Showing posts with label JOHN MNYIKA. Show all posts
Showing posts with label JOHN MNYIKA. Show all posts

10 Mar 2012


FRIDAY, MARCH 9, 2012

Mamlaka ya Urais yawezeshe uwajibikaji kumaliza mgogoro wa Serikali na Madaktari


Jana tarehe 8 Machi 2012 asubuhi nilitoa tamko kwa niaba ya CHADEMA la kutaka kauli ya haraka ya Rais Jakaya Kikwete ya kutengua uteuzi wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hadji Mponda na Naibu Waziri wa wizara husika Dk. Lucy Nkya kutokana na udhaifu wao mkubwa wa kiongozi waliouonyesha katika kushughulikia mgogoro wa madaktari ambao umedumu kwa muda wa takribani miezi miwili. 

Nilieleza kusitikitishwa na ukweli kwamba Rais Kikwete toka mgogoro utokee hajatumia ipasavyo mamlaka yake ya kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 34 na 35 na tarehe 5 Februari 2012 aliahidi kwamba atazungumzia kwa kina suala la mgomo wa madaktari lakini badala yake akalizungumza kwa ufupi tarehe 29 Februari 2012 katika hotuba yake kwa taifa bila kuchukua hatua za msingi hali inayoashiria ombwe la uongozi. 

Nilieleza kuwa iwapo Rais Kikwete haitatoa kauli viongozi wakuu wa CHADEMA wataeleza hatua za ziada ambazo chama kitachukua kuiwajibisha serikali. Jioni Serikali ilieleza kuwa leo Rais angezungumza na wazee wa Dar es salaam, na leo imetolewa taarifa kuwa atazungumza nao kesho.

Jana usiku na leo asubuhi masuala kadhaa yameendelea kuhusu mgogoro huu, mosi; hukumu ya mahakama ya kazi, pili; uamuzi wa serikali na wadau wake kufanya propaganda dhidi ya madaktari tatu; uamuzi wa serikali kufanya mawasiliano na uongozi wa madaktari.

Mkakati wa kufanya propaganda hautaisaidia Serikali badala yake iwekeze katika mawasiliano na uongozi wa madaktari kabla ya Rais kuzungumza ili Rais atoe kauli baada ya kuchukua hatua za msingi ikiwemo za kuwezesha uwajibikaji wa viongozi waliotajwa na pia kuanza kushughulikia madai ya madaktari na yale yanayohitaji kuingizwa kwenye bajeti kuwe na makubaliano ya utekelezaji. 

Izingatiwe kwamba matatizo ya Wizara ya Afya pamoja na udhaifu wa kiutendaji yalichangiwa pia na ufinyu wa bajeti, na bajeti husika iliandaliwa na serikali na kupitia kwenye baraza la mawaziri ambalo Rais ni mwenyekiti wake kabla ya kuletwa bungeni na wengine tuliipinga tukitaka fedha zitoke kwenye matumizi mengine ya anasa na kuelekezwa kwenye huduma muhimu za kijamii. 

Pia; kutokana na matatizo katika serikali kwenye wizara mbalimbali yenye madhara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika taifa tunasisitiza umuhimu wa Rais Kikwete kulivunja baraza la mawaziri ili kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kuongeza uwajibikaji kama ilivyoazimiwa pia na kamati kuu ya CHADEMA katika mkutano wake wa tarehe 3 na 4 Machi 2012.

Tarehe 7 na 8 Machi 2012 Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa mara nyingine tena alitoa taarifa kinyume na kauli za awali za tarehe 9 Februari 2012 ambazo badala ya kushughulikia vyanzo vya mgogoro vimeendeleza mgogoro na kusababisha mgomo mwingine wa madaktari wenye athari kubwa kwa wananchi.

Ndio maana nikatoa kauli ya kumtaka Waziri Mkuu kuweka wazi kwa umma taarifa ya uchunguzi uliofanywa na serikali kuhusu tuhuma dhidi ya viongozi wakuu na watendaji waandamizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, na kushughulikia madai ya msingi ya madaktari. 

