Showing posts with label CCJ. Show all posts
Showing posts with label CCJ. Show all posts

8 Jun 2011


Mafisadi CCM wageuka mbogo

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 June 2011

SASA ni piga ni kupige ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wanakataa kujiuzulu, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema walipoitwa mbele ya viongozi wakuu wa chama hicho – makamu mwenyekiti Pius Msekwa na katibu mkuu, Wilson Mukama - wanaoitwa na CCM kuwa “watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini,” walishikilia msimamo kuwa hawawezi kujiuzulu kwa kuwa hawana hatia.

Wanaotakiwa kujiuzulu na viongozi wakuu wa CCM ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge. Mkutano wa kuwashawishi wajiuzulu, ulifanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba, Dar es Salaam.
Taarifa zinasema katika mkutano huo, Msekwa na Mukama waliomba Lowasa ajiuzulu ili kukiokoa chama hicho, lakini yeye alipinga kwa hoja kuwa hana hatia.

MwanaHALISI lilipowasiliana na Msekwa kutaka kufahamu kilichojadiliwa katika mkutano wake na viongozi hao, haraka alisema, “…Umetoa wapi habari hizo?”

Alipoelewa ni vyanzo vya ndani ya chama na serikali, Msekwa alisema, “Hayo ni mambo ya ndani ya chama. Hatuwezi kuyaleta magazetini.”
Lowassa alipoulizwa juu ya kuwapo kwa kikao hicho, alisema ni kweli wamekutana. Hata hivyo, alisema hawezi kueleza walichojadili kwenye vyombo vya habari.

Rostam hakupatikana kueleza upande wake. Hata hivyo, MwanaHALISI limeelezwa na mtoa taarifa wake kuwa mbunge huyo wa Ingunga alitoka kwenye ukumbi wa mkutano akiwa amenuna na kuvurumisha “maneno makali.”

Anasema Rostam alitoka pale akiwa amenuna na kusema yeye hana hatia yoyote na kwa hiyo hastahili kushambuliwa. Amesema yote yanayotokea sasa yanatokana na uadui wa siasa za urais wa mwaka 2005 na ule wa 2015.


Hili linatokea wakati uongozi wa juu wa chama hicho ukishindwa kukabidhi barua ya kuwataka watuhumiwa hao wajiuzulu.
Kuchelewa kwa utekelezaji wa maazimio ya kuwawajibisha Lowassa, Rostam na Chenge kumezaa majungu na umbeya. Hivi sasa taarifa zinasema, Mukama anadaiwa kugoma kuandika barua ya kuwataka watuhumiwa hao kuachia nafasi zao za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) wanazozishikilia.

Baada ya Mukama kugoma kuandika barua hizo kwa hoja kuwa kilichoamuriwa na NEC hakifahamu kwa kuwa alikuwa hajateuliwa, ndipo Nape Nnauye, katibu wa itikadi na uenezi alipoandika barua hizo na kuzipeleka kwa Msekwa.

Naye Msekwa alizipokea barua na kuzirekebisha. Akazirejesha kwa Nape ili azipeleke kwa Mukama kuzisaini. Mukama akagoma. Zikapelekwa kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye taarifa zinasema, “amezifungia kabatini.”

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao hicho, Lowassa alifika Lumumba saa nne asubuhi. Mazungumzo kati yake, Msekwa na Mukama inakadiriwa yalichukua takribani saa moja.

Katika mazungumzo hayo, Msekwa ananukuliwa akimweleza Lowassa “unatakiwa ujiuzulu nyadhifa zako za uongozi katika chama ili kutekeleza maagizo ya NEC na falsafa ya chama ya kujivua gamba.”

Akijibu hoja hiyo, mtoa taarifa anasema Lowassa alijibu, “Kuhusu Richmond (kampuni feki ya kufua umeme wa dahurula), ukweli unafahamika…Katika hili, mimi sina makosa. Rais anafahamu hilo na kila mmoja anajua hivyo.”

Anasema Lowassa alisema kama kuwajibika kwa makosa yaliyotokana na Richmond tayari amefanya hivyo kwa niaba ya chama chake na serikali pale alipoamua kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu.
Anasema mbali na kueleza hilo, Lowassa alisikika akisema, “nilikutana na Rais Kikwete. Aliyonieleza si haya.”

