29 Mar 2009
26 Mar 2009
- 26.3.09
- Evarist Chahali
- BUNGE, HAKI NA USAWA
- 1 comment
Bunge mradi wa ulaji
na Mwandishi Wetu
WAKATI baadhi ya wabunge wakiendelea kulumbana kupitia katika vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maslahi ya taifa,imebainikawamekuwa wakichuma mamilioni ya fedha kupitia katika malipo yao halali ya mishahara, posho na fedha nyingine zisizotokana na malipo yao rasmi wanayostahili.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umethibitisha pasipo shaka kwamba, fedha ambazo wabunge wamekuwa wakichuma kwa njia mbalimbali kwa kutumia nafasi zao za uwakilishi, zinaweza zikawa sababu mojawapo muhimu ya kuibuka kwa makundi yanayosigana ndani ya Bunge na hususan miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, gazeti hili limefikia hatua ya kutilia shaka kwamba, mzozo wa hivi karibuni, kati ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na mwenzake wa Igunga, Rostam Aziz, kwa kiwango kikubwa unakuzwa kutokana na sababu za maslahi binafsi zaidi kuliko madai ya uzalendo na maslahi ya taifa.
Shaka hiyo ya Tanzania Daima Jumatano inatokana na ukweli kwamba, wabunge hao wawili ambao wote wawili ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa namna moja au nyingine wamepata kuwa au wanayo maslahi ya wazi na ya moja kwa moja katika sekta ya nishati.
Kauli ya hivi karibuni ya mmiliki wa Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, Mohammed Al Adawi, kukiri kwamba aliwekeza katika sekta ya nishati kwa ushawishi wa Rostam sambamba na ile ya kubainisha kuwa kampuni ya mbunge huyo ilipata kuingia katika zabuni ya kutaka kufanya kazi za ujenzi katika mradi wa kuzalisha umeme wa dharura, ni ushahidi wa wazi wa namna mwanasiasa huyo alivyo na maslahi ya moja kwa moja katika sekta ya nishati.
Kama ilivyo kwa Rostam, taarifa za hivi karibuni, zilizothibitishwa na Mwakyembe mwenyewe
kuwa ni mmoja wa wakurugenzi waanzilishi wa Kampuni ya Power Pool East Africa Ltd yenye malengo ya kuzalisha umeme wa upepo kutoka mkoani Singida, ni ushahidi kwamba naye anayo maslahi ya moja kwa moja katika sekta ya nishati.
Kuingia kwa Rostam na Mwakyembe katika sekta ya nishati, kwa kiwango kikubwa kunaonyesha namna wabunge, hususan wale wa CCM walivyojizatiti kutumia fursa zao za kisiasa kujinufaisha kiuchumi, nyuma ya kivuli cha uwekezaji
kupitia sheria ya soko huria.
Kama hiyo haitoshi, mzizi wa fitina kuhusu ukweli kwamba Bunge limekuwa likitumiwa kama kiota cha wanasiasa kuvuna mamilioni, zilithibitishwa mkoani Kilimanjaro juzi na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilibrod Slaa ambaye alisema mshahara anaolipwa mbunge kwa mwezi unafikia sh. milioni saba, hiyo ikiwa mbali na posho nyingine.
Dk. Slaa alitaja kiwango hicho cha mshahara wake wakati akihutubia wakazi wa mji mdogo wa Hedaru, wilayani Same katika mfululizo wa mikutano ya Operesheni Sangara inayoendeshwa na CHADEMA.
Wakati Dk. Slaa akibainisha ukweli huo, uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano umebaini pia kuwa wabunge wanaweza kujikusanyia mamilioni ya shilingi kwa kuhudhuria vikao mbalimbali vya kamati za kudumu za Bunge, semina na safari za ndani na nje ya nchi.
