundwa na maendeleo yake hadi kufikia hatua ya kusimamisha mgombea mmoja, yaweza kuwa ni moja ya vikwazo kwa umoja huo kufanikiwa kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika takriban miezi mawili na kitu kutoka sasa.
Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Lakini umoja tunaozungumzia hapa ni ule wenye kujengwa katika misingi ya kuaminiana. Tayari Tumeshuhudia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, akijiweka kando na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba akijiuzulu.
Ni rahisi kutoa majibu rahisi, kwa mfano kuwatuhumu wanasiasa hao ni wenye uchu wa madaraka, lakini ukweli ni kwamba ‘kujitenga’ kwao sio tu kuna athari bali pia kunaashiria mpasuko wa aina fulani katika umoja huo.
Kwahiyo Magufuli na CCM kwa ujumla wataingia katika uchaguzi huo wakiwa kitu kimoja, kwa kiasi kikubwa, ilhali UKAWA wakikabiliwa na ‘sintofahamu’ flani, sio tu ya kuhusu Dkt Slaa na Prof Lipumba, bali pia hizi taarifa zinazosikika kutoka katika baadhi ya majimbo ambapo ‘ndoa’ ya vyama hivyo imeshindikana, yaani licha ya kuafikiana kusimamisha mgombea mmoja, vyama vinavyounda umoja huo vimejikuta vikisimamisha wagombea tofauti.
Jingine limejitokeza katika uzinduzi wa kampeni za CCM Jumapili iliyopita ambapo chama hicho tawala, kama baadhi yetu tulivyotarajia, kimejaribu kujenga picha kuwa Chadema/UKAWA sasa ni kama kikosi cha pili cha CCM (CCM-B).

Magufuli na timu yake wakiweza kujenga hoja za kueleweka kwanini Lowassa na Chadema/UKAWA yake ni sawa tu na CCM ya waasi, kuna uwezekano wa wapigakura kutafuta hifadhi katika ‘jini linalokujua halikuli likakwisha.’CCM ‘halisi’ ni ‘jini’ wanalolijua, na pengine wasingetaka kufanya majaribio kwa ‘jini’ wasilolijua.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Magufuli na CCM kwa ujumla wanaweza kurahisishiwa kazi na ‘historia ya mahusiano kati ya Chadema na Lowassa. Kama kuna mwanasiasa wa CCM aliyeandamwa mno na Chadema kuhusu tuhuma za ufisadi basi si mwingine bali Lowassa.
Kwa kuzingatia muda uliopo, kati ya mwanasiasa huyo kuhama CCM na kujiunga na Chadema na tarehe ya uchaguzi mkuu, yayumkinika kuhitimisha kuwa ni vigumu mno kumsafisha.

Kimsingi, Chadema/UKAWA wamejiambukiza tatizo walilokuwa wakilipiga vita kwa nguvu zao zote. Hakuna ubishi kuwa mafanikio ya chama hicho kikuu cha upinzani yalichangiwa zaidi na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi.
Sasa leo hii wakisimama jukwaani sio tu na mwanasiasa anayetuhumiwa kujihusisha na ufisadi lakini pia Chadema wenyewe walimwandama kwa tuhuma hizo, kisha wajaribu kumsafisha au kukemea ufisadi, ni mkakati wenye dalili ya kutokuwa na mafanikio.
Awali kulikuwa na hisia za ‘mafuriko ya Lowassa’ kuikumba CCM, kwa maana ya wanasiasa wenye nguvu ndani ya chama hicho tawala kumfuata huko Chadema/UKAWA.
Kuna wawili watatu waliohama lakini si wenye ushawishi au nguvu kubwa ya kuiathiri CCM. Na tayari CCM, imewashusha hadhi na kuwaita ‘makapi’ sambamba na kujenga picha kuwa ni wenye uchu wa madaraka.
Kuhama kwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, kutoka CCM na kujiunga na UKAWA kunazidi ‘kuchanganya madawa.’ Kubwa zaidi ni kile kilichoonekana kuwa uhasama wa muda mrefu kati ya wanasiasa hao.
Wakati hii ingeweza kuwa turufu kubwa kwa UKAWA, kuwa na mawaziri wakuu wa zamani wawili ndani ya upinzani, lakini tayari zimeanza kusikika tetesi kuwa “Sumaye ameingia UKAWA kama ‘Plan B’ endapo lolote litamtokea Lowassa kiafya.”
Lakini makala hii si ya kuzungumzia mapungufu ya Chadema/UKAWA bali ni kumjadili Magufuli, japo ni vigumu kuzungumzia fursa alizonazo za kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu pasipo kujadili ‘urahisi’ unaotokana na kinachoendelea huko UKAWA.
Tukiweka pembeni niliyobainisha hapo juu, matumaini kuwa urais wa Magufuli utakuwa tofauti na huu wa Rais Jakaya Kikwete ni mdogo.
Hilo nilishaliongelea huko nyuma, ambapo yayumkinika kudhani kuwa mgombea huyo wa chama tawala anaweza kuwa na deni la fadhila kwa mtangulizi wake, hasa kwa kuzingatia ‘mahesabu’ yaliyofanyika katika machakato wa CCM kumpata mgombea wake.
Laiti Chadema/UKAWA wasingekuwa na kibarua cha kumsafisha mgombea wao, Lowassa, wangeweza kuwa katika nafasi nzuri kujenga picha kwa wapigakura kuwa miaka mitano ya utawala wa Magufuli haitokuwa tofauti na kumi ya Kikwete, na pengine kupigilia mstari kuwa mengi ya yaliyojiri katika utawala uliopo madarakani yanamhusu mgombea huyo wa CCM pia.
Hata hivyo, iwapo jitihada za kumsafisha Lowassa na kumtenganisha na CCM zitafanikiwa, basi UKAWA na mgombea wao wanaweza kufanya vizuri.
Mwisho, kama kuna kitu kinachoweza kuigharimu CCM na Magufuli ni kupuuzia ukweli kuwa kuna wapigakura wengi wamepoteza imani kwa chama hicho.
Na laiti mwenendo wa kampeni za Magufuli utafuata ‘busara’ za Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutumia lugha isiyo ya kistaarabu ya ‘mpumbavu na lofa’ basi sintoshangaa kuona Lowassa akinufaika na ‘kura za huruma’.

Ni muhimu kwa CCM kuongoza kwa mfano ikiwa ni pamoja na kuachana na kampeni za chuki au za ‘utoto wa kisiasa’ (political immaturity), iwaeleze Watanzania wapi ilipokosea hadi baadhi yao kutamani iondoke madarakani, na nini itawafanyia kurekebisha makosa yake.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.