25 Nov 2013
24 Nov 2013

KAMA nilivyoahidi katika makala yangu ndani ya toleo lililopita la gazeti hili maridhawa, wiki hii nitafanya uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015.
Kwa wanaofuatilia safu hii, niliwahi kugusia mada hii katika toleo la Oktoba 26, 2011 ikibeba kichwa cha habari “Mizengwe na mitego ya mgombea urais kutoka CCM.” Mengi yametokea kati ya wakati huo na sasa, na kwa vile Uchaguzi Mkuu unazidi kujongea, nimeona ni muhimu kurejea tena mada hii.
Pengine msomaji unaweza kubaini mabadiliko kidogo katika mtizamo wangu kuhusu uwezekano wa CCM kung’oka madarakani 2015. Ninaomba kukiri kwamba chokochoko zisizo na msingi zinazoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani (na tegemeo la wengi kuiondoa CCM madarakani, CHADEMA, zinanifanya nikubaliane na ukweli mchungu kuwa fursa za chama tawala kushinda tena katika uchaguzi mkuu ujao zinazidi kuongezeka.
Na moja ya mambo ya kusikitisha zaidi kuhusu CHADEMA ni kuibuka kwa kundi la ‘wahuni wa kisiasa’ waliojipachika joho la uanaharakati. Kwa wababaishaji hao, kuanza kukubalika kwa chama hicho kumetoa fursa kwao kufahamika kwa namna moja au nyingine. Ni tatizo lilelile sugu katika jamii yetu la kusaka umaarufu hata kwa mambo ya kipuuzi, Waingereza wanasema ‘famous for nothing.’
Sasa ‘wahuni’ hawa wamebinafsisha ajenda ya CHADEMA kupambana na ufisadi na kujipa hakimiliki kuwa wao pekee ndio wenye uelewa na mbinu za kukiwezesha chama hicho kufanikisha ajenda hiyo. Pasi kujali madhara ya uhuni wao kwa hatma ya chama hicho, wamejikuta wakitumiwa na maadui wa CHADEMA kwa njia isiyo ya moja kwa moja - kwa ‘remote control.’
Lakini kuashiria kuwa chama hicho kina wakati mgumu japo uongozi wake wa juu unaendeleza porojo za “njama za CCM na Usalama wa Taifa,” imefika mahala Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya mkoa anabandika tuhuma nzito dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, kwenye blogu yake. Hivi pamoja na madudu ya CCM unatarajia ‘utoto’ wa aina hiyo?
Tuelekee huko CCM sasa. Kwanza ninaomba kuweka bayana kuwa uchambuzi huu umeelemea katika uelewa wangu wa siasa za huko nyumbani, maongezi yangu na watu walio karibu na siasa hizo, na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari (vya ‘asili’ na vya ‘kisasa’)
Kwa mtizamo wangu, hadi muda huu wanasiasa wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete hapo 2015 ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kwa ‘pembeni’ kidogo kuna Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta. Kimsingi, majina mengine yanayosikika kama William Ngeleja, John Magufuli na wengineo ni ya ‘kuchangamsha gumzo’ zaidi kuliko kuwa na uzito wowote wa maana.
Pengine baadhi ya wasomaji wangetamani nisiandike hivi lakini kimsingi hauepukiki, kama mazingira yatabaki kama yalivyo muda huu (constant) ni vigumu kwa mwanasiasa yeyote yule ndani na nje ya CCM kumzuia Lowassa kuwa rais mwaka 2015. Ninaomba nikiri kuwa ninatamani isiwe hivyo (kwa sababu binafsi ninaamini kuwa hafai kuwa Rais) lakini ukweli una tabia moja: kuuchukia hakuufanyi uwe uongo.
Turufu kubwa ya Lowassa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha japo mwenyewe amekuwa akikanusha na kudai kuwa mamilioni anayoyamwaga katika harambee mbalimbali ni michango ya rafiki zake (hajawahi kuwataja wala kutueleza vyanzo vya utajiri wao).
Inaelezwa pia kuwa mwanasiasa huyo amejijenga mno ndani ya CCM kiasi cha kuwa sahihi kuhitimisha kuwa ana nguvu zaidi ya Mwenyekiti wa Taifa, Kikwete.