Alisema Rais Kikwete alimweleza kuwa hakuna maazimio yoyote ya NEC yaliyomtaka kujiuzulu. Akahoji, “Sasa nimwamini nani, ninyi mnaotaka nijiuzulu au rais aliyesema hakuna azimio kama hilo?”

Habari zinasema mara baada ya Lowassa kuwaeleza viongozi wake msimamo juu ya mazungumzo yake na Kikwete, ndipo Msekwa aliposikika akisema, “Lowassa acha mbio za urais.”

Naye Lowassa hakumkawiza Msekwa. Alijibu, “Lini nimetangaza kugombea urais? Lakini hata kama ninataka kufanya hivyo, ni haramu kugombea nafasi hiyo? Je, kuna mliowaandaa?”

Ni kauli hiyo ya Lowassa, iliyomshutua Msekwa na kusema, “Hapana. Hapana. Hakuna tuliyemuandaa…Haya mambo ya urais yatatuvuruga.”
Akihitimisha hoja zake kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, mtoa taarifa anasema Lowassa alikitaka chama chake kuisaidia serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi, badala ya kufanyia kazi kile alichoita, “majungu ya wanasiasa.”

Naye Chenge taarifa zinasema aliwaambia viongozi aliokutana nao kuwa yeye si fisadi na hafahamu maana ya ufisadi. Akataka kama tuhuma wanazomtuhumu wanaweza kuzithibitisha wamfikishe mahakamani ili aweze kujitetea. Hakuna maelezo ya ziada.

Hata hivyo, watu waliokaribu na kiongozi huyo wanasema, Chenge amejipanga kuhakisha kwamba hang’oki katika kiti chake cha NEC; ikibidi kuondolewa kwa nguvu ametishia kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.

Kwa upande wa Rostam Aziz, taarifa zinasema alitakiwa kujiuzulu ujumbe wa NEC kwa tuhuma za kuingiza nchini kampuni feki ya Richmond na baadaye Dowans.

Mtoa taarifa anasema, mara baada ya kuelezwa tuhuma hizo, Rostam alihoji, “Haya ni maamuzi ya NEC?” Naye Msekwa akajibu, “NEC imetaka chama kijivue gamba kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kwa kuondoa watu wote wanaotuhumiwa ufisadi.”

Habari zinasema, katika mazungumzo kati ya viongozi hao na Rostam, hakuna mahali popote ambapo Msekwa na Mukama walitaja ushiriki wa mbunge huyo wa Igunga, katika wizi wa fedha za umma kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kampuni ya Kagoda ni miongoni mwa makampuni 22 yaliyothibitika kuchota mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Gazeti hili limeshindwa kufahamu mara moja kilichosababisha Msekwa na wenzake kushindwa kumweleza Rostam ushiriki wake katika Kagoda. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka minne sasa, CCM imekuwa ikituhumiwa kunufaika na fedha za EPA hasa Sh. 40 bilioni zilizoibwa na Kagoda.

Wakati suala hilo likichukua sura hiyo, taarifa zilizofikia gazeti hili zinasema baadhi ya vigogo wa chama hicho wamepanga kupeleka hoja katika vikao vijavyo vya (CC) na (NEC) kushinikiza kufukuzwa ndani ya chama hicho wanaoitwa, “wasaliti ndani ya chama.”

Wanaopangiwa mkakati wa kufukuzwa ni spika wa zamani wa Bunge, Samwel Sitta na mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe wanaotuhumiwa kuanzisha Chama cha Jamii (CCJ) wakati wakiwa bado wanachama na viongozi wa CCM.

Wengine ni Nape Nnauye, Victor Mwambalaswa na Daniel Porokwa.
Habari kutoka ndani ya CCM zinawanukuu makada mawili; rais mstaafu, na mjumbe mmoja wa NEC wakitaka chama chao kuwafukuza waasisi wa CCJ kwa kukosa uaminifu.

MwanaHALISI limeelezwa na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CCJ, Dickson Ng’hily kwamba Sitta na Mwakyembe waliokuwa waanzilishi wa chama hicho, walimkatiza masomo yake nchini Afrika Kusini ili kusaidia kupatikana usajili wa chama hicho.

