17 Jul 2017

Kabla ya kuingia kwa kina kwenye uchambuzi huu, ni muhimu kueleza bayana kwamba japo maana, mbinu na ufanisi wa uchambuzi wa kiintelijensia ('intelligence analysis' kwa kimombo) kati ya mie niliyepo hapa Glasgow na afisa mchambuzi wa intelijensia aliyepo Dar zaweza kuwa karibu na sawa, mazingira kati yangu na ya afisa huyo ni tofauti. Tofauti sio kwa vile mie nipo Uingereza na afisa husika yupo Tanzania bali vitu kama shinikizo la kupata majibu upesi na nyenzo mbalimbali kama vile watoa habari, mafaili, nk.


Pili, nitajitahidi kadri nitakavyoweza kuepuka 'mtazamo wangu' na badala yake niongozwe na kanuni za uchambuzi wa kiintelijensia. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa moja ya nyenzo muhimu kwenye intelijensia ni mwanadamu, iwe kwenye kukusanya taarifa za kiintelijensia, kuchambua au kushauri. Kwahiyo, japo nitajitahidi kuepuka 'mtazamo wangu,' siwezi kuepuka ubinadamu wangu kama mchambuzi wa kiintelijensia wa somo husika.


Kwa kifupi, tuanze na tunachofahamu hadi muda huu. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mauaji yanayojumuisha eneo la Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) yalianza Januari 2015 na hadi sasa yamegharimu uhai wa watu 40 wakiwemo askari polisi 13.


Tukisema tuorodheshe mlolongo wa kauli za viongozi mbalimbali, wa serikali na wa jeshi la polisi, basi huenda itabidi kukesha hapa, au kuandika kitabu kizima. Hata hivyo, kwa kifupi, miongoni mwa kauli hizo ni kama ifuatavyo

Rais John Magufuli

Kwa ujumla, Rais Magufuli ametoa matamko makubwa matatu kuhusu mauaji yanayoendelea katika eneo la MKIRU. Tamko la kwanza ni salamu za rambirambi alizotoa kufuatia mauaji ya askari polisi wanane, ambapo alilaani mauaji hayo. Hiyo ilikuwa April 14 mwaka huu. 


Tamko la pili la Rais lilikuwa  majuzi alipofanya ziara mkoani Pwani ambapo Juni 20 aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali na vyombo vya dola ili kukomesha mauaji hayo. Rais alieleza kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya mauaji "tunakaa nao, tunawaficha, ni watoto wetu." Kadhalika, Rais Magufuli alieleza kuwa "serikali ya Awamu ya Tano sio ya kuchezewa" na kudai kuwa "(wauaji hao) wameshaanza kunyooka."


Hata hivyo, siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo ya kutia matumaini, askari polisi wawili waliuawa na gari lao kuchomwa moto, pengine ikiwa ni jibu la wauaji hao kwa Rais aliyedai kuwa "wameshaanza kunyooka."


Tamko la tatu la Rais, na pengine kali kuliko hayo mawili, lilitolewa jana  jijini Dar wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa Bandari ya Dar, ambapo katika kilichoonekana bayana kuwa majibu kwa rai ya Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kwa Rais Magufuli kumtaka atafakari kuhusu 'mashehe wa Uamsho' wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.


Katika tamko hilo Rais aliwaomba wanasiasa wanaosema kuwa hawa (mashehe wa Uamsho) wameshikiliwa kwa muda mrefu "wajizuwie midomo yao," na kudai kuwa "hata kuna watu kule Marekani walikaa Guantanamo muda mrefu," na kudai kuwa (wanaoongea kama Lowassa kuwa kesi yao ishughulikiwe) inaweza kuwafanya watu kuhisi (anayesema hivyo) ni "mmoja wao."


Rais Magufuli alihoji "kwanini hata siku moja mtu asijitokeze kualaani wanaouawa bila hatia kule (MKIRU), lakini kwa kutafuta sifa za kisiasa, mtu anatoka anasema watu wako ndani muda mrefu." Rais aliwataka polisi kufanya kazi yao, na kuwaagiza kuwakamata "hao wanaoropoka waisaidie polisi," na "msiogopee sura, awe na mwendo wa haraka, polepole au kukimbia, mkamateni kusudi akaisaidie polisi kule ndani."


Rais alidai pia mtu aliyekamatwa na sare 500 za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni "inaonekana anahusiana na walioko ndani (mashehe wa Uamsho)." 


Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wake  Yusuph Masauni


Kwa nyakati mbalimbali, viongozi hawa wawili wametoa kauli kadhaa kuhusiana na mauaji yanayoendelea huko MKURU. Kuorodhesha kauli zote kwahitaji makala nyingine pekee, lakini kwa kifupi, Waziri Mwigulu ameshanukuliwa akidai kuwa "mauaji hayo yana harufu ya kisiasa," na kuhoji "Ujambazi gani huo wa Wana CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.” 


Waziri Mwigulu alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa chanzo cha mauaji hayo ni chuki za vyama vya upinzani dhidi ya CCM.


Awali Waziri Mwigulu alieleza Bungeni kuwa serikali imeshabaini kuwa  wanaohusika na mauaji hayo wanatoka maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, na kwamba changamoto ya mauaji hayo ipo mbioni kutatuliwa.


Kwa upande wake, Naibu Waziri Masauni amenukuliwa akieleza kuwa serikali inalipa kipaumbele suala hilo na lazima mauaji hayo yadhibitiwe. "Tuweze kuharakisha zoezi hili ambalo kwa hakika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa sisi tunaosimamia haki na uhai wa raia wasio kuwa na hatia hii vita lazima tushinde inshaallah,” alinukuliwa Masauni hivi karibuni.


IGP Sirro na mtangulizi wake IGP Mangu:


Wakati IGP Simon Sirro ameanza jukumu hilo la ukuu wa jeshi la polisi wakati jeshi hilo likikabiliwa na changamoto za mauaji ya MKURU, mtangulizi wake IGP Mangu huenda akakumbukwa zaidi kwa onyo lake la kuwasaka "watu waliofurahia mauaji ya askari wanane," kauli ambayo ilionekana kama 'kusaka adui wa kufikirika.' Hata hivyo, suala hilo aliloongelea IGP Mangu lilipaswa kuibua tafakuri pana na endelevu kuhusu uhusiano mbovu kati ya jeshi la polisi na wananchi. 


Kadhalika IGP Mangu alieleza kuwa jeshi lake lingeanza kutumia nguvu ilizonazo kulazimisha upatikanaji wa taarifa kuhusu mauaji hayo.


Kwa upande wa IGP Sirro, masaa machache tu baada ya kukutana na wazee wa Kibiti na Rufiji kujadiliana nao kuhusu mauaji hayo, mkazi mwingine aliuawa na watu wasiojulikana. Awali, IGP Sirro aliwaeleza waandishi wa habari kuwa "wauaji hao hawatachukuwa muda mrefu kukamatwa" na kwamba "siku zao zinahesabika." Kadhalika, mkuu huyo mpya wa jeshi la polisi alidai kuwa maongezi yake na wazee wa Kibiti na Rufiji yatafanikisha kukamatwa kwa wauaji hao.


Baada ya kuteuliwa wadhifa huo, IGP Sirro alitangaza dau la shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.


Juni 25 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa jeshi lake halifahamu wahusika wa mauaji hayo, kauli iliyokinzana na ya bosi wake, Waziri Mwigulu kwamba chanzo cha mauaji hayo ni chuki ya vyama vya upinzani kwa CCM.

Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alieleza kuwa mauaji hayo ya MKIRO 'yana mkono kutoka nje ya nchi' bila kufafanua nchi gani inayohusika. Kadhalika, taarifa hiyo iliyaeleza mauaji hayo kama yaliyokuwa yakiendelea kwa takriban miaka mwili sasa.


Edward Lowassa: 


Rai ya Lowassa kwa Rais Magufuli kuhusu hatma ya 'mashehe wa Uamsho' nimeitaja hapo juu, lakini kwa urefu, habari hiyo ipo HAPA.


Zitto Kabwe


Kufuatia kilichotafsiriwa kama majibu ya Rais Magufuli kwa Lowassa, kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe alitoa maoni yake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook. 


 Uchambuzi wa kiintelijensia

Hadi muda huu, hakuna kikundi kilichojitokeza hadharani kudai kuhusika na mauji hayo. Hata hivyo, bila hata kuhitaji uzoefu wa kishushushu, sio vigumu kuhisi kuwa 


1. Mauaji hayo yanafanywa na kikundi maalum
2. Wahusika ni watu wenye uelewa/uzoefu wa mbinu za mauaji 

Hata hivyo, licha ya kutojitokeza kikundi chochote kudai kuhusika na mauaji hayo, taarifa zilizopatikana siku chache zilizopita zilieleza kwamba kuna ujumbe uliotumwa na 'wahusika wa mauaji hayo,' unaosomeka kama ifuatavyo
Tunawatangazia wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hadi nyumbani kwake. 

Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini.

Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!
Kwa mujibu wa taarifa, ujumbe huo uliandikwa kwa kalamu na kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Turudi nyuma kidogo hadi mwaka 2013 ambapo kulitokea uhasama mkubwa kati ya Polisi na baadhi ya wakazi wa Kibiti kufuatia kifo cha mkazi mmoja wa eneo hilo, Athuman Hamis aliyefariki kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo cha polisi (kwa mujibu wa maelezo ya wakazi hao).

Habari kamili ipo HAPA


Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia wa suala kama hilo la mauaji hayo ya MKIRU, yahitajika vitu viwili. Kwanza, kuwa na maelezo sahihi kuhusu tatizo husika, na pili, matokeo tarajiwa zaidi ni yapi.

Katika uchambuzi wa mauaji hayo ya MKIRU, ninatumia moja ya njia za uchambuzi wa kiintelijensia, inayojulikana kama ACH - Analysis of Competing Hypotheses - yaani Uchambuzi wa Dhana Zinazoshindana.

Hatua ya kwanza ni kutambua dhana husika. Ili kupata dhana hizo, niliendesha kura ya maoni isiyo ya kisayansi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Vipengele vinne vilivuounda swali husika vilitokana na maelezo mbalimbali yaliyokwishatolewa kuhusu zinazoweza kuwa sababu za mauaji huko MKIRU

Kama inavyoonekana katika 'tweet' hiyo yenye matokeo ya kura ya maoni, dhana kuu nne ni 
  1. Ugaidi
  2. Chuki za kisiasa
  3. Chuki za wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi
  4. Uhalifu kama mwingine
Kuorodhesha dhana hizo (kama ilivyo hapo juu) na kuzipitia kwa kina zaidi na kujumuisha 'ushahidi uliopo' kwa kila moja (kama inavyofuata hapa chini) ni hatua ya pili ya ACH.

Tuanze na dhana kuwa mauaji hayo yanatokana na chuki za wananchi. 'Ushahidi' kuhusu dhana hii ni wa aina mbili. Kwanza, Januari 23, 2013, kulijitokeza vurugu kubwa huko Kibiti zilizolazimu jeshi la polisi kutumia helikopta kuzidhibiti. Vurugu hizo zilitokana na kifo cha mkazi mmoja wa Kibiti aliyefariki Hospitali ya Taifa Muhimbili alikopelekwa kutibiwa majeraha ambayo ilidaiwa aliyapata kutokana na kupigwa na polisi.

Vurugu hizo zilipelekea Barabara ya Kilwa kufungwa kwa zaidi ya amsaa matatu, na hivyo kuathiri usafiri kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi; sambamba na wananchi kuvamia kituo kimoja cha polisi na kuchoma moto nyumba moja ya polisi.


'Ushahidi' wa pili wa dhana kuwa chanzo cha mauaji ya MKIRU ni chuki za wananchi dhidi ya jeshi la Polisi ni ripoti maalum ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi iliyochapishwa Mei 26 mwaka huu. 

Kwa kifupi, ripoti hiyo inaeleza kwamba wengi wa wakazi wa MKIRU ni masikini wenye elimu duni, na tegemeo lao kubwa la kipato ni kuvuna raslimali nyingi zilizopo eneo hilo na kuzuza. Biashara kubwa ambayo vijana wanajihusisha nayo ni uchomaji na uuzaji wa mkaa, uvunaji magogo kwa ajili ya mbao, uuzaji wa kuni na mazao mengine ya mashambani kama vile mpunga na mihogo, imeajiri vijana wengi katika maeneo hayo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofnywa na mamlaka za mitaa, maofisa wa Idara ya Maliasili, jeshi la mgambo na polisi. 

Licha ya mamlaka husika kuweka lundo la vizuizi, pia wananchi hao walilalamikia 'kodi za kukomoana.' Kwa miaka mingi sasa, wananchi wamekuwa wakilalamikia vizuizi hiyo kuwa kitovu cha dhuluma na uonevu mkubwa wanaofanyiwa wananchi na wasimamizi wa vizuizi ambao wamekuwa wakikadiria kodi za kukomoa, kutaifisha magunia ya mkaa na mbao na mali nyingine za wananchi.

Wananchi hao wanadai kuwa  uonevu na dhuluma  vimechokoza hasira za vijana wengi, ambao "kazi zao ndio mkaa, kuni na mbao au mihogo." Kuhusu matumizi ya silaha, ilielezwa kuwa  vijana wengi katika maeoeneo hayo  wana mafunzo ya mgambo na JKT huku wakiwa hawana ajira nyingine zaidi ya kutegemea biashara hizo.

