|
Mgao wa Tanesco ukiwa kazini |
Sio siri kwamba kinachowapa jeuri mafisadi kuwapalekesha Watanzania ni upole kupita kiasi walionao wanachi.Watu wanalipa kodi-kwenye mishahara kwa walioajiriwa,katika VAT kwenye manunuzi ya bidhaa mbalimbali,na utitiri mwingine wa kodi-lakini faida ya kodi hiyo inaonekana zaidi kwenye ukubwa wa vitambi vya viongozi wetu,thamani ya magari na mahekalu yao,na kuongezeka kwa idadi ya vimada na nyumba ndogo zao.
Sasa Tanesco wamekuja na kali kubwa kwa kutangaza mgao wa umeme usio na kikomo,masaa kumi kwa kila siku ya wiki.Ukienda huko Twitter utasikia "aah Tanesco wamechukua umeme wao".Wengine wanaishia kuitukana Tanesco kwa matusi ya "sehemu za siri za mama yake Tanesco".Hizi zote ni dalili za watu walioishiwa na mbinu zakudai haki zao.Hivi "kumtukana mama yake Tanesco" kutafupisha mgao wa umeme?
Imefika wakati Watanzania watambue kuwa mara nyingi HAKI HAITOLEWI KAMA ZAWADI BALI HUDAIWA...KWA NGUVU IKIBIDI.Hakuna uwezekano wa tatizo la mgao wa umeme kuisha kwa njia za kistaarabu.Utatuzi hauwezi kupatikana kwa vile sekta ya nishati,kama ilivyo ya madini ni kitega uchumi kikubwa kwa mafisadi wetu.Kukatika umeme kunawaingizia baadhi ya majambazi hao mamilioni ya shilingi kila siku.
Nina tatizo kubwa zaidi na Wtanzania wa tabaka la kati.Hawa ndio tunaokutana nao huko Twitter na Facebook...Kiingereza kiiingi huku nchi inateketea.Hawa ndio tunaowaona wakijirusha kwenye kumbi mbalimbali za "starehe".Kuna starehe gani kuwepo kwenye ukumbi unaobadilisha taa kutoka rangi moja kwenda nyingine (kwa kutumia jenereta) kisha kurudi nyumbani na kukumbana na kiza na joto kwa vile "Tanesco wamechukua umeme wao" na feni haiendeshwi kwa mafuta ya taa!
Kwanini nailamu middle class yetu?Ni kwa vile hiki ni kiungo muhimu kati ya tabaka tawala na tabaka la walalahoi.Hawa ndio wenzetu wenye shahada au stashahada katika fani moja au nyingine.Hawa ni watu wenye upeo na wanaweza kuihamasisha jamii kutambua na kudai haki zao.Wengi katika tabaka hili ni walalahoi wanaojaribu kuiga maisha ya wale wa tabaka la juu.
Uchaguzi ni wenu.Kujifanya mmezowea maumivu na mafisadi waendelee "kupeta" au kuweka kando "ubishoo na usistaduu" na kuungana na tabaka la walalahoi kuhamasisha mabadiliko katika nchi yetu.Akina sie tunatekeleza wajibu kwa namna kama inavyofanya makala hii.Sasa ni wajibu wa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ili kuinusu nchi yetu.
Enewei,hebu soma stori husika hapa chini
Tanesco yatangaza mgawo wa saa 10 kwa siku nchi nzima
Wednesday, 22 June 2011 21:06
Waandishi Wetu
SHIRIKA la Umeme (Tanesco), limetangaza mgawo mkubwa wa umeme usio na kikomo, utakaokuwa kwa saa 10, siku saba kwa wiki nchi nzima.
Maafisa wa shirika hilo na Wizara ya Nishati na Madini wamesema mgawo huo umetokana na upungufu wa maji katika bwawa la Mtera na transfoma zake kuzalisha umeme mdogo kuliko mahitaji.Kwa mujibu wa tangazo la ratiba ya mgao huo lililotolewa na Tanesco jana, mgao huo utakuwa wa kati ya saa sita hadi 10 kwa siku ambapo maeneo yatabadilishana muda wa mgawo.
Hata hivyo, tangazo hilo la Tanesco limekuja wakati maeneo mengi nchini yakiwa na mgawo wa muda mrefu na ambao unachukua muda wa saa zaidi ya zilizotangazwa jana na shirika hilo hali iliyosababisha malalamiko kwa wananchi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo mgawo huo utakuwa wa kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili ambapo baadhi ya maeneo yatakosa umeme mchana na mengine yatakosa usiku.Tanesco ilisema katika baadhi ya maeneo umeme utakatika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni, wakati maeneo mengine yatakosa umeme kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 5.00 usiku.
Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jana, Mhandisi Mkuu wa Tanesco, Juliana Pallangyo alisema mgawo huo unatokana na kupungua kwa kina cha maji katika bwawa la Mtera.
Alisema mahitaji ya umeme ni megawati 850 wakati uzalishaji ni megawati 600 hali inayochangia upungufu wa umeme.
“Mahitaji yaliyopo ni makubwa wakati umeme unaozalishwa ni mdogo, tunashindwa kumudu mahitaji ya watu wote kwa wakati mmoja na ndiyo maana tunakuwa na mgawo,” alisema Pallangyo.Aliongeza kuwa licha ya matatizo hayo shirika hilo lina malengo ya kusambaza umeme vijijini ambako bado hakujafikiwa na umeme.
Katibu adai mgawo utakuwa historia
Akizungumzia kuhusu mgawo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema mgawo huo unaweza kuwa historia katika miaka miwili ijayo na kwamba hali ya sasa inatokana na upungufu wa maji katika bwawa la Mtera ambalo linaweza kufungwa kwa sababu hiyo.
Katika hatua nyingine, Jairo alisema Serikali ya China itatoa mkopo wa dola za Marekani 778 milioni sawa na Sh1,167,000 bilioni, kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kufunga bomba kubwa la kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam, itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Alisema hatua hiyo itafanyika endapo Serikali ya Tanzania itafikia makubaliano na Serikali ya China katika mazungumzo baina yao yanayotarajia kuyafanya wiki ijayo.Iwapo mpango huo utafanikiwa kampuni ya China Petrolium Company ndiyo itakayozalisha umeme.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Jairo alisema, kiasi hicho cha fedha ni kulingana na upembuzi yakinifu uliofanywa na kwamba gesi itakayozalishwa itasaidia kupunguza tatizo la umeme na uharibifu wa mazingira nchini.
Alisema bomba linalozalisha gesi kwa sasa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni dogo likiwa na ukubwa inchi 30 hivyo uzalishaji wake pia ni mdogo.“Sisi kama wizara tunajitahidi kuweka mipango ya muda mfupi ya kukabiliana na tatizo la umeme lililopo nchini kwa hiyo Serikali ya China itatupa fedha hizo kama mkopo kwa ajili ya kuzalisha gesi hiyo,”alisema Jairo