Sasa, huhitaji japo kozi ya muda mfupi ya siasa za nchi yetu kufahamu kuwa katika zama hizi fedha ndio nyenzo muhimu zaidi ya kumwezesha mwanasiasa kushinda uchaguzi kuliko kitu chochote kile. Mpigakura mwenye njaa hana habari na sera ya chama bali anachofikiria ni pishi ya mchele, doti ya khanga au kilo ya sukari.
Kwa upande wa Membe, turufu zake muhimu zaidi ni tatu. Kwanza, nafasi yake kama Waziri wa Nje inamweka karibu sana na Rais Kikwete kwani wanasafiri pamoja takriban katika kila ziara ya Rais nje ya nchi. Huhitaji kuwa mdadisi kufahamu kuwa watu wanaosafiri pamoja kwa miaka 10 mfululizo wana ukaribu kiasi gani.
Pili, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Membe anaungwa mkono na familia ya Kikwete. Katika moja ya mahojiano, mmoja wa watoto wa Kikwete, Ridhiwani, alikiri bayana kuwa anadhani Membe anaweza na anafaa kuwa Rais. Siasa za kifamilia zinaweza kubadilika lakini kwa angalau kwa sasa hali ipo hivyo.
Tatu, na kwangu hii ndio turufu muhimu zaidi, Membe ni ‘shushushu mstaafu.’ Pengine ni vigumu kuelezea kwa undani umuhimu wa kigezo hiki, lakini kwa kifupi, ni vigumu sana kwa mwanasiasa kuingia Ikulu pasi kuungwa mkono na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika (angalau katika ‘demokrasia changa’). Mashushushu, kama watumishi wengine wa vyombo vya dola, wana tabia moja ya kumuunga mkono ‘mwenzao.’
Lakini sambamba na hilo ni kile kinachofahamika kama ‘sanaa za giza’ (dark arts), yaani kwa lugha ya kawaida, zile mbinu zinazosababisha kura kuyeyuka katika mazingira ya ajabu. Tukiamini kuwa mashushushu watamuunga mkono Membe, kwa nini basi wasiende mbali zaidi kuhakikisha kuwa anashinda kwa ‘gharama yoyote’ (na ‘gharama’ hapa si lazima iwe fedha)?
Kwa hiyo licha ya uwezo mkubwa wa kifedha wa Lowassa (tukiweka kando kukanusha kwake kuwa yeye si tajiri), Membe anaweza kumshinda kwa mbinu (ambazo kwa mtizamo wangu zinaweza kuhusisha watumishi wa sasa na wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa)
Kuhusu Sitta, nafsi yangu inanituma kuamini kuwa haitokuwa jambo la kushangaza endapo miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 tukakutana na kichwa cha habari kama hiki “Sitta: Lowassa ni chaguo la Mungu.” Kwa nini nina hisi hivyo? Binafsi ninamwona kama mwanasiasa asiyeaminika, anayeendeshwa na siasa za kusaka umaarufu na hata ‘rahisi kutulizwa.’ Kwa kifupi, Sitta anaendeshwa zaidi na imani (kuwa anaweza kuwa rais) kuliko uhalisia.
Kwa Sumaye, japo pengine ni mapema mno ‘kumpuuza,’ nafasi pekee ya yeye kuwa rais ni nje ya CCM. Tatizo kubwa kwa mwanasiasa huyu ni kwamba lugha anayoongea haieleweki ndani ya chama hicho. Naam, amejitokeza kuwa msemaji wa wanyonge na mkemeaji mkubwa wa ufisadi lakini sote tunafahamu kuwa hiyo sio sera ya CCM (angalau kwa vitendo na si kauli za majukwaani).
Nafasi hairuhusu kuangalia ‘odds’ dhidi ya Lowassa na Membe (ninataraji kufanya hivyo katika matoleo yajayo), lakini muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nilishiriki katika mjadala mzito kuhusu hatma ya Tanzania yetu hususan jinsi ya kuzuia uwezekano wa kumpata Rais atakayetokana na rushwa. Pia tulijadili tatizo la rushwa na namna ya kulimaliza.
Kwa bahati nzuri, mjadala huo uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ulimvutia mwanasiasa kijana na Mbunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi. Kwa kifupi, alitueleza kiini cha tatizo la rushwa, na nini kinaweza kufanyika kupambana na tatizo hilo sugu. Bila kuingia undani kuhusu mjadala huo, ulipofikia tamati takriban kila mshiriki alikiri kuwa “kumbe CCM bado ina hazina zaidi ya hayo majina tunayoyasikia kila siku.”
