6 Dec 2013

WIKI iliyopita nilizungumza na rafiki yangu mmoja, Mtanzania mkazi wa hapa Uingereza, ambaye alikuja likizo huko nyumbani hivi karibuni. Katika maongezi yetu, rafiki yangu huyo alionekana kuguswa na mambo kadhaa aliyoyashuhudia huko. Pengine kushangazwa kwake huko kulichangiwa na ukweli kwamba amekuwa mkazi wa hapa Uingereza kwa takriban miaka 20, na hutembelea huko nyumbani kwa nadra.
Katika hali ya kusikitisha, alikaribishwa nyumbani na 'wahalifu wa kola nyeupe' (white collar criminals), ambao katika mazingira ya kushangaza walifanikiwa kumwibia simu tatu. Kwa maelezo yake, wizi huo unaelekea kufanywa na wahusika katika uwanja wa ndege, lakini kilichomkera ni suala hilo kuonekana la kawaida kabisa kwa aliowaeleza.
Baada ya tukio hilo la wizi alipata fursa kadhaa za 'kuyaona maisha halisi ya Tanzania zaidi ya simulizi za mtandaoni au kwingineko. Anasema wakati kwa kuangalia haraka haraka, Jiji la Dar es Salaam limepiga hatua kubwa kwa majengo na idadi ya magari, hali huko vijijini ya kusikitisha mno. Alibainisha kuwa wakati wengi wa ndugu, jamaa na marafiki jijini Dar walionekana kuridhika na maisha (angalau kimaongezi), hali ya vijijini imetawaliwa na kukata tamaa ya maisha, huku dalili za umasikini zikiwa zimetawala kila kona.
Lakini moja ya mambo yaliyomgusa zaidi ni uwajibikaji ofisini. Alinieleza kuwa alipokuwa Dar alikaribishwa katika baadhi ya ofisini na rafiki zake kadhaa wenye nyadhifa muhimu katika sehemu wanapofanya kazi. Kwa kiwango kikubwa, wengi wa mabosi hao hawakuonekana kuchukulia majukumu yao ya kiofisi kwa umakini na baadhi hawakusita kumwambia "hii ndiyo Bongo bwana," kwa maana ya 'Who cares?' (Nani anajali?) hata wakiboronga kazi.
Alichobaini ni kwamba wengi wa mabosi hao 'wanakula vizuri' na mabosi walio juu yao, aidha makao makuu au wizarani. Kadhalika, katika nyingi ya ofisi alizotembelea aligundua kuwa wengi wa mabosi ni kama 'miungu-watu' kiasi kwamba uwezekano wa watumishi wa chini kuwakosoa mabosi wao, hata kama ni kwa manufaa ya ofisi husika, haupo.
Kingine alichoshuhudia ni jinsi ofisi za mabosi hao zilivyosheheni samani za gharama kubwa. Japo rafiki yangu huyo ni mmoja wa mameneja wachache Watanzania hapa Uingereza, alibaki mdomo wazi kuona sofa, televisheni na vikorombwezo vingine vya thamani ya juu katika takriban kila ofisi ya bosi aliyemtembelea. Alieleza kuwa inaonekana kama ni fasheni fulani kwa kila kiongozi katika taasisi kuhakikisha ofisi yake ni kama Ikulu ndogo kutokana na kusheheni samani za gharama na vitu vingine vya gharama kubwa.
Kadhalika, licha ya wengi wa marafiki zake hao wenye nyadhifa kumjulisha kuwa wanalipwa mishahara minono, walionekana kutumia muda mfupi ofisini, huku katika muda huo mfupi wakiwa ‘bize’ na masuala binafsi kuliko ya kiofisi. Anasema baada ya maongezi ya takriban nusu saa katika ofisi ya kigogo fulani, alijisikia kama anachukua muda muhimu wa kigogo huyo na hivyo kuamua kuaga. Kwa mshangao, kigogo huyo alimlazimisha waendelee na maongezi huku akidai hana jambo muhimu la kufanya ilhali taasisi anayoiongoza inalalamikiwa na wananchi kwa utendaji kazi kwa 'kasi ya konokono.'
Kuhusu ufisadi, alinihakikishia kuwa umekuwa ni kama utamaduni muhimu katika taasisi nyingi (angalau alizozitembelea huko nyumbani). Alinipa mfano wa ofisa mmoja mwandamizi katika taasisi moja ya umma ambaye amepangishiwa nyumba na taasisi hiyo na analipiwa dola 1,500 za Marekani (sina hakika ni kwa mwezi au kwa mwaka). Kichekesho ni kwamba yeye ndio mmiliki wa nyumba hiyo. Kwa hiyo licha ya kukaa bure katika nyumba anayoimiliki bado analipwa kodi ambayo ni mamilioni ya shilingi za Kitanzania.
