Showing posts with label LUDACRIS. Show all posts
Showing posts with label LUDACRIS. Show all posts

24 Jan 2008

Alfajiri hii nimepata barua-pepe kutoka kwa mtu mmoja anayeelekea kuumia moyo kwa namna navyoshutumu ufisadi na mafisadi.Mzembe huyo ametoa shutuma lukuki kuhusu makala zangu magazetini na humu "bloguni" kuhusiana na suala la ufisadi.Kwa kutompa ujiko aliokuwa anatafuta,nimeamua kupuuza barua-pepe hiyo na sikumjibu.Binafsi,nilikuwa natambua bayana kwamba mafisadi wameshabaini kwamba mtandao una nguvu pengine zaidi ya magazeti yetu huko nyumbani,hasa ikizingatiwa kwamba ni machache tu yaliyopo kwenye mtandao.Mapepe aliyeniandikia barua-pepe amejitahidi kadri ya uwezo wake mdogo alionao kuni-discourage kuandika chochote dhidi ya mafisadi,huku akidai kwamba sie tulio ughaibuni tuna tabia ya kujifanya tunajua kila kitu (cha ajabu ni kwamba naye anadai yuko ughaibuni,tena hapahapa Uingereza).

Sitaki kuifanya case yangu kuwa universal lakini naamini kwamba teknolojia ya habari kupitia mtandao imetokea kuwa silaha kubwa dhidi ya wanyonge na wakati huohuo ikiwa mwiba mkali dhidi ya ufisadi na mafisadi.Kuna watakaopambana nasi tunaopigia kelele ufisadi kwa vile wao ni vibaraka wa mafisadi na wengine watasigishana nasi kwa vile wao wenyewe ni mafisadi.Wito wangu kwa wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wameamua kusimama kidete kupigania haki na usawa kwa kila Mtanzania,Mwafrika na raia wengine wa dunia wanaonaoporwa stahili zao,ni huu:kila kelele ya fisadi itafsiriwe kama full tank za mafuta ya mtambo wa kukabiliana na maovu kwenye jamii.

Kwa fisadi "wangu" Mapepe,pokea zawadi hii kutoka kwa Ludacris kwenye clip ya Get Back (Caution: explicit lyrics)


20 Jan 2008

Siku chache zilizopita,ndege aina ya Boeing 777 ya British Airways ilinusukirka kusababisha maafa makubwa baada ya kupata matatizo wakati linajiaandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Heathrow.Marubani na wafanyakazi wengine wa ndege hiyo (iliyokuwa na abiria 152) waliibuka mashujaa kwa namna walivyoweza kuepusha balaa hilo.Kwa mujibu wa takwimu zilizopo,uwanja huo wa Heathrow ni wa tatu duniani kwa idadi ya abiria nyuma ya Hartsfield-Jackson Atlanta International Airport na O'Hare International Airport (vyote vya Marekani).Ukweli kwamba uwanja wa Heathrow uko pembezoni (magharibi) kidogo tu ya katikati ya jiji la London,inamaanisha kwamba laiti ndege hiyo ingeanguka kungetokea maafa makubwa.

Awali pongezi nyingi zilikuwa zikielekezwa kwa rubani mkuu wa ndege hiyo,Kapteni Peter Burkill,lakini alipohojiwa kwenye mkutano na vyombo vya habari alieleza kwamba shujaa halisi alikuwa rubani msaidizi ambaye ndiye aliyekuwa kwenye "usukani" wakati ndege hiyo inahangaika kutua,na alitumia jitihada zake zote kuepusha maafa makubwa.Kichekesho ni kwamba kwa Kiswahili jina la shujaa huyo ni MSALITI,anaitwa John COWARD.Baadhi ya magazeti yakapata element ya kuchekesha katika habari hizo kwa vichwa vya habari kama hiki (kwenye gazeti la The Daily Mail):A Hero Called Coward (yaani "shujaa aitwaye msaliti")

Lakini kama hiyo haitoshi,moja ya magazeti ya udaku ya hapa,News of The World,leo limetoa picha za zamani za Kapteni Burkill akiwa nusu mtupu wakati anakula maraha kwenye likizo nchini Marekani.Katika baadhi ya picha hizo,rubani huyo anaonekana akiwa amemwagiwa chokoleti huku akinadada wawili wakijibidiisha kumlamba.Katika moja ya vimbwanga hivyo,rubani huyo ambaye wakati ho alikuwa mwajiriwa wa shirika la ndege la Caledonian,alilazwa sakafuni na chokoleti kumwagwa kwenye makali yake katika mchezo uliolenga kufananisha suala la kuendesha ndege.

Clip hii ya Ludacris ft Nate Dogg katika wimbo Area Codes inaweza kuwa mwafaka kwa stori hii ya ndege na airports (Caution: explicit lyrics)18 Jan 2008


Nimekuwa mwandishi wa makala magazetini tangu mwaka 1998,takriban miaka 10 sasa.Mtu aliyenipa changamoto la kufanya hivyo anaitwa Albert Memba,mwandishi wa zamani wa habari za michezo katika gazeti la Nipashe na Guardian.Huyu jamaa anaimudu lugha vilivyo.Nilianzaia kwenye magazeti "ya udaku" kama Sanifu (lilifariki zamani hizo) na baadaye Kasheshe na Komesha,ambako nilikuwa naandika unajimu "wa kuchekesha usio na chembe ya ukweli" (tuuite humorous horoscope) kwa kutumia jina la uandishi Ustaadh Bonge (hadi leo baadhi ya rafiki zangu wanaendelea kuniita hivyo).Baadaye nikamahimia kwenye uandishi wa makala za mambo muhimu zaidi ya vichekesho na udaku.Anyway,ni hadithi ndefu.

