Miongoni mwa vyanzo vya 'matatizo' katika matumizi ya mitandao ya kijamii ni uelewa mdogo wa wengi wanaoitumia mitandao hiyo. Ni vigumu kubainisha sababu moja inayochangia uelewa huo mdogo lakini yayumkinika kuhisi kwamba baadhi ya wenzetu hawapendi kujishughulisha kusaka maarifa/ uelewa.
Lakini pengine kikwazo kikubwa zaidi katika kupata uelewa, si tu kwa matumizi ya mitandao pekee bali kila kitu, ni 'kiburi' cha aidha kutotaka kuuliza pale mhusika haelewi au kufinya anaelewa ilhali haelewi, au kibaya zaidi, kuwavunja moyo wale wanaojitahidi kueneza uelewa wa masuala mbalimbali (mara nyingi huitwa 'wajuaji' kana kwamba kujua kitu na kuki-share ni kosa la jinai).
Tuliopitia JKT twafahamu 'kanuni ya kwanza unapowasili kambini,' yaani kufahamu mahali pa kujisaidia (kichekesho ni kwamba mara nyingi kambi za porini - na nyingi ya kambi za JKT enzi hizo zilikuwa maporini- hazina vyoo, na vikiwepo ni kwa matumizi ya maafande tu. Makuruta hupaswa kutengeneza vyoo katika muda wao binafsi).
Kadhalika, japo ni jambo linalopuuzwa na wengi, ni muhimu kwa kila mtumiaji wa mtandao wa kijamii, na kwa hakika mtandao wowote ule, kujibidiisha kufahamu japo kanuni na taratibu za msingi za mtandao husika, hususan haki na wajibu wake na wa mwenye mtandao. Uelewa huu si tu ni muhimu kwa kurahisisha 'maisha yetu mtandaoni' bali pia waweza kumsaidia mtumiaji kuepuka matatizo ya kisheria pindi akikiuka taratibu na kanuni hizo.
Kwa mtandaoni, kila mtandao, uwe wa kijamii au 'wa kawaida,' una kanuni na taratibu zake. Moja ya taratibu muhimu ni pamoja na haki za mtumiaji na wajibu wake. Miongoni mwa haki hizo ni pamoja na 'taarifa za mtumiaji' wa mtandao husika. Ndio maana ikitokea mtandao ukaweka hadharani anwani ya mtumiaji pasi ridhaa yake, unaweza kufunguliwa mashtaka kwa kukiuka haki za mtumiaji.
Kadhalika, mtandao ukiruhusu (makusudi au kwa bahati mbaya) mtu asiye na mamlaka kisheria kuweka taarifa 'nyeti' za mtu mtandaoni pasi ridhaa ya mhusika, unaweza kujiingiza katika matatizo makubwa ya kisheria
Sasa nimeona huko katika mtandao wa Twitter 'harakati' zinazofanyika kuhusu haja ya kufungwa kwa akaunti ya Twitter ya ndugu yetu, marehemu Betty Ndejembi, aliyefariki hivi karibuni.
Na pengine harakati hizo zinaisaidia jamii kuonyesha umuhimu wa HARAKATI japo kuna baadhi ya wenzetu wanaotafsiri uana-harakati kama kosa la jinai.Binafsi nadhani tatizo la watu wa aina hii ni kuzowea mno kufanyiwa mambo na serikali, taasisi au watu wengine (kwa mfano wanasiasa) kiasi kwamba wanapoona mtu binafsi anachukua msimamo katika suala flani wanamtafsiri ndivyo sivyo. Harkati chanya ni kitu kizuri kwa jamii kwani zaondoa haja ya utegemezi kwa taasisi kama serikali na kuwezesha 'nguvu ya umma.'
Harakati hizo za kutaka akaunti ya marehemu ifungwe zimehusisha ombi kwa mwanasiasa mmoja maarufu ashughulikie suala hilo. Binafsi sina tatizo na waliotoa ombi hilo bali laiti wangejihangaisha japo ku-Google 'how to request Twitter to close a deceased account' (jinsi ya kuiomba Twitter ifunge akaunti ya mtu aliyefariki) wasingehitaji kutuma ombil hilo kwa mwanasiasa huyo. Naomba ieleweke kuwa si dhambi kuomba msaada kwa mtu yeyote yule, let alone mwanasiasa. Lakini kuna masuala ambayo yapo ndani ya uwezo wetu ila tatizo ni uelewa mdogo au kutokuwa na uelewa.
Taratibu za kuiomba Twitter ifunge akaunti ya mtu aliyefariki ziko hivi (tafsiri ya Kiswahili ni yangu):
"Kuwasiliana na Twitter kuhusu mtumiaji aliyefariki...
Kinapotokea kifo cha mtumiaji wa Twitter, twaweza kushirikiana na mtu mwenye mamlaka ya kushughulikia mali (estates) za marehemu au mwanafamilia aliyethibitishwa wa marehemu kuwezesha kufunga akaunti ya marehemu.