“Si suala la kidini. Ni manyanyaso tu. Leo unadhulumu watano, kesho kumi, hawa wakiji-organise unatarajia nini?” aliuliza mkazi mmoja wa eneo hilo, na kuongeza kuwa ingawa dhehebu moja la kidini lina vijana wengi lakini halina uhusiano na mauaji.
Kuhusu dhana nyingine kwamba mauaji ya MKIRU yantokana na ugaidi, kuna 'ushahidi' wa matukio mbalimbali kwa takriban miaka mitano sasa ambayo japo serikali imekuwa ikiyaita kuwa ni ujambazi, yana viashiria vya ugaidi.
Moja ya vitu vinavyoleta ugumu katika kutanabaisha ugaidi au lani kasumba iliyoshamiri kitambo ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wepesi kuwatuhumu wapinzani wao wa kisiasa kuwa wanapanga au wanajihusisha na vitendo vya kigaidi kwa minajili tu ya uhasama wa kisiasa.
Baadhi ya wanasiasa wa chama tawala CCM, kwa nyakati tofauti wamewahi kuvituhumu vyama vya upinzani vya CUF na Chadema, na baadhi ya viongozi na wanachama wake, kuwa wahusika wa ugaidi, tuhuma ambazo mara zote hazikuweza kuthibitishwa.
Japo magaidi hupendelea wafahamike kuwa ndio wahusika wa tukio la kigaidi, kunapojitokeza watu wasio na hatia kutuhumiwa kuwa ndio magaidi, hiyo inaweza kurahisisha kazi ya magaidi halisi.
Katika mlolongo wa matukio mbalimbali yenye viashiria vya ugaidi, Julai 2 mwaka huu, Rais Magufuli aligusia kuhusu 'mashehe wa UAMSHO' ambao wapo gerezani kwa zaidi ya miaka minne sasa wakisubiri hatma ya mashtaka ya ugaidi yanayowakabili. Katika hotuba yake jijini Dar, Rais Magufuli aliashiria kuwa kuna uhusiano katika ya mauaji ya MKIRU na mashehe hao wa UAMSHO, huku akiibua taarifa mpya kuwa hata sare 500 za jeshi zilizokamatwa jijini Dar zilikuwa na uhusiano na mashehe hao/ 'ugaidi' huko MKIRU.

Kadhalika, Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa mauaji ya MKIRU yana 'mkono wa nchi za nje.' Kingine cha muhimu katika maelezo ya IGP Sirro ni kubainisha kuwa mauaji ya MKIRU yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili.

Tukio jingine ni pamoja na lile la Mei mwaka jana huko Mwanza ambapo kulitokea mapambano makali kati ya askari wa jeshi la polisi wakisaidiwa na wenzao wa Jeshi la Wananchi dhidi ya kilichoelezwa na serikali kuwa ni genge la majambazi. Mapambano hayo yalielezwa kuwa na uhusiano na uvamizi kwenye msikiti wa Rahman jijini humo, ambapo kulitokea mauaji ya kutisha baada ya watu wasiofahamika kuvamia msikiti huo na kuwauwa kwa kuwachinja  Imamu aliyekuwa akiswalisha swala ya Isha, Ferouz Elias (27) na waumini wawili, Mbwana Rajab na Khamis Mponda.
[​IMG]
Tukio jingine lilitokea Novemba 22 mwaka jana ambapo Jeshi la Polisi lilikamatwa wanawake wanne na watoto wannewaliodaiwa kuwa katika mafunzo ya kigaidi, huko Vikindu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam


Tukio jingine ni lile la Machi 2 mwaka juzi ambalo lililozua taharuki miongoni mwa Watanzania wengi kufuatia kuibuka kwa video yenye ujumbe ulioashiria uwepo wa kundi linalopambana na jeshi la polisi kwa sababu za kidini


Kadhalika, Juni mwaka 2015, taasisi ya ACLED ilitoa taarifa iliyoonyesha kulikuwa na ongezeko la matukio yenye viashiria vya ugaidi. Ripoti hiyo iliyoambatana na majedwali yanayoonyeshwa mwenendo wa matukio hayo ilitokana na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari vya Tanzania.
Figure 1 Number of Conflict Events & Fatalities in Tanzania, from June 1, 2014 - May 25, 2015

Taarifa hiyo ambayo unaweza kuisoma HAPA ilibainisha kwamba Tanzania ina vikundi vidogo vya kigaidi vyenye uhusiano na kundi la Al-Shabaab la Somalia au Al-Hijra la Kenya. Vikundi hivyo ni pamoja na Ansar Muslim Youth Centre cha mjini Tanga.