Ng’hily ambaye mahojiano yake yatachapishwa kikamilifu katika toleo lijalo amesema, aliyemwingiza yeye CCJ ni Sitta na Dk. Mwakyembe na anasikitishwa na hatua ya viongozi hao kutaka kuficha ukweli.

“Hawa watu ndio waanzilishi hasa wa CCJ. Mimi na Makonda tulipewa jukumu la kutafuta usajili wa chama. Lakini naona wenzangu wameamua kuficha ukweli kwa maslahi binafsi. Hii si sahihi,” ameeleza.

Ng’hily anaonyesha nyaraka za muhtasari wa vikao walivyoshiriki viongozi wakuu wa CHADEMA, John Mnyika, Anthony Komu na Tundu Lissu kuwa ni miongoni mwa watu walioshiriki katika majadiliano ya kuunganisha nguvu kati ya CCJ ya Sitta na CHADEMA.

“Tulikubaliana kama CCJ itakosa usajili, basi mheshimiwa Sitta atagombvea urais kupitia CHADEMA. Lakini kama tutafanikiwa kusajili chama chetu, basi Sitta angegombea urais kupitia CCJ na CHADEMA wangetuunga mkono,” anaeleza Ng’hily.

Kuibuka kwa Ng’hily kuelezea ushiriki wa Sitta na Dk. Mwakyembe katika kuanzisha na kusimamia usajili wa CCJ kumekuja wiki tatu baada ya Fred Mpendazoe kumtaja Nape Nnauye kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa kwanza wa CCJ.

Mpendazoe aliuambia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Njombe kuwa yeye, Sitta na Mwakyembe ndio walianzisha CCJ; bali yeye alitangulia kutoka CCM ili kurahisisha usajili wa chama hicho. Wenzake walikuwa wamfuate baadaye.

CHANZO: Mwanahalisi

31 Mar 2010


Mwaka 1996 nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza pale Mlimani nilipata 'somo' moja muhimu kuhusu wanasiasa wa Tanzania.Ilikuwa ni kwenye mhadhara (lecture) ya Dr (Profesa kwa sasa) Max Mmuya katika somo Siasa na Serikali Tanzania na Nchi Nyingine za Afrika Mashariki (PS 102),ambapo mhadhiri huyo alitupatia wasifu wa wagombea urais wanne walioshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.Pasipo kuingia sana kiundani,wagombea hao wote walikuwa 'wawakilishi wa tabaka tawala'.Hakuna mmoja kati yao ambaye tungeweza kumtambua kama 'mlalahoi'.Ni katika minajili hiyo ndipo makala hii inajaribu kuangalia kama ujio wa CCJ utakuwa na lolote jipya kwa 'mlalahoi' (mtu wa kawaida mtaani)Binafsi,tafsiri yangu ya kwanza ya ujio wa CCJ katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu hauna tofauti sana na wanasiasa wanaobadili vyama pindi wakiona hawana nafasi ya kupitishwa na vyama vyao kugombea nafasi flani au wale ambao hawakupitishwa na vyama hivyo.Japo hiyo ni haki yao ya kikatiba,jamii inapaswa kuwaangalia wanasiasa hao kwa jicho la shaka pia.Je wanafanya hivyo kwa minajili ya kupata fursa ya kuutumikia umma au ni maslahi binafsi?Historia inaweza kutusaidia katika kupata jibu la swali hili.Mara nyingi tumesikia wanasiasa wakipita huku na kule wakijaribu kutuaminisha kuwa bila wao hatuwezi kupata maendeleo.Cha kuchekesha ni kwamba baadhi ya wanaotueleza hivyo,wamekuwa madarakani miaka nenda miaka rudi na badala ya kusonga mbele maendeleo yetu yanazidi kudorora.