“Ndugu zangu, afadhali msijue mshahara anaolipwa Dk. Slaa kama mbunge, mkijua nalipwa shilingi ngapi mnaweza hata kunipiga mawe,” alisema Dk. Slaa wakati akihutubia mkutano huo na kuitikiwa na sauti za wananchi wakimtaka ataje mshahara wake.
“Mnataka kuujua mshahara wangu, ninalipwa sh milioni saba kwa mwezi. Haki iko wapi? Mimi nalipwa milioni saba, na posho yangu kwa siku ni sh 135,000. Haya ni malipo makubwa mno, fedha ninayopata kwa siku inaweza kuzidi hata mshahara wa mwezi mzima wa polisi. Muulizeni yule polisi pale analipwa shilingi ngapi msikie.
“Juzi nimetaja posho za wabunge na kusema zipunguzwe, lakini Spika wa Bunge analalamika eti naingilia haki na madaraka ya Bunge, sasa leo nasema ninalipwa jumla ya shilingi milioni saba kwa mwezi, acha posho za bungeni. Kweli hii ni haki?” alisema Dk. Slaa.
Alisema kuwa akiwa raia huru, ana haki ya kutaja kwa hiari yake kiwango cha mshahara wake, hasa pale anapoona kuwa kulipwa kiwango hicho ni kutowatendea haki mamilioni ya Watanzania maskini wanaolipa kodi zao wakitegemea serikali iwakomboe kutoka kwenye lindi la umaskini.
Dk. Slaa alisema wabunge wengi wa CCM akiwamo Spika wa Bunge, Samuel Sitta, hawawezi kuunga mkono hoja hiyo kwa vile wapo bungeni kwa ajili ya kutafuta maslahi yao binafsi.
“Wafanyakazi wengi na Watanzania wanateseka kwa mishahara midogo na maisha duni, mamilioni haya ya fedha kwenda mifukoni mwa watu ni aibu kwa nchi na CHADEMA tunasema hapana, fedha hizi ziende katika masuala ya kusaidia jamii na kuongeza mishahara ya walimu, polisi, mahakimu na watendaji wengine,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wakazi wa Hedaru waliohudhuria mkutano huo.
Alirejea kauli yake ambayo amekwishakaririwa akiitoa mara kadhaa kuwa Spika Sitta, anapaswa kujiuzulu nyadhifa alizonazo katika CCM, ili awe huru kuliongoza Bunge kwa maslahi ya Watanzania badala ya kushinikizwa na maslahi ya chama chake.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, kushangazwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuendelea kuwateua wabunge wa CCM kuwa wajumbe katika bodi za mashirika ya umma.
Akizungumza wiki iliyopita katika mkutano uliondaliwa na Jukwaa la Wahariri, Prof. Lipumba alisema, hatua hiyo ya Rais Kikwete mbali na kuwahalalishia wabunge ulaji, inazoretesha utendaji wao katika kuyasimamia ipasavyo mashirika hayo ambayo utendaji wake wa kazi unapaswa kusimamiwa na taasisi hiyo muhimu ya dola.
Wakati hali ikiwa hivyo katika mishahara ya wabunge, Tanzania Daima Jumatano limebaini kuwa wabunge wamekuwa wakilipwa mamilioni ya fedha wakati wanapokutana na baadhi ya taasisi za umma ambazo kamati za Bunge zinazisimamia shughuli zake.
Taarifa za hivi karibuni ambazo gazeti hili limezipata zinaonyesha kuwa, Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) lilitumia jumla ya sh milioni 16 kwa ajili ya kulipa posho na usafiri wabunge kutoka majimboni mwao, pamoja na makatibu wawili waliohudhuria kikao cha dharura kilichowakutanisha Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Kamati ya Bunge ya Kamati ya Nishati na Tanesco.
Taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Bunge, zinaeleza kuwa licha shirika hilo kuwa na hali mbaya kifedha, lililazimika kuingia gharama hizo baada ya ofisi ya Bunge kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kuwagharamia wabunge hao kwa sababu Bunge halikuwa na fedha katika kikao chake cha Desemba mwaka jana.
