21 Aug 2014

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.


20 Aug 2014

Nianze makala hii kwa kuomba samahani kutokana na kuchelewesha mfululizo huu wa makala kuhusu taaluma ya ushushushu. Baadhi ya wasomaji wamehoji ukimya huo, huku wengine wakidhani kwamba 'wahusika' wamenizuwia. Ninapenda kurejea nilichokiandika katika sehemu ya kwanza ya makala hii kwamba mfululizo huu unazingatia sheria na maadili na 'wahusika' hawana sababu ya kuuzuwia.

Kwa kukumbushana tu, sehemu ya kwanza iliitambulisha taaluma ya ushushushu kwa ujumla, wakati sehemu ya pili ilielezea jinsi mashushushu wanavyopatikana (recruitment). Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia mafunzo ya mashushushu wanafunzi.

Ninakumbuka siku moja niliwahi kuulizwa swali na rafiki yangu flani huko Twitter iwapo walinzi wa viongozi (bodyguards) nao ni mashushushu kwa maana ya kupitia mafunzi kama 'mashushushu wa kawaida.' Jibu langu kwake litatoa mwelekeo wa makala hii, kwamba, kwanza japo taaluma ya ushushushu ina maeneo flani yanayofanana mahala popote pale duniani, vitu kama mazingira, mahitaji ya nchi/taasisi ya kishushushu, na pengine uwezo wa kiuchumi hupelekea tofauti kati ya taasisi moja na nyingine. Nitoe mfano. Kwa nchi kama Marekani, taasisi ya kishushushu inayohusika na ulinzi wa viongozi (US Secret Service) 'inajitegemea' kwa maana ya ajira,mafunzo na utendaji kazi. Wanaojiunga na taasisi hiyo ni lazima wapitie kozi ya awali ya upelelezi wa jinai (Basic Criminal Investigator Training) inayodumu kwa wiki 10, na inayofanyika katika chuo cha Federal Law Enforcement Training Centre kilichopo Glynco, Georgia, na kisha kufanya kozi nyingine ya wiki 17 inayojulikana kama Speicla Agent Basic Training, inayofanyika katika chuo cha James J. Rowley Training Centre, nje kidogo ya jiji la Washington DC.

Kwa minajili ya kuepuka mkanganyiko, nitatumia mfumo unaotumiwa na Idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) katika maelezo kuhusu mafunzo ya mashushushu. Tofauti na Marekani, Idara yetu ya Usalama ni taasisi moja yenye vitengo mbalimbali. Na katika jibu nililompatia rafiki yangu ailiyeniuliza huko Twitter, maafisa usalama wanaolinda viongozi wetu huajiriwa kama afisa usalama mwingine yeyote yule. Katika mazingira ya kawaida, baada ya Idara ya Usalama wa Taifa kumaliza mchakato wa kuwapata mashushushu watarajiwa (process niliyoieleza kwa undani katika makala iliyopita), hatua inayofuata ni mafunzo. 

Kwa huko nyumbani, kila shushushu mpya hupatiwa mafunzo kupitia kozi ya awali ya uafisa (Junior Basic Course) katika chuo chao kilichopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. Urefu wa kozi hutegemea vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya Idara yenyewe. 

Muundo wa mafunzo:

Kimsingi, na katika mazingira ya kawaida, kozi hiyo ya awali hugawanywa katika sehemu kuu tatu: mafunzo ya kijeshi na ukakamavu, mafunzo ya mapambano pasipo silaha (unarmed combat) na mafunzo ya ushushushu 'halisi.'

Mafunzo ya kijeshi na ukakamavu hujumuisha 'kwata' za kijeshi (kama zile wanazofunzwa 'makuruta' katika Jeshi la Kujenga Taifa). Kabla ya kuanza kozi hii, mashushushu watarajiwa hufanyiwa uchunguzi wa kiafya kubaini iwapo wataweza kumudu shuruba zinazoambatana na kozi hiyo. Na kwa hakika ni hatua ngumu mno, ambapo kwa takriban kila 'intake' kuna 'wanafunzi' wanaoamua kuomba ruhusa ya kuondoka baada ya kushindwa kustahilimi ugumu wa mafunzo hayo. 