Je, wanasiasa kama Abdullah, mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi wanaweza kuwa chaguo mbadala (alternative choice) hasa ikizingatiwa kuwa hawana ‘mawaa’ kama ya Lowassa au Membe (nitayajadili mbeleni)?
Nihitimishe makala yangu kwa kusisitiza jambo moja: japo kwa jinsi hali ilivyo ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kuiona CCM ikiendelea kuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, bado kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kikongwe kupumzishwa kwani kimeshindwa kazi.
Si Lowassa, Membe, Sitta au Sumaye anayeweza kuibadili CCM irejee misingi aliyoasisi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Tegemeo dogo katika chama hicho ni damu mpya kama za akina Abdulla Mwinyi, japo pengine ni mapema mno kuhitimisha hilo.
ITAENDELEA...
23 Nov 2013
18 Nov 2013
18.11.13
Evarist Chahali
Prof JUMA KAPUYA
No comments

Kapuya aibua mapya
KASHFA ya kumbaka na kutishia kumuua msichana wa miaka 16, inayomkabili Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), imeibua mambo mapya.
Wakati serikali inakusudia kufungua mashtaka mawili ya kubaka na kutishia kuua dhidi ya Profesa Kapuya, waziri huyo wa zamani bila woga ameendelea kutuma ujumbe mfupi kupitia simu yake ya mkononi kwa binti huyo na kusisitiza kuwa lazima amuue.
Mbali na kutishia kumuua binti huyo na ndugu yake na mtu mwingine yeyote atakayejitokeza kumsaidia, gazeti hili limenasa baadhi ya mawasilino ya simu za ujumbe mfupi wa kuhamisha fedha kutoka kwa Profesa Kapuya kwenda binti huyo ambaye juzi kupitia baadhi ya vyombo vya habari Kapuya alikana kumfahamu na kwamba hajawahi kukutana naye.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa mara baada ya taarifa ya gazeti hili jana kuandika mwendelezo wa kashfa hiyo, huku likimkariri Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, akihoji ukimya wa serikali katika kashfa hiyo, Profesa Kapuya alituma ujumbe mwingine wa kutishia kumuua binti huyo.
Ujumbe huo kutoka simu namba 0784993930 inayomilikiwa na Kapuya kwenda kwa namba inayomilikiwa na binti huyo, unasomeka hivi:
“Ni lazima nitakuua wewe na ndugu yako na atakaetaka kuwasaidia, huyo Sita asijiingize kwenu, yaani nitakuua tena sijui leo mtalala wapi! We unadhani nani atakayenifunga? Ndo nishakupa ukimwi, sasa nakutaka uache mara moja kuongea na mtu, nitakuwinda popote tuone!” inasomeka sehemu ya ujumbe huo unaodaiwa kutoka kwa Kapuya.
Ujumbe huo wa vitisho vya kuuawa, unafanana na ule uliokaririwa na gazeti hili ambao pia unadaiwa kutoka kwa Profesa Kapuya kwenda kwa binti huyo anayedai kubakwa na Kapuya.
Sehemu ya ujumbe uliopita unasomeka: “Mkiuawa itakuwa vizuri….itawapunguzia gharama za kuishi; usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe.
“Sisi ndiyo wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe sasa mwambieni nyumba ya kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu wanaingiza hela nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue wiki hii haitaisha; nitapiga kambi kote. Jana si walikuficha? Tuone kama utalindwa milele; maana washatengeneza hela lazima mvae sanda tu hilo sio ombi ni wajibu wenu. Mnajitia na nyie Mafia watoto siyo!!?
“Watoto wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani atapingana nasi!?”
Katika kuthibitisha kwamba Kapuya amekuwa na mawasiliano na binti huyo na kwamba anamjua tofauti na anavyodai kuwa hamjui, gazeti hili limenasa mawasiliano ya kutumiana fedha kutoka kwa Kapuya kwenda kwa binti huyo.
Baadhi ya mawasiliano hayo ni pamoja na yale yaliyofanyika Agosti 31 mwaka huu kupitia simu ya Kapuya ambapo alituma sh 300,000 kwenda kwa binti huyo kama sehemu ya makubaliano ya kutuma pesa kila mwezi kwa ajili ya matunzo.
