Na Frederick Katulanda, Busanda
KAMPENI za uchaguzi za CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda jana zilizidi kukumbana na upinzani mkali baada ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na makamu mwenyekiti wa zamani, John Malecela, kujikuta wakizomewa wakati walipokuwa wakijinadi katika mkutano uliofanyika Nyarugusu wilayani Geita.
Mbali na vigogo hao wa CCM, mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo, Lolencia Maselle Bukwimba na mumewe, Maselle Buziku walizomewa wakati walipotambulishwa kwenye mkutano huo wa kampeni.
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya chama hicho kujikuta kikiwa na watu wachache wakati wa kuzindua kampeni zake kwenye kata ya Kaseme, tofauti na mikutano ya vyama pinzani vya Chadema na CUF.
Dalili za hali mbaya katika mkutano huo zilianza wakati viongozi hao wakiingia eneo la Nyarugusu ambalo ni maalumu kwa wachimbaji wa dhahabu. Viongozi hao walipokelewa na alama ya vidole viwili kila walikopita. Alama ya vidole viwili hutumiwa na Chadema.
Zomea zomea hizo ziliwakabili viongozi hao wa CCM wakati walipokuwa wakimnadi mgombea wao. Hali mbaya ilianza kwa katibu mwenezi na uhamasishaji, Simon Mangelepa wakati aliposimama jukwaani na kuanza kuwatambulisha wageni walioambatana nao na kufuatiwa na mbunge wa viti maalum mkoani Mwanza, Maria Hewa ambaye alizomewa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa wanapaswa kutulia.
Kutokana na hali hiyo mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina alisimama jukwaani kabla ya kumkaribisha Malecela ili amnadi mgombea wa chama hicho na kuwaeleza kuwa anazo taarifa kuwa kuna watu ambao wamepangwa hapo kwa ajili ya kuzomea, naye kuzomewa.
Baadaye ikawa zamu ya Malecela ambaye baada ya kusimama jukwaani aliwaeleza wananchi kuwa shutuma za ufisadi hazina nafasi katika kampeni kwa sasa na kuwataka wenye ushahidi wa ufisadi kuupeleka polisi, kauli ambayo iliwafanya wananchi ambao walikuwa wametulia, kuanza kuzomea wakimtaka aondoke huku wakionyesha vidole viwili.
Hata hivyo, Malecela aliwatuliza na kuwaeleza kuwa hiyo ndio njia sahihi ya kushughulikia mafisadi na kuendelea kuwaeleza wananchi kuwa iwapo wataichagua CCM katika uchaguzi huo watapatiwa umeme pamoja na kutengewa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
“
Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.
Kutokana na hali hiyo Malecela aliamua kuwatuliza na kuomba Busanda isigeuke kama Tarime na kwamba wao CCM wanataka kampeni za amani na utulivu.
Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.
Hata hivyo zomea zomea hizo hazikuweza kuhatarisha amani katika mkutano huo na mgombea huyo alijieleza bila ya matatizo na kupiga magoti lakini alipoomba kura, naye akajikuta anazomewa.
Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amekiri kuwa kuna hali ngumu kwenye Jimbo la Busanda na kuwataka viongozi wa chama hicho kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha jimbo haliangukii mikononi mwa upinzani kwa kuwa machungu ya kushindwa Tarime anayajua.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamba juzi mchana wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika mkutano wa ndani kwenye ofisi za CCM wilayani Geita baada ya kuwasili kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni wa chama chake zilizofanyika juzi katika kata ya Kaseme.
Makamba alikiri kuwa hali ni ngumu na hivyo kuwaomba kila mmoja kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda, akilalamika kuwa makali ya kushindwa alishayaonja Tarime.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa chama wilayani humo zimeeleza kuwa Makamba aliamua kufanya mkutano huo kwa lengo la kuwekana sawa kutokana na CCM kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wale walioenguliwa katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho.