Nilipata wazo la ku-blog katikati ya mwaka juzi.Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintampongeza Ndesanjo Macha,kwani mwongozo wake wa namna ya kuanzisha blogu ndio ulionifanya niwe hapa nilipo.Wazo la kuanzisha blog hii lilitokana na ukweli kwamba gazeti lililokuwa linatoa makala zangu halikuwa na tovuti,hivyo awali blog hii ilikuwa kwa ajili ya kuwawezesha watu wote wanaojua Kiswahili popote walipo duniani wapate fursa ya kusoma makala hizo ambazo hazikuwa mtandaoni.Baadaye nikatanua wigo wa uandishi wa makala kwa kuanza kuandika kwenye magazeti ya Mtanzania na Raia Mwema ambako makala zangu hutoka mara moja kwa wiki.

Mmmoja ya watu waliosaidia sana kuitangaza blog ni hii ni rafiki yangu Haki Ngowi.Huyu hana hiana linapokuja suala la kupromoti blog ya bloga mwenzie.Nakumbuka waungwana flani waliwahi "kunitosa" nilipowatumia ombi la kubadilishana vinganishi (exchange links) kwa vile sikuwa naendana na maudhui ya blog yao.Nawashukuru kwani walinipa changamoto kubwa sana.

Mie ni muumini wa msemo "beauty should never be imprisoned",kitu kizuri shurti kisifiwe.Lakini mpewa sifa asibweteke bali anapaswa kuendeleza jitihada (sio kwa ajili ya kupata sifa zaidi) bali kuhalalisha kwamba waliompa sifa hapo awali hawakuwa "wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa",au kwa lugha ya mtaani, hawakuwa "wanamzuga".Nawashukuru nyote mnaonitumia barua-pepe za pongezi kuhusu makala zinazotoka kwenye magazeti nayoandikia pamona na zile zinazotoka kwenye blog hii.Nyie ndio chachu ya ya mafanikio ya makala hizo.

Nina tabia moja ambayo imenitengenezra marafiki na maadui wengi,nayo ni kusema ukweli.Huwa sioni aibu kukiri kwamba nimejifunza kitu flani kutoka mahala flani,kama ambavyo huwa sioni dhambi kumkosoa mtu naedhani amekosea jambo flani.Huko nyuma nilishawahi kuingia kwenye mgogoro na kampuni flani ya magazeti kwa vile tu niliwakosoa pale nilipoona wamepotoka.Tofauti na matarajio yangu,waungwana hao wakaanza kuhoji kuhusu maendeleo yangu ya elimu.Binafsi,huwa sipendi kabisa majadiliano kuhusu masuala ya shule yangu kwani naamini ni suala binafsi (only exception,ni pale majadiliano hayo yanapokuwa ya kitaaluma).

Kuna bloga anaitwa Mpayukaji Msemaovyo.Laiti kungekuwa na mashindano ya kutafuta blogu zenye "kiwango cha juu cha uchungu kwa nchi" basi naamini Mpayukaji angekamata nafasi ya juu kabisa.Simsifii kwa vile tu napenda anachaondika,bali ni ukweli kwamba blog yake imekuwa ni darasa zuri kwangu kujifunza "uchungu kwa nchi yangu na mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi".Uzuri wa makala za Mpayukaji,ambazo hupatikana pia kwenye gazeti la Tanzania Daima,ni ile tabia yake ya kuliita jiwe ni jiwe na sio tofali (calling a spade a spade).Unajua,kuna kusifia kitu kwa matarajio ya kupewa asante flani (kitu ambacho nakipinga kwa nguvu zote) na kuna kusifia kitu kwa vile kina kila sababu ya kusifiwa,na hicho ndicho nachokifanya hapa.Kuna wakati huwa nasoma makala za Mpayukaji huko Tanzania Daima mpaka najikuta naijiwa na taswira ya nyuso za mafisadi zinavyokunjamana kwa hasira iliyochanganyika na aibu+maumivu (truth pains) kutokana na uzito wa hoja za Mpayukaji.

Nitaendelea kuwapongeza waandishi na bloggers wengine ambao wanawatumia Watanzania kwa upenyo huu "mpya" uliojitokeza (mtandao) kuwasilisha vilio,kero,manung'uniko,lawama na hata pongezi kuhusu taifa letu.Pia nitaendela kuwapongeza wenzetu wanaotuletea habari kwa njia ya picha kwani taswira (image) inaweza kuwakilisha maneno elfu kadhaa kwa wakati mmoja.

(Picha ya Mpayukaji nimeipata kutoka kwenye profile ya blogu yake pasipo idhini yake,nitaomba idhini baadaye).

Almanusura nisahau.Hivi huko nyumbani watoto wangapi wanaoamua kutoroka majumbani kwao kutokana na sababu moja au nyingine?Je kuna mahauzigeli wangapi wanaoamua kutoroka kwa waajiri wao kutokana na manyanyaso yaliyopita kiasi?Katika mfumo ambao mnyonge licha ya kutokuwa na haki ananyang'anywa hata ile haki ndogo aliyozaliwa nayo (utu),kundi hili linabaki kuwa halina mtetezi.Clip hii ya Ludacris ft Mary J. Blidge katika wimbo Runaway Love inaweza kutukumbusha wajibu wetu kama jamii


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.