Haya ni mafunzo ya kijeshi 'halisi' kwa maana ya drills za kijeshi, mafunzo ya msingi ya kivita ikiwa ni pamoja na usomaji ramani katika uwanja wa mapambano, ulengaji shabaha, uelewa kuhusu silaha mbalimbali, nk. Sambamba na mafunzo hayo ni mazoezi makali ya viungo na ukakamavu. Kadhalika, mafunzo hao huambatana na kujenga nidhamu ya kijeshi pamoja na uvumilivu (ni jambo la kwaida kwa 'wanafunzi kupitisha usiku kadhaa bila kulala). Mafunzo haya huendeshwa na wakufunzi wa kijeshi ambao pia ni waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Hatua inayofuata ni kozi ya mapambano bila silaha (unarmed combat). Katika kozi hii, mashushushu watarajiwa hufundishwa jinsi ya kupambana na adui kwa kutumia mwili pekee, yaani bila kuwa na silaha. Walimu wa kozi hii huitwa Sensei na kozi hujanyika katika ukumbi ujulikanao kama dojo. Kadhalika, 'wanafunzi' huvaa ' mavazi maalum' yajulikanayo kama Kimono.

Pasipo kuingia ndani zaidi, kozi hii hufuata mfululizo wa hatua zinazojulikana kama 'kata.' Kwa lugha nyepesi, kata ni movements za mtu mmoja mmoja au zaidi, na kila moja ni mfumo wa mapambano. Kila kata ina jina, na majina hayo yana asili ya Mashariki ya Mbali, ambapo fani ya mapambano bila silaha ni sehemu muhimu ya utamaduni kwa nchi kama China,Japan, Korea, nk. Ili kujifunza kata inayofuata ni lazima kuimudu kata ya awali. Ni kama vile hatua za makuzi ya mtoto, hawezi kuanza kukimbia kabla ya kutamaa.

Kwa minajili ya kurahisisha maelezo, kozi hii hujumuisha karate, judo,ngumi,nk. Kadhalika, japo mafunzo yanaitwa mapambano bila ya silaha, ukweli ni kwamba kuna baadhi ya kata huhusisha matumizi ya/ kujilinda dhidi ya silaha ndogo japo hatari kama vile visu, jambia la mapambano, minyororo, nk. Katika kozi hii, 'wanafunzi' hufunzwa pia kuhusu 'sehemu za udhaifu katika mwili wa binadamu' (weak points) kwa minajili ya kutambua eneo gani la mwili wa adui likidhibitiwa anakuwa 'hana ujanja.'

Hatua ya tatu ni mafunzo 'halisi' ya ushushushu. Kwa ujumla, mafunzo haya humfundisha shushushu mtarajiwa mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama kwa siri, kuzichambua na 'kuzifanyia kazi.' Kwa ujumla pia, kozi hii hugawanywa katika makundi mawili: ushushushu ndani ya nchi na ujasusi ushushushu nje ya nchi. Kadhalika, masushushu wanafunzi hufunzwa  kitu kinachoitwa 'shughuli za adui' yaani ujasusi (espionage), uzandiki (subversion), hujuma (sabotage) na ugaidi (terrorism). Vilevile, hufunzwa mbinu za kunasa mawasiliano (bugging), ufuatiliaji wa siri (surveillance), jinsi ya kupata watoa habari (recruitment of sources) na jinsi ya kuwamudu, ikiwa na pamoja na jinsi ya 'kuwamwaga' (kuachana nao) pale wanapopoteza umuhimu. 

Pengine la kuchekesha katika hatua hii ya mafunzo ya ushushushu ni hisia kwamba 'mashushushu hufundishwa kutongoza.' Kuna aina flani ya ukweli katika hilo japo kinachofundishwa sio jinsi ya kutongoza mwanamke bali kutongoza kwa minajili ya kupata taarifa. Na pengine neno 'kutongoza' sio stahili kwani lina connotation na mambo ya ngono. 

