Tarehe 24 mwezi
huu, Rais Dokta John Magufuli alimteua Dokta Modestus Kipilimba kuwa Mkurugenzi
Mkuu (DGIS) wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Uteuzi huo umefanyika kufuatia
kustaafu kwa mkurugenzi aliyemaliza muda wake, Othman Rashid.
Makala hii
inajikita katika uchambuzi wa uteuzi huo kwa kuangalia changamoto na fursa
zinazomkabili kiongozi huyo mkuu wa taasisi hiyo nyeti kabisa. Kwa mtizamo
wangu, kama kuna kitu ambacho kinaweza kuzua maswali kuhusu uteuzi huo basi ni
wadhifa wa Director of Risk Management alioshikilia Dokta Kipilimba huko nyuma
alipokuwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania.
Sote twafahamu
jinsi Benki Kuu yetu imekuwa ikiandamwa na matukio mfululizo ya ufisadi,
kuanzia EPA hadi Tegeta Escrow. Kwa wadhifa wake katika taasisi hiyo, kuna
uwezekano wa bosi huyo mpya wa mashushushu kuonekana ‘sehemu ya mfumo
ulioshindwa kudhibiti ufisadi.’ Hata hivyo, utetezi unaweza kuwa huenda yeye
alitekeleza majukumu yake vema lakini walio juu yake hawakuchukua hatua
stahili.
Kadhalika, huko
mtandaoni kuna ‘tuhuma’ kadhaa kuhusu Dokta Kipilimba, lakini itakuwa sio
kumtendea haki yeye, blogu hii na mie mwenyewe kujadili tuhuma ambazo hazina
ushahidi wowote. Ni muhimu kutambua kuwa Tanzania yetu licha ya kuwa kisiwa cha
amani pia ni kisiwa cha majungu, uzandiki, fitna, umbeya na uzushi.
Changamoto kubwa
kwa Dokta Kipilimba ni pamoja na kurejesha hadhi na heshima ya Idara ya Usalama
wa Taifa. Katika miaka ya hivi karibuni, taasisi hiyo muhimu kabisa imekuwa
ikishutumiwa kuwa inachangia ustawi wa ufisadi, ujangili, biashara ya madawa ya
kulevya, nk.
Wanaoilaumu
taasisi hiyo hawamaanishi kuwa watumishi wake wanahusika katika matukio hayo ya
kihalifu as such bali kushindwa kwa Idara hiyo kukabiliana na kushamiri kwa
matendo hayo ya kihalifu, ambayo kimsingi ni matishio kwa usalama wa taifa, na
kazi kuu ya Idara hiyo ni kukabiliana na matishio kwa usalama wa taifa la
Tanzania.
Ninaamini kuwa
Dokta Kipilimba anafahamu kanuni muhimu kuhusu ufanisi au mapungufu ya idara ya
usalama wa taifa popote pale duniani, kwamba “kushamiri kwa vitendo
vinavyotishia usalama wa taifa lolote lile ni kiashiria cha mapungufu ya idara
ya usalama wa taifa ya nchi husika, na kudhibitiwa kwa vitendo vinavyotishia
usalama wa taifa popote pale duniani ni kiashiria cha uimara wa idara ya
usalama wa taifa ya nchi husika.”
Kwahiyo, kwa
kuzingatia kanuni hiyo, kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya, ujangili,
rushwa, na ufisadi mwingine ni viashiria vya mapungufu ya Idara yetu ya Usalama
wa Taifa.
Changamoto
nyingine kwa Dokta Kipilimba ni tuhuma za mara kwa mara dhidi taasisi hiyo
muhimu kabisa kuwa katika utendaji kazi wake imegeuka kuwa kama ‘kitengo cha
usalama cha chama tawala CCM.’ Idara hiyo imekuwa ikituhumiwa kuwa kwa kiasi
kikubwa imeweka kando taaluma ya ushushushu (tradecraft) na kutekeleza majukumu
yake kisiasa.
Madhara ya muda
mfupi ya kasoro hiyo ni taasisi hiyo kujenga uhasama na vyama vya upinzani na
kwa namna flani kupoteza heshima na uhalali wake. Lakini la kuogofya zaidi ni
madhara ya muda mrefu, ambapo watu wanaoweza kuwa ni matishio kwa usalama wa
taifa letu wanaweza kutumia ‘urafiki’ unaodaiwa kuwepo kati ya Idara ya Usalama
wa Taifa na CCM, wakitambua bayana kuwa ‘Idara haina muda na makada wa chama
tawala,’ na hatimaye kufanikiwa kutimiza azma zao ovu.
Baadhi ya
watumishi wa zamani wa taasisi hiyo walijikuta matatizoni kwa vile tu
walitekeleza majukumu yao dhidi ya wanasiasa wa chama tawala, na wakaishia
kuonekana kama wahaini.
Changamoto
nyingine kwa Dokta Kipilimba ni tuhuma zinazoikabili taasisi hiyo kuhusu mfumo
wa ajira ambapo inadaiwa kuwa zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo kwa ndugu na
jamaa za ‘vigogo.’ Tatizo kubwa hapa ni kwamba utiifu wa ‘ndugu na jamaa hao wa
vigogo’ haupo kwa taifa bali kwa vigogo hao waliowaingiza Idarani. Pengine sio
vibaya kufikiria ‘utaratibu wa wazi’ katika ‘recruitment’ kama inavyofanywa na
wenzetu wa CIA, NSA, MI5, MI6, HGCQ, nk wanaotangaza nafasi za ajira kwenye
vyombo vya habari.