Mawasiliano hayo ni kama ifuatavyo:
R93NY448 ImethibitishwaUmepokea Tsh505,000kutoka kwa JUMA KAPUYA
Tarehe 21/6/13 saa 11:07 AM
Salio lako la M-PESA ni Tsh 505,000
U26UG365. Imethibitishwa Umepokea Tsh 300,000
kutoka kwa JUMA KAPUYA
Tarehe 31/8/13 saa 3:28 PM
Salio lako la M-PESA ni Tsh 300,000
V04EU470 Imethibitishwa Umepokea Tsh 400,000
kutoka kwa JUMA KAPUYA
Tarehe 24/9/13 saa 2:38 PM
Salio lako la M-PESA ni Tsh 400,040
Tayari serikali kupitia jeshi lake la polisi, limesema linakusudia kufungua mashtaka mawili dhidi ya mbunge huyo.
Mashtaka yanayotajwa kumkabili mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri katika awamu tofauti za uongozi kuwa ni pamoja na ya ubakaji na kutishia kuua.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia gazeti hili juzi kuwa jeshi hilo halitakuwa na sababu ya kumuacha mbunge huyo kuendelea kutamba mitaani huku akituma ujumbe wa vitisho kwa binti wa miaka 16 anayedaiwa kumbaka.
Wakati Kamanda Kova akisema hawatakuwa na ajizi na tuhuma za kubaka na kutishia kuua zinazomkabili Profesa Kapuya, Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete imekerwa na kauli ya mbunge huyo wa Urambo Magharibi kuwa serikali haiwezi kumfanya jambo lolote.
Pia CCM ambayo baadhi ya maafisa wake walijitahidi kutoa Kapuya kwenye kashfa hiyo, kimeamua kumtosa mbunge huyo aliyewahi kuongoza Wizara ya Elimu na Ulinzi kwa nyakati tofauti baada ya kumtaka aache kukihusisha chama na kashfa yake ya kubaka.
Mbunge huyo anadaiwa kumbaka binti huyo kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo ndani ya ofisi yake katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda kuchukua ada kwa mara ya pili.
Kutokana na mfululizo wa habari hiyo ambayo imekuwa ikichapishwa na gazeti hili, Profesa Kapuya kupitia kwa wakili wake Yasin Memba, ametishia kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya siku saba.
Mbali na kutishia kulipeleka gazeti hili na baadhi ya mitandao ya kijamii mahakamani pia Profesa Kapuya alikana kumfahamu binti anayedai alibakwa huku akikanusha kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa vitisho.
CHANZO: Tanzania Daima
17 Nov 2013
17.11.13
Evarist Chahali
Prof JUMA KAPUYA
No comments
TAMKO LANGU KWA UMMA JUU YA UZUSHI UNAOENEZWA DHIDI YANGU.Ndugu wanahabari,Baada ya kumshukuru na kumtukuza mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Natanguliza salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu mwanazuoni na mwanaharakati mwenzangu Dkt Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya Haki siku chache zilizopita huko Afrika ya kusini.Ndugu zangu wanahabari,Wengi mnanifahamu na kuifahamu vema historia yangu katika utendaji kazi na utumishi wa umma wa Watanzania. Nimekuwa nikiitumikia nchi yangu kwa kipindi kirefu katika Nyanja na sekta mbali mbali kuanzia Darasani mpaka kwenye siasa.Kwa msingi huo, mimi Profesa Juma Kapuya, siku zote ninajikuta mwenye wajibu endelevu wa kuendelea kulitumikia Taifa langu kila siku mpaka kufikia mwisho wa Nguvu zangu.Ndugu wanahabari,Hivi karibuni nikiwa huku jimboni kuendelea na shuhuli za utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi kumezuka Tuhuma kadhaa zilizoelekezwa dhidi yamgu zikiasisiwa na wanasiasa wenzangu wa ndani na nje ya chama changu ili kudhoofisha juhudi na utendaji wangu wa kila siku.Tuhuma hizo zisizokuwa na kichwa wala miguu na pia kutokuwa na ukweli wowote, wamekuwa wakizitoa kwa kumtumia msichana anayedai amefanyiwa