NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na kushindwa kuwaletea makala katika toleo lililopita. Hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Ninaomba pia kutumia fursa hii kuwatakia ndugu zangu Waislamu mfungo mwema wa mwezi Mtukukufu wa Ramadhani.
Katika makala ya hii nitaendelea kuzungumzia kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu. Na zaidi nitaelemea katika nafasi ya urais, hususan mchakato unaoendelea ndani ya chama tawala, CCM, ambapo hadi wakati ninaandaa makala hii, makada 37 wa chama hicho wameshajitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho kuwapitisha kuwania nafasi hiyo.
Lakini kabda sijaingia kwa undani, pengine ni muhimu tukumbushane kuwa wakati idadi ya makada 37 (ambayo huenda ikaongezeka) ni ya kihistoria, suala la kushtua zaidi ni ukweli kwamba miongoni mwao ni pamoja na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mawaziri kamili saba, bila kujumuisha manaibu waziri.
Nimekumbushia suala hili kwa sababu ni vigumu kufahamu serikali yetu muda huu inaendeshwaje, hasa ikizingatiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete nae amekuwa katika safari za mara kwa mara nje ya nchi (wakati ninaandika makala hii yupo nchini India).
Ukiondoa Makamu wa Rais, ambaye anakuwa kaimu Rais wakati Rais anapokuwa nje, licha ya majukumu ya kiwaziri, Waziri Mkuu na hao mawaziri wengine pia ni wabunge. Katika hili ni vigumu kufahamu wanamudu vipi kugawa muda wao kwa majukumu yao ya kiserikali, kiubunge na hayo ya kuwania kuteuliwa kuwania nafasi ya Urais.
Hata hivyo, si vigumu kudhani kwamba kwa muda huu, akili na nguvu kubwa kwa makada wote waliotangaza nia zitakuwa zimeelekezwa kwenye kinyang’anyiro cha Urais. Kwa kiasi gani hilo linaathiri utumishi wao kwa umma, ni vigumu kwa sisi wengine kufahamu.
Nikirejea kwenye suala la makada wa CCM kutangaza nia zao kuwania urais, jina lililosikika zaidi wiki iliyopita lilikuwa la Jaji Mkuu wa zamani, Augustino Ramadhan. Japo jina lake lilishawahi kutajwa huko nyuma kama mmoja wa watu ‘wanaoweza kuokoa jahazi,’ lakini kwa kiasi kikubwa habari zilizosikika huko nyuma zilionekana kama tetesi tu pasi uthibitisho.
Angalau mara mbili, gazeti hili la Raia Mwema lilibeba habari zilizohusu uwezekano wa Jaji Ramadhani kugombea urais kwa tiketi ya CCM.
Binafsi, kwanza ninaheshimu uamuzi wa Jaji Ramadhani kwani ni haki yake ya Kikatiba kuchukua uamuzi huo. Hata hivyo, tayari kuna baadhi ya wananchi walioshtushwa kumsikia Jaji huyo akielezea kuwa amekuwa mwanachama wa CCM tangu miaka ya sitini.
Kwanza ninadhani alipitwa tu kutoa kauli hiyo kwa sababu CCM iliundwa mwaka 1977 baada ya TANU na ASP kuungana. Kwahiyo, hakukuwa na CCM miaka ya sitini.
Jaji huyo alieleza kuwa alijiondoa CCM mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya sheria, ambapo mfumo wa vyama vingi uliruhusiwa na hiyo kupelekea watumishi wa umma kutoruhusiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa.
Japo Jaji Ramadhan anasema alijiondoa CCM wakati huo, kuna wanaokwenda mbali zaidi na kutaka uthibitisho katika suala hilo. Sote tunaijua Tanzania yetu, na kwa hakika tunawafahamu vema viongozi na wanasiasa wetu. Ni kwa mantiki hiyo, kuna wanaotaka uthibitisho kuwa kweli Jaji huyo alijiondoa CCM na kutokuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa katika utumishi wake, ikiwa ni pamoja na Ujaji Mkuu.
Na kauli hiyo ya uana-CCM wake, kwa namna flani, imerejesha tena suala la hukumu iliyotolewa na Jaji huyo kwa kushirikiana na majiji wengine dhidi ya kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila aliyetaka mahakama itamke kuwa sheria inayozuwia mgombea binafsi ni kinyume cha Katiba.
Pasi kuingiza kiundani katika kesi na hukumu hiyo, binafsi ninaichukulia hukumu hiyo kuwa moja ya hiba (legacies) kuu za utumishi wa Jaji Ramadhani.
Kwa baadhi yetu tunadhani Jaji huyo angebaki shujaa kwa demokrasia kwa sababu mfumo wa sasa unaolazimisha wawania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa pamoja na urais kuwa wanachama wa vyama vya siasa unatupunja fursa ya kupata viongozi wa kisiasa wazalendo lakini wasiotaka kujihusisha na vyama vya siasa.
Hata hivyo, ili kumtendea haki, ni muhimu kutambua kuwa hukumu hiyo haikuwa maamuzi binafsi ya Jaji Ramadhani bali licha ya kuwahusisha majaji wengine pia, ilikuwa ni ya kisheria na sio hisia binafsi.
