Na Waandishi Wetu
ZAIDI ya wafanyakazi 5,000 nchini wanaochukua mishahara yao kupitia Benki ya National Microfinance Bank (NMB) watalazimika kutolipwa wiki hii kutokana na mgomo wa nchi nzima wa wafanyakazi wa benki hiyo ulioanza jana.
Wafanyakazi hao waligoma wakiishinikiza Serikali kuwalipa mafao na kupewa asilimia tano ya hisa zilizotengwa kwa ajili yao wakati Serikali ilipoamua kuuza hisa zake.
Mgomo huo umekuja baada ya Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), kutoa notisi ya saa 48, Septemba 19 mwaka huu ikieleza kusudio la kugoma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu mgomo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Bw. Ben Christiaanse, alisema hatua iliyochukuliwa na wafanyakazi hao katika matawi 121 nchini, ni kubwa kuliko tatizo lililopo.
Aliulaumu uongozi wa TUICO kwa kile alichodai mbali ya kusababisha matatizo mengine, umekiuka amri ya mahakama kwa kuwa suala la wafanyakazi hao bado lilikuwa linashughulikiwa na kusisitiza, kwamba mgomo huo umesababisha matatizo makubwa kwa mamilioni ya Watanzania.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwanasheria wa NMB, Bw. Rosan Mbwambo, alisema jana asubuhi benki hiyo iliwasilisha ombi rasmi mahakamani la kukiukwa amri hiyo iliyotolewa Januari 21 mwaka huu na kutaka wahusika kuchukuliwa hatua za kijinai.
Alisema baada ya kuwasilisha ombi hilo, mahakama hiyo iliagiza pande mbili, Benki na Chama cha Wafanyakazi, kufika mahakamani leo asubuhi.
Aliwataja viongozi wa TUICO wanaotakiwa mahakamani leo kuwa ni Katibu Mkuu wa TUICO, Bw. Boniface Nkakatisi, naibu wake Alquine Senga, Mwenyekiti wa NMB TUICO Tawi na Kamati ya Majadiliano, Bw. Joseph Misana na Katibu wa Tawi la NMB, Bw. Abdallah Kinenekejo.
Kutoka Tanga, Benedict Kaguo anaripoti kuwa wateja wa Benki ya NMB waliulalamikia uongozi wa benki hiyo kwa kushindwa kusikiliza madai ya watumishi wao hadi kusababisha mgomo mkubwa ulioleta adha kubwa.
Wakizungumza kwa jazba nje ya ofisi za benki hiyo tawi la Madaraka jana baada ya kukuta tangazo lililowaomba radhi wateja kuwa hakutakuwa na huduma, wateja hao walidai jambo hilo limetokana na kupuuzwa hoja za wafanyakazi hao.
Walieleza kutofurahishwa na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Bw. Christiaanse kung’ang’ania kuwa mgomo huo ni batili bila kueleza chochote ama ni hatua gani amechukua kutekeleza madai ya wafanyakazi wake.
“Sisi tunamshangaa huyu Mkurugenzi wa NMB, anaacha kueleza ni nini atawafanyia wafanyakazi hawa ili wasigome, yeye anang’ang’ania kuwa mgomo ni batili haya ni mambo ya ajabu sana,” alisema Mwalimu Deo Temba.
Alieleza kuwa NMB ni benki kongwe nchini, hivyo kitendo cha kutowajali watumishi wake kinaifedhesha benki hiyo ndani ya jamii.
Kutoka Shinyanga, Suleiman Abeid anaripoti kuwa mgomo ulichukua sura mpya baada ya wafanyakazi benki hiyo kutishia kuwashawishi na kuwaomba wafanyakazi wa sekta nyingine nao wagome kuishinikiza Serikali ikubali kutekeleza madai yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini humo jana, wafanyakazi hao wakiongozwa na viongozi wao wa chama chao, ngazi ya tawi na mkoa, walisema watafanya chini juu kuwaomba wafanyakazi wenzao wawaunge mkono, ili Serikali ishughulikie haraka madai yao.
“Iwapo madai yetu hayatapatiwa ufumbuzi mapema, sisi tutaendelea na mgomo wetu na ni wazi wafanyakazi wenzetu hawataweza kulipwa mishahara yao na hata baadhi ya wafanyabiashara watapata shida, tutawaomba nao wagome katika maeneo yao,” alieleza Bw. Emmanuel Samara Katibu TUCTA mkoani hapa.
Naye Katibu wa TUICO Shinyanga, Bw. Gabriel Melchior, alisema wafanyakazi wa NMB hawajagoma bali wanaendeleza mgomo ulioanzishwa na Serikali na mwajiri wao.
Naye Francis Godwin kutoka Iringa anaripoti kuwa mgomo wa wafanyakazi NMB ulikabiliwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) baada ya kutanda benki hiyo huku wateja wakiwa wamepanga foleni tangu asubuhi wakisubiri kuchukua fedha zao katika ATM.
Kutokana mgomo huo baadhi ya wananchi walimtaka Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo, kuchukua hatua ya kujiuzulu haraka kwa kushindwa kumudu nafasi hiyo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wateja hao wengi wao wakiwa ni walimu na watumishi wa Serikali wakisubiri milango ya benki hiyo ifunguliwe, kutokana na kutokuwapo tangazo lolote lililoonesha kuwapo mgomo katika benki hizo. Matangazo hayo yalibandikwa saa 5 asubuhi.
Kutoka Mwanza Jovin Mihambi anaripoti kuwa wafanyakazi katika matawi mawili ya NMB jijini humo walisema wataendelea na mgomo licha ya Menejimenti na Serikali kupuuza mwito wa kuwataka kukutana nao kutatua matatizo yao.
Wakizungumza na Majira katika ukumbi wa DVN maeneo ya Posta jijini hapa, walisema awali walikubaliana na uongozi wa benki hiyo kupitia kwa Meneja wake, Bw. Methusela Israel, kuwa wangekutana kujua hatma ya nyongeza ya mishahara yao ambayo walisema kuwa ni asilimia tano.
Katibu wa TUICO Mkoa wa Mwanza, Bw. Renatus Chimola, ambaye aliungana na wafanyakazi wa benki hiyo, alisema kama menejimenti na viongozi wa Serikali hawatatokea katika kikao hicho, mgomo huo utaendelea hadi leo mpaka uongozi huo utakapokutana nao na kujadili matakwa yao.
Alisema wananchi ambao ni wateja katika matawi hayo watapata usumbufu, yeye na wafanyakazi hao, hawatajali usumbufu huo kwa madai kuwa wanachodai ni maslahi yao ambayo yatawawezesha kutenda kazi yao kwa ufanisi zaidi kama benki zingine nchini |