vitendo visivyofaa na mimi. Mimi simfahamu na sijui hizi shutuma zinatokea wapi.Ndugu wanahabari,Kwa tamko hili ninapenda kuwaambia kuwa nimefedheheshwa sana na uwezo mdogo wa kisiasa unaofanywa na hawa watu kwa kuwa dhamira yao haitatimia. Napenda niwakumbushe ndugu zangu kwamba tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na wapinzani wangu wameanza kunichafua ili nionekane sifai.Ninapenda kuwaambia watanzania na wananchi wa jimbo langu kuwa wanatakiwa wazipuuze taarifa hizi kwa kuwa hazina ukweli wowote na kwamba ni za kutungwa zenye lengo la kunidharirisha na kuniondolea heshima yangu niliyojijengea kwenye jamii kwa kipindi kirefu sasa. Waswahili wanasema dawa ya mjinga ni kumpuuza.Na hili linajidhihirisha zaidi kwa habari hii kuandikwa na chombo kimoja tu cha habari kinachotumiwa na chama kimoja cha siasa na baadhi ya wanasiasa wa chama changu wasiokitakia heri chama chetu, naomba kuwashukuru na kuwapongeza vyombo vingine vya habari kwa umakini wenu wa kuwa na nauelewa wa kutoandika kitu bila kukifanyia uchunguzi na kubaini ukweli ulivyo.Chombo hiki cha habari kiliwahi kuripoti mwaka jana kuwa kuna mitambo imeingizwa nchini inayoweza kuandika ujumbe na kisha kuufanya uonekane umetoka kwenye namba Fulani, kwa kipindi kile sikuwaelewa, lakini sasa ninawaelewa na nimewaona kuwa wako sahihi na wao ndio waliouingiza mtambo huu na sasa wameamua kuutumia dhidi yangu kwa kutengeneza meseji na kuzihusianisha na mimi. Ninaamini ukweli utawaumbua muda si mrefu.Ndugu wanahabari,Nimeijenga heshima yangu na familia yangu kwa jamii yangu kwa kipindi kirefu mno, kwa hivyo siwezi kuruhusu heshima niliyoijenga kwa miongo kadhaa karibiwa na kupotezwa na watu wachache tena kwa muda mfupi namna hii.Hivyo basi nimechukua hatua za kisheria kuhakikisha heshima yangu inaendelea kulindwa na utu wangu unaheshimiwa.Nimemwagiza mwanasheria wangu afungue kesi na tayari amewashitaki watu wote wanaohusika kwenye mpango huu na tayari wameshapokea taarifa ya kuitwa mahakamani.Nitaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaoendelea kutaka kujipatia umaarufu ama wa kisiasa au wowote ule kwa kutumia jina langu.Hayo yote ni kwa kuzingatia ukweli kwamba nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya kisheria na kufuata na kuheshimu haki na wajibu wakila mmoja wetu.Kwenye hilo ninawaambia ‘’janja yao nimeigundua, na hawatafanikiwa’’Ninatoa Rai kwa yeyote mwenye kuona hilo jambo lina ukweli alipeleke kwenye vyombo husika ili lishuhulikiwe kwa mujibu wa sheria na sio kutumia vyombo vya habari kuchafuana.Mwisho ninasisitiza kuwa nitaendelea kuilinda na kuitetea heshima yangu niliyojijengea kwa jamii kwa muda mrefu sasa na sitaruhusukuiona ikiharibiwa na wajanja wachache kwa maslahi yao binafsi.
Tuendelee kuijenga nchi yetu,
Mungu Ibariki Tanzania
Imetolewa leo tarehe 15.11.2013 nami
Prof. Juma A.Kapuya
Mbunge – urambo magharibi
S.L.P 45 Kaliua Tabora
Simu 0784993930
15 Nov 2013
15.11.13
Evarist Chahali
RAIA MWEMA
No comments
MARA kadhaa katika makala zangu za huko nyuma nimekuwa nikimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa tabia aliyojijengea ya kuzungumza na Watanzania mara kwa mara. Licha ya pongezi hizo wakati mwingine kuambatana na kumkosoa hasa pale anapochelea kuzungumzia baadhi ya masuala ambayo wananchi wana kiu ya kuyasikia kutoka kwa Rais wao, ukweli tu kuwa angalau anatilia mkazo kuongea nao (pasi kujali sana yaliyomo kwenye hotuba zake) anastahili pongezi.
