19 Mar 2020

Ili uielewe vema makala hii ni vema ufanye kulinganisha kinachojiri Tanzania muda huu baada ya kutangazwa kuingia kwa Coronavirus na kinachojiri katika nchi jirani ambazo pia zimekumbwa na janga hilo la kimataifa.

Tuanze na Kenya. Mara baada ya kuthibitika kuwa taifa hilo lina mgonjwa mmoja aliyeambukizwa maradhi hayo, Rais Uhuru Kenyatta aliongea na Wakenya ambapo pamoja na mambo mengine aliwahakikishia kuwa serikali yake ipo nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu.
Twende Afrika Kusini. Mara baada ya kufahamika kuwa nchi hiyo imekumbwa na Coronavirus, Rais Cecil Ramaphosa aliwapatia Waafrika Kusini taarifa hiyo huku akitanabaisha kuwa hakuna sababu yakuona aibu wala kuficha taarifa hiyo kwa sababu ugonjwa huo umezikumba nchi nyingine pia.
Kwa majirani zetu wa Rwanda, Rais Paul Kagame alikwenda hatua kadhaa mbele kwa kujipanga vilivyo dhidi ya Coronavirus kabla haijaingia nchini humu ambapo licha ya kuweka sehemu za kuosha mikono katika maeneo mbalimbali,
Rais Kagame alimtimua Waziri wake wa Elimu kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu vifaa kwa ajili ya Coronavirus.
Na baada ya nchi hiyo kukumbwa na janga hilo, Rais huyo aliongea na Wanyarwanda na kuwataka wachukue hatua za tahadhari badala ya kuwa na hofu tu.
Na kwa majirani zetu wa DRC, Rais Felix Tshisekedi alihutubia taifa na kueleza mikakati mbalimbali ya serikaliyake katika kupambana na janga hilo la Coronavirus.
Nchini Ethiopia, Waziri Mkuu Ahmed Abiy amekwenda mbali zaidi ya kuwajali Waethiopia wenzie na amefanikiwa kupata sapoti ya mmoja wa matajiri wakubwa duniani Jack Ma, kutoa sapoti kwa mataifa mengine ya Afrika kupambana na janga la Coronavirus.

Na huko Uganda, licha ya nchi hiyo kutokuwa na maambukizi yoyote ya Coronavirus, Rais Yoweri Museveni amehutubia taifa na kutangaza hatua kadhaaza kujikinga dhidi ya janga hilo
Sasa turudi Tanzania kwetu. Mara ya mwisho kwa Rais Magufuli kusikika na kuonekana hadharani ni majuzi ambapo sio tu alidai kuwa Coronavirus haijaingia nchini Tanzania (japo masaa machache baadaye Waziri wake, Ummy Mwalimu alitangaza kuwa in fact tayari Tanzania ina mgonjwa mmoja mwenye maradhi hayo) bali pia hakutangaza hatua zozote za msingi kukabiliana na ujio wa janga hilo. Na kama mzaha vile, alikiri kuwa alikosea kusababisha mkusanyiko wa watu kusikiliza hotuba yake.

Lakini siku hiyohiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Abbasi aliongea upuuzi mkubwa dhidi ya Watanzania walioonyesha hofu kuhusu janga la Coronavirus.
Masaa machache baadaye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akatangaza kuwa Tanzania ina mgonjwa mmoja wa Coronavirus.
Na Waziri Ummy amegeuka simulizi baadaya kupatikana video hii ambapo anatanabaisha kuwa Tanzania haiwezi kukabiliana na Coronavirus.
Tangu tutangaziwe uwepo wa ugonjwa huo hatujamsikia tena Magufuli. Sijui amejificha wapi. Na kama ilivyozoeleka katika nyakati za majanga, "ghafla" Waziri Mkuu Kassim Majaliwa "amekuwa Waziri Mkuu tena"
 ambapo ndio amekuwa "sauti ya serikali" kuhusu hatua mbalimbali dhidi ya janga hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ya kufunga shule za awali, msingi na sekondari na vyuo.

Lakini uzeofu unaonyesha kuwa kila inapotokea Tanzania kukumbwa na janga fulani, Magufuli hukwepa dhamana aliyonayo kama "comforter-in-chief," yaani "mfariji mkuu wa taifa." Uthibiisho kuhusu hilo upo kwenye matukio mengi lakini pengine tukio lililoacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa Watanzania ni dharau alizowafanyia wahanga wa tetemeko la ardhi huko Kanda ya Ziwa.

Licha ya yeye kuwa mzaliwa wa eneo hilo, alikaa muda mrefu bila kwenda kuwapa pole wahanga wa tetemeko hilo, na alipokwenda "akawasemea ovyo."

Huu si wakati wa kulaumiana lakini pia huu si wakati wa kuzembea. Ni kwa minajili hiyo nimekuwa nikitoa wito kwa viongozi wakuu wa Upinzani, Mheshimiwa  Zitto Kabwe, Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Maalim Seif kutoa ninachokiita "uongozi mbadala wakati huu ambapo Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la Coronavirus.
Na endapo Magufuli hatobadilika, kwa maana ya "kuendelea kujificha," basi Watanzania watakuwa na kila sababu ya kutomhitaji tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba mwaka huu

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia umuhimu wa kuchukua hatua binafsi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu hatari wa Coronavirus. Nimekutengenezea video hii fupi

 Mungu atulinde sote. Amen.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.