Somo: Kuvuliwa uanachama Bernard Membe, Waziri Wa Zamani wa Mambo ya Nje, Mbunge wa zamani, kada mkongwe na mmoja wa wana CCM walioingia "tano bora" ya kutafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
Key subject(s):
- Bernard Kamilius Membe
- John Pombe Magufuli
- Jakaya Mrisho Kikwete
- Modestus Kipilimba
Dhana ya kwanza: Membe "anakubali matokeo," anaamua kuachana na siasa.
Dhana ya pili: Membe "anafanyiziwa."
Dhana ya tatu: Membe "anakubali matokeo," anaamua kujiunga na chama cha upinzani
Dhana ya nne: Membe hakubali matokeo, anaamua "kutafuta haki yake" CCM.
Dhana ya tano: Membe hakubali matokeo, anaamua "kutafuta haki yake" nje ya CCM
Ushahidi: Hadi muda huu Membe hajatoa tamko rasmi kuhusu mustakabali wake. Kwahiyo dhana zote nne zinasimama kama zilivyo kwa vile hakuna ushahidi wa kupelekea kuziondoa.
Kipimo/Vipimo: Haipo muda huu mpaka Membe atoe tamko rasmi. Dhana zote zinaendelea kubaki hai.
Mchujo: Kwa kuzingatia kuwa Membe hakuomba msamaha alipoitwa kwenye vikao husika, na kwa kuzingatia "damu mbaya" (bad blood)kati yake na Rais John Pombe Magufuli, tangu mwanzo wa Awamu ya Tano, yayumkinika kuamini kuwa uwezekano wa Membe "kutafuta haki yake" CCM ni hafifu.
Vigezo hivyo vinafanya uwezekano wa Dhana Ya Nne kutimia kuwa ni hafifu. Kwa mantiki hiyo, dhana hiyo inaondoshwa (yaweza kurejeshwa huko mbeleni)
Walakini: Hakuna
Unyeti: upo katika maeneo yafuatayo
- Membe ni mmoja wa makada zaidi ya 40 wa CCM waliojitokeza kuwania kupitishwa na chama hicho kwenye nafasi ya urais wa JMT.
- Membe alikuwa mpinzani mkuu wa Edward Lowassa kada aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kuwa mrithi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, na ambaye baada ya kutopitishwa CCM alihamia Chadema, japo baadaye alirudi tena CCM.
- Membe alikuwa miongoni mwa "tano bora" pamoja na Magufuli, January Makamba, Amina Ali na Asha Rose MigiroMigiro
- Membe ni swahiba mkubwa wa Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete
- Membe ni mwanachama wa kwanza wa CCM "mwenye hadhi ya kitaifa"kufukuzwa uanachama.
Uchambuzi:
Uzito wa dhana ya kwanza kwamba Membe atakubali matokeo na kuachana na siasa upo kwenye hoja kwamba kutokana na uzoefu wake ndani ya CCM, anafahamu kuwa jaribio lolote la kuendelea na "maisha ya kisiasa" litakumbwa na upinzani na vikwazo vingi kutoka kwa Magufuli na CCM kwa ujumla.
Kadhalika, kama shushushu wa zamani, Membe anafahamu kuwa yeye sasa ni "high value target" huko Idara ya Usalama wa Taifa, ambapo kila nyendo yake sio tu itafuatiliwa kwa karibu bali pia anaweza "kuchanganywa akili" kwa kufanyiwa "overt surveillance" (kumfuatilia mlengwa bila kificho, lengo likiwa kumjulisha kuwa anafuatiliwa. Mbinu hii hutumika zaidi "kumchanganya akili" mlengwa).
Mapungufu ya dhana ni ukweli kwamba Membe ni "high value target" pia kwa vyama vya upinzani, na kwa kuzingatia kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, anaweza kupewa fursa ya "kulipa kisasi dhidi ya Magufuli kwa kupitishwa kuwa mgombea wa chama cha upinzani."
