Asalam aleykum,
Katika makala yangu iliyopita,nilizungumzia kuhusu kile ambacho wachambuzi wa siasa za kimataifa wanakiona kama kurejea kwa kasi kwa mbio za silaha (arms race) zenye uwezo mkubwa na wa kisasa zaidi kuliko hapo awali au sasa.Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeonekana kuguswa na namna Russia inavyoongeza kasi katika teknolojia na uzalishaji wa silaha za kisasa.Muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii,nimeona taarifa moja inayoeleza kuwa Russia imefanikiwa kufanya majaribio ya kile inachokiita “Baba wa Mabomu Yote” (Father of all Bombs).Teknolojia hiyo mpya inaelezwa kuwa na uwezo mara nne zaidi ya ile ya Marekani inayojulikana kama “GBU-43 Massive Ordnance Air Blast” (MOAB) au “Mother of all Bombs” (yaani “Mama wa Mabomu Yote”) ambayo ilifanyiwa majaribio yenye mafanikio mwaka 2003.Tofauti na teknolojia ya awali ya mabomu,hilo la kisasa la Russia ni la “thermobaric,” yaani linatumia oksijeni iliyopo hewani (atmospheric oxygen) kusababisha mlipuko badala ya kutumia kemikali nyingine (oxidizing agent) kuleta matokeo hayo (mlipuko).Silaha za ki-“thermobaric” zina tabia ya kutoa nishati kubwa zaidi kuliko zile zisizotumia teknolojia hiyo,na inaelezwa kwamba bomu hilo jipya la Russia lina uwezo wa kuteketeza kabisa maisha katika eneo mzunguko la maili nne.
Kinachochochea mbio za silaha ni sawa na kile wanafalsafa wanachokiita “domino effect” yaani badiliko (change) moja linapelekea badiliko jingine jirani,nalo linapekea badiliko jingine,na jingine kwa jingine,na kadhalika.Yaani ni kama kugongwa gari la kwanza kwenye foleni ndefu ambapo la kwanza litaligonga la pili,la pili litaligonga la tatu,na kadhalika,na kadhalika.Kwa Russia kutambulisha mafanikio yake hayo,ni dhahiri kwamba Wamarekani nao watakuna vichwa ili waibuke na teknolojia kali zaidi ya hiyo ya Russia (pengine wataamua kuiita “babu wa mabomu yote” maana tayari tuna “baba” na “mama,” na si ajabu Russia nao watajibu mapigo kwa kuja na “bibi wa mabomu yote”).Wajuzi wa mambo wanadai kuwa miongoni mwa mambo yanayoichochea Russia kuelekeza nguvu zake kwenye uboreshaji wa teknolojia ya silaha ni faida kubwa inayopata nchi hiyo kwenye biashara ya mafuta na gesi,na ukweli kwamba Rais Putin alikuwa shushushu mwandamizi ndani ya shirika la kijasusi la uliokuwa Muungano wa Jamuhuri za Kisovieti (USSR) ambapo shirika hilo lilikuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya teknolojia ya silaha.
Habari nyingine “nyepesi” kutoka Russia zinasema kwamba jiji la Ulyanovsk nchini humo limetoa “off” kwa wafanyakazi wote ili wapate fursa ya kufanya tendo la ndoa katika maadhimisho ya “Siku ya Kutunga Mimba jijini Ulyanovsk” (the Day of Conception in Ulyanovsk).Ruhusa hiyo ya mapumziko imetolewa kama sehemu ya mpango wa manispaa ya jiji hilo ujulikanao kama “Give Birth to a Patriot” (Zaa Mzalendo) ambapo watakaofanikiwa kudunga au kudungwa wanaweza kuibuka na zawadi ya gari,fedha au friji.Jiji hilo ndipo alipozaliwa Vladmir Lennin, na mpango huo wa kuhamasisha uzazi ni sehemu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Lenin mwezi huu.Washindi wanatarajiwa kupatikana kwa kuzingatia heshima ya ndoa yao pamoja na sifa bora kama wazazi,na watapatikana kutokana na maamuzi ya jopo la majaji.Mambo hayo!!
Kabla ya kugeukia masuala ya huko nyumbani,ngoja nizungumzie suala moja ambalo mie binafsi linanigusa.Nilipokuwa Mlimani (UDSM) nilibahatika kuchukua somo liitwalo “Gender and Family Relations” (yaani Jinsia na Mahusiano ya familia).Naomba kukiri kwamba kabla ya hapo,sikuwa na uelewa wa kutosha kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii na picha nzima ya usawa wa kijinsia katika jamii mbalimbali.Sasa majuzi nilisoma gazeti la Guardian la hapa Uingereza na kukutana na habari isemayo kwamba serikali (ya hapa) ina mpango wa kuwachukulia hatua wanaume wanaonunua huduma ya ngono.Kimsingi,huduma nyingi,ikiwemo ngono,huhusisha mtoaji huduma na mpokeaji huduma,lakini katika dunia yetu ambayo tumezowea kuyaona makosa ya wanawake pekee ilhali yetu wanaume yakionekana ni ya “ya kishujaa,” suala la ukahaba limeendelea kwa kiasi kikubwa kuwa kosa la wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo kuliko wateja wao ambao ni wanaume (hapa sizungumzii ukahaba kati ya watu wa jinsia moja).Neno “malaya” ni maarufu zaidi kuliko neno “fuska” na baadhi ya wachambuzi wa mahusiano ya jamii wanadai hiyo inasababishwa na tabia ya kuona matendo hasi (negative) ya mwanamke kuwa mabaya zaidi ya yale hasi ya mwanaume.Hata linapokuja suala la nyumba ndogo,tunashuhudia kuwa ni rahisi kwa mwanaume kuwa nazo hata 10 kama ana uwezo wa kuzimudu lakini mwanamke akijaribu hilo basi muda si mrefu anaweza kujikuta anafungashiwa virago vyake.Nchi za Magharibi zimepiga hatua flani katika kuleta usawa wa kijinsia,na miongoni mwa mitihani mikubwa katika eneo hilo ni ugombea (candidacy) wa Hillary Clinton kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat.Na mshawasha zaidi unaeletwa na mgombea mwingine kutoka jamii ambayo hadi sasa bado inaonekana ni ya kuongozwa zaidi badala ya kuongeza,yaani watu weusi (Blacks).Historia inasubiri kuandikwa iwapo Hillary atafanikiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Marekani,au Barack Obama atafanikiwa kuwa Mweusi wa kwanza kuwa rais.Bibi,mama na dada zetu wanastahili pongezi (au hukumu) sawa na sie akina kaka,baba na babu.
