4 Mar 2020



Kuna njia mbalimbali za kufanya uchambuzi wa kiintelijensia, njia zinazotegemea vigezo mbalimbali, kigezo muhimu zaidi kikiwa tukio husika na/au "key players" (kwenye ushushushu tunawaita "subjects") katika tukio hilo.

Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia kuhusu tukio la jana ambapo Rais Magufuli alikutana na viongozi wakuu watatu wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, na Ibrahim Lipumba wa CUF, nitatumia kanuni ijulikanayo kama 'Linchpin,' ambayo ni mwafaka zaidi pale ambapo "ukweli mzima" upo bayana (au "vipande vya ukweli).



Kanuni hii ya Linchpin ilibuniwa na Naibu Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), Douglas MacEachin, na inahusu "matukio ya ghafla/ya kushangaza," ambapo aliitumia kanuni hiyo kueleza tukio la ghafla na Iraki kuivamia Kuwait mwaka 1990. 

Katika kanuni hii, uchambuzi wa kiintelijensia unatathmini tukio/matukio husika kwa kuzingatia "ukweli uliopo/unaofahamika," kitu tofauti kidogo na mbinu nyingine za uchambuzi wa kiintelijensia zinazoanza na hisia au dhana (kama ile ya ACH -Dhana Zinazoshindana -nilioutumia majuzi kuchambua tukio la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM)

Kwa vile lengo la makala hii sio kutoa darasa la "mbinu za uchambuzi wa kiintelijensia," bali kutumia kanuni ya Linchpin kueleza "tukio la ghafla," la Jiwe kukutana na Maalim Seif, Mbatia na Lipumba, ni vema nikahamia kwenye uchambuzi husika.

Kwa kutumia kanuni hiyo, kuna "ukweli " (facts) kadhaa ambao ni msingi wa uchambuzi huu. Ukweli mkubwa zaidi ni kitu nilichokiongea wiki iliyopita baada ya mwandishi Erick Kabendera kuachiwa baada ya kuwekwa jela kwa uonevu kwa zaidi ya miezi sita.



Awali nilieleza kuhusu hilo la "Jiwe kukaliwa kooni na mabeberu" katika chapisho langu hili


Kwahiyo ukweli mmoja - na muhimu zaidi - uliopelekea "tukio hilo la ghafla" ni shinikizo la mabeberu. Shinikizo ambalo wiki iliyopita lilipelekea mwandishi Kabendera kuachiwa, na wiki hii limepelekea Jiwe kukutana na viongozi hao watatu wa upinzani.

Nimetanabaisha kuwa huo ni "ukweli muhimu zaidi" kwa sababu kuna ukweli mwingine japo sio wenye uzito sana. 

Uamuzi wa Jiwe kukutana na akina Maalim Seif jana ni sawa na "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Kwa upande mmoja amefanikiwa kutuliza shinikizo la mabeberu ambao wameweka bayana msimamo wao kuwa wanaweza kutochangia bajeti ijayo endapo ukandamizwaji wa demokrasia na haki za binadamu utaendelea. Amewatuliza mabeberu kwa kuwaonyesha kuwa "demokrasia ipo" na ndio maana ameweza kukutana na sio kiongozi mmoja tu wa upinzani bali watatu kwa mkupuo.

Nimesema "ameua ndege wawili kwa jiwe moja." Na "ndege" wa pili ni Membe. Mkutano wake huo na akina Maalim Seif unafikisha salamu muhimu kwa Membe aliyefukuzwa uanachama wa CCM wiki iliyopita, kwamba "hao unaotaka kujiunga nao ndo hawa niko nao hapa Ikulu kwangu."

Kama nilivyoeleza katika uchambuzi kuhusu tukio hilo la Membe kufukuzwa uanachama wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa mwanasiasa huyo kujiunga na ACT-Wazalendo. Na kwa vilekufukuzwa kwake CCM ni matokeo ya uoga wa Jiwe kuhusu upinzani kwenye nafasi ya urais, Membe "kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo" ni worst nightmare kwa Jiwe. 

Naomba nirudie kusisitiza kuwa uoga huo wa Jiwe hauna msingi kwa sababu Membe hana uwezo wa kumwangusha Jiwe kwa sababu nilizowahi kutanabaisha katika makala hii.



Kwahiyo Jiwe akiweza kumzuwia Membe kisaikolojia asiwaamini Wapinzani itakuwa ni nafuu kubwa kwake na uoga wake.

Ukweli mwingine kuhusu mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao wa upinzani ni "busara ya kisiasa" inayosema "kuwa karibu na marafiki zako, lakini kuwa karibu zaidi na maadui zako."

Ukweli mchungu kuhusu wanasiasa wetu - wa CCM na hao wa upinzani - ni huu: wote wapo katika "tabaka tawala" (ruling class). Hapana, simaanishi kuwa akina Seif, Mbatia na Lipumba ni sehemu ya utawala wa Jiwe bali ukiangalia kwa undani wasifu wa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, unaweza kubaini kuwa "wote ni wale wale."