Lakini kwangu, licha ya dalili zinazoonekana wazi kuwa kana kwamba CCM imeshapata mgombea wake urais kufuatia uamuzi wa Jaji Ramdhan kutangaza nia, nina wasiwasi kidogo kuhusu ufanisi wake.
Kubwa zaidi ni ukweli kwamba Idara ya Mahakama, ambayo licha ya Jaji Ramadhan kuitumikia muda mrefu bali pia aliwahi kuwa mkuu wake kwa maana ya ujaji mkuu, imeendelea kuwa moja ya taasisi sugu kwa rushwa. Takribani kila ripoti inayotolewa kuhusu tatizo la rushwa katika taasisi mbalimbali za serikali nchini mwetu, Idara ya Mahakama haikosekani, na tena ikishika nafasi za juu.
Mara baada ya kuchukua fomu kuomba CCM imteue kuwania Urais, Jaji Ramadhan aliwaambia waandishi wa habari kuwa atatumia uzefu wake kupambana na ufisadi. Swali la msingi: uzoefu upi? Huohuo ulioshindwa ukiondoa Idara ya Mahakama katika orodha ya taasisi zinazoongoza kwa rushwa?
Kwa upande mwingine, Jaji Ramadhan alikuwa mjumbe wa ‘Tume ya Warioba’ iliyokusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba. Sote twakumbuka yaliyomsibu Jaji Joseph Warioba na baadhi ya wasaidizi wake kupigania sio tu kazi nzuri iliyofanywa na tume yao bali pia mustakabali wa Katiba mpya.
Kwanini Jaji Ramadhani amekuwa kimya sana katika suala hilo? Je ukimya wake ulitokana na kufahamu kuwa siku moja angeomba kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM?
Na katika hilohilo, kwa vile mapendekezo ya Tume hiyo iliyomshirikisha Jaji Ramadhani yalikuwa muungano wenye muundo wa serikali tatu, je kwa vile CCM ambayo jaji huyo anaiomba ridhaa ya kumteua awe mgombea wake ina msimamo wa serikali mbili kama ilivyo sasa, hilo si tatizo angalau kimsimamo na kimtizamo?
Hadi muda huu, Jaji Ramadhani ni Rais wa Mahakama ya Afrika kuhusu haki za binadamu. Sihitaji kuorodhesha matukio lukuki ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Tanzania lakini miongoni mwa matukio makubwa ni pamoja na ukatili unaofanywa na Jeshi la Polisi na rushwa (naam, rushwa sio tu adui wa haki bali pia inachangia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu).
Je Jaji Ramadhani amekuwa wapi wakati ukiukwaji wa haki za binadamu ukiendelea kushamiri na kuwa kama umehalalishwa na Katiba yetu? Ni nani anaweza kusimama hadharani na kuwaambia Watanzania kuwa ‘Urais wa Jaji Ramdhani katika Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika umechangia hili na lile katika kutetea au kudumisha haki za binadamu nchini Tanzania’?
Niwe mkweli, binafsi ninamwona Jaji Ramadhani kama Rais Kikwete alipojitambulisha mwaka 2005 kuwania urais na hatimaye kushindwa nafasi hiyo.
Alionekana mtu mwadilifu, aliyeitumikia nchi kwa muda mrefu, na pengine kubwa zaidi, msafi (asiye na kashfa). Sifa hizo zinalingana na tunazosikia kuhusu Jaji Ramadhan. Je, kwa mfano, kuwa msafi ni sawa na kuwa na uwezo wa kuongoza nchi?
Lakini la mwisho kuhusu kada huyo ni taarifa za awali kuwa amekuwa akiombwa na baadhi ya wana-CCM kuwania nafasi ya urais (kuna wanaodai kuwa ndio mtu pekee anayeweza kumudu ‘kumzuia’ Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa asiingie Ikulu, na wengine wanasema Jaji huyo ndio ‘msafi zaidi’ kuliko makada wengine wanazowania nafasi hiyo).
Swali la msingi: je hao waliomwomba (kama ni kweli) hawafanyi hivyo kwa maslahi yao binafsi? Na je, kumwomba huko (kama ni kweli) hakutopelekea urais wa Jaji Ramadhan (iwapo atashinda) ukaishia kuwa kama ‘deni la kwa wanamtandao’ lilivyouandama utawala wa Rais Kikwete?
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha tena Watanzania wenzangu kuwa ni muhimu tujiulize na kuwauliza wawania urais maswali magumu ili tusije kuishia kujiulaumu huko mbeleni.
Nchi yetu ipo katika wakati mgumu; umasini wa kupindukia huku ufisadi ukizidi kuimarika, uhaba mkubwa wa uzalendo, utovu mkubwa wa maadili ya uongozi ikiwa na pamoja na uhuni katika matumizi ya fedha za umma, shilingi inayporomoka kama ipo kwenye mashindano ya marathoni na kadhalika.
Tunahitaji rais ambaye si tu anajua matatizo yetu bali pia ana uzalendo na uwezo wa kukabiliana nayo. Hatuhitaji Rais msafi lakini mwoga wa kupambana na maharamia wanaoibomoa nchi yetu kila kukicha.
Hatuhitaji mtu anayeahidi kupambana na rushwa ilhali hana mfano japo mmoja wa jinsi alivyowahi kupambana na rushwa.
-