Kwanza,
bila kujali ukada wa CCM au Chadema au kutokuwa kada, ni muhimu kutambua kuwa
katika Tanzania yetu ya sasa – na pengine katika nchi nyingi za Dunia ya Tatu –
alichofanya Rais John Magufuli kinastahili pongezi.
Ofkoz,
alichofanya ni kazi yake, tunamlipa mshahara kama Rais wetu ili atutumikie, na
uamuzi wa kuunda tume mbili zakufuatilia kuhusu usafirishaji wa mchanga wa
madini ni sehemu ya kazi tuliyomwajiri aifanye.
Hata
hivyo, uzoefu watuonyesha kuwa katika Dunia ya Tatu, viongozi kuanzia viranja
darasani to wakuu wa nchi, hugeukia kuwa viumbe wa ajabu kabisa, na kusahau
kabisa watu waliowawezesha kupata madaraka husika.
Sote
tumeshuhudia jinsi watu wanavyotumia ovyo madaraka yao, kuanzia viranja shuleni
hadi wenyeviti wa vikao vya harusi, kutoka kwa “ma-admini” kwenye Whatsapp
groups hadi kwa wazazi kwenye familia, kutoka wajumbe wa nyumba kumi hadi mabosi
wetu makazini. Kwahiyo, katika mazingira tunayoishi, ni kama inatarajiwa kuwa “kiongozi
atende kinyume na matarajio ya wananchi waliomwajiri kuwatumikia.”
Kwamba
tumezowea kushuhudia vituko vya watawala wetu, wapole na wanyenyekevu wakati
wanaomba kura, lakini maharamia pindi wakiingia madarakani.
Wakati
mwingine tatizo sio viongozi hao as such bali wapambe, viumbe wanaonufaika kwa
uwepo wa fulani madarakani. Mfano wa hivi karibuni kuhus hili ni jinsi kundi la
“Mtandao” lililokuwa na mchango mkubwa kumwingiza madarakani Rais wa Awamu ya
Nne, Jakaya Kikwete, na likamfanya kuwa kama “mateka wao” kwa takriban miaka
yote 10 ya utawala wake.
Kwahiyo,
japo Magufuli amefanya kazi tuliyomwajiri kuifanya, anastahili pongezi kwa vile
“ameamua tu” kufanya jambo zuri. Twampongeza kwa kuamua kufanya jambo zuri
badala ya kufuata “utamaduni uliozoeleka” wa “bora liende.” Na kubwa zaidi,
hata angeamua kutofanya lolote, asingeathiriwa na lolote lile. Kwa kiongozi
kuamua kufanya kitu asichotegemewa kufanya, na ambacho hata kama asingekifanya
kisingemsababishia matatizo yoyote, basi hatuna budi kumpongeza bila kujali
itikadi zetu.
Baada
ya pongezi hizo, tuelekee kwenye ripoti husika. Kwa vile ninaamini watu wengi
wameshazisoma ripoti hizo, sintorudia kueleza yaliyomo kwenye ripoti hizo. Kama
hujazisoma, fanya urafiki na Google, andika “ripoti ya mchanga” utakutana nazo.
Makala
hii inaangalia maeneo makuu matatu: tulikotoka, tuliko na tuendako. Katika eneo
la kwanza, ninawaomba ndugu zangu wa Chama Cha Mapindui CCM waturuhusu tu
tuwalaumu kwa makosa yaliyopelekea Tanzania yetu kujikuta katika hali
tuliyonayo.
Rafiki
yangu Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM amekuwa akiniambia
kuwa “nina chuki binafsi” (sijui chuki binafsi na nani, ikizingatiwa nilikuwa
na mchango wangu japo kiduchu katika kampeni za Magufuli katika uchaguzi mkuu
uliopita mwaka 2015) kila ninapoishutumu CCM kwa mchango wake katika ufisadi
kwenye sekta ya madini.
Simalumu
Bwana Polepole kwa sababu ajira yake ni Msema Chochote (MC) wa chama tawala.
Tunapolumbana nae kwenye mitandao ya kijamii, mnufaika ni yeye maana analipwa “kusema
chochote.” Na kama nilivyoeleza hapo awali, madaraka huwabadili watu kuwa
viumbe wa ajabu kabisa. Polepole, mmoja wa watu walionnekana kuwa wenye busara
mno wakati wa mchakato wa Katiba mpya, leo anadiriki kutoa kauli zinazotubagua Watanzania
tunaoishi Ughaibuni, kama kwamba si Watanzania kamili, kwa vile tu baadhi yetu
tunaikosoa CCM.