Japo mbinu za kukusanya taarifa za kiusalama (methods of elicitation) ni maalum kwa matumizi ya mashushushu, kimsingi zinatumika katika fani nyingine, kwa mfano watafiti wanapofanya mahojiano kwa ajili ya tafiti zao.Tofauti ya msingi ipo kwenye usiri unaoambatana na mbinu husika, kwa mfano mtu kuhojiwa pasi kujua anahojiwa na shushushu. Mfano mmoja wa mbinu hizo ni kinachotwa 'incorrect supposition.' Mbinu hii inatumia udhaifu wa kawaida wa binadamu kutotaka kuelezwa isivyostahili. Kwa mfano, katika kutaka kufahamu kama mtumishi wa kawaida tu ana 'fedha zaidi ya uwezo wake.' shushushu anaweza kumwambia mtu huyu "ah inadaiwa wewe ni masikini tu ambaye hata kodi ya nyumba ya kupanga inakusumbua." Katika mazingira mwafaka, mhusika atakurupuka na kujigamba, "ah wapi bwana. Utawaweza waswahili kwa uzushi? Mie nina nyumba kadhaa hapa mjini, na lile duka la spea pale Kariakoo ni langu..." Kwahiyo wakati mwingine ukiskia mtu anang'ang'ania kusema kitu kisicho sahihi dhidi yako, usikimbilie kudhania anakudhalilisha au hajui ukweli.Yawezekana 'anakulengesha' umpatie ukweli anaohitaji.

Mbinu nyingine ni ya 'nipe nikupe.' Nakupa unachodhani ni taarifa za siri (naam, pengine ni za siri kweli lakini hazina madhara) ili nawe unipe taarifa ninazohitaji. Ni kile wanaita 'Quid Pro Quo.'

Jambo jingine ambalo mashushushu wanafunzi hufundishwa muda wote ni kitu kinachofahamika kama constant vigilance of an officer, yaani afisa usalama wa taifa anapaswa kuwa macho muda wote, huku akitambua kuwa uhai wa taifa lake upo mikononi mwake muda wote. Pengine tafsiri ya kanuni hiyo ni 'kujitambua muda wote.' Kutambua dhamana aliyonayo afisa usalama kwa taifa. Kadhalika, mafunzo huhusisha pia kujenga na kuimarisha matumizi ya 'hisia ya sita.' Kama nilvyoeleza katika makala ya kwanza, binadamu tuna hisia tano: kuona kwa kutumia macho, kusikia kwa kutumia masikio, kunusa kwa kutumia pua, ladha kwa kutumia ulimu na kuguswa (touch) kwa kutumia ngozi. Hisia ya sita ni kitu cha zaida ya hivyo vitano. Ni vigumu kueleza katika mazingira ya kawaida ila labda kwakifupi ni ule uwezo wa kwenda mbali zaidi ya uwezo wa kawaida wa hisia: kuamini au kutoamini pale inapopaswa kuamini au kutoamini, kutambua hatari hata bila ya kupewa tahadhari, nk.

Awali nimetaja kuhusu vitendo vya adui, yaani ujasusi, uzandiki, hujuma na ugaidi. Kimsingi japo hivi ni vitendo vya adui na njia ya kupambana nayo ni kinachojulikana kama counterintelligence au CI kwa kifupi, mashushushu wanafunzi hufunzwa pia mbinu 'za kiadui.' Ni hivi, kuna nyakati serikali au taasisi ya usalama hulazimika kupelekea amshushushu wake nje ya nchi, na kimsingi hawa ndio wanaoitwa spies, na kitendo chenyewe ndio espionage (ujasusi), lengo si 'kutengeneza maadui' bali kuwapatia mashushushu uwezo wa kukusanya taarifa za kiusalama nje ya nchi. Miongoni mwa kanuni anazofundishwa shushushu mwanafunzi ni pamoja na uwezekano wa kukanwa na nchi yake pindi akikamatwa kwenye operesheni za nje ya nchi. Vilevile, mashushushu hufunzwa kuhusu kitu kinachofahamika kama 'kifuniko' (cover ) yaani utambulisho bandia. Kwa mfano, balozi takriban zote duniani huwa na majasusi wanaojipachika vyeo kama 'mwambata wa siasa' au mwabata wa ulinzi.' Ieleweke kuwa japo ushushushu ni fani inayokubalika, serikali rafiki ikitambua shughuli za maafisa usalama wa nchi nyingine rafiki, yaweza kupelekea matatizo makubwa. Na mara nyingi ukisikia serikali imewafukuza maafisa ubalozi flani basi mara nyingi watu hao ni mashushushu 'waliojificha' kama maafisa ubalozi.