Lakini kama ilivyo kawaida katika maisha, kitu kikitokea mara nyingi kinaweza kujenga hali ya kuzoeleka, pengine katika hali halisi. Kwa vile hotuba za Rais zimekuwa nyingi, yayumkinika kuna nyakati baadhi ya wananchi hupatwa na hisia kama “aah ni mwendelezo tu wa hotuba, hakuna jipya...”
Hata hivyo, katika hotuba yake ya hivi karibuni bungeni mjini Dodoma sio tu anastahahili pongezi kwa kuendeleza utaratibu aliojiwekea kuwahutubia Watanzania bali pia yaliyomo kwenye hotuba hiyo yalikuwa na uzito mkubwa.
Pengine utajiuliza; “huyu Bwana Chahali vipi tena? Anamsifiaje Rais kwa kutimiza wajibu wake (yaani majukumu yake kama kiongozi wa nchi yanayompa stahili ya mshahara)”? Ni vema kuielewa vyema Afrika yetu na siasa zake. Ukweli usiopendeza ni kwamba kwa ujumla uongozi katika Bara letu ni suala la fadhila zaidi kuliko stahili. Kwamba japo kiongozi anapaswa kutekeleza majukumu yaliyopelekea kupewa dhamana ya kuongoza, utekelezaji wa majukumu husika unabaki kuwa suala la hiari ya kiongozi husika. Haistahili kuwa hivyo lakini ndivyo ilivyo.
Lengo la makala hii sio kuchambua hotuba nzima ya Rais Kikwete aliyoitoa huko bungeni Dodoma bali kujadili baadhi tu ya masuala muhimu hususan nafasi ya wasaidizi wa Rais katika kufanikisha uongozi wa taifa letu.
Msimamo wa Rais Kikwete alioubainisha katika hotuba hiyo kuhusu hatima yetu kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki licha ya ‘kumpaisha’ katika anga za siasa za kitaifa na kimataifa kama kiongozi mwenye visheni, pia unaweza kutoa tafsiri isiyopendeza sana kwa wanasiasa wawili mahiri wa huko nyumbani, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Binafsi nimekuwa nikifuatilia kwa karibu nyendo za mawaziri hawa, sio tu kutokana na umuhimu wa nyadhifa zao bali pia ukweli kwamba majina yao yamekuwa yakitajwa sana katika kinyang’anyiro cha kumsaka ‘mrithi wa Rais Kikwete’ katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.
Sio siri kwamba, kulingana na wadhifa wake, Waziri Membe hulazimika kutoa matamko mbalimbali yanayohusu siasa na sera za nje za nchi yetu. Nadhani wengi wetu mnakumbuka kauli zake katika matukio mawili makubwa ya hivi karibuni, ambapo hali ya maelewano kati yetu na jirani zetu wa Malawi na Rwanda haikuwa nzuri sana.
Huhitaji kuwa mjuzi wa uchambuzi wa kauli kubaini tofauti kati ya lugha aliyokuwa akitumia Waziri Membe na Rais Kikwete walipozungumzia uhusiano wetu na Rwanda. Japo pengine ni muhimu kuonekana ‘tough’ kwenye siasa za kimataifa, ‘tone’ kama ya Waziri Membe kuwa “hatutaiomba radhi Rwanda” haikusaidia kupunguza fukuto la uhasama kati yetu na nchi hiyo, kinyume cha hotuba ya Rais Kikwete mkoani Kagera ambayo ilisheheni busara na kiu ya kudumisha ujirani mwema.
Lakini pengine ‘kali zaidi’ ilikuwa ni katika chokochoko zilizojitokeza kati yetu na Malawi. Wakati mmoja, Waziri Membe alinukuliwa akidai kuwa “Malawi iache kutapatapa” baada ya taarifa kutoka Lilongwe kuashiria kuwa nchi hiyo ilikuwa inataka kuwasilisha suala la mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.
Si kwamba “kutapatapa” ni tusi bali busara ndogo tu inatanabaisha kuwa moto hauzimwi kwa moto bali maji. Kadhalika, kuna msemo kuwa “ukibishana na mlevi, itawia vigumu watu kutofautisha nani mzima na nani mlevi.” Na kama nilivyobainisha katika makala yangu katika toleo lililopita kuhusu Kanuni za Nguvu (Laws of Power), wakati mwingine matendo yanayoambatana na ukimya badala ya maneno au kelele huwa na matokeo chanya zaidi.
