Wakati habari kuhusu chama tawala CCM "kujivua magamba" zinaendelea kukamata nafasi ya juu,ni vema tukakumbushana magamba halisi yanayopaswa sio kuvuliwa tu bali kutekeketezwa kwa moto wa gesi.CCM wanaweza kutuchezea shere kwa usanii wao lakini ukweli unabaki kuwa ni migongano ya kimaslahi miongoni mwao ndio inayopelekea hizi ngonjera za kujivua magamba.Ufisadi katika taasisi za umma na serikalini kwa ujumla ndio magamba halisi yanayopaswa kuchunwa kwa nguvu badala ya kuwaruhusu wenye magamba hayo wajivue kwa hiari.By the way,tangu lini uchafu ukajiondoa wenyewe pasipo kutumika nguvu ya sabuni na mkono aumashine ya kufulia?
Soma habari hii ujionee mwenyewe namna Tanzania yetu inavyozidi kuwa shmba la bibi
Kashfa mpya ya Ufisadi TanescoTuesday, 26 April 2011 10:14
CAG ADAI IMEILIPA DOWANS BILIONI MOJA ISIVYO HALALIMwandishi WetuSHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeingia katika kashfa nyingine ya ufisadi baada ya kubainika kuwa limeilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans dola za Marekani 1.2 milioni ikiwa ni gharama ya kusafirisha mitambo ya kampuni hiyo kuja nchini kwa ndege badala ya dola 120,000.
Matumizi hayo ya ziada yanayokadiriwa kufikia Sh1.4 bilioni za Tanzania yanaelezwa kwamba yaliingizwa katika akaunti ya Dowans kimakosa.
Hata hivyo, mpaka sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema Tanesco imeshindwa kumpelekea ripoti ya matumizi ya fedha hizo alizoziita kuwa ni ufisadi.
Mbali na hivyo CAG amelitaka shirika hilo limpelekee mchanganuo wa matumizi ya dola za Marekani 4,865,000 sawa na Sh6.8 bilioni.
Jana, alipotakiwa kufafanua kuhusu ripoti hiyo, CAG Ludovic Utoh alisema: “Nashukuru kwa kunipigia, lakini nyie si mnazo ripoti hizo, mnaweza mkasoma na kuendelea kuripoti.”
Kwa mujibu wa gazeti la The East African, toleo la Aprili 25, mwaka huu, ripoti ya CAG iliyoishia Juni 30, 2010 inaonyesha kuwa Tanesco ilifanya malipo hayo kupitia akaunti ya gharama za mikutano.
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa Tanesco ilishindwa kutoa maelezo kuhusu malipo hayo kwa ajili ya kukodisha ndege maalumu ya kusafirishia mitambo hiyo. Pia inaonyesha kuwa kiasi cha Sh13,000,000 ziliripotiwa kimakosa kama Sh1,300,000,000 kwenye kifungu cha matumizi ya vikao na pia kiasi cha Sh11.0 bilioni kinachohusu malipo kupitia barua ya mkopo (letter of credit) na kuingizwa katika akaunti ya makusanyo ya shirika kupitia benki ya NBC.CAG pia alibaini kuingizwa mara mbili kwa Sh101 milioni katika akaunti ya mitambo ya Tanesco kinyume na taratibu.
CAG alisema kuwa ndani ya Tanesco hakufanyiki usuluhishi wa mapato yatokanayo na mauzo katika matawi yake kukiwemo pia jumla ya Sh103,000,000 za masurufu ambazo hazijarejeshwa. Pia umeme unaozalishwa na ule unaouzwa unaonyesha kwamba shirika hilo linapata hasara kutokana na sababu za kiufundi.
Ripoti hiyo inasema, Tanesco ilionyesha hasara za uniti 1,188 KwH’m kutoka katika uniti 4,831 KwH’m inazozalisha ikionyesha kwamba kuna hasara katika mapato. Hasara hizo zinachangiwa na kuwepo kwa wateja wasio waaminifu, bili za uongo na uunganishaji haramu wa umeme.
Imeeleza kwamba hata wateja waliokatiwa umeme, wanaendelea kutumia huduma hiyo kama kawaida licha ya kudaiwa wastani wa dola za Marekani 65,000.CAG, Utouh alikaririwa akisema manunuzi katika shirika la Tanesco yalirekodiwa kimakosa na kwa udanganyifu.
Utouh alisema wakati wa ukaguzi, iligundulika kwamba Tanesco, hawakuwa wakifanya ‘reconciliation’ (upatanisho) ya mwezi kati ya mauzo na mapato.Kwa mujibu wa CAG, kuna hasara katika idara za uzalishaji na usambazaji wa umeme kwenda wateja.
“ Kuna mapendekezo niliyoyatoa yanayotakiwa kuchukuliwa hatua na Serikali, Bunge, Kamati ya Hesabu za Serikali, Bodi ya Wakurugenzi na maofisa watendaji wakuu kupitia ripoti ya fedha iliyoishia Juni 30,2009,” ilisema ripoti hiyo.
Katika ripoti hiyo, CAG alisema katika ripoti ya mwaka uliopita ya ukaguzi katika mamlaka za umma na bodi nyingine kuna mapendekezo 15 yaliyotolewa kwa utekelezaji: “Lakini hadi sasa mapendekezo hayo hayajatekelezwa kikamilifu.”
Alisema mapendekezo hayo ambayo hayajatekezwa yanahitaji ufumbuzi wa Serikali ili kuyawezesha mashirika mengine ya umma kufanya vizuri.
Badra Masoud, Meneja mahusiano wa Tanesco hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hiyo baada ya simu yake kuita muda wote bila kupokelewa huku simu ya Mkurugenzi wa Tanesco William Mhando ikiwa haipatikani.
CHANZO: Mwananchi