Showing posts with label PIUS MSEKWA. Show all posts
Showing posts with label PIUS MSEKWA. Show all posts

23 Apr 2011


Nimekutana nayo huko Jamii Forums:

Kichuguu;

Mimi kama mmoja wa wanachama waandamizi wa Jamii Forums ambapo nimekuwa mwanchama kwa karibu miaka mitano sasa tangu ikiwa Jambo Forums kabla ya kubadili jina na kuwa Jamiiforums nimekerwa sana na matamshi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM kuwa forums hii ni ya vijana wa CHADEMA. Naona kuwa amenivunjia sana heshima yangu mbele ya wenzangu kwa kunipa image ya kuwa mimi ni mpiga propaganda wa CHADEMA.

Baada ya kutafakari kwa kina matamshi ya Pius Msekwa na jinsi yalivyoathiri image yangu kama mwanachama wa JamiiForums, nimeamua kumfungulia mashtaka ya defamation kwenye mahakama ya Douglas County hapa Omaha Nebraska nchini Marekani. Nimejadiliana na mwanasheria wangu ambaye amenipatia kifungu cha sheria kinachoniruhusu kumshitaki raia wa nchi ya nje kwenye mahakama hii, iwapo marekani ina uhusiano wa kibalozi na nchi ya mshitakiwa. Sasa hivi tuko katika hatua za mwisho mwisho za kukusanya ushahidi imara.

Nimeshapata nakala za magazeti ya kiswahili na kiingereza ila nimekuwa natafuta video clip yenye kumwonyesha Msekwa akiwa anasema maneno hayo. Vile vile bado tunashauriana kiwango cha malipo ya Punitive Damages na Compensatory Damages; mwanasheria anashauri kuwa viwango hivyo vipimiwe zaidi kwa kuangalia jinsi gani Msekwa binafsi na chama chake walivyofaidika au watakavyofaidika kutokana na matamshi yake hayo, na kwa kiasi kidogo jinsi gani yalivyoathiri image yangu binafsi kama mwanachama mwanadamizi ambaye hujitambulisha kwa wenzagu wote kuwa mimi ni Premium Member wa JamiiForums.

Tukikamailisha taratibu zote, nitawaarifuni au mtasikia kwenye vyombo vya habari Msekwa akiwa subpoenaed kwenye kesi hii ambayo pamoja na mambo mengine ninataka kuwadhibiti wanasiasa wasiwe wanaropoka mambo bila kuwa na uhakika nayo.

Ngoma inogile

7 Jul 2010


Demokrasia katika jamii isiyojali utawala bora ni sawa na kufukia makaratasi ardhini kwa matarajio ya kuota mmea wenye matunda ya noti.Ni mithili ya kualika timu ya Taifa ya Brazil kwa mabilioni ya shilingi kisha mechi husika ituache na bili kubwa pasipo manufaa yoyote.Hebu tafakari.Mwezi Oktoba Watanzania kwa mamilioni yao watapiga kura kumchagua Rais na Wabunge.Japo shughuli hiyo ni ya siku moja tu,maandalizi yake yanagharimu mabilioni ya shilingi.Wenyewe wanasema ndio gharama ya demokrasia.Lakini baada ya uchaguzi,wengi-kama sio wote-wa tutakaowachagua watasahau kabisa kwanini tumewachagua,huku wakiwa bize kutafuta namna ya kufidia gharama walizotumia kuingia madarakani.

Zamani hizo tuliambiwa kuwa demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyama vingi vya siasa.Takriban miongo miwili baadaye Watanzania wameshuhudia namna uwepo wa vyamahivyo vingi vya siasa ulivyoshindwa kulikwamua taifa letu kutoka kwenye lindi la umasikini.Sanasana umasikini umekuwa ukizidi kuongezeka huku wanasiasa wetu wakibadili kauli mbiu kila baada ya muhula (kwa mfano kutoka Ari Mpya,Kasi Mpya na Nguvu Mpya kuwa Ari Zaidi,Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi).Tumeshuhudia pia mlolongo wa sera,mikakati,mpingo na vitu kama hivyo,from MKUKUTA to MKURABITA to KILIMO KWANZA.Na kwa mawazo mapya hatujambo,shughuli ipo kwenye utekelezaji.