Aidha, pamoja na kuunganisha nguvu za pamoja kuhakikisha mgomo unakwisha ili kuepusha athari zaidi kwa umma, ni muhimu hatimaye tathmini huru ikafanyika kuhusu matokeo ya mgogoro na mgomo toka ulipoanza mpaka sasa ikiwemo kueleza wazi idadi ya vifo vilivyotokea na madhara yaliyojitokeza katika hospitali za umma tofauti na kauli potofu iliyotolewa bungeni tarehe 3 Februari 2012 na Waziri husika.

Rais Kikwete alipaswa kabisa kuchukua hatua kuiongoza serikali kufanya maamuzi ya msingi mara baada ya matokeo ya kikao kati ya ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wanataaluma wa kada ya afya sanjari na mkutano kati ya madaktari na wawakilishi wa kada nyingine za sekta ya afya katika utumishi wa umma vilivyofanyika tarehe 9 Februari 2012; kwa kuzingatia pia ushauri tuliotoa tarehe 10 Februari 2012.

Kwa upande mwingine, jana nilirudia kutoa mwito tuliotoa tarehe 30 Januari 2012 kwa TUGHE, MAT na kamati ya muda ya madaktari kuendelea kutoa ushirikiano unaostahili kwa chama, kambi rasmi ya upinzani na wadau wengine ili kuweza kuunganisha nguvu ya pamoja katika kushughulikia madai ya msingi ya madaktari yenye kuathiri sekta ya afya nchini na maisha ya wananchi kwa ujumla. 

Naendelea kuwashukuru wanaharakati kwa kuunganisha nguvu katika kutaka uwajibikaji wa viongozi wa serikali katika kushughulikia mgogoro na madaktari na kinaitaka Serikali kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari na makundi mengine katika jamii yanapotumia uhuru wa kikatiba kwa kukusanyika, kujadiliana na kuhoji kuhusu uwajibikaji wa serikali na viongozi wake kwa kuzingatia ibara za 8, 18 na 20 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete anapaswa baada ya mawasiliano yanayoendelea kutoa hotuba yenye kuleta matumaini badala ya kurudia tena maelezo yasiyoridhika kama yale yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda tarehe 9 Februari 2012 na 7 na 8 Machi 2012 kuhusu namna ambavyo imeshughulikia mgogoro huu na madai ya madaktari, watumishi wengine wa umma katika sekta ya afya nchini pamoja na uboreshaji wa huduma katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini.

Narudia kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono madai ya msingi ya madaktari ili kuhakikisha kwamba hospitali za umma nchini zinakuwa mahali salama kwenye huduma bora za kulinda maisha ya wananchi hususan wasio na uwezo wa kudumu gharama za matibabu katika hospitali binafsi za ndani na nje ya nchi. 

Pamoja na madai ya maslahi ya madaktari ambayo ni kwa maslahi ya umma, madaktari wanataka pia serikali ichukue hatua za kuboresha huduma za afya. Serikali inaingia gharama kubwa kupeleka baadhi ya watanzania wengi wao wakiwa viongozi kwenda kutibiwa nje ya nchi huduma katika hospitali za umma zinazidi kuzorota kutokana na ukosefu wa madawa, vifaa tiba na wataalamu wa kutosha katika hospitali za umma. 

Aidha, serikali inashindwa kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kisingizio cha kutokuwa na uwezo wakati ambapo inafanya matumizi mengine ya anasa kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru. Serikali inachelewa kushughulikia madai ya posho za madaktari kama nyongeza ya posho ya kulala kazini (on call allowance) na posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (risk allowance) wakati huo huo serikali hiyo hiyo inazungumzia nyongeza ya fedha katika matumizi mengine ya serikali yasiyokuwa ya lazima. Serikali ishughulikie vyanzo vya migogoro ya kijamii badala ya matokeo.

