Ushushushu unaendelea kuwa ni moja ya taaluma hatari kabisa kwa maana ya kutembea na roho mkononi pindi mambo yakienda mrama. Tatizo kubwa la ushushushu sio kutoka kwa maadui wa nje (kwa maana ya taifa la nje au maadui wasio wa kitaifa- non-state actors) bali pia hata maadui wa ndani. Kiasili, migogoro au kukosana ni sehemu ya 'kawaida' katika maisha yetu wanadamu.
Mie katika familia yetu tumejaaliwa kuwa na mapacha. Vitinda mimba katika familia yetu ni Kulwa na Doto. Hawa walipishana kuzaliwa kwa dakika chache tu, na wamefanana mno kiasi kwamba ninapokutana nao baada ya kupotean kidogo tu inabidi niwaulize yupi ni Kulwa na yupi ni Doto. Pamoja na hali hiyo, kuna nyakati hutofautiana na hata kugombana.
Kwa mantiki hiyo, si suala la ajabu kwa mwajiriwa kukosana na mwajiriwa wake. Wakati kukosana na mwajiri wako katika taaluma nyingine kwaweza kupelekea kushushwa cheo, kuhamishwa au kupoteza ajira, kwa ushushushu hali ni tofauti kabisa. Kutibuana na mwajiri kwaweza kupelekea kifo, kama stori hii hapa chini inavyotanabaisha.
Ukisoma au kusikia balaa lililomwandama Alexander Litvinenko (pichani juu) hadi kifo chake, waweza kudhani ni simulizi kutoka kwenye filamu au riwaya flani. Litvinenko aliwa shushushu wa shirika la ushushushu la Russia, FSB, katika kitendo cha kubaliana na uhalifu mkubwa (organised crime). Kabla ya kuwa shushushu, Litvinenko alikuwa mwanajeshi ambapo alipanda cheo hadi kufikia ngazi ya ukamanda wa platuni.
Mwaka 1986, Litvinenko alianza kuingia kwenye taaluma ya ushushushu baada ya kuwa 'recruited' kuwa mtoa habari (informant) Shirika la zamani la ushushushu la Russia KGB, katika kitengo cha kupambana na ujasusi (counterintelligence). Miaka miwili baadaye, Litvinenko alihamishiwa rasmi KGB kwenye Kurugenzi Kuu ya Tatu iliyokuwa inahusika na military counterintelligence. Mwaka huohuo, baada ya kuhudhuria mafunzo ya ushushushu, Litvinenko akawa shushushu kamili katika eneo la kupambana na ujasusi hadi mwaka 1991, ambapo alipandishwa cheo na kuingia katika Federal Counterintelligence Service, shirika la ushushushu baada ya KGB, ambalo lilidumu kutoka mwaka 1991 hadi 1995lilipoundwa upya kuwa shirika la sasa la ushushushu la Russia yaani FSB. Shushushu huyo alipangiwa kitengo kilichohusika na kukabiliana na ugaidi sambamba na kujipenyeza (infiltration) kwenye makundi ya uhalifu mkubwa. Kadhalika, alikuwa na jukumu la kufuatilia 'maeneo ya moto' (hot spots), yaani maeneo nyeti ndani ya Russia na katika nchi znyingine zilizokuwa ndani ya USSR. Wakati wa vita ya Chechnya, Litvinenko alifanikiwa kupandikiza mashushushu kadhaa ndani ya Chechnya.
Mwaka 1994, Litvitenko alikutana na mmoja wa waliokuwa matajiri wakubwa nchini Russia, Boris Berezovsky (pichani chini) alipokuwa anafuatilia jaribio la mauaji dhidi ya tajiri huyo.
Hatimaye akaanza kufanya kazi za pembeni kwa ajili ya Boris, na baadaye akawa msimamizi mkuu wa ulinzi wa kibopa huyo. Ofkoz 'ajira' hiyo ya Litvitenko kwa tajiri huyo ilikuwa sio halali lakini dola iliwavumilia hasa ikizingatiwa kuwa mishahara ya mashushushu kama yeye ilikuwa kiduchu.
Mwaka 1997 shushushu huyo alipandishwa cheo na kuingia Kurugenzi ya Uchambuzi na Ukandamizaji wa makundi ya uhalifu mkubwa, akiwa na wadhifa wa mtendaji mwandamizi na naibu mkuu wa Idara ya Saba.
Mwishoni mwa mwaka huo, shushushu huyo alitoa tuhuma nzito kuwa alipewa amri ya kumuua Boris.Mwaka uliofuata, Boris alimtambulisha Litvinenko kwa Vladmir Putin, rais wa sasa wa Russia lakini wakati huo akiwa shushushu mwandamizi wa FSB.
Putin akiwa amezungukwa na walinzi wake |
Tatizo ni kwamba Litvinenko alikuwa akipeleleza ufisadi ambao Putin anadaiwa kuwa mhusika. Mwaka huohuo, shushushu huyo na baadhi ya wenzake wallijitokeza hadharani kueleza kuhusu njama za kutaka kumuuwa tajiri Boris.Baada ya tukio hilo, shushushu huyo alitimuliwa FSB na Putin alitanabaisha kuwa ndiye aliyetoa uamuzi huo.