Siku chache zilizopita nilitundika makala kuhusu utata wa kauli za Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe na zile za Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa kuhusu suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi.Wakati Waziri Chikawe aliahidi kuwa mahakama hizo zingeanza kazi mwakani,Msekwa alitamka bayana kuwa suala hilo haliwezekani.Hadi leo hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu suala hilo ila kilicho bayana ni kuwa CCM imeamua kuachana nalo baada ya kuliingiza kwenye manifesto yake ya Uchaguzi mwaka 2005.Kwa vile sie ni mahiri zaidi wa kuhangaika na mambo kwa mtindo wa zimamoto tunasubiri liwake la kuwaka ndipo tuanze kuhangaika namna ya kudhibiti.Taasisi zenye majukumu ya kuwa proactive (yaani kuazuia majanga kabla hayajatokea) ziko busy zaidi na kuhakikisha CCM inarejea madarakani kwa ushindi wa kishindo badala ya kujishughulisha na jukumu lao la msingi la kulinda na kutetea ustawi wa taifa letu.Kwao,siasa (yaani CCM) ndio nchi na ndio kila kitu.

Majuzi umejitokeza utata mwingine wa kauli kati ya mawaziri wawili waandamizi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship).Na kichekesho ni kwamba tofauti na ule mgongano wa kauli kati ya Chikawe na Msekwa,safari hii mgongano wa kauli za mawaziri hao umejiri ndani ya jengo la Bunge katika kikao kinachoendela cha bajeti ya mwaka 2010/11.Awali,Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha alilieleza Bunge Tukufu kuwa serikali imeamua kuwa huu sio wakati mwafaka kwa suala la uraia wa nchi mbili,na kwamba serikali anaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu (permanent residency).Waziri Masha alieleza kuwa serikali inaandaa hoja kuhusu suala hilo la permanent recidency kwa minajili ya kuileta bungeni ijadiliwe. "Huu sio wakati mwafaka kuruhusu uraia wa nchi mbili,serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu badala ya uraia wa nchi mbili", alisema Masha.

Wakati Masha akisema hivyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alilieleza Bunge hilohilo kuwa serikali imeridhia suala la uraia wa nchi mbili na kwamba Wizara yake iko kwenye mchakato wa kuwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Barza la Mawaziri.Pia Membe alieleza kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.

Kadhalika,inadaiwa kuwa Waziri Membe aliwaeleza Watanzania waliohudhuria mkutano wa Diaspora jijini London hivi karibuni kwamba suala hilo limeshajadiliwa na baraza la mawaziri na linasubiri kuwasilishwa bungeni ili upitishwe au kupingwa na wabunge.Mimi sikuhudhuria Mkutano huo wa Diaspora kwa vile niliamini ungenipotezea muda wangu tu kwa sababu viongozi wetu ni mahiri sana katika kuahidi mambo mazuri kwenye hadhara,na hujifanya wasikivu sana lakini utekelezaji ni zero,sifuri,zilch!

Ni dhahiri kwamba mmoja kati ya mawaziri hawa anadanganya.Wakati sina la kusema kuhusu kauli ya Waziri Masha,kauli za Waziri Membe huko Bungeni na London zinaleta utata unaoweza kuyumkinisha kuwa kuna urongo wa namna flani.Je kauli ipi ni sahihi kati ya hiyo alotoa London kuwa suala hilo limeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na hiyo ya bungeni kuwa suala hilo bado liko wizarani huku likifanyiwa mchakato wa kulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri?

Unajua kwanini mmoja wao anadanganya?Sababu ni kadhaa,lakini kwa ufupi,moja,ni kwa vile mdanganyifu huyo anafahamu bayana kuwa wabunge wanaoelezwa suala hilo wapo bize zaidi kufikiri namna watakavyorudi bungeni baada ya uchaguzi (sambamba na kuwazia posho zao nono za vikao vya bunge) kuliko kumkalia kooni waziri aeleze kinagaubaga.Ndio maana mwanzoni mwa makala hii nilibainisha uselessness ya demokrasia yetu.Tunapoteza mabilioni ya shilingi (sambamba na muda wetu kusikiliza porojo za "mkituchagua tufafanya hiki na kile") kuwachagua watu wa kutuwakilisha bungeni lakini wakishafika huko wanakuwa bize zaidi na maslahi yao binafsi.