Na ukiangalia wasifu wa Maalim Seif, Mbatia na Lipumba hutoshindwa kubaini kuwa ni watu ambao tumekuwa tukiwasikia "miaka nenda miaka rudi" lakini "wakiwa upande wa pili," kwa maana "sio upande wetu" watu wa tabaka la chini. Kwa kuazima neno la mtaani, hawa ni "vigogo."

Ukweli mwingine ni kwamba mkutano huo wa Jiwe na akina Maalim Seif "ndio siasa ilivyo." Kuna kitu kwenye siasa kinaitwa "realpolitik" ambacho kwa tafsiri isiyo rasmi ni "siasa ilivyo kimatendo kuliko kinadharia/kiitikadi." 

Sasa kwenye "siasa halisi" iwe ya kitaifa au ya kimataifa, "hakuna marafiki au maadui wa kudumu bali maslahi tu." Na ndio maana licha ya msimamo wake msimamo wake mkali dhidi ya vikundi vya kigaidi, na kauli maarufu kuwa "we don't negotiate with terrorists," majuzi Marekani ilifikia makubaliano na kundi la kigaidi la Taliban.

Na jana ilifahamika kuwa Rais wa nchi hiyo Donald Trump aliwapigia simu viongozi wa kundi hilo, kitu ambacho kabla ya tukio hilo kilikuwa sio rahisi kukifikiria.



Baada ya kuangalia "ukweli"(facts) huo unaojenga msingi wa uchambuzi huu, kanuni ya Linchpin inawezesha kujenga picha ya matarajio yanayohusiana na tukio/watu husika. Hapa ninamaanisha kuwa hadi kufikia hapa, yawezekana kueleza nini kinaweza kujirihivi karibuni au huko mbeleni.

Moja ni hiyo sintofahamu inayoweza kumkumba Membe baada ya kumuona Maalim Seif akiwa Ikulu na Jiwe. Ikumbukwe tu Lowassa alipoonekana Ikulu bila kutarajiwa "waumini"wake walimtetea na kuamini porojo zake kuwa kaambiwa arudi CCM lakini amegoma. Baadaye ukweli ukadhihirika baada ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kurejea CCM.

Simaanishi kuwa Maalim Seif atakubali kurudi CCM. La hasha. Kinachoweza kutokea ni Jiwe kujaribu tena "kuua ndege wawili kwa JIWE moja." Anaweza kumfarakanisha Maalim Seif na Zitto na hapohapo kupunguza tishio kubwa kwake kutoka kwa Zitto kama Zitto, na Zitto akiwa na Maalim Seif.

Ikumbukwe tu kuwa japo Lowassa alikuwa kama 'mungu-mtu' huko Chadema, kitendo chake cha kuonekana Ikulu na Jiwe kiliwafanya hata baadhi ya "waumini" wake waanze kuwa na hofu nae.

Sina uhakika hali ikoje huko ACT-Wazalendo baada ya Maalim Seif kukutana na Jiwe, lakini ni siri ya wazi kuwa Jiwe na Zitto "picha haziivi," na wala sio jambo la kushangaza kuona Zitto hakualikwa kwenye mkutano huo.Na wala  sina hakika kama angekubali mwaliko wa Jiwe.

Kuhusu Mbatia na Lipumba, hakuna haja ya kupoteza muda kuwajadili maana "wapo kama hawapo." 

Moja ya maswali muhimu kuhusu Malim Seif kwenda Ikulu kukutana na Jiwe ni je alipata ridhaa ya Zitto na chama kwa ujumla? Na je tukio hili linaweza kuzua mpasuko huko ACT-Wazalendo? Pengine kukusaidia kuelewa vema "siasa za ACT-Wazalendo," pitia uchambuzi wangu huu nilioufanya mara baada ya Maalim Seif kujiunga ACT-Wazalendo.

Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za Tanzania yetu kubaini kuwa mnufaika mkubwa wa mkutano huo kati ya Jiwe na viongozi hao watatu wa upinzani ni Jiwe mwenyewe. 

Hilo lipo wazi. Lisilo wazi ni "yanayoweza kujiri" kutokana na mkutano huo. Je Maalim Seif anaweza kuangaliwa kama "msaliti" kwa kukubali "kukutana na dikteta ambaye majuzi tu akiwa Zanzibar alikuwa anamwaga sumu kwa Dkt Shein kuhusu jinsi ya kumdhibiti Maalim Seif?"

Kwa upande mwingine, kama kweli Jiwe alikuwa na nia njema ya kukutana na viongozi wa upinzani basi pengine wa kwanza kabisa kupewa kipaumbele cha kukutana nae angekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye majuzi tu alimuomba Jiwe kuwe na MARIDHIANO. Lakini ni vema "kuweka akiba ya maneno" kwani haitokuwa jambo la kushangaza tukimuona Mbowe Ikulu kama alivyoongozana na timu yake Mwanza kwenye sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka jana. 

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kutahadharisha kuwa intelijensia sio sayansi timilifu (intelligence is not exact science) licha ya uchambuzi huu kuongozwa na kanuni ya Linchpin ambayo ina ufanisi mkubwa penye uwepo wa ukweli kuhusu tukio/mtu husika.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.