Lakini wakati alishuhudia baadhi ya Watanzania wenzetu wanaoishi maisha ambayo hata kwa sie huku Uingereza ni ya kufikirika tu, kuna hali tofauti kabisa aliyoshuhudia hapo hapo jijini Dar es Salaam. Alinieleza kuwa katika baadhi ya maeneo aliyoyaita ya 'uswahilini' alishuhudia kilo ya sukari ikiuzwa kwa vijiko ili wananchi wasio na uwezo wamudu kununua ‘vijiko’ kadhaa kwa ajili ya chai. Binafsi, nilishawahi kusikia taarifa kama hiyo kabla kuja huku lakini sikupata fursa ya kushuhudia bayana.
Kwa mujibu wa maelezo ya rafiki yangu huyo, kuna baadhi ya familia 'uswahilini' jijini Dar es Salaam zinaishi katika chumba kimoja, ambapo baba, mama na watoto hawana faragha yoyote. Kadhalika, alieleza kuwa katika maeneo hayo ni jambo la kawaida kwa binti kuondoka 'kwenda kutafuta hela' na wazazi hawana kizuizi kwani bila hivyo siku inaweza kupita bila 'mkono kwenda kinywani.'
Kufikia hapa, ninapenda kukuomba samahani msomaji mpendwa kwa 'simulizi' hii ndefu. Lakini nimekusudia kuifanya mada ya makala hii ili angalau iibue tafakuri kuhusu mwelekeo wa jamii yetu na hatma ya taifa letu. Katika maelezo ya rafiki yangu, kitu kimoja kilicho bayana ni pengo kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho (nafasi hairuhusu kuelezea uzoefu wa rafiki yangu kuhusu 'vijana wenye utajiri wa ajabu' ilhali shughuli wanazofanya hazieleweki).
Pengo hilo linachangia sana hali ya 'who cares' kwani kimsingi kwa wenye uwezo, mtizamo ni 'nani anajali ilimradi mie nile kama mbuzi ninayekula kwa urefu wa kamba yangu?' Na kwa walalahoi nao, mtizamo ni huo huo wa 'nani anajali kama wanafilisi nchi yetu ilhali nimemudu kupeleka mkono kinywani?'
Kuna tatizo jingine ambalo niliwahi kulizungumzia katika moja ya makala zangu huko nyuma; upungufu wa tabaka la kati unaochangia kukwamisha jitihada za kulisaidia au kulikomboa tabaka la walalahoi au kupambana (angalau kwa njia za amani) na tabaka la vigogo ili angalau kujenga jamii yenye usawa. Kwa tabaka la kati (ninatambua kuna wanaohoji kama kweli Tanzania yetu ina tabaka hilo), wengi wa waliomo humo wanatamani kuwamo ndani ya tabaka la vigogo na pale matamanio hayo yanapokuwa magumu basi wanajifariji kwa kuishi kama vigogo. Mfano mwepesi ni wababaishaji tunaowashuhudia wakituza maelfu ya shilingi kwenye dansi au sherehe ilhali hali zao binafsi kiuchumi ni taabani.
Na kama kuna kasumba ‘kongwe’ kwa tabaka hili, au pengine 'ugonjwa' unaosumbua Watanzania wengi ni kupenda sifa zisizo na msingi. Si jambo la ajabu kushuhudia mtu mwenye kipato cha wastani tu akijihangaisha kuishi 'maisha ya maonyesho' kwa minajili tu ya kupata sifa mtaani. Na baadhi ya 'mabishoo' hawa ni watu wasio na msaada wa familia na jamii hususan katika maeneo yao ya asili. Sasa ni wazi kuwa ni vigumu kwa ‘kizazi hiki cha wapenda sifa' kuwa na mchango wowote kuunganisha nguvu na tabaka la walalahoi kulibana tabaka la vigogo kujenga jamii iliyo sawa.
Nimalizie makala hii kwa kukuhamasisha wewe msomaji wa makala hii kufikiria zaidi ya maslahi yako binafsi. Msingi wa maendeleo ya nchi kama hapa Uingereza ulijengwa na vizazi vilivyoishi miongo, kama si karne, kadhaa zilizopita. Je, tunapata fursa ya kutafakari Tanzania yetu itakuwaje angalau miaka 50 ijayo? Tukumbuke kuwa pasipo jitihada za makusudi kubadili mwenendo wa mambo huko nyumbani, basi hatutokuwa na jinsi ya kuzuia wajukuu zetu kuyashambulia makaburi yetu kwa hasira huku wakishangaa jinsi tulivyowaachia nchi iliyo tupu kwa raslimali na jamii iliyo tupu kimaadili.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