Pili,anayedanganya kati ya mawaziri hao anafahamu kuwa aliyemteua hatamwajibisha.Kama kuna mtu alimudu kumzuga Rais kwa kuchomekea ishu kadhaa kwenye muswada wa sheria za gharama za uchaguzi na kisha akasalimika,kwanini basi mdanganyifu huyo katika suala hili la uraia mbili awe na hofu?

Tatu,waziri anayedanganya kati ya hao wawili anafahamu udhaifu wa Watanzania katika kudai haki zao za msingi.Kiongozi anaweza kudanganya waziwazi kwenye umati wa watu lakini bado akaishia kupigiwa makofi na vigeregere.Ule wimbo wa "Ndio Mzee" wa Profesa Jay unawakilisha hali halisi ya namna Watanzania wengi wanavyoridhia kuzugwa na wanasiasa wababaishaji.Hebu angalia namna harakati za kuirejesha tena madarakani CCM zinavyopamba moto huko nyumbani.Kwa mgeni,anaweza kudhani labda chama hicho ni kipya na hakihusiki kabisa na kashfa za ufisadi,kubebana,kubomoa uchumi wetu na madudu mengine chungu mbovu yanayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya raslimali lukuki iliyojaaliwa kuwa nazo.Binafsi naamini kuwa unyonge huo wa Watanzania umechangiwa sana na siasa za chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya Mungu-mtu,hakosei,lazima ashangiliwe hata akiongea utumbo,sambamba na suala la kujikomba kwa viongozi kwa matarajio ya kujikwamua kwa namna moja au nyingine.

Na kwa vile vyama vya upinzani vimetuthibitishia kuwa uwezo wao katika kuing'oa CCM madrakani ni kama haupo,basi mazingaombwe kama hayo ya Chikawe na Msekwa,na haya ya sasa kati ya Masha na Membe yataendelea kuwepo kwa muda mrefu sana.Unaweza kuhisi kama nimekata tamaa vile kwa namna ninavyoandika.Hapana,ila safari yetu ni ndefu sana,na tatizo sio urefu tu bali ni kiza kilichotanda kwenye njia yetu ambayo imejaa mashimo kadhaa.Ni sawa na kipofu kumsaka paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayumo chumbani humo.

26 Jun 2010

Sijui ni ukosefu wa mawasiliano au uzembe tu,au pengine ni mkakati wa makusudi wa kutoa kauli zinazotofautiana ili baadaye iwe rahisi "kuziruka kimanga",lakini ni dhahiri kuwa mmoja kati ya viongozi hawa anatudanganya.Wakati Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe akirejea ahadi kama ya mwaka 2005 (wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu) kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi,Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa anasema bayana kuwa suala hilo halipo (labda Waislamu wenyewe walishughulikie "kivyao").Hebu soma kwanza hapa chini

Kwa mujibu wa Gazeti la Tanzania Daima: SERIKALI imesema Mahakama ya Kadhi itaanza katika mwaka wa fedha 2010/11 baada ya jopo la wanazuoni wa Kiislamu wanaoziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu kukamilisha kazi hiyo.

Jambo hilo lilibainishwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe wakati akisoma hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2010/2011 ambapo ameliomba Bunge limuidhinishie kiasi cha sh bilioni 116.8

Alisema kuwa jopo hilo linaziangalia na kuzihuisha sheria za Kiislamu zinazohusiana na ndoa, mirathi na urithi kwa madhumini ya kuziorodhesha ili zitambuliwe chini ya sheria za dini ya Kiislamu (Islamic Law resstatment act).

Aliongeza kuwa jopo hilo lilianza kazi hiyo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na Mufti, Sheikh Mkuu, Issa Bin Shaaban Simba, na kukubaliana kuwa waanzishe mchakato wa Mahakama ya Kadhi.

