SWALI LA MSINGI HAPA NI JE KWA KUKOMESHA MALUMBANO HAYO NDIO UFUMBUZI WA "KINACHOLUMBANIWA" UTAKUWA UMEPATIKANA?BUSARA NDOGO TU INAWEZA KUTUELEZA KWAMBA MTOTO ANAPOLIA INAWEZA KUASHIRIA KUWA ANA TATIZO (NJAA,KIU,ANAUMWA,NK).KUMFINYA MTOTO HUYO ANYAMAZE BADALA YA KUCHUNGUZA KINACHOMLIZA HAIWEZI KUWA SOLUTION YA TATIZO.
Wenyeviti wastaafu wa CCM waonya
Wenyeviti wastaafu wa mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamevunja ukimya na kuwataka viongozi wa chama hicho wanaotaka kuyatumia mapambano dhidi ya rushwa kama mtaji wa kisiasa na kujipatia umaarufu, kuacha mara moja. Sambamba na hilo, wazee hao wametaka mapambano dhidi ya rushwa yasiwe kichaka cha kuficha ubovu wa uongozi na kushindwa kuwajibika. Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wastaafu wa chama hicho Dar es Salaam jana, Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alisema mapambano dhidi ya rushwa ni ya CCM na si mwanachama binafsi au kikundi cha wanachama wachache.
“Tunashuhudia baadhi ya viongozi wa CCM kurushiana maneno wenyewe kwa wenyewe kwa kutaka kuonyeshana nani zaidi na nani ni vinara kuliko wengine katika mapambano dhidi ya rushwa, hii si sawa,” alisema Ndejembi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Tanzania. “Tusingependa kuona mapambano haya yanatumiwa kama njia ya kujipatia umaarufu binafsi, mwenyekiti wetu Rais Kikwete ambaye ndiye jemedari wa mapambano haya humsikii anafanya hivyo na sisi wengine tusifanye hivyo…. kama wewe ni kiongozi na hutekelezi wajibu wako kwa wapiga kura wako wakikuuliza uko wapi, usisingizie kupigwa vita na mafisadi,” walionya.
Ndejembi aliyeambatana na wenyeviti wastaafu Hemed Mkali (Dar es Salaam), Tasil Mgoda (Iringa) na Jumanne Mangara (Pwani), alisema wazee hao wamesikitishwa na malumbano ya hadharani baina ya viongozi wa CCM ambao wengine wa ngazi ya juu ya uongozi ndani ya chama. Alisema tabia inayoonyeshwa na viongozi hao ya kushutumiana, kunyoosheana vidole, kuwekeana visasi, kuonyeshana ubabe na kuwekeana nadhiri ya kupambana baina ya viongozi, kunadhoofisha na kukipunguzia heshima chama hicho.
“Lakini pia kufanya hivyo hadharani, kwa nia ya kutaka kuungwa mkono katika shutuma na visasi hivyo kunajenga chuki, uhasama na migawanyiko katika jamii, viongozi hatupaswi kuwajaza watu chuki na uhasama ndani ya mioyo yao,” alisema Ndejembi kwa niaba ya wenzake na kutaka neno ufisadi lisitumiwe kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani. Alisema kumuita mtu fisadi kwenye vyombo vya habari haitoshi katika kushinda mapambano dhidi ya rushwa, bali watu waipigie kelele serikali iimarishe taasisi na vyombo vya kupambana na rushwa kama Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mahakama ambako watuhumiwa wanafikishwa.
Licha ya kuwapo malumbano baina ya viongozi hao wa CCM, wastaafu hao walisema kuhitilafiana ni kitu cha kawaida na kamwe watu wasitarajie chama hicho kitameguka. Wastaafu hao walieleza kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete iwapo atagombea tena urais mwakani na kutaka watu wengine wamuunge mkono, kwa maelezo kuwa anafaa kuongoza nchi. Walitoa sababu za kumuunga mkono kuwa ni kukubalika na anaowaongoza, anawapenda watu wote, mvumilivu, mkereketwa wa maendeleo ya wananchi na hana jazba.
Wazee hao walisema wameamua kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo hayo ili ujumbe uwafikie viongozi, wanachama na mashabiki wa CCM, lakini yote hayo waliyoyaeleza wameshayawasilisha kwenye vikao wanavyoshiriki vya matawi na mashina na wamezungumza na viongozi wa sasa wa chamahicho. Ingawa wastaafu hao hawakuwataja kwa majina viongozi wa CCM waliolumbana hadharani, lakini hivi karibuni Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ni mwanahisa wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo ya East Africa Power Pool, amelumbana na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Dk. Mwakyembe anadai Rostam anatumia vyombo vyake vya habari kumchafua huku Rostam akitaka mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwandishi wa habari, kuelezea mgongano wa maslahi wakati alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Mbali na wazee hao, pia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara ambaye ni Mbunge wa Mtera, John Malecela alitaka malumbano hayo yakome, kwani hayana faida kwa mwananchi na wahusika watumie vyombo husika vya chama kufikisha malalamiko yao.
CHANZO: HabariLeo