Makamba amesema "jamani kushindwa ni kubaya, mwenzenu Tarime nilionja ubaya wake mpaka ilibidi nitoroshwe na Green Guard ili kuepuka kuzomewa, sasa tusiposhikamana mambo yatakuwa magumu tutoe tofauti zetu,'” alisema mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kikao hicho akimnukuu Makamba.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo Makamba alishtuka na kuhoji iwapo walikuwemo waandishi wa habari ukumbini humo na kuonya utoaji wa taarifa hizo baada ya kujibiwa hawakuwemo.
Aidha baada ya kujibiwa kuwa hakuna waandishi Makamba alishtuka baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mpiga picha wa chama na kumuagiza kuhakikisha mkanda huo anaukabidhi kwa katibu wa CCM wa mkoa.
Makamba alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa hajawahi kukiri kuwepo kwa hali ngumu kwa vile hana wasiwasi na uchaguzi huo na kusema alikuwa akieleza masuala ya kushikamana.
“Wewe unataka nikueleze mikakati yangu, kama nilikuwa nawahimiza watoto wangu kulima we unakutakia nini,” alihoji katibu huyo wa CCM alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kikao hicho.
Sambamba na hatua hiyo Makamba alimtaka mjumbe wa halmshauri kuu ya chama hicho mkoani Mwanza, Anthony Diallo kutumia uwezo wake kuhakikisha kampeni hizo zinakuwa na hamasa ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurusha taarifa zake katika vyombo vya habari.
Uchaguzi katika jimbo la uchaguzi la Busanda umepangwa kufanyika Mei 24 kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Faustine Kabuzi Rwilombe.
Vyama vingine vinavyowania kiti hicho ni Chadema, CUF na UDP.
WANACHOHITAJI CCM NI BUSARA ZA KI-UTU UZIMA,YAANI KUKIRI PALE WALIPOKOSEA,NA KUAHIDI KUJIREKEBISHA BADALA YA KUENDELEZA AHADI HUKU ZILE WALIZOTOA MWANZO ZIMEENDELEA KUBAKI AHADI TU PASIPO KUZITEKELEZA.WAINGEREZA WANASEMA " A PROMISE MEANS NOTHING UNTIL DELIVERED."
HALAFU HIZI KAULI ZA KIBAGUZI KUWA "ICHAGUENI CCM IWALETEE HIKI AU KILE" (AS IF AWALI ILIYOCHAGULIWA ILIKUWA CHADEMA AU CUF) NI KUWAFANYA WAPIGA KURA WAJINGA AU WASAHAULIFU.KAMA WALIKUWA NA NIA YA KULETA HUO UMEME,SI WANGEFANYA HIVYO WAKATI WAPIGA KURA WALISHAWAPA HESHIMA YA KUMCHAGUA MGOMBEA WA CCM KWENYE UCHAGUZI ULIOPITA?SASA HIZI HABARI KUWA MKITUCHAGUA TENA NDIO TUTAFANYA HIKI AU KILE NI MITHILI YA KUWAHADAA WANANCHI.
I HOPE WAPIGAKURA WA BUSANDA HAWATAISHIA KUFIKISHA UJUMBE KWA CCM KWA KUZOMEA TU BALI PIA KUINYIMA KURA ILI IKIAMSHE CHAMA HICHO KUTOKA USINGIZINI KWAMBA THIS IS 2009,AND SO FAR THE ASSESSMENT OF HOW THE PARTY HAS IMPLEMENTED ITS ELECTION MANIFESTO LEAVES A LOT TO BE DESIRED.KAMA TARIME WALIWEZA,BUSANDA PIA WANAWEZA.NA KAMA WOTE WASIORIDHIKA NA MWENENDO WA CCM WATAAMUA KUWA ENOUGH IS ENOUGH,NO MORE FALSE PROMISES,THEN CHANGE IS NOT ONLY COMING BUT WILL EVENTUALLY BE ACHIEVED.
AS OBAMA SAID,YES WE CAN IF WE BELIEVE IN CHANGE.