Lakini Gazeti la Majira linaripoti kwamba:

Katika hatua nyingine, Bw. Msekwa amefafanua sababu za ilani ya CCM mwaka huu kutohusisha kipengele cha uanzishwaji wa Mahakam ya Kadhi kama ilivyokuwa mwaka 2005.

Alisema kuwa ahadi hiyo iliyotolewa 2005 tayari utekelezaji wake umekamilika.

Katika ilani hiyo, kifungu namba 108(b) CCM iliahidi kulipatia ufumbuzi suala la kuanzishwa mahakama ya kadhi Tanzania bara, ambalo limekamilika kwa kukabidhi wenye dini yenyewe wahusike katika uanzishwaji wa mahakama hiyo, kwa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siyo ya kidini.

"Serikali inaweza kukubali au kukataa, ndiyo maana ya kulipatia ufumbuzi lakini watu wanalitafsiri vibaya kuwa
serikali kupitia kifungu hicho imekubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo wakati sivyo," alisema Bw. Msekwa.

Alibanisha kuwa serikali ilifanyia kazi kupitia Tume ya Kurekebisha sheria ambayo ilishauri kwamba haitakuwa sahihi kwa mahakama ya kadhi kuundwa na serikali kwa kuwa ni suala linalohusu taratibu za dini ya kiislamu.

Aliongeza kuwa baada ya serikali kupata ushauri huo ilifanya uamuzi kwamba haitaunda mahakama ya kadhi lakini kwa kuwa suala hilo linahusu taratibu za dini la kiislamu, waislamu wapo huru kuunda mahakama hiyo ndani ya taratibu za dini yao.

14 Oct 2009


Na Fredy Azzah

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, amesema kashfa za ufisadi zinazowakabili baadhi ya viongozi wake, zimekiumbua chama hicho pamoja na serikali yake.

Akiwahutubia wanafunzi wa matawi ya CCM ya vyuo vikuu vilivyopo jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere jana, alisema ufisadi ambao umewakumba wengi umesababishwa na tabia ya viongozi kulindana na kutosimamia kikamilifu maadili ya uongozi yaliyoainishwa ndani ya katiba ya CCM.

Alisisitiza kuwa tabia hiyo ni kinyume na misingi ambayo Baba wa Taifa, aliwaachia Watanzania....ENDELEA

WAKATI HUOHUO

WASOMI na wanazuoni nchini, wamesema nchi haina dira na kwamba kuna mpasuko mkubwa ambao usiposhughulikiwa mapema, nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.

Wakizungumza juzi katika baraza lililopewa jina la Mbongi, lililoandaliwa na Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Julius Nyerere, walisema mpasuko hiyo ni pamoja na ya udini, ukabila, ukanda, matatizo ya vitambulisho Zanzibar pamoja na hofu ya kuvunjika muungano...ENDELEA

CHANZO: Mwananchi

8 May 2009


Na Frederick Katulanda, Busanda

KAMPENI za uchaguzi za CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda jana zilizidi kukumbana na upinzani mkali baada ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na makamu mwenyekiti wa zamani, John Malecela, kujikuta wakizomewa wakati walipokuwa wakijinadi katika mkutano uliofanyika Nyarugusu wilayani Geita.

Mbali na vigogo hao wa CCM, mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo, Lolencia Maselle Bukwimba na mumewe, Maselle Buziku walizomewa wakati walipotambulishwa kwenye mkutano huo wa kampeni.

Tukio hilo limetokea siku moja baada ya chama hicho kujikuta kikiwa na watu wachache wakati wa kuzindua kampeni zake kwenye kata ya Kaseme, tofauti na mikutano ya vyama pinzani vya Chadema na CUF.

Dalili za hali mbaya katika mkutano huo zilianza wakati viongozi hao wakiingia eneo la Nyarugusu ambalo ni maalumu kwa wachimbaji wa dhahabu. Viongozi hao walipokelewa na alama ya vidole viwili kila walikopita. Alama ya vidole viwili hutumiwa na Chadema.