Ili kutuwezesha kushughulikia kufunga akaunti (ya marehemu), tafadhali tupatie taarifa zifuatazo:
1. Jina (username) la marehemu katika akaunti yake ya Twitter, yaani katika ishu ya marehemu Betty itakuwa @BettyNdejembi au twitter.com/BettyNdejembi
2. Nakala ya cheti cha kifo cha marehemu.
3. Nakala ya kitambulisho kilichotolewa na serikali (kwa mfano leseni ya udereva au hata hati ya kusafiria)
4. Tamko (statement) lililosainiwa linalojumisha vitu vifuatavyo-Jina la kwanza na la mwisho la anayetuma ombil la kufungwa kwa akaunti ya marehemu-Barua pepe ya mwombaji-Mawasiliano (simu, anwani,nk)-Uhusiano wa mwamobaji na marehemu au mali za marehemu (estate)-Dhima ya ombi kwa Twitter (kwa mfano ; ninaomba Twitter ifunge akaunti ya marehemu')-Maelezo mafupi ya kuthibitisha kuwa akaunti husika ni ya marehemu, iwapo jina lililopo kwenye akaunti hiyo halifanani la lililopo kwenye hati ya kifo cha marehemu)-Kiungo (link) cha tanzia (obirtuary) au nakala ya tanzia kutoka gazetini (sio lazima-optional)
5 Tafadhali tutumie nyaraka hizo kwa faksi au barua-pepe kwa anwani ifuatayo:
Twitter, Incc/o Trust & Safety1355 Market St., Suite 900San Fransisco, CA 94103Fax: 1-415-865-5405
Zingatia: Hii ni namba ya Marekani, kwahiyo hakikisha ina namba sahihi ya kipiga simu za kimataifa (international dialing code) iwapo unatuma kutoka nje ya Marekani.
Tunafanya mawasiliano yetu yote kwa kutumia barua-pepe, iwapo tutahitaji taarifa nyingine, tutawasiliana nawe kwa anwani ya barua-pepe uliyotupatia. Iwapo una swali lolote, waweza kuwasiliana nasi kwa [email protected]
Sasa, kwa kuangalia tu utaratibu huu, hutoshindwa kutambua kuwa hili ni suala la kifamilia zaidi kuliko lenye kuhitaji mwanasiasa ashughulikie, unless mwanasiasa husika ni mwanafamilia ya marehemu.
Kuna kitu twaweza kujifunza hapa. Kwa wenzetu huku nchi za Magharibi, kufanya maandalizi ya 'nini kifanyike baada ya kifo changu' ni jambo la kawaida. Licha ya huduma kama bima ya kifo, kuna taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na huduma za maandalizi baada ya kifo kama vile kushughulikia maiti yako utapofariki ikiwa ni pamoja na mahali utapozikwa, usimamizi wa mirathi, nk.
Lakini pia kuna huduma mbalimbali za bure mtandaoni kuhusu hatma yetu mtandaoni baada ya vifo vyetu. Kimsingi, mada ya 'kifo na mtandao' (Death and the Internet) ina maingizo 242,000,000 katika tovuti ya kutafutia taarifa (search engine) ya Google
Ninatambua kuwa kwa mujibu wa mila na desturi mbalimbali za Kiafrika, kuchukua hatua hizi za maandalizi ya baada ya kifo kwaweza kutafsiriwa kama 'uchuro,' licha ya ukweli kwamba siku moja kila mmoja wetu atakuwa marehemu kwani kifo haikiepukiki.
Nimalizie kwa kutanabaisha kuwa lengo la makala hii sio kudhihaki harakati za wanaotaka akaunti ya marehemu Betty ifungwe (hasa nikiwa natambua uwepo wa 'uhuni usiopendeza hata chembe' wa baadhi ya watu wanaojifanya ku-tweet kana kwamba ni marehemu mwenyewe ana-tweet "kudai atendewe haki" japo tweet husika haikutoka katika akaunti ya marehemu) bali ni kuelimisha kuhusu utaratibu wa kuomba akaunti ya Twitter ya mtu aliyefariki ifungwe, suala ambalo kwa wenye uelewa ni la kifamilia zaidi kuliko kuhitaji 'msaada' kutoka kwa wanasiasa.
Ushauri wangu kwa wanaotaka kuona akaunti hiyo ikifungwa ni kuwasiliana na familia ya marehemu na kuwafahamisha utaratibu husika (iwapo hawafahamu). Ikumbukwe kuwa akaunti ya marehemu, iwe Twitter au katika mtandao wowote ule, ni mali ya marehemu, kama ilivyo akaunti yake ya benki, hati yake ya kusafiria, hati ya kiwanja, au mali yake yoyote ile. Ili, kwa mfano kuweza kufunga akaunti yake benki, ni lazima ipatikane ridhaa ya wenye mamlaka na marehemu, kwa mfano maelekezo katika wosia wake au maamuzi ya famili yake. Kadhalika, ili akaunti yake ya Twitter iweze kufungwa, ni lazima kupata ridhaa ya marehemu kupitia wosia wake au uamuzi wa wanafamilia yake.
Mungu amlaze marehemu Betty mahala pema peponi, Amen.