1 Sept 2016

WIKI iliyopita, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Modestus Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu (DGIS) wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Uteuzi huo umefanyika baada ya kustaafu kwa mkurugenzi mkuu aliyemaliza muda wake, Othman Rashid.
Kwa mtizamo wangu, kama kuna kitu ambacho kinaweza kuzua maswali kuhusu uteuzi huo basi ni wadhifa wa Mkurugenzi wa Majanga (Director of Risk Management) alioshikilia Dk. Kipilimba akiwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania.
Tunafahamu Benki Kuu imekuwa ikiandamwa na matukio mfululizo ya ufisadi, kuanzia EPA hadi Tegeta Escrow. Kwa wadhifa wake katika taasisi hiyo, kuna uwezekano wa bosi huyo mpya wa mashushushu kuonekana sehemu ya mfumo ulioshindwa kudhibiti ufisadi. Hata hivyo, utetezi unaweza kuwa huenda yeye alitekeleza majukumu yake vema lakini walio juu yake hawakuchukua hatua stahili.
Changamoto kubwa kwa Dk. Kipilimba ni pamoja na kurejesha hadhi na heshima ya Idara ya Usalama wa Taifa. Wanaoilaumu taasisi hiyo hawamaanishi kuwa watumishi wake wanahusika katika baadhi ya matukio ya kihalifu bali kushindwa kwa Idara hiyo kukabiliana na kushamiri kwa matendo hayo ya kihalifu, ambayo kimsingi ni matishio kwa usalama wa taifa, na kazi kuu ya Idara hiyo ni kukabiliana na matishio kwa usalama wa taifa la Tanzania.
Ninaamini kuwa Dk. Kipilimba anafahamu kanuni muhimu kuhusu ufanisi au upungufu wa idara ya usalama wa taifa popote pale duniani, kwamba kushamiri kwa vitendo vinavyotishia usalama wa taifa lolote lile ni kiashiria cha upungufu katika idara ya usalama wa taifa ya nchi husika na kudhibitiwa kwa vitendo vinavyotishia usalama wa taifa popote pale duniani ni kiashiria cha uimara wa idara ya usalama wa taifa ya nchi husika.
Kwahiyo, kwa kuzingatia kanuni hiyo, kushamiri kwa biashara ya dawa ya kulevya, ujangili, rushwa na ufisadi mwingine ni viashiria vya kasoro ya Idara yetu ya Usalama wa Taifa.
Changamoto nyingine kwa Dk. Kipilimba ni tuhuma za mara kwa mara dhidi taasisi hiyo muhimu kabisa kuwa katika utendaji kazi wake imegeuka kuwa kama kitengo cha usalama cha chama tawala CCM. Idara hiyo imekuwa ikituhumiwa kuwa kwa kiasi kikubwa imeweka kando taaluma ya ushushushu (tradecraft) na kutekeleza majukumu yake kisiasa.
Madhara ya muda mfupi ya kasoro hiyo ni taasisi hiyo kujenga uhasama na vyama vya upinzani na kwa namna fulani kupoteza heshima na uhalali wake. Lakini la kuogofya zaidi ni madhara ya muda mrefu, ambapo watu wanaoweza kuwa ni matishio kwa usalama wa taifa letu wanaweza kutumia ‘urafiki’ unaodaiwa kuwepo kati ya Idara ya Usalama wa Taifa na CCM, wakitambua bayana kuwa Idara haina muda na makada wa chama tawala na hatimaye kufanikiwa kutimiza azma zao ovu.
Baadhi ya watumishi wa zamani wa taasisi hiyo walijikuta matatizoni kwa vile tu walitekeleza majukumu yao dhidi ya wanasiasa wa chama tawala na wakaishia kuonekana kama wahaini.
Changamoto nyingine kwa Dk. Kipilimba ni tuhuma zinazoikabili taasisi hiyo kuhusu mfumo wa ajira ambapo inadaiwa kuwa zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo kwa ndugu na jamaa za vigogo. Tatizo kubwa hapa ni kwamba utiifu wa ndugu na jamaa hao wa vigogo haupo kwa taifa bali kwa vigogo hao waliowaingiza Idarani. Pengine sio vibaya kufikiria ‘utaratibu wa wazi’ katika ‘recruitment’ kama inavyofanywa na wenzetu wa CIA, NSA, MI5, MI6 au HGCQ wanaotangaza nafasi za ajira kwenye vyombo vya habari.
Pia kuna tatizo la baadhi ya maofisa usalama wa taifa ‘kujiumbua’ kwa makusudi kwa sababu wanazojua wao wenyewe, kubwa ikiwa kutaka sifa tu, au waogopwe mtaani. Hii inaathiri sana ufanisi wa maafisa wa aina hiyo kwani ni vigumu kutekeleza majukumu yao ipasavyo pasi usiri.
Sambamba na hilo ni kasumba ya muda mrefu ambapo baadhi ya maafisa wa Idara hiyo waliopo kwenye vitengo mbalimbali kuwepo huko kwa muda mrefu mno kiasi cha kuathiri utendaji wao.
Changamoto nyingine kubwa ni uwepo wa majasusi kibao nchini mwetu, hususan kutoka nchi moja jirani, huku wengi wa majasusi hao wakiwa wameajiriwa katika taasisi za umma na binafsi. Hili ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa letu. Licha ya hilo, kiintelijensia, kila ‘nchi rafiki’ ni ‘adui yetu’ muda huu tulionao au siku zijazo.
Kwa upande wa fursa kwa Dk. Kipilimba, licha ya kuwa ‘mwenyeji’ katika taasisi hiyo muhimu, wasifu wake kitaaluma unamweka katika nafasi nzuri sana kukabiliana na changamoto za karne ya 21 ambayo imetawaliwa zaidi na teknolojia ya kisasa.
Dk. Kipilimba ni msomi aliyebobea kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na yayumkinika kuamini kuwa anaweza kutumia usomi wake kuibadilisha Idara ya Usalama wa Taifa kwenda na wakati, kufanya kazi kama taasisi ya kishushushu ya karne ya 21.
Fursa nyingine kwa Dk. Kipilimba ni matarajio ya kuungwa mkono vya kutosha kutoka kwa Rais Magufuli ambaye kama alivyoahidi wakati wa kampeni za kuwania urais, mapambano dhidi ya ufisadi yamepewa kipaumbele cha hali ya juu kabisa.
Sambamba na hilo ni Idara hiyo kuangalia uwezekano wa kutumia hazina kubwa tu ya maafisa wake wa zamani, hususan wastaafu. Ikumbukwe kuwa wengi wao ni watu wanaowindwa na makundi au taasisi mbalimbali zinazolenga kulihujumu taifa letu.
Nimalizie makala hii kwa kutoa pongezi za dhati kwa Dk. Kipilimba na Naibu wake (DDGIS) Robert Msalika, sambamba na kumtakia mapumziko mema Mkurugenzi mstaafu Othman na kumkaribisha uraiani.
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.