Vilevile, katika muda wote wa mafunzo, mashushushu watarajiwa huhamasishwa kuhusu uzalendo, thamani ya nchi yao, umuhimu wa kuilinda muda wote, umuhimu wa taaluma hiyo katika ustawi na mustakabali wa taifa lao,nk. Na siku ya kuhitimua mafunzo, kila shushushu huapa kwa kushika alama muhimu za taifa- katiba/bendera ya taifa, na kuweka kiapo cha kuitumikia nchi yake kwa uwezo wake wote, sambamba na viapo vingine vya kikazi (kwa mfano kamwe kutotoa siri za nchi na za Idara). Japo kuna hisia 'mtaani' kwamba watu walioacha au kuachishwa ushushushu huogopa kutoa siri kwa kuhofia kuadhibiwa, ukweli ni kwamba kiapo wanachokula wakati wa kuhitimu mafunzo ni 'kizito' mno kiasi kwamba katika mazingira ya kawaida, mhusika atajiskia nafsi inamsuta kusaliti kiapo hicho. 

Licha ya mafunzo ya darasani, kuna mafunzo ya nje ya darasa ambapo mashushushu watarajiwa 'humwagwa mtaani' kufanya mafunzo ya vitendo. 

Kubwa zaidi wakati mafunzo yanaendelea ni usiri wa hali ya juu. Katika mazingira ya kawaida, kila shushushu mwanafunzi huwa amefika ukweli kuwa anaenda/ yupo mafunzoni. Na kuficha huko si kwa marafiki tu bali hata wazazi na ndugu wa karibu. Na hapa ni muhimu kueleza kwamba moja ya vitu anavyokumbushwa afisa usalama wa taifa tangu hatua za mwanzo za kujiunga na taaluma hiyo hadi katika maisha yake ya kila siku ni KUWA MAKINI NA IMANI, au kwa lugha nyingine USIMWAMINI MTU YEYOTE. Wanasema TRSUT WILL GET YOU KILLED, yaani IMANI (kwa mtu au kitu)  ITAKUUWA. Kwahiyo si jambo la ajabu kwa shushushu kutomwamini hata mzazi, ndugu au mwenza wake. 

Kwa leo ninaomba kuishia hapa. Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hii, ambapo toleo lijalo litaangalia kidogo kuhusu aina nyingine za mafunzo na kuangalia kwa undani kuhusu 'maisha ya shushushu mtaani,' yaani baada ya kuhitimu mafunzo yake. Unaweza kusoma habari za intelijensia kirahisi zaidi kwa kuonyeza INTELIJENSIA hapo kwenye menu ya blogu hii.




.

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.



"Hao Chadema ni watu hatari kabisa. Eti ndio 'government-in-waiting' (chama kinachotarajia kushinda uchaguzi na kuunda serikali)." Haya ni maneno ya msomi mmoja, mtu ambaye kwa hakika ana uelewa mkubwa wa masuala mbalimbali hususan yanayoihusu Tanzania yetu. 

Hii ndio Tanzania, na hawa ndo watu wake. Ni vigumu mno kutofautisha kati ya msomi na mbumbumbu yanapokuja masuala yanayohitaji kuuhangaisha ubongo. Wanasiasa matapeli wameshatambua udhaifu huo mapema, na wanautumia ipasavyo.

Hivi kweli mtu mwenye akili nzuri anaweza japo kupoteza muda wake kusikia porojo kuwa 'Chadema ni chama cha kigaidi, na ndicho kilichopanga mauaji ya kinyama ya mwandishi Daudi Mwangosi'? Ndio, kuna wanaoichukia Chadema kwa sababu 'ni chama cha Kikristo.' Kuna wanaoichukia kwa vile 'ni chama cha Wachagga.' Kunawanayoiona Chadema ni ya kitapeli kwa vile 'Mwenyekiti wake Freeman Mbowe alikuwa mpigisha disko (DJ) huko nyuma.' Na kuna wanaoitazama Chadema kama kundi la wazushi kwa vile Katibu wake Mkuu, Dkt Willbrod Slaa 'aliacha upadri na kuingia kwenye siasa.'