MTEMBELEE MHESHIMIWA MNYIKA KATIKA BLOGU YAKE INAYOPATIKANA http://mnyika.blogspoti.com.PIA UNAWEZA KUMFUATA TWITTER www.twitter.com/jjmnyika NA UKURASA WAKE WA FACEBOOK NI http://www.facebook.com/pages/John-Mnyika/113913842009362

1 Mar 2012


Maelezo yafuatayo ni ya Mheshimiwa John Mnyika,Mbunge wa Ubungo wa tiketi ya Chadema.Nayawasilisha kama yalivyo:

Hatua nilizochukua kuhusu barabara ya Kibangu-Makoka na fidia ya Riverside

Nilichukua hatua kuhusu barabara Kibangu-Makoka na Januari nilikwenda Makuburi kuchangia matengenezo ya barabara husika , leo nimemweleza diwani kazi iharakishwe na kuhusu fidia ya wananchi wa Riverside Manispaa imenihakikishia kuwa italipwa mwezi Machi 2012; kesho nitakuwepo tena Makuburi kwa ajili ya kufuatilia masuala ya maji.


Kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Kama sehemu ya wajibu huo nilitumiwa SMS na baadhi ya wananchi wa Kibangu na Makoka katika kata ya Makuburi kuhusu ubovu wa barabara ulioongezeka mara baada ya mafuriko ya mkoa wa Dar es salaam. Pamoja na kuwa barabara hii ni ya ngazi ya mitaa kwa maana ya halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, nilichukua hatua ya kuunganisha nguvu pamoja na diwani na wananchi kwa ujumla.

Izingatiwe kwamba kuhusu barabara hii nilitimiza wajibu wa uwakilishi baada ya kukutana na wananchi wa eneo husika mwaka 2010 na kunitaka niipe kipaumbele katika bajeti, kwa kushirikiana na diwani tulifanya hivyo na hatimaye barabara hii imetengewa fedha takribani milioni 100 kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo na Manispaa ya Kinondoni katika mwaka huu wa fedha 2011/2012.

Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko ya siku za karibuni nilifika tena tarehe 7 Januari 2012 na kufanya mkutano na wananchi katika shule ya msingi Mabibo/Makuburi kwa ajili ya kuanza harambee ya kuunganisha nguvu ya wananchi kufanya ukarabati wa dharura wakati ambapo matengenezo makubwa ya Manispaa yakisubiriwa.

Katika mkutano huo paliundwa kamati ya wananchi wenyewe na sisi wengine tulichangia fedha na kamati ikapaswa kuwaona wadau wengine zaidi ili kazi iweze kufanyika kwa haraka. Kamati ilikuwa ni ya wananchi wenyewe lakini tulikubaliana kwamba iangaliwe kwa karibu na Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa husika ili kuhakikisha kwamba fedha zinatumika vizuri na kazi inafanyika kwa ufanisi.

Hata hivyo, kamati haikuweza kuanza kazi kwa wakati kwa kuwa walipaswa kupata utambulisho toka kwenye mamlaka husika lakini kukawa na vikwazo kwenye ngazi ya serikali za mitaa. 

Kwa maelezo niliyopewa na diwani ni kwamba pamekuwa na mvutano baina yake na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangu kwa kuwa mwenyekiti husika amekuwa akinufaika na ukusanyaji wa fedha za “KITENGO”, ambazo ana hofu kwamba mchakato huu wa kuwashirikisha wananchi unaweza kutishia maslahi hayo. Diwani amenieleza kuwa kufuatia hali hiyo mwenyekiti huyo amekuwa akitumia baadhi ya vijana kupinga harakati hizo za maendeleo suala ambalo lilimlazimu diwani kuitisha wenyeviti wa mitaa yote ya kata bila kujali vyama kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata (WDC) kufanya maamuzi ya pamoja.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari wamekaa kikao husika, wenyeviti wengine wamehudhuria na kubariki kazi hiyo iendelee isipokuwa mwenyekiti wa Kibangu ambaye alitoka kwenye kikao kwa kususia. 

Wenyeviti wengine na diwani wamekubaliana kuendelea na utekelezaji wa kazi hiyo ya matengenezo ya barabara, kazi ilichelewa kidogo kuanza baada ya mabadiliko ya mtendaji kata kufanyika kwenye kata ya Makuburi. 

Leo tarehe 29 Februari 2012 nimemweleza diwani aendelee kusimamia kwa karibu suala hili ambalo liko kwenye ngazi yake ili ukarabati wa barabara ufanyike kwa haraka, na amenijulisha kwamba tayari walishaanza na maeneo korofi zaidi ili kupunguza adha ya usafiri. 