Katika nyakati tofauti, mawaziri Membe na Sitta wamekuwa wakitoa kauli za ‘ajabu ajabu’ kuhusu ‘sekeseke’ la Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Huku Membe akidai “Tunasubiri talaka Afrika Mashariki” Sitta akakurupuka na mawazo mapya ya ‘jumuiya mpya’ kati yetu na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Na kwa vile suala la ‘Jumuiya ya Afrika Mashariki’ linaangukia katika eneo la utendaji kazi la mawaziri wote wawili, kwa Sitta ilikuwa ni kama fursa adimu kwake kuwathibitishia Watanzania ‘umahiri wake katika siasa za kimataifa’ huku Membe akionyesha ‘uzoefu wake’ katika ‘kukabiliana na nchi korofi.’
Kwa nini basi hotuba ya Rais Kikwete ilielemea zaidi katika kuleta maelewano na sio kuendeleza malumbano ilhali kauli za mawaziri wake Membe na Sitta zilikuwa zikijenga taswira ya nchi yetu sio tu kuelekea kujitoa katika umoja huo bali pia chombo hicho hakina manufaa kwa taifa letu?
Jibu langu kwa swali hili ni la kufikirika tu lakini linaweza kuwa na mantiki ndani yake. Kwa mtizamo wangu, nadhani kauli za mawaziri hao wawili zililenga zaidi katika maslahi yao binafsi kuliko ya nchi yetu. Yaani yayumkinika kuhisi kuwa ‘msimamo wao wa ubabe’ ulilenga kuimarisha credentials (sifa) zao katika sera na siasa za nje za Tanzania pengine kigezo muhimu katika hekaheka za kumpata ‘mrithi wa Kikwete’ kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mafundisho ya Biblia Takatifu yanaangaliwa kwa kuzingatia kinachoitwa ‘sheria za kisasi’ na ‘sheria za mapatano’ (yaani kwa Kiingereza, ‘laws of retaliation’ na ‘laws of reconciliation.’) Hizo za ‘kisasi’ ni zaidi katika Agano la Kale, enzi za kina Nabii Musa, ambapo tunasikia vitu kama ‘jicho kwa jicho’ au jino kwa jino,’ ilhali katika Agano Jipya (zama za Yesu) msisitizo ni katika upendo na vitu kama ‘ukipigwa shavu la kushoto geuza na shavu la kulia.’
Katika dunia ya sasa ambapo mataifa tajiri na yenye nguvu kama Marekani, Uingereza, Ujerumani yanahangaika kujenga ushirikiano imara, hata na nchi masikini zaidi yao, sie tutaonekana kituko kudhani tunaweza kutohitaji ushirikiano na majirani zetu.
Sawa, Ushirikiano wa Afrika Mashariki una matatizo kadhaa yanayohitaji mjadala mrefu lakini matatizo ni sehemu ya maisha, na busara zinatuasa kuwa “huwezi kutafuta tatizo kwa kulikimbia.” Binafsi ninaamini kuwa matatizo ya ushirikiano huo yanazungumzika (lakini kwa lugha za kistaarabu na sio ubabe) na yanaweza kabisa kutatulika (lakini si kwa kufikiria Ushirikiano ‘mpya’ kama alionekana kuashiria Waziri Sitta).
Nimalizie makala hii kwa ahadi kuwa nitalijalidi suala la Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upana zaidi siku zijazo. Pili, pamoja na kumkosoa Waziri Membe katika makala hii bado namwona kama mmoja ya wanasiasa wa CCM wanaoweza kumrithi Kikwete (hapa simaanishi kuwa anafaa au hafai bali ‘possibility’ ya kuwa Rais).
Panapo majaliwa, makala yangu ya wiki ijayo itarejea tena kujadili kinyang’anyiro cha urais 2015 kwa tiketi ya chama hicho na nitabainisha hoja hiyo ya ‘uwezekano wa Membe kuwa Rais.’ Lakini mwisho, ni muhimu kwa sote kama Watanzania kwenda mbele (to move forward) na kuzitafsiri criticisms (hoja za ukosoaji) kama changamoto zinazotukabili katika kujenga ushirikiano na majirani zetu sambamba na maendeleo kwa taifa letu.
UMOJA NI NGUVU
Subscribe to:
Comments (Atom)











