Zomea zomea hizo ziliwakabili viongozi hao wa CCM wakati walipokuwa wakimnadi mgombea wao. Hali mbaya ilianza kwa katibu mwenezi na uhamasishaji, Simon Mangelepa wakati aliposimama jukwaani na kuanza kuwatambulisha wageni walioambatana nao na kufuatiwa na mbunge wa viti maalum mkoani Mwanza, Maria Hewa ambaye alizomewa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa wanapaswa kutulia.

Kutokana na hali hiyo mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina alisimama jukwaani kabla ya kumkaribisha Malecela ili amnadi mgombea wa chama hicho na kuwaeleza kuwa anazo taarifa kuwa kuna watu ambao wamepangwa hapo kwa ajili ya kuzomea, naye kuzomewa.

Baadaye ikawa zamu ya Malecela ambaye baada ya kusimama jukwaani aliwaeleza wananchi kuwa shutuma za ufisadi hazina nafasi katika kampeni kwa sasa na kuwataka wenye ushahidi wa ufisadi kuupeleka polisi, kauli ambayo iliwafanya wananchi ambao walikuwa wametulia, kuanza kuzomea wakimtaka aondoke huku wakionyesha vidole viwili.

Hata hivyo, Malecela aliwatuliza na kuwaeleza kuwa hiyo ndio njia sahihi ya kushughulikia mafisadi na kuendelea kuwaeleza wananchi kuwa iwapo wataichagua CCM katika uchaguzi huo watapatiwa umeme pamoja na kutengewa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.


Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.

Kutokana na hali hiyo Malecela aliamua kuwatuliza na kuomba Busanda isigeuke kama Tarime na kwamba wao CCM wanataka kampeni za amani na utulivu.

Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.


Hata hivyo zomea zomea hizo hazikuweza kuhatarisha amani katika mkutano huo na mgombea huyo alijieleza bila ya matatizo na kupiga magoti lakini alipoomba kura, naye akajikuta anazomewa.

Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amekiri kuwa kuna hali ngumu kwenye Jimbo la Busanda na kuwataka viongozi wa chama hicho kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha jimbo haliangukii mikononi mwa upinzani kwa kuwa machungu ya kushindwa Tarime anayajua.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamba juzi mchana wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika mkutano wa ndani kwenye ofisi za CCM wilayani Geita baada ya kuwasili kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni wa chama chake zilizofanyika juzi katika kata ya Kaseme.

Makamba alikiri kuwa hali ni ngumu na hivyo kuwaomba kila mmoja kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda, akilalamika kuwa makali ya kushindwa alishayaonja Tarime.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa chama wilayani humo zimeeleza kuwa Makamba aliamua kufanya mkutano huo kwa lengo la kuwekana sawa kutokana na CCM kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wale walioenguliwa katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Makamba amesema "jamani kushindwa ni kubaya, mwenzenu Tarime nilionja ubaya wake mpaka ilibidi nitoroshwe na Green Guard ili kuepuka kuzomewa, sasa tusiposhikamana mambo yatakuwa magumu tutoe tofauti zetu,'” alisema mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kikao hicho akimnukuu Makamba.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo Makamba alishtuka na kuhoji iwapo walikuwemo waandishi wa habari ukumbini humo na kuonya utoaji wa taarifa hizo baada ya kujibiwa hawakuwemo.

Aidha baada ya kujibiwa kuwa hakuna waandishi Makamba alishtuka baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mpiga picha wa chama na kumuagiza kuhakikisha mkanda huo anaukabidhi kwa katibu wa CCM wa mkoa.

Makamba alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa hajawahi kukiri kuwepo kwa hali ngumu kwa vile hana wasiwasi na uchaguzi huo na kusema alikuwa akieleza masuala ya kushikamana.

“Wewe unataka nikueleze mikakati yangu, kama nilikuwa nawahimiza watoto wangu kulima we unakutakia nini,” alihoji katibu huyo wa CCM alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kikao hicho.

Sambamba na hatua hiyo Makamba alimtaka mjumbe wa halmshauri kuu ya chama hicho mkoani Mwanza, Anthony Diallo kutumia uwezo wake kuhakikisha kampeni hizo zinakuwa na hamasa ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurusha taarifa zake katika vyombo vya habari.