Lakini Chadema imejitengenezea maadui kadhaa kutokana na matatizo yake na mwanachama wake machachari Zitto Kabwe. Huyu ni mtu mwenye ushawishi mkubwa, hususan miongoni mwa vijana. Ana marafiki wengi, hususan mtandaoni. Matatizo kati yake na Chadema, ambayo binafsi ninayatafsiri kama 'kutanguliza hisia mbele ya akili' (puitting emotions in front of common sense) yanachukuliwa na marafiki zake kama moja ya sababu kuu za kuichukia Chadema.

Pengine ni vema nikatanabaisha kuwa si lazima kila mtu aipende Chadema, kama ambavyo hakuna anayelazimishwa kuichukia CCM au kuipenda CUF. Ndio demokrasia, kupenda au kuchukia kitu. Lakini kupenda au kuchukia huko kuna kuwa na maana kama kutatokana na sababu za msingi. Siasa si mtu japo ni kwa ajili ya watu. Ni vigumu mtu kuchukua nafasi ya taasisi hata awe na umaarufu kiasi gani. 

Tuweke kando sababu 'za muhimu' za kuichukia Chadema. Majuzi zimeibuka mbinu chafu za kukichafua TENA chama hicho. Nasema 'tena' kwa sababu hii si mara ya kwanza. Mengi yashatokea huko nyuma, na makala hii haitoshi kuyaorodhesha yote. Lakini tuhuma kubwa dhidi ya Chadema ni ugaidi. Alipokufa aliyekuwa Makamu wake wa Mwenyekiti Chacha Wangwe, ambaye nae kama Zitto alikuwa na matatizo na viongozi wenzie, chama hicho kilituhumiwa kumuua kwa kisingizio cha ajali. Angalau uzushi huo ungeweza kuaminiwa na mzembe yeyote yule wa kufikiri kwani sote twafahamu kuwa wakati mwingine njia mwafaka ya kudili na adui yako ni kummaliza. Lakini Wangwe alikuwa adui wa nani? Majibi ya haraka yatakuwa 'Mbowe' kama sio 'Slaa.'

Ni hivi, Chadema bado ni chama kichanga kiumri. Na katika jithada zake za kujijenga lazima kitahusishwa na majina ya viongozi wake wachache badala ya chama kizima. Hata CCM na ukongwe wake bado ina majina flani ambayo ni kama chama, watu kama Kingunge au Lowassa. Kwahiyo si jambo la ajabu, baya au hata zuri la Chadema likahusishwa na majina flani ya viongozi wake maarufu. Na kwa namna flani huo ni mtihani ambao Chadema wanalazimika kuushinda: kujenga taswira ya chama badala ya majina ya viongozi wachache.

Kifo cha Wangwe kitaendelea kuiandama Chadema kwa muda mrefu, pengine hadi CCM itakapopoteza nguvu zake, kwa sababu chama hicho tawala kimeishiwa kabisa na mbinu za kupambana na Upinzani isipokuwa kujenga picha ya uadui kati ya Upinzani na wananchi.

Ni hivi, huhitaji kuwa msomi, mjuzi wa siasa au mwenye ubongo 'mkubwa' kama wa Albert Einstein, kutambua kuwa tuhuma za hivi karibuni dhidi ya Chadema zinahusiana moja kwa moja na uhuni unaoendelea huko Dodoma kwa jina la Bunge la Katiba. Ni mkakati fyongo unaolenga sio tu kuifarakanisha Chadema na washirika wenzie huko UKAWA bali pia kuipotezea uhalali wake kwa wananchi.

Hebu kwa minajili tu ya mjadala huu, tupumzishe ubongo na kuamini kuwa kweli Chadema walimuua marehemu Mwangosi. Kwanini suala hili lilifichika hadi muda huu? Mchange (Habib) hakuhama Chadema leo, na amekuwa akiishutumu Chadema tangu aondoke/atimuliwe katika chama hicho. Kipi kilmkwama kooni hadi akashindwa kuituhumu Chadema kwa mauji ya Mwangosi wakati huo? Kwanini iwe sasa?