Nimemwambia Diwani aongeze nguvu zaidi ili pamoja na michango ya wananchi kufanya ukarabati katika kipindi hiki cha mpito mpaka pale Manispaa ya Kinondoni itakapokuwa na fedha na kukamilisha mchakato wa zabuni wa matengenezo yaliyotengewa fedha.

Kwa upande mwingine, kumekuwepo na tatizo la miaka mingi la njia ya kwenda Makoka kwenye eneo la Riverside kumegwa na Mto Kibangu kwa kiwango cha barabara kutopitika na hivyo wananchi wenye magari kuzunguka umbali mrefu. Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Ubungo nilifanya uchambuzi wa Hansards za miaka ya nyuma na kuiandikia serikali itekeleze wajibu wa kuwalipa fidia wananchi husika ili njia mbadala kuweza upatikana, suala hili nimelifuatilia kwa karibu kwa nyakati mbalimbali kwa mamlaka zote zinazohusika. 

Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Makuburi pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na hatimaye nikafanikisha wananchi hao kukutana na watendaji wa Manispaa na fedha zao za fidia kutengwa.

Hata hivyo, kabla ya kukabidhiwa fedha hizo baadhi yao wamekataa kiwango ambacho walikuwa wamekubaliana awali kwa maelezo kwamba thamani za nyumba zao zimepanda baada ya serikali kuchelewa kuwalipa kwa miaka mingi, hawajaridhika na kiwango cha riba kilichowapa nyongeza kwa miaka husika kwa kutozingatia bei ya soko.

Nimeendelea kufuatilia suala husika kupitia mikutano ya baraza la madiwani tarehe 25 Februari na 28 Februari 2012 na Manispaa imeahidi kufanya majadiliano nao tena kuweza kutoa nyongeza inayowezekana ili malipo yafanyike mwezi Machi. Nimemwelekeza diwani afuatilie kwa karibu utekelezaji na iwapo akikwama anijulishe ili niweze kuchukua hatua za kuingilia kati.

Natoa mwito kwa wakazi wa Makuburi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa diwani katika kuhakikisha kwamba masuala husika yanafanyika kwa wakati, na iwapo hatua za kibunge zinahitajika msisite kunijulisha. Maslahi ya Umma Kwanza.


23 Feb 2012


Tamko la Mbunge wa Ubungo kupitia Chadema,Mheshimiwa John Mnyika kuhusu tatizo za upatikanaji wa maji jijini Dares Salaam na ubabaishaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasco):


THURSDAY, FEBRUARY 23, 2012


DAWASCO imekiuka mikataba; hatua za haraka zinahitajika kuboresha upatikanaji wa maji DSM

Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) imekiuka mikataba miwili muhimu inayoongoza kazi zake na kusababisha matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.


Imenibidi nitoe taarifa hii kwa umma kwa nilitumia taratibu za kawaida za kiofisi tarehe 14 Februari 2012 kuiandikia barua DAWASCO kuchukua hatua kuhusu tatizo la kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.


Hata hivyo DAWASCO haikujibu barua husika kueleza hatua ambazo imechukua, hivyo natoa mwito wa wazi wa siku tatu kwa DAWASCO kufanya ukaguzi wa mtandao wa maji na kurekebisha kasoro zilizopo na kutoa taarifa kwa umma kuhusu matitizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo. 


Kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba ni kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia serikali hivyo nakusudia kuchukua hatua zaidi za kibunge dhidi ya DAWASCO iwapo haitazingatia masharti ya mikataba husika na kushughulikia matatizo ya maji yanayoendelea hivi sasa katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo.


Ikumbukwe kuwa DAWASCO ni shirika la umma lililoundwa kwa tangazo la Serikali nambari 139 la tarehe 20 Mei 2005 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992.


Tarehe 1 Julai 2005 DAWASCO ilipewa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) na DAWASA ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.


Aidha, katika kutekeleza mkataba huo DAWASCO inapaswa kuzingatia mkataba wa huduma kwa wateja (Client Service Charter) ambao unaitaka DAWASCO kushughulikia kwa muda maalum malalamiko ya wateja na kutoa taarifa kwa umma kila panapokuwa na matatizo ya maji.


Kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa wateja DAWASCO inapaswa kushughulia malalamiko ya wateja na kuyajibu ndani ya siku tano na iwapo matatizo yaliyopo yanahitaji hatua za kiufundi; DAWASCO inatakiwa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku 30.


Kuanzia mwishoni mwa mwezi Disemba 2011 mara baada ya maafa ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es salaam mpaka leo tarehe 22 Februari 2012 nimepokea malalamiko mbalimbali toka kwa wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo sio nzuri kama ilivyokuwa baada ya hatua ambazo tulichukua kwa nyakati mbalimbali kuanzia Januari 2011 mpaka Septemba 2011.


Itakumbukwa kwamba tarehe 5 mwezi Septemba 2011 nilifanya maandamano ya kwenda DAWASCO nikiwa na wawakilishi wa wananchi wa kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo ambapo tulifanya mkutano na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO. 


Kufuatia mkutano huo DAWASCO ilichukua hatua mbalimbali ambazo ziliboresha mgawo wa maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo kabla ya ratiba ya mgawo kuvurugika kufuatia mafuriko yaliyokumba mkoa wa Dar es salaam.


Hata hivyo, baada ya mafuriko hayo DAWASCO haikuchukua hatua zinazostahili kwa wakati na kuachia kurejea tena kwa mtandao haramu wa biashara ya maji wenye kuhujumu wananchi hususan wa kipato cha chini katika Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.


Hivyo, bodi ya wakurugenzi ya DAWASCO chini ya uenyekiti wa Mhandisi Suleiman Said Suleiman na Mtendaji Mkuu wa kampuni Jackson Midala wanapaswa kurekebisha kwa haraka mfumo mzima wa ufuatiliaji wa DAWASCO kuwezesha ukaguzi wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji.


Katika kipindi hiki cha matatizo makubwa ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ikiwemo katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo DAWASCO iache kuwatumia wafanyakazi wanaohusika na ukaguzi kufanya kazi tofauti za kusoma mita na kugawa Ankara badala yake wafanyakazi tajwa wafanye ufuatiliaji wa dharura wa ufanisi wa mtandao mzima wa maji katika maeneo mbalimbali.


Baadhi ya maeneo ambayo yanapaswa kutembelewa ni kata za Makuburi, Kimara, Saranga, Mbezi Luis, Msigani, Kwembe, Goba, Kibamba, Sinza, Makurumla, Mabibo, Manzese, Ubungo na Mburahati. 


Kwa upande mwingine, kwa kuwa mkataba wa huduma kwa wateja unatoa haki kwa wateja wa DAWASCO lakini pia unaeleza wajibu; natoa mwito kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kutimiza wajibu wa kuwaelekeza wakaguzi husika mitaa yenye matatizo katika mtandao wa maji ili hatua ziweze kuchukuliwa.


Mkataba huo unawataka wateja wa DAWASCO kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu, wizi wa maji na kuhusu matatizo ya maji hivyo wananchi watoe taarifa husika na kufuatilia wakaguzi kufika maeneo yao kwa kupiga nambari ya bure 0225500240 au 0762979627 za DAWASCO makao makuu.


Pia, wananchi wanaweza kuwasilisha kero za maji kwa ofisi ya DAWASCO zilizo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na kupitia nambari zifuatazo: Temeke +255 775016184, Ilala +255 775048556, Magomeni +255 775016179, Boko/Tegeta +255 775048553, Tabata +255 775016181, Kawe +255 775016185, Kinondoni +255 775016180 na Kimara +255 775048554. 


Wananchi watumie pia nafasi hii kuwasilisha kwa DAWASCO maelezo na vielelezo kuhusu maeneo ambayo hakuna miundombinu ya maji kabisa au miundombinu iliyopo haijawahi kutoa maji kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kutaka hatua za ziada. 


Matatizo ya maji katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo yamedumu kwa miaka mingi, wananchi wametupa wajibu wa kuwawakilisha kuisimamia serikali na mamlaka zake kupunguza kero husika kwa haraka hivyo wananchi watarajie vitendo zaidi vya kushinikiza uwajibikaji kwenye sekta ya maji katika kipindi cha karibuni.