Mapungufu mengine katika dhana ya kwanza ni "dalili za awali" kuwa "huu sio mwisho wa Membe kisiasa."
Uzito wa dhana ya pili upo katika ukweli kwamba Magufuli " hana mshipa wa aibu." Kama aliweza "kuamuru Lissu afanyiziwe," hashindwi kutoa maagizo kama hayo dhidi ya Membe.
Uzito mwingine upo kwenye ukweli kwamba shushushu wa zamani Membe nje ya CCM anabaki kuwa tishio kuliko alipokuwa mwanachama "anayebanwa na taratibu za chama."
Uzito mwingine ni ukweli kwamba Membe ni swahiba na watu wawili muhimu kwenye siasa za Tanzania, na ambao huenda wakawa na influence kwenye uchaguzi mkuu ujao, Rais Mstaafu Kikwete na Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa, na sasa balozi wa Tanzania Namibia, Dkt Modestus Kipilimba. Japo watu hawa wawili, kama ilivyo kwa Membe sasa, nao ni "high value targets" ambao sio tu wanafuatiliwa na mawasiliano yao kusikilizwa (uwepo wa walinzi unarahisisha zoezi hilo), lakini wanaweza kuwa nguzo muhimu kwaMembe "kulipa kisasi."
Kwa vile Kipilimba yupo nje ya nchi, na Kikwete huwa safarini mara kwa mara, kuwafuatilia kwa utimilifu wa asilimia 100 ni kugumu, na ikizingatiwa kuwa Membe ni shushushu wa zamani, anaweza kufanikisha mawasiliano nao na kuepa "surveillance" (kufuatiliwa) na "bugging" (kunasa mawasiliano).
Mapungufu ya dhana yapo kwenye ukweli kuwa japo "Magufuli hana mshipa wa aibu," na hivyo anaweza "kumfanyizia" Membe, lolote litakalomtokea Membe kati ya sasa na Oktoba litatafsiriwa moja kwa moja kuwa ni "mkono wa Magufuli." Na hilo linaweza kuwafanya "mabeberu kumrukia kama mwewe."
Na ikumbukwe kama Waziri wa Mambo ya Nje kwa miongo miwili, Membe atakuwa na "connections" kubwana nzito huku ughaibuni. Akidhuriwa na Magufuli, yawezekana kabisa "mabeberu" wakaamua kuharakisha utekelezaji wa mkakati wa kumng'oa kiongozi huyo.
Uzito wa dhana ya tatu ni ukweli kwamba kujiunga na chama cha upinzani sio tu kunaweza kumpatia fursa ya "kulipa kisasi kwa Magufuli, kwa kuwa mpinzani wake kwenye uchaguzi mkuu ujao (kwa kuamini kuwa atapitishwa kuwa mgombea urais katika chama chochote atakachohamia)," pia itakuwa nafasi adimu kwake kufanya jaribio jingine la kuwania urais wa Tanzania.
Uzito mwingine wa dhana hii ni kauli za Kiongozi Mkuu wa chama cha Wazalendo (ACT),Zitto Kabwe baada ya tangazo kuhusu kufukuzwa kwa Membe huko CCM, Kauli hizo zilikuwa na harufu ya "karibu kwetu."
Mapungufu ya dhana hii yapo kwenye ukweli kwamba hata kama Membe ataamua kujiunga na chamacha upinzani, vikwazo na usumbufu kutoka kwa Magufuli kupitia Idara ya Usalama wa Taifa vinaweza kumfanya "atamani ardhi immeze."
Kingine ni ukweli kwamba "Membe sio msafi kihivyo," na hiyo inaweza kumrahisishia Magufuli "kumzulia kesi ya utakatishaji fedha na/au uhujumu uchumi."
Vivilevile, Idara ya Usalama wa Taifa inaweza kumshurutisha Membe asijiunge na chama kingine, hasa ikizingatiwa kuwa Magufuli amekuwa akiitumia taasisi hiyo kuwatisha na kuwahujumu wapinzani wake au/na wakosoaji/wanaharakati.