Ni vigumu kuamini kuwa CCJ italeta mabadiliko yoyote ya maana kwa vile kimsingi chama hicho hakina tofauti na CCM,Chadema,CUF au chama kingine cha siasa.Labda tofauti kubwa ni kuwa CCJ si chama tawala,lakini kama ni hilo basi hata Chadema au NCCR Mageuzi navyo si vyama tawala.Labda tofauti nyingine ni upya wake.Lakini historia pia inatuusia kuwa si kila kipya ni kinyemi.Upya wa chama si jambo la muhimu kwa wananchi bali ufanisi wake katika kuwatumikia.Je katika mazingira tuliyonayo,CCJ inaweza kweli kuwa mkombozi wa Watanzania?Jibu linaweza kupatikana kutoka kwa waasisi wa CCJ na sie wananchi wenyewe.Kwa viongozi wa chama hicho,so far hawajatuthibitishia kuwa ujio wa chama chao utaleta lolote jipya zaidi ya maneno mataaaamu just like ilivyo kwenye miongozo mbalimbali ya CCM.Kama nilivyowahi kuandika mara kadhaa,tatizo la Tanzania (na pengine Afrika kwa ujumla) halijawahi kuwa katika kuunda mawazo au mipango mizuri.Siku zote kikwazo chetu ni usimamizi na utekelezaji wa mawazo/mipango hiyo.

Ni katika minajili hiyo ndipo wananchi wanapaswa kuhoji kama CCJ sio CCM kwenye jezi nyingine.Yani mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya.Na kibaya zaidi,kwa kuzingati tukio la jana ambapo mmoja wa wabunge wa CCM Fred Mpendazoe ametangaza kujiunga na CCJ,chama hicho kipya kina kila dalili ya kuwa CCM-B.Hilo halina ubaya iwapo wanaotoka CCM na kujiunga na CCJ watakuwa wanasiasa wenye uchungu wa dhati kwa nchi yetu na wenye nia ya kuutumikia umma kwa uadilifu.Lakini miaka arobaini na ushee ya uhuru wetu imeshatupa darasa zuri kuhusu wanasiasa wetu.Wengi wao wametawaliwa na ubinafsi huku wakiamini kuwa ni wao pekee ndio wenye ujuzi,nguvu,mamlaka na haki ya kutuongoza.Kibaya zaidi,kwa kiasi kikubwa wengi wao wamechangia mno kutufikisha hapa tulipo:hohehahe wa kutupwa huku raslimali za nchi yetu zikiibiwa kana kwamba hazina mwenyewe.

Pengine siitendei haki CCJ kwa kuiona kama shati chakavu lililopigwa pasi na kunyunyiziwa uturi.Lakini nina kila sababu ya kuhofia ujio wake.Japo natambua kuwa katika siasa timing is everything,lakini kwa muda huu mchache uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu,yayumkinika kuamini kuwa chama hicho kitakuwa washiriki tu badala ya kuwa serious contenders.Hilo si baya sana iwapo matokeo mabaya kwenye uchaguzi ujao hayatopelekea hadithi kama za NCCR Mageuzi mwaka 1995.Tatizo la vyama vinavyofikiria uongozi tu badala ya utumishi kwa umma ni kwamba vikishindwa uchaguzi basi ndio inakuwa mwisho wa safari.Yani vinakuwa kama mapenzi ya pesa,ukiwa nazo utaonekana mfalme,'ukifulia' unabwagwa.

Nimalizie kwa hitimisho lisilopendeza kwa wale wanaotaka kuiona CCM ikidondoka kwenye uchaguzi mkuu ujao.Kinyume na fikra zinazoelekea kupata umaarufu kuwa ujio wa CCJ ni kilio kwa CCM,ukweli ni kwamba chama hicho kimekuja kugawa kura za wapinzani.Hilo linaweza tu kuepukika iwapo CCJ itaamua kushirikiana na chama kingine/vingine kwenye uchaguzi mkuu ujao.Lakini kinachokwaza ushirikiano wa vyama vyetu vya upinzani sio kutofautiana kwa sera zao bali ubinafsi.Wapinzani wataendelea kuwa wapinzani kwa muda mrefu huku CCM 'ikipeta' licha ya kulea ufisadi na kuipeleka nchi kusikoeleweka.Kwa wapiga kura,CCM inabaki kuwa the devil they know.Ni uamuzi mbovu lakini at the end of the day unaendelea kuiweka CM madarakani.

Na nisisahau.CCJ ina kazi ya ziada ya kukabiliana na 'nguvu za giza' zinazotumia pesa za walipa kodi kuhakikisha CCM inatawala milele.Na si ajabu miongoni mwa wanaopigia debe CCJ,au watakaojiunga hivi karibuni, ni wawakilishi wa nguvu hizo za giza.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.