Showing posts with label TANZANIAN DAIMA. Show all posts
Showing posts with label TANZANIAN DAIMA. Show all posts

18 Jan 2008


Nimekuwa mwandishi wa makala magazetini tangu mwaka 1998,takriban miaka 10 sasa.Mtu aliyenipa changamoto la kufanya hivyo anaitwa Albert Memba,mwandishi wa zamani wa habari za michezo katika gazeti la Nipashe na Guardian.Huyu jamaa anaimudu lugha vilivyo.Nilianzaia kwenye magazeti "ya udaku" kama Sanifu (lilifariki zamani hizo) na baadaye Kasheshe na Komesha,ambako nilikuwa naandika unajimu "wa kuchekesha usio na chembe ya ukweli" (tuuite humorous horoscope) kwa kutumia jina la uandishi Ustaadh Bonge (hadi leo baadhi ya rafiki zangu wanaendelea kuniita hivyo).Baadaye nikamahimia kwenye uandishi wa makala za mambo muhimu zaidi ya vichekesho na udaku.Anyway,ni hadithi ndefu.

Nilipata wazo la ku-blog katikati ya mwaka juzi.Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintampongeza Ndesanjo Macha,kwani mwongozo wake wa namna ya kuanzisha blogu ndio ulionifanya niwe hapa nilipo.Wazo la kuanzisha blog hii lilitokana na ukweli kwamba gazeti lililokuwa linatoa makala zangu halikuwa na tovuti,hivyo awali blog hii ilikuwa kwa ajili ya kuwawezesha watu wote wanaojua Kiswahili popote walipo duniani wapate fursa ya kusoma makala hizo ambazo hazikuwa mtandaoni.Baadaye nikatanua wigo wa uandishi wa makala kwa kuanza kuandika kwenye magazeti ya Mtanzania na Raia Mwema ambako makala zangu hutoka mara moja kwa wiki.

Mmmoja ya watu waliosaidia sana kuitangaza blog ni hii ni rafiki yangu Haki Ngowi.Huyu hana hiana linapokuja suala la kupromoti blog ya bloga mwenzie.Nakumbuka waungwana flani waliwahi "kunitosa" nilipowatumia ombi la kubadilishana vinganishi (exchange links) kwa vile sikuwa naendana na maudhui ya blog yao.Nawashukuru kwani walinipa changamoto kubwa sana.

Mie ni muumini wa msemo "beauty should never be imprisoned",kitu kizuri shurti kisifiwe.Lakini mpewa sifa asibweteke bali anapaswa kuendeleza jitihada (sio kwa ajili ya kupata sifa zaidi) bali kuhalalisha kwamba waliompa sifa hapo awali hawakuwa "wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa",au kwa lugha ya mtaani, hawakuwa "wanamzuga".Nawashukuru nyote mnaonitumia barua-pepe za pongezi kuhusu makala zinazotoka kwenye magazeti nayoandikia pamona na zile zinazotoka kwenye blog hii.Nyie ndio chachu ya ya mafanikio ya makala hizo.

Nina tabia moja ambayo imenitengenezra marafiki na maadui wengi,nayo ni kusema ukweli.Huwa sioni aibu kukiri kwamba nimejifunza kitu flani kutoka mahala flani,kama ambavyo huwa sioni dhambi kumkosoa mtu naedhani amekosea jambo flani.Huko nyuma nilishawahi kuingia kwenye mgogoro na kampuni flani ya magazeti kwa vile tu niliwakosoa pale nilipoona wamepotoka.Tofauti na matarajio yangu,waungwana hao wakaanza kuhoji kuhusu maendeleo yangu ya elimu.Binafsi,huwa sipendi kabisa majadiliano kuhusu masuala ya shule yangu kwani naamini ni suala binafsi (only exception,ni pale majadiliano hayo yanapokuwa ya kitaaluma).

Kuna bloga anaitwa Mpayukaji Msemaovyo.Laiti kungekuwa na mashindano ya kutafuta blogu zenye "kiwango cha juu cha uchungu kwa nchi" basi naamini Mpayukaji angekamata nafasi ya juu kabisa.Simsifii kwa vile tu napenda anachaondika,bali ni ukweli kwamba blog yake imekuwa ni darasa zuri kwangu kujifunza "uchungu kwa nchi yangu na mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi".Uzuri wa makala za Mpayukaji,ambazo hupatikana pia kwenye gazeti la Tanzania Daima,ni ile tabia yake ya kuliita jiwe ni jiwe na sio tofali (calling a spade a spade).Unajua,kuna kusifia kitu kwa matarajio ya kupewa asante flani (kitu ambacho nakipinga kwa nguvu zote) na kuna kusifia kitu kwa vile kina kila sababu ya kusifiwa,na hicho ndicho nachokifanya hapa.Kuna wakati huwa nasoma makala za Mpayukaji huko Tanzania Daima mpaka najikuta naijiwa na taswira ya nyuso za mafisadi zinavyokunjamana kwa hasira iliyochanganyika na aibu+maumivu (truth pains) kutokana na uzito wa hoja za Mpayukaji.

Nitaendelea kuwapongeza waandishi na bloggers wengine ambao wanawatumia Watanzania kwa upenyo huu "mpya" uliojitokeza (mtandao) kuwasilisha vilio,kero,manung'uniko,lawama na hata pongezi kuhusu taifa letu.Pia nitaendela kuwapongeza wenzetu wanaotuletea habari kwa njia ya picha kwani taswira (image) inaweza kuwakilisha maneno elfu kadhaa kwa wakati mmoja.

(Picha ya Mpayukaji nimeipata kutoka kwenye profile ya blogu yake pasipo idhini yake,nitaomba idhini baadaye).

Almanusura nisahau.Hivi huko nyumbani watoto wangapi wanaoamua kutoroka majumbani kwao kutokana na sababu moja au nyingine?Je kuna mahauzigeli wangapi wanaoamua kutoroka kwa waajiri wao kutokana na manyanyaso yaliyopita kiasi?Katika mfumo ambao mnyonge licha ya kutokuwa na haki ananyang'anywa hata ile haki ndogo aliyozaliwa nayo (utu),kundi hili linabaki kuwa halina mtetezi.Clip hii ya Ludacris ft Mary J. Blidge katika wimbo Runaway Love inaweza kutukumbusha wajibu wetu kama jamii


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.