Pia kuna tatizo
la baadhi ya maafisa usalama wa taifa ‘kujiumbua’ kwa makusudi kwa sababu
wanazojua wao wenyewe, kubwa ikiwa kutaka sifa tu, au waogopwe ‘mtaani.’ Hii
inaathiri sana ufanisi wa maafisa wa aina hiyo kwani ni vigumu kutekeleza
majukumu yao ipasavyo pasi usiri.
Sambamba na hilo
ni kasumba ya muda mrefu ambapo baadhi ya maafisa wa Idara hiyo waliopo kwenye
vitengo mbalimbali kuwepo huko kwa muda mrefu mno kiasi cha kuathiri utendaji
wao. Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na ‘vituo muhimu’ na kwenye ofisi za
balozi zetu nje ya nchi. Ikumbukwe kuwa unless afisa ametengeneza deep cover,
uwepo wake kwa muda mrefu katika sehemu aliyokuwa ‘penetrated’ au kituo chake
cha kazi kwingineko (mfano ubalozini) unaweza kupelekea ‘akaungua’ (burned).
Changamoto
nyingine kubwa ni uwepo wa majasusi kibao nchini mwetu, hususan kutoka nchi
moja jirani, huku wengi wa majasusi hao wakiwa wameajiriwa katika taasisi za
umma na binafsi. Hili ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa wa Tanzania yetu.
Kwa upande fursa
kwa Dokta Kipilimba, licha ya kuwa ‘mwenyeji’ katika taasisi hiyo muhimu,
wasifu wake kitaaluma unamweka katika nafasi nzuri sana kukabiliana na
changamoto za karne ya 21 ambayo imetawaliwa zaidi na teknolojia ya kisasa.
Dokta Kipilimba
ni msomi aliyebobea kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na
yayumkinika kuamini kuwa anaweza kutumia usomi wake kuibadilisha Idara yetu ya
Usalama wa Taifa kwenda na wakati, kufanya kazi kama taasisi ya kishushushu ya
karne ya 21, ambayo licha ya kutegemea HUMINT inaweza pia kutumia njia nyingine
za kukusanya taarifa za kiusalama kwa kutumia teknolojia (GEOINT, MASINT, SIGINT,
CYBINT, FININT na TECHINT kwa ujumla)
Na katika kwenda na teknolojia ya kisasa, basi pengine si vibaya iwapo Idara yetu ikafikiria haja ya uwepo wake kwenye mtandao, kwa kuwa na tovuti yake kamili na pia kufungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter na Facebook. Hii sio tu inaweza kusaidia kutengeneza "human face" ya intel service bali pia yatoa fursa nzuri katika OSINT.
Na katika kwenda na teknolojia ya kisasa, basi pengine si vibaya iwapo Idara yetu ikafikiria haja ya uwepo wake kwenye mtandao, kwa kuwa na tovuti yake kamili na pia kufungua akaunti kwenye mitandao ya kijamii, hususan Twitter na Facebook. Hii sio tu inaweza kusaidia kutengeneza "human face" ya intel service bali pia yatoa fursa nzuri katika OSINT.
Fursa nyingine
kwa Dokta Kipilimba ni matarajio ya sapoti ya kutosha kutoka kwa Rais Dokta
Magufuli ambaye kama alivyoahidi wakati wa kampeni za kuwania urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania mwaka jana, mapambano dhidi ya ufisadi yamepewa
kipaumbe cha hali ya juu kabisa. Kama ‘sponsor’ na ‘consumer’ wa taarifa za kila
siku usalama, inatarajiwa kuwa Dokta Magufuli atatekeleza ushauri wa Idara
katika kukabiliana na matishio mbalimbali ya usalama wa taifa letu.
Dokta Kipilimba
ana fursa ya kuleta mageuzi kwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuangalia
uwezekano wa kuwafikia watu walio nje ya taasisi hiyo, hasa pale uwezo wa Idara
yetu unapokuwa limited. Nitoe mfano. Katika kupata taarifa mwafaka wa kudumu kuhusu,
kwa mfano, mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar, Idara inaweza ku-reach out wanazuoni
wa historia ya taifa letu walipo ndani na nje ya nchi yetu.
Ikumbukwe kuwa
sio rahisi kwa taasisi hiyo kuwa na maafisa au watoa habari katika kila eneo.
Wenzetu wa nchi za Magharibi wamekuwa wakikabiliana na hali hiyo kwa kufanya
kazi na ‘makandarasi’ (contractors), ambao of course, wamekidhi taratibu kama
vile vetting.
Sambamba na hilo
ni Idara hiyo kuangalia uwezekano wa kutumia hazina kubwa tu ya maafisa wake wa
zamani, hususan wastaafu. Ikumbukwe kuwa wengi wao ni watu wanaowindwa na ‘subjects’
mbalimbali wanaolenga kulihujumu taifa letu.
Nimalizie makala
hii kwa kutoa pongezi za dhati kwa Dokta Kipilimba na Naibu wake (DDGIS) Robert
Msalika, sambamba na kumtakia mapumziko mema Mkurugenzi mstaafu Othman, na
kumkaribisha ‘uraiani.’
MUNGU IBARIKI TANZANIA,
MUNGU IBARIKI IDARA YETU YA USALAMA WA TAIFA
0 comments:
Post a Comment