Laiti tukitumia ubongo wetu ipasavyo tutaweza kirahisi tu kujumlisha moja na moja na kupata mbili: jithada za kuichafua Chadema muda huu hazihusiani na 'uhalifu uliozoeleka katika chama hicho' bali ni suala k
la Katiba mpya. CCM inataka kulazimisha upatikanaji wa Katiba mpya kwa njia za kihuni, lakini imefika mahala na kutambua kuwa japo yaweza kutumia ubabe wake kupitisha Katiba hiyo, lakini inaweza kukosa uhalali. Sasa njia nyepesi ni 'kuwakoroga' UKAWA, wapoteza hadhi yao kwa Watanzania, na hiyo itapelekea umauzi wowote utakaofikiwa na CCM kuonekana ni wa maslahi ya taifa. Nani anataka kuhusiana na mtizamo wa chama cha wauaji?

Kuna tetesi kuwa mwana-Chadema mwingine aliyehusishwa na ajali iliyopelekea kifo cha Wangwe, Deus Mallya, nae yupo katika hatari ya kutumiwa na CCM kutangaza kuwa Chadema ilihusika na kifo cha Wangwe. Jitihada hizi za kuichafua Chadema kwa nguvu nyingi muda huu lazima ziwe na uhusiano na suala la Katiba mpya, na hii haihitaji usomi au kuwa mpenzi wa Chadema.

Ofkoz, CCM wana 'kisingizio cha asili' kinachosubiri muda tu kitumike ipasavyo. Hapa ninazungumzia tihsio la Ebola. Maji yakizidi unga, tutachanganywa akili kuhusu Ebola na kwa vile sie ni wepesi sana kuzugwa, tutasahau kila kitu kuhusu Bunge la Katiba na Katiba mpya. ;Lakini kwa vile Ebola ni ishu nyeti, na ni vigumu kuihusisha na Chadema, mkakati rahisi unaonekana kuwa huu wa kuinajisi Chadema kwa wana-UKAWA wenzie, na kwa upana zaidi, kwa wananchi.

Ninatambua kuna watakaohoji: "sasa Bwana Chahali, kwa vile unaipenda sana Chadema haimaanishi kuwa chama hicho hakiwezi kuwa cha kigaidi." Suala sio mie kuipenda Chadema, na kuipenda sio dhambi, na pia mie si mwanachama au mfuasi wa chama hicho bali ninaunga mkono harakati zake dhidi ya ufisadi. Suala la msingi ni jinsi mbinu za kihuni zinavyotumukia kutuzuwia kupata Katiba mpya 

Ni muhimu kuushughulisha ubongo, na umeumbwa kwa ajili hiyo. Yaani polisi wetu ni dhaifu mno kiasi cha muda wote huu kushindwa kufahamu kuwa miongoni mwao walitumiwa na Chadema kumuua Mwangosi? Kinachochukiza zaidi katika suala hili ni kutumia mauaji ya kinyama ya mwandishi huyo kama mtaji fyongo wa kisiasa. Hadi leo marehemu Mangosi hajatendewa haki, na hata ikitendeka haitmrejeshea uhai wake. Kwanini kumtesa huko alipo kwa kutumia kifo chake kwa minajili ya kisiasa?

Nimalizie makala hii kwa kukumbusha kuwa CCM imefika mahala pa kutumia njia yoyote kuendeleza maslahi yake binafsi. Ipo tayari kwa lolote. Na kimsingi sio suala la CCM kama chama bali maslahi binafsi. Katiba mpya inaonekana kama mkombozi wa walalahoi, chombo kitakachowarejeshea baadhi ya nguvu walizoporwa na wanasiasa. Sasa ni wazi kuwa chama ambacho uhai hake unategemea katika kuwakandamiza walalahoi hao lazima kitafute kila mbinu ya kuhakikisha aidha Katiba halisi-kwa maana ya yenye maslahi kwa mlalahoi haipatikani, au ikipatikana basi iendelee kuwa ya maslahi ya watawala wetu na CCM kwa ujumla.

Pengine kuna maneno niliyotumia katika makala hii ni makali na ya kukera, kwa mfano kuita watu 'wazembe wa kufikiri.' Lengo sio kumdhalilisha mtu yeyote bali kuamsha tafakuri. Ni muhimu tusiruhusu wahuni wa kisiasa kutupelekesha kama maboya. Ni muhimu kujenga na kuimarisha uwezo wa independent thinking, tafakuri inayojitegemea, isiyosukumwa na matukio-halisi au ya kubuni- bali hali halisi.  


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.