Uchaguzi katika jimbo la uchaguzi la Busanda umepangwa kufanyika Mei 24 kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Faustine Kabuzi Rwilombe.

Vyama vingine vinavyowania kiti hicho ni Chadema, CUF na UDP.

CHANZO: Mwananchi

WANACHOHITAJI CCM NI BUSARA ZA KI-UTU UZIMA,YAANI KUKIRI PALE WALIPOKOSEA,NA KUAHIDI KUJIREKEBISHA BADALA YA KUENDELEZA AHADI HUKU ZILE WALIZOTOA MWANZO ZIMEENDELEA KUBAKI AHADI TU PASIPO KUZITEKELEZA.WAINGEREZA WANASEMA " A PROMISE MEANS NOTHING UNTIL DELIVERED."
HALAFU HIZI KAULI ZA KIBAGUZI KUWA "ICHAGUENI CCM IWALETEE HIKI AU KILE" (AS IF AWALI ILIYOCHAGULIWA ILIKUWA CHADEMA AU CUF) NI KUWAFANYA WAPIGA KURA WAJINGA AU WASAHAULIFU.KAMA WALIKUWA NA NIA YA KULETA HUO UMEME,SI WANGEFANYA HIVYO WAKATI WAPIGA KURA WALISHAWAPA HESHIMA YA KUMCHAGUA MGOMBEA WA CCM KWENYE UCHAGUZI ULIOPITA?SASA HIZI HABARI KUWA MKITUCHAGUA TENA NDIO TUTAFANYA HIKI AU KILE NI MITHILI YA KUWAHADAA WANANCHI.
I HOPE WAPIGAKURA WA BUSANDA HAWATAISHIA KUFIKISHA UJUMBE KWA CCM KWA KUZOMEA TU BALI PIA KUINYIMA KURA ILI IKIAMSHE CHAMA HICHO KUTOKA USINGIZINI KWAMBA THIS IS 2009,AND SO FAR THE ASSESSMENT OF HOW THE PARTY HAS IMPLEMENTED ITS ELECTION MANIFESTO LEAVES A LOT TO BE DESIRED.KAMA TARIME WALIWEZA,BUSANDA PIA WANAWEZA.NA KAMA WOTE WASIORIDHIKA NA MWENENDO WA CCM WATAAMUA KUWA ENOUGH IS ENOUGH,NO MORE FALSE PROMISES,THEN CHANGE IS NOT ONLY COMING BUT WILL EVENTUALLY BE ACHIEVED.
AS OBAMA SAID,YES WE CAN IF WE BELIEVE IN CHANGE.

27 Oct 2008


CCM haihusiki na OIC-Msekwa

27 Oct 2008
By Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeukana mpango wa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) na kusema kwa hilo vyombo vya habari na maaskofu wanakionea. 

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, alisema suala la kujiunga na OIC limo mikononi mwa Serikali na CCM haihusiki. 

``Mbona mnanionea jamani, kwa kweli kuniuliza juu ya jambo hili mnatuonea. Suala la kujiunga na OIC sio la CCM na wala aliyesema maneno hayo sio mimi wala kiongozi wa Chama,`` alisema. 

Pamoja na Msekwa kuukana mpango huo, lakini maamuzi makubwa yanayohusu nchi hayawezi kuamuliwa na serikali bila chama tawala kutoa baraka zake. 

Hata hivyo, Msekwa alisema hawezi kuingia kwa undani kujibu kauli iliyotolewa na maaskofu 58 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwamba watauangalia upya uhusiano wao na Serikali pamoja na Chama tawala, iwapo mipango wa kuiingiza nchi katika jumuiya hiyo pamoja na kuruhusu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi itaendelea. 

Alisema hawezi kuamini kwamba ni kweli maaskofu walitoa kauli hiyo, kwa vile katika mkutano huo yeye hakualikwa na wala hakuhudhuria. 

Alipoulizwa kwamba Serikali inaweza kuchukua uamuzi mkubwa kama huo (wa kujiunga na OIC) bila kupata baraka ya Chama tawala, Msekwa alizungumza kwa hasira huku akilalamika kwamba maswali hayo yana lengo la kumuonea. 

