Mali za ATCL zakamatwa
Benki ya Stanbic Tanzania Limited, Makao Makuu ya Kinondoni, Dar es Salaam, inayashikilia magari sita ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), baada ya kushindwa kulipa deni la Sh bilioni mbili iliyochukua kama mkopo.
Fedha hizo zinazodaiwa kushindwa kulipwa kwa miezi miwili sasa zilikopwa na wafanyakazi wa kampuni kwa mikopo na kutokana na kushindwa kuwalipa mishahara watumishi wake, makato ya kila mwezi yameshindikana kukatwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka ATCL na katika benki hiyo jana zilithibitisha kushikiliwa kwa magari matano aina ya Toyota Land Cruiser VX, kuanzia Jumanne jioni wiki iliyopita na gari la sita limekamatwa likiwa mjini Moshi, Kilimanjaro na lilipelekwa katika benki hiyo jana na kufanya idadi ya magari hayo kuwa sita.
Namba za magari hayo ambazo ‘HabariLeo’ jana ilizipata katika eneo la chini la maegesho yalikohifadhiwa magari hayo japo uongozi wa benki uliokuwapo haukuwa tayari kuzungumza kwa madai kuwa msemaji yupo likizo, ni SU 37079, SU 37081, SU 37082, SU 37086, SU 37083 na lililofikishwa jana ni SU 37084.
Habari zaidi kutoka eneo la benki yalikohifadhiwa magari hayo zilieleza jana kuwa yataendelea kushikiliwa mpaka deni hilo lililipwe na uamuzi huo ulifikiwa baada ya hofu kuwa huenda kampuni hiyo ikafa na hivyo benki hiyo ikakosa kila kitu.
Gazeti hili lilifika makao makuu ya Stanbic makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni, na mhudumu wa mapokezi alieleza kuwa wasemaji waliokuwapo hawakuwa tayari kulizungumzia, na mwenye dhamana ya kutoa taarifa hiyo ni Mkurugenzi Mkuu, Bashir Awale, yuko likizo.
Hata hivyo, taarifa za ndani ya benki hiyo zililieleza gazeti hili kuwa deni wanaloidai ATCL ni Sh bilioni mbili kwa mwezi huu na kwamba uamuzi wa haraka ulichukuliwa baada ya akaunti ya kampuni hiyo kwa benki hiyo kuonyesha haina fedha za kulipa deni hilo wala haitarajii kuwa nazo kwa siku za karibuni.
Chanzo chetu cha habari ndani ya ATCL kilieleza kuwa magari hayo yalikamatwa tangu wiki iliyopita isipokuwa la Mkurugenzi Mtendaji ATCL, David Mattaka. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL, Balozi Mustafa Nyang’anyi, alithibitisha jana kupata taarifa ya kukamatwa kwa magari hayo na ameitisha kikao cha dharura kitakachokaa leo makao makuu ya kampuni hiyo.
Alisema pamoja na suala hilo, pia watajadili mambo mengine likiwamo la kurejeshewa leseni ya kurusha ndege waliyonyang’anywa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Desemba 8, mwaka huu.
ATCL ilinyan’ganywa leseni hiyo baada ya kubainika kuwa na dosari za kiufundi zinazosababisha kutokuwa na viwango stahili vya kiusalama vya kuwaruhusu kurusha ndege; ukaguzi uliowataka warekebishe dosari hizo ulifanywa Oktoba mwaka jana na leseni hiyo iliisha kazi tangu Aprili mwaka huu, lakini walikuwa wakiongezewa muda mpaka iliposhindikana wakanyang’anywa leseni hiyo.
“Hilo jambo na mimi nimepewa taarifa, lakini kusema ni kiasi gani au ni deni linahusu nini, mimi siyo menejimenti, mpigie Mattaka, ila ninachoweza kusema ni kwamba deni hilo si kitu cha ajabu maana tulikabidhiwa kampuni na deni la shilingi bilioni kumi na tisa,” alisema Balozi Nyang’anyi na kuongeza: “Ufafanuzi zaidi sina.
Mnashangaa hilo, kuna na la BP, pia waliokuwa wanatusambazia chakula kwenye ndege… na mengine mengi, yote hayo tutayajadili kesho katika kikao cha dharura na menejimenti nilichokiitisha, tutazungumza hayo na mengine mengi.”
Alisema katika kikao hicho pia watazungumzia mishahara ya wafanyakazi ambayo mpaka jana walikuwa hawajapata na pia kupanga namna ya kurudi tena katika uzalishaji mara watakaporejeshewa leseni ya kurusha ndege tena.
Mattaka alipoulizwa jana kuhusu kushikiliwa kwa magari, alikanusha kwa kudai taarifa hizo si za kweli, lakini alikiri kuwapo kwa kikao cha Bodi na Menejimenti alichokiita kuwa ni kikao cha kawaida si cha dharura. “Hizo habari umetoa wapi? Si kweli, nasema si kweli?” alisema huku mwandishi akiendelea kumhoji.
“Kuhusu kikao ni kweli kipo, lakini si cha dharura, ni cha kawaida……naomba unitafute kesho baada ya kikao kuhusu hilo unalotaka kujua,” alisema Mattaka. Hivi sasa TCAA inaendelea kupitia nyaraka za ATCL na kuna taarifa kuwa leo w.anaenda kukagua namna ya wafanyakazi wa kitengo cha dharura ndani ya ndege wanavyoweza kuchukua hatua pindi tatizo linapotokea.