Oktoba 2000, Litvinenko alitoroka Russia na familia yake na kwend Uturuki ambako aliomba hifadhi ya ukimbizi katika Ubalozi wa Marekani jijini Ankara lakini maombi yake yalikataliwa. Inaaminika kuwa kukataliwa huko kulitokana na hofu kuwa kuyakubali maombi hayo kungezua matatizo kati ya Marekani na Russia. Mwaka huohuo,shushushu huyo alinunua tiketi ya kusafiri kwa ndege kutoka Ankara kwenda Moscow kupitia London, Uingereza. Alipofika uwanja wa ndege wa Heatrhow kusbiri ndege ya kwenda Moscow, shushushu huyo aliomba hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa, ambapo maombi yake yalikubaliwa mwaka mmoja baadaye, si kwa sababu ya uelewa wake wa mambo ya ushushushu bali kwa sababu za kibinaadamu (humanitarian grounds).
Wakati akiwa London, Litivnenko alijihusisha na uandishi wa habari, sambamba na kumsapoti tajiri Boris (aliyekimbilia Uingereza) katika mapambano ya kiharakati dhidi ya utawala wa Putin. Oktoba 2006, shushushu huyo alipatiwa uraia wa Uingereza.
Wakati huohuo, gazeti la Independent la hapa, liliripoti kuwa Litvinenko alikuwa akitumia na shirika la ujasusi la Uingereza, MI6 kutokana na ushahidi wa malipo yaliyokuwa yakifanywa na shirika hilo kwa shushushu huyo.
Makao makuu ya shirika la ujasusi la Uingereza MI6 kwenye kingo za Mto Thames, eneo la Vauxhall, jijini London |
Mwaka 2007, gazeti moja la Poland lilidai kuwa picha ya Litvinenko ilikuwa ikitumika kwenye mazoezi ya kulenga shabaha (kama huelewi, hiyo ni ishara ya kuwindwa kuuawa). Kabla ya hapo, mwaka 2002, shushushu mmoja wa FSB, Mikhail Trepashkin, alimwonya Litvinenko kuwa kulikuwa na mpango wa kumuuwa uliokuwa ukiandaliwa na FSB. Mwaka huohuo, shushushu huyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za rushwa, japo alikuwa nje ya Russia.
Nembo ya Shirika la Ushushushu la Russia FSB |
Hata hivyo, wakati flani, wasifu wa shushushu huyo ulichafuka baada ya kupatikana taarifa kuwa alikuwa akiwatishia kuwaumbua matajiri kadhaa wa Russia kuhusu uhusika wao kwenye uhalifu mkubwa, na kudai pauni 10,000 kila mara ili asiwaumbue.
Wakati wa uhai wake, shushushu huyo alitoa tuhuma kadhaa dhidi ya Putin, Russia na mwajiri wake wa zamani FSB. Miongoni mwa tuhuma hjizo ni Russia kuhusika na mashambulizi katika bunge la Armenia yaliyopelekea kifo cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo Vazgen Sargsyan, FSB kufanya mauaji nchi Russia na kuwalaumu magaidi wa nje ili kupata uhalali wa kufanya ubabe nje ya nchi hiyo, mdai ya uhusiano kati ya Russia na Al-Qaeda, nk.
Novemba 2006, Litvinenko aliugua ghafla na kulazwa. Baadaye, vipimo vilibaini kuwa alidhuriwa kwa kemikali ya sumu ya Radionuclide Polonium-210.
Litvinenko akiwa hospitalini jijini London baada ya kudhuriwa na sumu |
Katika mahojiano, shushushu huyo alieleza kuwa alikutana na mashushushu wawili wa FSB Dmitry Kovtun na Andrei Lugovoi.Japo wote wawili walikanusha kumdhuru shushushu mwenzao, nyaraka zilizovuja za Ubalozi wa Marekani zinaeleza kuwa chembechembe za kemikali iliyomdhuru Litvinenko zilikutwa kwenye gari alilotumia Kovtun huko Ujerumani.
Andrei Lugovoy (kushoto) na Dmitr Kovtun |
Baadaye mwezi huo, Litvinenko alifariki baada ya moyo wake kushindwa kufanya kazi kutokana na sumu iliyomdhuru. Kabla ya kifo chake, shushushu huyo aliandika taarifa iliyoeleza ameuawa.
Juzi, taarifa ya uchunguzi wa kifo chake ilieleza kuwa njia iliyotumika kumuuwa ilikuwa ni ya hatari zaidi kutokea katika Nchi za Magharibi.
Dokta Nathaniel Cary alieleza kuwa kifo cha shushushu huyo mwili wake ulidhurika vibaya mno kabla ya kifo chake kiasi kwamba ililazimu awekwe katika wodi maalum amapo wagonjwa hutengwa kwa ajili ya uchunguzi wa hali ya juu. Alisema kuwa shushushu huyo aliuawa kwa mionzi ya sumu. Kifo chake kilitokea takriban wiki tatu baada ya kunywa chai ambayo baadaye ilifahamika kuwa ilinyunyiziwa sumu ya Polonium.
Dokta Cary alieleza kuwa yye na timu yake walilazimika kuvaa suti mbili za kujikinga (kama zile za matabibu wa Ebola) ambazo ziliwekwa hewa ndanikupitia mirija maalum ili kukwepa athari za sumu husika. Alisema, "uchunguzi huo wa maiti ulikuwa ni usio wa kawaida kabisa katika historia ya nchi za Magharibi"
Natumaini habari hii imekusaidia msomaji kutambua hatari zinazowakabili mashushushu katika utendaji kazi wao, na hasa pale 'wanapotibuana' na aidha waajiri wao au watawala.