#Thread: Awali nilipangilia kuwa thread hii iwe maalum kwa ajili ya kueleza jinsi hali ilivyo hapa Uingereza kuhusiana na janga la #Coronavirus kwa matarajio kwamba nanyi huko nyumbani au kwingineko duniani mnaweza kuwa na moja au mawili ya kujifunza.
Hata hivyo, katika pitapita zangu kabla ya kuandika thread hii nilikutana na makala moja ndefu kuhusu jinsi janga la jorona lilivyoibuka nchini Italia na kwanini nchi hiyo imeathirika vibaya mno, na pia endapo kinachojiri nchini humo ni "template" ya yatayojiri kwingineko.
Kwahiyo nadhani ni vema nikianza kuongelea kwa kifupi kuhusu makala hiyo, maana ina funzo kwa sie tulioko huku na kwa nyie mliopo huko.
Kwa kifupi kabisa, moja ya sababu iliyopelekea maambukizi kuwa makubwa na ya kasi nchini Italia ni kusuasua kwa mamlaka kuchukua hatua stahili.
Kwa mujibu wa makala hiyo, Italia ilikuwa na fursa nzuri ya kujikinga na janga hilo endapo tu kusingekuwepo dhana kwamba "korona ni sawa na mafua tu," (nikamkumbuka MwanaFA na madai yake ya "malaria ni hatari zaidi kuliko korona") na hisia kuwa "korona ni tatizo la China pekee. "
Kilichopaswa kufanywa na mamlaka za taifa hilo ni
(a) "kuyatenga" maeneo yenye maambukizi
(b) kuzuwia movements za watu kitaifa na kuhakikisha sheria kali zinatumika kuhakikisha utekelezaji
(c) mfumo wa mawasiliano usiokanganya kutoka kwa mamlaka husika kwenda kwa wananchi.
Inaelezwa kuwa katika siku za mwanzo za mlipuko wa janga hilo, Waziri Mkuu wa Italia Conte na viongozi wengine wa ngazi zajuu walijaribu kujenga picha kuwa ugonjwa huo sio tishio kwa nchi hiyo. Walijenga imani feki kuwa mambo ni shwari #tupovizuri.
Na hata maambukizi yalipozidi kukua, maelezo yaliyotolewa ni kwamba ongezeko hilo ni matokeo ya "aggressive testing" yaani jitihada kubwa za kupima watu mbalimbali bila hata kujali kama wana dalili za maambukizi. Na kulijitokeza lawama dhidi ya approach hiyo.
Kama ambavyo sura ngumu Polepole alivyodai majuzi kuwa Tanzania ikifunga mipaka itaathiri sekta ya utalii, awali baadhi ya viongozi wa Italia ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Conte walikuwa namtazamo kuwa hatua kali dhidi ya korona zingeathiri uchumi wa nchi hiyo.
Lakini pengine kikubwa zaidi ni kwamba Italia iliangalia kilichokuwa kinatokea China kama "filamu ya sayansi ya kutunga (science fiction movie) ambayo haiwahusi Wataliano."
Kichekesho ni kwamba hali ilipoanza kuwa mbaya nchini Italia, nchi nyingi hasa barani Ulaya na Marekani ziliangalia kinachotokea huko kama "tatizo la Italia tu" kama ambavyo awali Italia ilivyoiangalia korona kuwa ni "tatizo la China tu."
Mtu anayedhaniwa kuwa ndio "msambazaji wa kwanza wa korona" (Patient One) ni mwanaume wa miaka 38 ambaye Februari 18 alikwenda hospitali akiwa na mafua makali lakini hakuna aliyebaini kuwa ni mwathirika wa korona. Na kibaya zaidi, mgonjwa huyo alikataa kulazwa/
Hata hivyo, siku hiyohiyo jamaa huyo alirudi tena hospitalini hapo na kulazwa kwenye wodi ya kawaida (yaani isiyo maalum kwa ajili ya wagonjwa flani). Siku mbili baadaye alizidiwa mno, akapelekwa ICU ambako vipimo vilionyesha ana maambukizi ya korona
Kabla ya kukutwa na korona, mtu huyo alizunguka sehemu mbalimbali ambapo miongoni mwa matukio muhimu ni kuhudhuria pati tatu, alikwenda kucheza futiboli na pia alishirki kwenye jogging na timu ya soka. Yote hayo yalijiri wakati mtu huyo tayari ana maambukizi ya korona
Lakini la kupigia mstari ni kwamba hakuwahi kukutana na mtu yeyote kutoka China wala kutembelea China.
Maana yake ni kwamba mtu huyo aliambukizwa humohumo Italia, which means kabla yake tayari kulikuwa na mtu/watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Kwa kumalizia kuhusu kilichojiri Italia, moja ya vitu vilivyochangia sana mkanganyiko katika siku za awali ni kitu wanaita "infodemic" yaani kama "pandemic ila inayohusu information."
Kwa hapa Uingereza, hali ni mbaya. Na inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.
Tatizo la hapa ni kama ilivyokuwa Italia, ambapo kulikuwa na kusuasasua kuchukua hatua stahili. Kwa mfano, badala ya "kufunga kila kitu" mapendekezo ya mwanzo yalikuwa kitu kinaitwa "herd immunity."
Herd immunity ni kuacha maambukizi yasambae kisha wingi wa walioambukizwa upelekee kinga ya baadaye dhidi ya wasioambukizwa.