Hivi aliyetoa kauli ya OIC ni mtendaji wa Serikali au mtendaji wa CCM? alihoji na kuongeza: Unataka ufafanuzi juu ya uhalali au ubaya wa hicho unachouliza, tafadhali muoneni huyo huyo aliyesema, Chama hakihusiki, mbona mnaendelea kunisakama kwa jambo nisilolijua. 

Msekwa alisema anaamini Serikali ina majibu mazuri na yenye uhakika kwa vile haiwezi kufanya jambo ambalo halina maslahi. 

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Kamillius Membe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa suala la kujiunga na OIC halina madhara kwa taifa. 

Kauli hiyo iliamsha wasikwasi wa maaskofu ambao licha ya kukemea kauli ya Membe na kumtaka ajiuzulu, pia walisema kitendo hicho ni uvunjaji wa Katiba ya nchi na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa. 

Hata hivyo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilipinga kauli ya maaskofu kwa kupitia kwa Kaimu Mufti, Sheikh Suleiman Gorogosi, kuwa inalengo la kupotosha. 

Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeunga mkono mpango wa Serikali ya Muungano wa Tanzania wa kutaka kujiunga na OIC kwa kuwa itasaidia juhudi za kukuza uchumi na ustawi wa wananchi wake. 

Tamko hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alipokuwa akizungumza mjini Zanzibar baada ya kujitokeza kwa tofauti kati ya taasisi za kidini dhidi ya uamuzi wa Serikali ya Muungano. 

``Zanzibar tunaunga mkono uamuzi wa Serikali ya Muungano wa kufikiria Tanzania kujiunga na OIC kwa vile suala hilo halihusiani na mambo ya dini na litanufaisha jamii katika ustawi wa maendeleo, alisema Hamza. 

Alisema ndio maana Zanzibar imekuwa ikitetea kila mara Tanzania ijiunge na Jumuiya hiyo kwa vile misaada na mikopo inayotolewa na OIC ikiwemo miradi ya elimu na huduma za kijamii itanufaisha Watanzania wote bila ya kujali itikadi zao za imani ya dini. 

Alisema kuna mataifa mengi yaliyojiunga na Jumuiya hiyo licha ya nchi hizo kuwa na waumini wachache wa dini ya kiislamu na kuzitolea mfano nchi hizo kuwa ni Uganda na Msumbiji ambazo tayari zimeshanufaika na mfuko wa maendeleo wa OIC katika sekta za elimu, afya na viwanda. 

Akizungumiza suala laMahakama ya kadhi,, Waziri Hamza alisema wananchi waondoe hofu kwa vile mahakama hiyo si jambo geni kutokana na mfumo huo kuwepo visiwani Zanzibar bila ya kuathiri madhehebu mengine ya dini. 

Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengodo Mvungi, amesema kunahitajika meza ya mazungumzo itakayokutanisha makundi yote ya Watanzania kujadili masuala mazito yanayowakabili kama kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na la kujiunga na OIC. 

Akizunguza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mvungi alisema malumbano yaliyozuka hivi karibuni, na ambayo bado yanaendelea yanaonyesha dalili mbaya kwa mustakabali wa kitaifa. 

Alisema matatizo yaliyopo nchini, yanasababishwa na mambo mengine, lakini lililokubwa zaidi ni ile tabia ambayo imejengeka nchini kwamba hakuna anayetaka kumsikiliza mwenzake. 

``Hoja kama OIC au Mahakama ya Kadhi zinatakiwa zijadiliwe kwa lugha ya utaifa, pande zote zinazohusika zikutane, zikae pamoja na zijadiliane kwa maslahi ya kitaifa, tuache pembeni dini zetu, kabila zetu na koo zetu,`` alisema na kuongeza ``Katika mambo mazito kama yanayoendelea nchini lazima utaifa utangulizwe mbele, vinginevyo tutaishia kulumbana na kugombana lakini hatutapata jawabu la matatizo yetu, alisema. 

SOURCE:Nipashe

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.