Enewei,
makala hii si kumhusu kada huyo. Hoja yangu ni kwamba katika kuangalia tulikotoka,
hatuwezi kukwepa kuzungumzia Ilani za uchaguzi za CCM, miswaada mbalimbali ya
sheria iliyoungwa mkono na wabunge wa CCM, upinzani mkali wa CCM kupitia kwa
marais wake, mawaziri wake, wabunge wake na makada wake mbalimbali dhidi ya
mashujaa kutoka kambi ya upinzani – akina Dkt Slaa, Zitto, Tundu Lissu, Lema,
nk – waliopigana kufa na kupona kutetea raslimali zetu, na wakaishia kuadhibiwa
na uongozi wa Bunge ambao siku zote umekuwa kama muhuri wa kuidhinisha matakwa
ya awamu mbalimbali za serikali za CCM.
Kwa
vile kwa kupitia Ripoti mbili za mchanga tumeweza kufahamu ni kwa jinsi gani
tumefisadiwa, ili tuweze kusonga mbele na jitihada za kujiondoa kwenye ufisadi,
hatuwezi kuepuka “kuwajua wabaya wetu.” Huwezi kutibu maradhi kwa kuepuka
kuwafahamu bakteria au virusi waliosababisha madhara husika.
Kwahiyo,
japo twafahamu inawauma, ndugu zetu wa CCM “wawe wapole tu” wakati Watanzania
wanatoa hasira zao dhidi ya viongozi mbalimbali wa CCM walioshiriki kuwezesha
ufisadi kwenye sekta ya madini.
Baada
ya kuangalia tulikotoka, tunahamia kwenye tuliko muda huu. Ndio, tushasomewa
ripoti mbili zinazoeleza jinsi ambavyo tunaibiwa kwenye sekta ya mdani. Lakini
sidhani kama kuna Mtanzania anashangazwa na kilichomo kwenye ripoti hizo. Kama
mikataba ya madini inafanyiwa usiri kuliko tendo la ndoa, basi ni wazi kuna
masuala flani ambayo wananchi wa kawaida hawapaswi kuyajua. Na hawapaswi
kuyajua kwa vile yanawapora raslimali zao.
Halafu
hapa pia, CCM haiwezi kukwepa lawama kwa sababu kwa kiasi kikubwa – pamoja na
mzuri mengi ya chama hicho tawala – kimekuwa kichaka cha ufisadi. Sio siri
kwamba Watanzania wengi wanaiangalia CCM kwa jicho la mashaka linapokuja suala
la kulinda raslimali za nchi yetu. Rekodi ya chama hicho kwenye ufisadi
inatosha kabisa kukipatia OSCAR ya ufisadi: EPA, Kagoda,Richmond, Kiwira,
Buzwagi, Escrow…orodha ni ndefu mno.
Lakini
sote twajua lawama pekee hazijengi. Sawa, CCM haiwezi kukwepa lawama kwa kutufikisha hapa, lakini hatuwezi kuendelea
kulaumu milele bila kufanya jitihada za kusonga mbele. Na hata tukitaka
kuendelea kulaumu, ni muhimu kukumbuka kuwa sio tu Magufuli aliyechukua hatua
hizi ni mwana-CCM pia lakini vilevile angetaka kuendeleza kasumba ya CCM,
angeweza kabisa kupuuzia suala hilo.
Kwa
sasa, tunafahamu kiasi gani tumeibiwa. Hatua za kuchukua ni pamoja na
- - Makampuni ya madini ‘kukaliwa kooni’ yarejeshe tunachowaidai.
- - Watanzani wenzetu walioshiriki katika ufisadi huo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zao ili waturejeshee haki yetu
- - Tutengeneze mazingira ya kuepusha kujikuta tena katika hali kama hii huko mbeleni. Moja ya solutions ni Katiba Mpya (japo kwa bahati mbaya au makusudi, Rais Magufuli ameonyesha kuwa hiki sio kipaumbele chake)
- - Yanapokuja masuala la muhimu kwa nchi yetu, tusiangaliane kwa lesni ya “huyu wa CCM” AU “huyu mpinzani.” Ni wazi kuwa laiti tungesikiliza vilio vya akina Dkt Slaa, Zitto, Lissu, nk basi tusingefika hapa. Tofauti za kiitikadi sio uadui. Na hili pia ni fundisho kwa Bwana Polepole: akina Chahali kuwepo nje ya nchi hakumaanishi wanachopigia kelele kuhusu nchi yao ni “chuki binafsi.”
- - Pengine huu ni wakati mwafaka kuangalia uwezekano wa reforms kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwani ufisadi wote uliojiri katika sekta ya madini ulifanyika wakati ndugu zangu hao wakiwa ‘macho’ kazini.
Mapendekezo
ni mengi lakini angalau kwa sasa tunaweza kuanza na hayo.
Lakini
pengine kubwa zaidi ni kwamba kwa wakati huu tunapaswa kuwa kitu kimoja. Ni
muhimu tukubaliane kwamba tunapokumbana na mwizi, kila mtu ata-react kwa namna
yake. Kuna uwezekano mkubwa kwa wale waliowahi kutuambia “huyu mwizi”
tukawapuuza, wakatunyooshe vidole na kutukumbusha “tuliwaambia.” Haina haja ya kuwachukua,
Wanatukumbusha na kutuambia ukweli. Kama kina Lissu walinyanyaswa na
kubughudhiwa kwa hayahaya tunayoyashangaa leo, kuna dhambi gani kwa wao
kutukumbusha kuwa walishatutahadharisha huko nyuma?