Matarajio ni kwamba mtu akishaambukizwa virusi vya ugonjwa husika na kupona, anakuwa na kinga ya kuzuwia kuambukizwa tena.
Lakini wazo hilo la herd immunity lilipingwa vikali hasa baada ya kubainika kuwa lingeweza kupelekea vifo laki mbili unusu au zaidi.
Kwahiyo serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson ikaja na mkakati wa "watu kujitenga" (social distancing).
Social distancing inamaanisha hatua kama wafanyakazi kutokwenda makazini na kufanyia kazi kutoka majumbani, sambamba na watu kukwepa kukutana kusiko kwa lazima.
Kadhalika, mkazo umewekwa kwenye kuongeza kasi ya kupima watu wenye dalili za maambukizi ya korona.
Sambamba na hilo ni hatua kali dhidi ya mikusanyiko, na kufungashule, sehemu za starehe mabaa, na kupunguza safari za vyombo vya usafiri. Kadhalika, serikali imewekeza vya kutosha kwenye tafiti mbalimbali za kusaka kinga na tiba ya korona.
Vilevile serikali imechukua jukumu la kulipa asilimia 80 ya mishahara ya waajiriwa ili kuwezesha waajiri kuruhusu wafanyakazi wao wasiende kazini au wafanye kazi kutokea nyumbani. Ikumbukwe pia kuwa hapa watu wasio na kazi hulipwa posho ya kujikimu na ya makazi.
Inatarajiwa kuwa wiki 12 zijazo zitakuwa ngumu sana kwa nchi hii kwa sababu ndio kipindi ambapo jitihada kubwa zinafanyika kuzuwia maambukizi mapya sambamba na kuzuwia kusambaa kwa maambukizi yaliyopo huku ikitarajiwa kuwa mamilioni ya watu wataweza kujipima wenyewe majumbani.
Tayari makampuni mbalimbali yamesitisha uzalishaji wa bidhaa zao na kuelekeza nguvu kwenye uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika katika kipindi hiki cha janga la korona hapa Uingereza. Lakini ni ngumu kubaishiri kuwa hatua hizo zinazochukuliwa muda huu zitafanikiwa kukabili janga hilo.
Kwa upande mmoja, ugonjwa huo ni mpya na upya huo unapelekea ugumu wa kuuelewa vizuri. Kwa mfano hakuna uhakika wa kutosha kuwa mtu akipona hatoambukizwa tena.
Kuhusu huko nyumbani, kwa kweli mie binafsi nina wasiwasi mkubwa. Kwa upande mmoja, licha ya majigambo ya watawala wetu, sie ni masikini wa kutupa. Hatuna uwezo wa lolote bila kutegemea wafadhili. Kibaya ni kwamba wafadhili wetu nao wapo vitani dhidi ya korona.
Lakini pengine adui mbaya zaidi kwetu ni kasumbailiyoota mizizi ya kufanya kila jambo kuwa ni la kisiasa. Majuzi mmemsikia sura ngumu Polepole akiufananisha ugonjwa wa korona na wapinzani. Na akajigamba kuwa kama wanavyomudu kupambana na wapinzani basi wataimudu korona pia.
Wakati ambapo taifa linapaswa kuwa kitu kimoja, hawa wahuni wanaleta mzaha wa siasa. Lakini korona hii si ya kuchezewa maana haibagui kati ya huyu wa chama tawala na huyu mpinzani wala kiongozi na raia wa kawaida.
Pia tuna tatizo la "infodemic."Pandemic ya information. Kwa upande mmoja ni jitihada za akina Bashite kutumia watu kuhadaa kuwa hali ni shwari, kosa ambalo kama umefuatilia vema thread hii linaigharimu Italia na hata Uingereza na Marekani.
Lakini pengine baya zaidi ni taarifa ninazopokea kila siku kuwa sehemu kadhaa wananchi wamepigwa marufuku "kuongelea korona," ikiwa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya kutishwa kwamba wakiripoti matukio ya korona kwenye hospitali zao wataadhibiwa.
Mwisho, tuna Bwana @MagufuliJP ambaye hadi leo sijui siku ya ngapi hajaona umuhimu wa kujitokeza hadharani kuongea na Watanzania. Hizi sio dharau tu bali ni kukosa utu. Lakini hali hiyo imeshazoeleka sasa. Kila linapotokea janga anaingia mitini.
Hata hivyo, tunashukuru tumefanikiwa kupata uongozi mbadala wa Mheshimiwa @zittokabwe ambaye juzi alihutubia taifa kuhusu janga la korona, hotuba bora kabisa yenye taarifa za kutosha na iliyojaa upendo kwa Watanzania. Icheki hapa (youtu.be/Jc7ZD3PDrXc)
Nimalizie kwa kuwasihi nyote mchukue tahadhari dhidi ya janga hili. Pia ni muhimu kukazania sala/dua. Pia tufahamishane taarifa mbalimbali hususan zinazofichwa kwa minajili ya kisiasa au zozote zile zitakazoisaidia jamii kukabiliana na korona.
Be safe. Jumapili njema
UPDATE: Hatimaye Rais Magufuli amehutubia Taifa japo baadhi ya kauli zake zinaweza kuwa kukwaza jitihada za mapambano dhidi ya #coronavirus. Pichani ni baadhi ya kauli hizo
0 comments:
Post a Comment