Showing posts with label PROFESA NYANG'ORO. Show all posts
Showing posts with label PROFESA NYANG'ORO. Show all posts

12 Dec 2010



Majuzi kulifanyika uzinduzi wa kitabu kinachoelezea wasifu wa Rais Jakaya Kikwete.Tukio hilo linaelekea kuwa na uzito wa kipekee kwani baadhi ya picha zilionyesha sehemu kubwa ya familia ya mkuu huyo wa nchi ilihudhuria uzinduzi huo.Sina hakika kuhusu kilichomo kwenye kitabu hicho lakini yayumkinika kuamini kuwa laiti wasifu huo ungegusia masuala kama "Wanamtandao na mchango wao katika ushindi wa Kikwete 2005",au "Uswahiba kati ya Kikwete,Lowassa na Rostam Aziz na jinsi unavochangia kufilisika kwa Tanzania", au "wasifu wa wateuliwa mbalimbali wa Kikwete na namna wanavyohusiana nae",nk isingekuwa rahisi kwa Rais Kikwete kujitokeza kwenye uzinduzi huo.

Mwandishi wa kitabu hicho ni Profesa Julius Nyang'oro.Wakati mwingine najiuliza kama baadhi ya maprofesa wa aina hii wameishiwa na mada za muhimu kwa jamii na badala yake wanageukia kujikomba kwa watawala kwa kuandika wasifu mithili ya pambio.Unaweza kunilaumu kwa kutoa tuhuma kabla sijasoma kilichomo katika kitabu hicho.Hata hivyo,huhitaji upeo wa juu kubashiri yaliyomo katika kitabu hicho,maana laiti ingekuwa ni wasifu wa Kikwete huyu ambaye utawala wake umetuzalishia msamiati wa "ufisadi",sambamba na kugubikwa na ishu za Kagoda,EPA,Dowans,Richmond na uzururaji njeya nchi,basi si mkulu huyo wala wanafamilia yake wangetia mguu kwenye uzinduzi huo.

Sasa sijui Profesa Nyang'oro kajaza nini kwenye wasifu huo!Mamia ya ahadi za Kikwete na kisha kuichambua moja baada ya nyingine ( kwa mtizamo chanya usiomuudhi mtawala) au ni hadithi za namna Jakaya alivyozaliwa katika familia ya kawaida,akajiendeleza pasipo makeke,akashika hatamu za uongozi lakini akiendelea kuwa "mtu wa watu" na hatimaye akapata urais ( bila kutaja mchango wa wanamtandao) na ameendelea kuwa mwenye upendo na upole sio kwa walalahoi pekee bali hata mafisadi.

Huenda wasifu huo pia ukagusia udaktari wa falsafa (wa heshima) wa Rais Kikwete.Inawezekana atapomaliza miaka yake 10 hapo 2015 (na kama hatafanya mbinu za kutaka aongezewe muda madarakani) ataweka historia nyingine ( on top ya ile ya kumpiku Vasco da Gama kwa safari) ambapo atakuwa kiongozi pekee aliyezawadiwa shahada nyingi za uzamifu kuliko mwingine duniani.Sijui mpaka sasa ana PhD ngapi,ila nakumbuka ile ya Uturuki,nyingine sijui ya Uganda kama sio Kenya,hii ya juzijuzi Dodoma na Muhimbili nao wamemzawadi shahada ya Afya ya Jamii.


Na kwa vile utawala wa Kikwete umetawaliwa na usanii wa namna flani,yayumkinika kuhisi kuwa hizo PhDs zinatolewa baada ya wahusika "kupigwa somo" au "kupewa kilicho chao".Ungeweza kuhisi kuwa ilikuwa hivyo hata Profesa Nyang'oro,lakini "mnyonge mnyongeni haki yake mpeni" hapo itakuwa mtu tu kaamua kujikomba.

Na kama ilivyozoeleka,wanahabari wetu (pamoja na baadhi ya mabloga) walichokumbuka ni picha za tukio na maelezo ya picha hizo (captions) tu,utadhani kwa kuangalia picha hizo msomaji atapata summary ya jumla ya kilichomo katika kitabu hicho.Hapa "simpigi mtu dongo" ila natoa changamoto kwa wenzetu mliobobea kwenye picha,mkumbuke kuwa picha pekee si habari kamili.Hivyo,inapowezekana mtupatie habari zaidi ya picha husika.Ni ushauri tu,tena wa bure buleshi.

Nakumbuka mwaka 2005 kulikuwa na kitabu cha wasifu wa Kikwete.Nahisi hapa katikati kuna waliojipendekeza na kuja na wasifu mwingine.Sasa tuna wasifu huu "mpya" kutoka kwa Profesa Nyang'oro na huenda hapo 2015 kutakuwa na wasifu mwingine wa "miaka 10 ya mafanikio ya kihistoria chini ya utawala wa Jakaya Kikwete".Mtu mmoja wasifu kibao!

Enewei,hiyo ndio Tanzania yetu.Na ukiwa na kiongozi mpenda sifa basi wajanja hawachelewi kumpamba kwa sifa hii au ile.Na kwa vile hawagusii yale yatakayomfanya mtawala atambue kuwa "hajafunga zipu" basi kwa upande mmoja watoa sifa hao wanapata wanachotegemea kupata (sifa,hela,kupiga picha na rais,kualikwa ikulu,na pengine kuzawadiwa U-DC) na kiongozi mpenda sifa anaendelea kuamini yeye ni chaguo la Mungu ndio maana sifa zinaendelea kumiminika kumhusu yeye.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.