Imetolewa tarehe 22 Februari 2011 na:


John Mnyika (Mb) 

18 Jul 2011


BRILLIANT BUDGET SPEECH, HONGERA SANA! 
Nd. Mnyika,
Nimesoma hotuba yako bungeni hapa chini kwa makini sana na kupata faraja kubwa – hongera nyingi, na kama wasemavyo wataliano – BRAVISSIMO!  Pia nimefurahi zaidi baada ya kuona baadhi ya yale ninayoandika na kushauri, hususan maswala ya urani (uranium), kupewa hisa watanzania, STAMICO na TPDC, maswala ya kulinda na kuhufadhi vizuri mazingira ya nchi wakati wa uchumbaji wa madini, haja ya kuchunguza na kubadilisha mikataba mibovu ya madini ikiwa ni pamoja na ulaghai wa kampuni kama Williamson Diamonds, TanzaniteOne, uzembe uliofanyika kuingia mikataba mibovu ya gesi asilia n.k., haya mambo yote umeyachambua ipasavyo na hata kwenda mbele zaidi kwa kuweka bayana baadhi ya mambo mengine ambayo mimi kama mtaaalamu sikuwa nayafahamu kuwa yanatendeka Tanzania hivyo kuweza kunipa habari ambazo zitanisaidia kuyachambua kitaalamu, tena kwa kina. Nimepaka rangi baadhi ya sehemu kwenye hotuba yako kuonyesha yale ambayo yamenigusa zaidi na mambo ambayo niliwahi kuyakemea na kusisitiza yachunguzwe na kubadilishwa kwa muda mrefu.
Nadhani utakuwa umesoma barua zangu za hivi karibuni zinazohusu maswala ya madini nchini Mongolia na Sudani Kusini – ziko hapa. Ni matumaini yangu mtazichambua barua hizi pamoja na wenzako wa kambi ya upinzani Bungeni na muangalie namna gani mnaweza kuhakikisha yale muhimu kwa taifa letu yanaweza yakatekelezwa Tanzania. Ndani ya barua hizo utaona pia maoni yangu kuhusu mauaji ya Tarime uliyoniuliza hapo awali ingawa msimamo wangu kuhusu hili jambo niliwahi kuzungumzia vikali kwenye baadhi ya barua zangu zikiwezo hizi hapa: 1 (soma kuhusu mamillionea wa kimya kimya - Silent Millionaires – walivyowadanganya watu wetu Bulyanhulu. Baadhi ya hawa mamillionea ni/au walikuwa wafanyakazi wa serikali). Soma pia hapa 2, pamoja na hapa 3.
Pia hapa chini nakutumia tovuti za makala kadhaa ambazo nadhani ni muhimu kuzisoma hasa baada ya kuona kuwa ni mambo ambayo uliyazungumzia kwenye hotuba yako na mimi pia nimekuwa nikisisitiza kwa muda mrefu yafanyiwe kazi na serikali. Ni matumaini yangu utaendela na msimamo wako imara wa kuibana serikali ifanye marekebisho pale ambapo inaonekana kuwa rasilimali za taifa haziwanufaishi watanzania, na wale waliongia nchini kama wawekezaji wa kigeni, na hata raia na makampuni yetu ya Tanzania, wanakiuka na kuvunja sheria za sekta ya madini. Ni muhimu makosa makubwa tunayoyafanya kwenye sekata ya madini, gesi asilia na petroli yarekebishwe, tena haraka sana. Kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako, hakuna sababu yeyote ya msingi watanzania waishi kwenye umaskini wa kutupwa huku wakiwa na utajiri mkubwa wa madini kama tulionao, utajiri ambao serikali yetu inautoa, hata niseme, kuutupa kwa wageni – hii si sahihi hata kidogo. Nitashukuru kama utakuwa unaniarifu mara kwa mara maendeleo ya jitihada zenu kufanikisha azma hii.
Ahsante, na pongezi nyingi kwa ujasiri na uimara wako Bungeni.
Shaaban
Moscow, Urusi.     

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.