Pamoja
na pongezi kwa Magufuli kwa kuchukua hatua ya kuanzisha tume ya kuchunguza
kuhusu mchanga wa madini, ninamlaumu kwa lugha yake ambayo haiwezi kutusaidia
katika kipindi hiki tunachohitaji ushairikiano bila kujali itikadi zetu.
Maagizo yake kwa Spika Ndugai (mtu ambaye hapaswi kuongea lolote kuhusu wizi wa
madini yetu kwa sababu ‘kila Bunge la CCM’ limekuwa wawezeshaji wa wizi huo)
yanajenga mfarakano tu badala ya umoja tunaohitaji kipindi hiki.
Sijui
kwanini Rais Magufuli anapenda sana kutengenezea ‘bifu’ zisizo na umuhimu. Hivi
akitoa wito kuwa Watanzania wote tushirikiane, na kuwakaribisha wapinzani
katika mapambano haya, atapungukiwa nini? Mbona ‘kiongozi mkuu wa upinzani’
Edward Lowassa, kammwagia pongezi Magufuli kwa hatua alizochukua kuhusu suala
hilo la madini? Ni muhimu kwa Rais wetu kukumbushwa kuwa siasa za uhasama sio
tu hazina fursa katika Tanzania yetu bali pia hazina faida.
Kuhusu
jinsi ya kuwashughulikia watu waliohusika katika ufisadi kwenye sekta ya madini,
tuna njia mbili tu: aidha, kufumba macho na kumsomba kila aliyehusika, na hii
itajumuisha marais wastaafu, au, tuendeshe mambo Kiswahili, tuchukue hatua kwa
wale tu ‘wasio na madhara makubwa,’ na kuwastiri ‘watuhumiwa muhimu’ kama vile
marais wastaafu.
Tatizo
la hiyo approach ya pili ni kwamba hao ‘wasio na mdhara makubwa’ watajitetea
kirahisi tu kuwa maamuzi yao yalitokana na ridhaaza ‘watuhumiwa muhimu.’
Je
inawezekana suala hili ambalo linanapaswa kushughulikiwa na mkono mrefu wa
sheria likafanywa bila kuingiza siasa? Yes, inawezekana lakini sio rahisi kwa
Tanzania yetu hii. Ila ni mapema mno kutoa hukumu. Acha muda uongee.
Tunakolekea?
Well, Sie kama Watanzania tunapaswa kuacha kuwa ‘wapole’ kupita kiasi. Muda huu
tulipaswa kuandamana kulaani waliotuibia, lakini kama kutakuwa na maandamano
basi ni ya kisiasa ya kumpongeza Magufuli kutueleza kile ambacho tunakifahamu
muda mrefu tu. Ni lini Watanzania wataamka na kudai – kwa amani – haki zao za
msingi? Hivi ni lini Watanzania watashinikiza viongozi wetu waweke mbele
maslahi ya nchi yetu badala ya maslahi yao binafsi?
Na
kufumbukiwa macho suala la mikataba ya madini kuwe mwanzo wa safari ndefu ya “kudai
chetu.” Tunataka mikataba ya gesi na
mafuta sio tu iwekwe wazi bali itafsiriwe kwa Kiswahili ili kila Mtanzania
aisome.
Tunataka
pia mikataba ya ununzi wa Bombadier nayo iwekwe wazi, ili huko mbeleni
tusijikute tukilazimika kuunda tume nyingine.
Tunataka
mikataba ya utalii, iwekwe hadharani. Tujue nani anatorosha wanyamapori wetu,
nani baada ya kupewa Ukatibu Mkuu ghafla biashara ya ujangili nayo ikaanza
kupaa, tuambiwe watu waliondoka na magunia ya fedha kwenye utapeli wa Escrow ni
akina nani (sio wale tulitajiwa kuhusu ‘benki ya waswahili’ bali Stanbic),
tunataka kila kilichofichwa kiwekwe wazi.
Lakini
ili hayo yote yawezekana, ni muhimu sote wenye uchungu wa nchi yetu tuwe kitu
kimoja. Na nitumie fursa hii kumwomba tena Rais Magufuli ajaribu ku-embrace
consensual politics (siasa za kufikia mwafaka) badala ya hizi za mifarakano
(conflictual politics). Afterall, Haijalishi mtu ni CCM, Chadema, CUF au hana
chama, sote ni Watanzania.
Uchambuzi
huu ni endelevu. Kwa leo naomba kuishia hapa. Swaumu njema kwa ndugu zangu
Waislamu. Asanteni