Katika hali ya kushangaza, habari za wanakamati hao wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kulipwa posho na gharama zao nyingine na Tanesco wakati wakihudhuria kikao hicho zimewafanya wabunge, Katibu wa Bunge na Spika kutofautiana.
Spika Sitta, jana alilithibitishia Tanzania Daima Jumatano kuwa, wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini walilipwa posho na gharama za usafiri kwa sababu Bunge halikuwa na fedha wakati Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja alipotaka kukutana na kamati hiyo ili kupata ushauri.
“Lolote linaweza kutokea kutegemea na nani amewaita, kama wameitwa kusaidia jambo ambalo halimo kwenye utaratibu wa Bunge wanalipwa na aliyewaita. Na katika hili ilikuwa hivyo, ninalifahamu vizuri sana, waziri aliomba kukutana na kamati wakati muda wa Bunge ukiwa umepita, Katibu wa Bunge alimuandikia akimueleza kuwa Bunge halina fedha ila kama wizara yake inaweza, basi ilipe posho na gharama za wabunge hao kusafiri hadi Dar ili aweze kukutana
nao.
“Hivyo ndivyo ilivyokuwa, sasa mimi sijui kama ililipa wizara, Tanesco au nani, la msingi hawakulipwa na Bunge, na kama wabunge ambao ni wanakamati wanakanusha hili, ni watu wa ajabu kwa sababu sijui wanaogopa nini kueleza ukweli,” alisema Spika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo (CCM), alipozungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani, alikana kupokea senti tano kutoka Tanesco wakati wakihudhuria kikao hicho na kueleza kuwa, kamati yake iliitwa na Spika na malipo yalifanywa na Bunge.
“Hatukumuomba mtu hela, sielewi lolote, sisi tuliitwa na Spika na malipo yetu yalishughulikiwa na Bunge,” alisema Shellukindo na kusisitiza kuwa, kanuni za Bunge zinaeleza wazi kuwa wabunge wanapokuwa katika vikao vilivyo na baraka za Spika, iwe bungeni au nje ya Bunge, posho na gharama zao nyingine zinalipwa na Bunge na si taasisi nyingine yoyote.
Alipoulizwa kuhusu hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja alieleza kuwa Tanesco ililazimika kulipa gharama hizo kwa wabunge licha ya kikao hicho kufanyika kwa ridhaa ya Spika, baada ya Bunge kueleza kuwa halikuwa na fedha kwa ajili ya kulipa posho na gharama za usafiri kwa wabunge.
Wakati wanasiasa hao wakivutana kuhusu mfumo huo wa ulipaji posho, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipotafutwa na Tanzania Daima Jumatano
ili kutoa ufafanuzi wa jambo hilo, alieleza kuwa wabunge wote wanapokuwa katika shughuli za Bunge, ikiwamo vikao vya kamati za kudumu za Bunge, posho na gharama zao nyingine zinalipwa na ofisi ya Bunge, na si vinginevyo.
Alisisitiza kuwa, Tanesco haiwezi kuliwalipa posho wabunge wakiwa katika kikao cha kamati ya kudumu ya bunge na kuongeza kuwa katika utumishi wake ndani ya taasisi hiyo, hajawahi kuona fedha za Tanesco zikitolewa kwa ajili ya kulipa posho wa wabunge.
MHESHIMIWA SPIKA ANASEMA WABUNGE WA KAMATI HUSIKA WALILIPWA NA TANESCO.WAZIRI NGELEJA NAE ANATHIBITISHA HILO.MBUNGE SHULIKINDO ANAKATAA TAARIFA KUWA WALILIPWA JAPO SENTI TANO,NA KATIBU WA BUNGE ANAWEKA BAYANA TARATIBU ZA MALIPO KWA WANAKAMATI ZA BUNGE.