Sasa mambo ya huko nyumbani.Nilipigwa na butwaa niliposoma habari katika gazeti moja la nyumbani kuwa huko Mwanza kampeni za kugombea uongozi wa CCM ziligeuka kuwa uwanja wa vita pale washabiki wa kambi za wagombea flani walipoamua “kufanyiana kweli” na kutupiana mawe.Sijui wangapi walijeruhiwa katika patashika hiyo lakini nachoshindwa kuelewa ni namna kila raslimali,ikiwemo vurugu,inavyotumika kutafuta uongozi wa kisiasa.Hivi kuna nini huko kwenye uongozi hadi watu watake kutoana roho?Yaani ukereketwa umekolea namna hiyo hadi watu wawe tayari kuweka rehani usalama wao kwa ajili ya mgombea flani?Cha kusikitisha ni kwamba si ajabu wapambe hawa hawa ndio watakuwa wa kwanza kulalamika kuwa mgombea wao “hafai” pale atapowatelekeza baada ya kupata anachohitaji (uongozi).Pasipo busara za haraka kutumika tunaweza kujiwekea katika mahali pabaya sana kama tutawaruhusu baadhi ya watu kuhatarisha amani kwa vile tu wanataka kupata uongozi.
Nimesoma pia ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM,Philip Mangula,ambaye baada ya kubwagwa huko Iringa alitahadharisha kwamba kuna wakati itafika uongozi wa chama hicho utagombewa kwa mfumo wa tenda (bid) na “bidder” mkubwa ndiye atakayeibuka kidedea.Pengine ana hoja ya msingi hapo,lakini inaweza kufunikwa na ukweli kwamba haya anayoyaona sasa yamekuwa yakitokea kwa muda mrefu,na kipindi hicho alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya sio tu kukosoa bali hata kukomesha matumizi ya “takrima” kwenye kusaka uongozi.Hata wazo lake kwamba ni vema kwa wanachama wa CCM wenye madaraka mengine (kama ubunge au uwaziri) wakatoa mwanya kwa wale wasio na madaraka (japo sio kosa,si ajabu baada ya uchaguzi huu kumkuta mtu akiwa na vyeo zaidi vitano) mawazo hayo yangekuwa na “mwangwi” mkubwa zaidi iwapo yangetolewa katika kipindi ambacho Mangula alikuwa madarakani.Yayumkinika kusema kuwa ni vigumu kurekebisha mapishi pindi ukiwa nje ya jiko,na majaribio ya kufanya hivyo nje ya jiko yanaweza kutafsiriwa tofauti na baadhi ya watu.
Na huko Morogoro,baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa miongoni mwa nafasi katika mkoa huo,Waziri Ngasongwa nae “aliwatolea macho” TAKUKURU kwa kile alichodai walishindwa kuzuwia baadhi ya wagombea kutoa “takrima” kwa wapiga kura.Swali pana zaidi ni je waziri anadhani taasisi hiyo ilishindwa (kwa mujibu wake) kutekeleza majukumu yake kwa vile ni sehemu ya mapungufu yake ya kila siku au ni katika tukio hilo tu?Iwapo jibu ni hilo la pili basi wapo wanaoweza kuhisi kuwa waziri ameweza kuona matatizo hayo kwa vile tu yamemgusa yeye binafsi. “Bottom line” ni kwamba iwapo mlolongo wa vimbwanga vinavyoendelea kwenye uchaguzi wa CCM vitachukuliwa kuwa ni mambo ya kawaida tu basi tunaweza kufika mahala tukajilaumu huku tukisema “laiti tungejua wakati ule…”Bahati mbaya,kwa wakati huo tutakuwa tumechelewa kuweza kufanya mabadiliko yoyote ya msingi.Ushauri huu sio wa kupandikiza chuki bali ni kwa ajili ya hatma ya taifa letu kwa manufaa yetu sasa na kwa vizazi vijavyo.
Neno la mwisho kabisa ni kuungana na wapenzi na mashabiki wa msanii maarufu anti Shenaz ambaye alikutana na mauti kwenye ajali ya basi huko Mbeya.Kwa tunaomfahamu,dada huyo alikuwa akipendezesha kila shughuli aliyokuwepo.Na tofauti na umaarufu wake,alikuwa mcheshi na asiye na chembe ya dharau.Mungu airehemu roho ya marehemu,Amina.
Alamsiki