4 Dec 2013

28 Nov 2013


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

27 Nov 2013

Eneo la Canary wharf london ambalo Balozi Peter Kallaghe alifanya  ziara ya kutembelea kampuni ya Kitanzania, Meru Services LTD. 
Tarehe 23 Novemba 2013, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe alifanya ziara ya kutembelea kampuni ya Meru Services inayomilikiwa na watanzania waishio jijini London, Uingereza.

Katika ziara hiyo iliyofanyika katika kitovu cha sekta ya biashara na fedha nchini Uingereza, Canary Wharf , Balozi Kallaghe alijionea huduma zinazotolewa  na kampuni hiyo katika Benki ya Kimataifa ya Credit Suisse. Pia alikutana na kuzungumza na baadhi ya watanzania wanaofanya kazi za aina mbalimbali za kuhudumia Benki hiyo .
Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni ya Meru Services LTD, Bw. Dullah Meru akiongea machache na balozi Peter Kallaghe
Balozi Kallaghe alifurahishwa na taarifa aliyopewa kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma katika Benki ya Credit Suisse kwa bidii ,ujuzi na uaminifu mkubwa kwa takriban miaka 15. Aidha imekuwa ikitoa fursa za ajira kwa makundi mbalimbali ya watanzania wakiwemo wanafunzi waishio jijini London.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Axis Europe PLC Bw Dean Richards akimuelezea balozi Kallaghe Umuhimu kuwepo kwa kampuni ya Meru Servives katika eneo hilo la canary wharf.
Katika nasaha zake, Balozi Kallaghe aliitaka kampuni ya Meru Services kutambua kuwa kuaminika kufanya kazi katika kitovu cha sekta ya biashara na fedha nchini Uingereza si jambo dogo na kuisihi kampuni hiyo iendelee kuitunza heshima hiyo kwa niaba ya watanzania wote. 

Balozi pia alitoa changamoto kwa  kampuni hiyo na watanzania waishio nchini Uingereza kutumia ujuzi na uzoefu wanaopata ughaibuni kama mtaji wa kuwekeza katika sekta ya huduma inayozidi kukuwa nchini Tanzania.

Balozi alihitimisha ziara yake kwa kuahidi kuwa ataendelea kushirikiana na kampuni za kitanzania na vijana wa kitanzania wanaoishi Uingereza katika kuwaunganisha na fursa za kiuchumi zinazojitokeza nchini Tanzania wakati huu.
Balozi Kallaghe na Afisa ubalozi Allen Kuzilwa wakifuatila jambo kutoka kwa Dean
Ahmed na Dullah Meru Mkurugenzi mmiliki wa Meru Services LTD wakisikiliza kwa makini
Said Surur akimuelezea Balozi jambo wakati wa mkutano pembeni yake kulia ni Allen Kuzilwa Afisa Ubalozi
Balozi katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanayakzi wa Meru Services Ltd

PICHANI CHINI NI BAADHI YA KAZI ZINAZOFANYA NA MERU SERVICES LTD. NA  ZILIZO KAMILIKA




Mgahawa wa wafanyakazi uliofanyiwa ukarabati na kampuni ya Meru Services 

Vijana wakiwa kazini kuweka nafasi ya kwa ajili ya wafanyakazi wapya 210 wanao hamia Credit Suisse London. 
Huu ndo muonekano baada ya kazi kukamilika .
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati
Picha za kushoto ni kabla ya ukarabati na kulia ni baada ya ukarabati



26 Nov 2013


.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.



Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.