Kadhalika, licha ya Zitto kuonyesha dalili za awali za uwezekano wa "Membe kuhamia ACT-Wazalendo," kwa kuwa hatujui Maalim Seif na "ACT-Zanzibar" wana mtazamo gani kuhusu "ujio wa Membe," na ukweli kuwa wanaweza kumkataa, yawezekana Membe kuhamia chama hicho kusitokee.
Uzito kwenye dhana ya tano upo kwenye ukweli kwamba endapo atatumia vema ujuzi wake kama shushushu mstaafu, na endapo atapata sapoti kutoka kwa Kikwete na Kipilimba, Membe anaweza kuwa tishio nje ya CCM bila hata kujiunga na chama kingine cha siasa.
Ukweli kwamba kuna wana-CCM wengi tu wanaotamani Magufuli aondoke hata kesho unaweza kumsaidia Membe kupata "marafiki" wengine muhimu ndani ya chama hicho, ambao pamoja nao wanaweza kuanzisha harakati za kumng'oa Magufuli.
Mapungufu ya dhana hii ukweli kwamba kwa nchi ambayo "ili nguvu za kisiasa shurti uwe mwanasiasa," uwezekano wa Membe kuwa na "nguvu" nje ya mfumo wa kisiasa ni mdogo.
Mchanganuo: Kwa upande mmoja, uamuzi wa Magufuli kumfukuza Membe unaelezea zaidi kuhusu yeye kuliko kilichompata Membe. Ukweli kwamba jina la Membe limekuwa likitajwa mara kadhaa kuhusiana na kinyang'anyiro cha urais mwaka huu, uamuzi huo wa Magufuli unatafsiriwa kuwa ni UOGA. Kwa kifupi, Magufuli amemuogopa Membe akiwa ndani ya CCM na ndio maana akashinikiza afukuzwe chamani.
Hofu ya Magufuli kwa Membe haina mashiko. Membe hakupaswa kushika nafasi ya tano kwenye "tano bora" ya kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM, huku akiambulia kura 120 tu, nyuma ya JanuaryMakamba (124), Migiro (280),Amina Ali (284) na Magufuli (290). Hakupaswa kushika nafasi hiyo kwa sababu kuu mbili. Kwanza, yeye ndiye alikuwa "front runner," kwa kuzingatia kuwa ndiye alikuwa mpinzani mkuu wa Lowassa.Na pili ni uswahiba wake na Kikwete na familia yake. Kingine cha kuongezea hapo ni ukaribu wake na maafisa mbalimbali wa Idara ya Usalama wa Taifa ambayo aliwahi kuitumikia huko nyuma.
Membe hakuwa na sababu moja ya msingi ya kutoibuka mshindi kwenye kinyang'anyiro hicho. Sasa sijui hiyo hofu ya Magufuli inatoka wapi.
Ubashiri: Endapo Magufuli "hatomfanyizia" Membe, kuna uwezekano mwanasiasa huyo akajiunga na ACT- Wazalendo. Lakini kujiunga huko kutategemea endapo Maalim Seif na "ACT - Zanzibar) wataridhia. Hata hivyo, intelijensia sio sayansi timilifu, na matokeo ya ubashiri huu yanaweza kuwa tofauti.
Hitimisho: Suala hili lina sura mbili. Moja ni ukweli kwamba udikteta wa Magufuli sasa umepiga hodi ndani kabisa ya CCM.Pili, mpira upo mikononi mwa Membe. Akipanga karata zake vizuri, anaweza kutoa upinzani japo kidogo kwa Magufuli hapo Oktoba. Anaweza kuwa Rais ajaye wa Tanzania? Uwezekano huo ni hafifu japo wanasema "never say never in politics."
Uchambuzi huu ni endelevu. Utakuwa updated kadri kunapotokea maendeleo mapya.