Pia, Novemba mwaka 2013, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu 69 waliokuwa kwenye kilichoelezwa kuwa ni mafunzo ya kigaidi kuhusu kundi la Al-Shabaab. 

Vilevile, takriban mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, watu  wengine 11 walikamatwa na Polisi mjini Mtwara wakituhumiwa kujihusisha na kundi la Al-Shabaab.

Kadhalika, mwezi huohuo,  mfanyabishara Juma Abdallah Heri alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kufadhili vikundi vya kigaidi nchini Tanzania.

Mwendelezo wa matukio hayo ni pamoja na lile la April mwaka jana ambapo zilipatikana taarifa kuwa Mtanzania Issa James Mwesiga aliuawa na kundi la Al-Shabaab nchini Somalia kwa tuhuma za ujasusi. Inaelezwa kuwa Mtanzania huyo alijiunga na kundi hilo la kigaidi mwaka 2013.


Agosti 2015, Watanzania sita walikamatwa huko Garissa, nchini Kenya wakiwa njiani kuelekea Somalia kujiunga na kundi la Al-Shabaab. Walikutwa na mabomu saba na bastola saba.


Awali, Machi mwaka huohuo, mwanamke mmoja, Ummur Kayr Sadir, alikamatwa na wenzie wawili wakiwa safarini kwenda Somalia kujiunga na kundi hilo la kigaidi.

Septemba mwaka jana, taasisi ya Intergovernmental Authority on Development (IGAD) ilitoa ripoti iliyoeleza kuwa kundi la Al-Shabaab lilikuwa ikifanya jitihada kubwa kupata wafuasi wa kiume na kike wa kujiunga na kundi hilo, hata nje ya Somalia (lilipo kundi hilo) na Tanzania, Uganda, Ethiopia na Djibouti zilikuwa zilikilengwa katika jithada hizo.

Februari 28 mwaka jana, watu watatu waliuawa na polisi jijini Arusha, huku taarifa zikieleza kuwa watu hao walikuwa wanakikundi wa Al-Shabaab.

Juni mwaka jana, watu wanane waliuawa kinyama huko Tanga, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya tukio jingine la kinyama jijini Mwanza ambapo Imamu wa msikiti wa Rahman na waumini wawili walichinjwa.

Oktoba mwaka jana, polisi walimkamata mwalimu mmoja wa madrasa huko Bagamoyo kufuatia taarifa za wananchi kwa polisi. Mwalimu huyo alikamatwa akiwa na watoto 22 ambapo polisi pia walikuta maandiko mbalimbali ya kuhusu ugaidi na walikuta bomu la gesi nyumbani kwa mwalimu huyo.

Mei mwaka jana, kikundi kilichojitambulisha kama Ahl Kalf Mujahidina kilitoa wito kwa Waislam kuwa wajiunge nacho, ambapo kilieleza kuwa kimeweka makazi yake kwenye mapango ya Amboni huko Tanga. 


April mwaka jana zilipatikana taarifa za kuundwa kwa kundi jipya la kigaidi linalofahamika kama Jahba East Africa ambalo lilijitangaza kuwa wafuasi wa kundi hatari la kigaidi la ISIS. Kadhalika kundi hilo lilidai kuwa miongoni mwa wafuasi wa filisofia yake wapo nchini Tanzania.

 

Kwahiyo hadi hapa, tumeshaona dhana mbili na 'ushahidi' wake, na sasa tumalizie na dhana mbili zilizosalia. Dhana nyingine ni kwamba mauaji hayo ya MKIRU yanayokana na chuki za kisiasa. 'Ushahidi' pakee katika dhana hii ni kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kwamba mauaji hayo 'yananuka siasa.'

Na dhana ya nne na ya mwisho ni kwamba mauaji hayo ni matukio ya uhalifu kama matukio mengine. 'Ushahidi' kuhusu dhana hiyo ni ukweli kwamba takwimu za uhalifu nchini Tanzania kwa mwaka 2013 na 2014  na 2015 zinaonyesha mauaji kama kosa kubwa la pili kwa ukubwa (wingi) nyuma ya ubakaji katika kundi la makosa dhidi ya binadamu.

Hatua ya tatu ya ACH inahusisha kuandaa 'matrix' yenye dhana husika, kwa minajili ya kupima 'consistency' au inconsistency.' Pia kuna fursa ya kupima kuaminika na kulandana kwa kila dhana. 



Hatua ya nne ya ACH inahusisha kuangalia 'diagnosticity' - uwezekano wa dhana kuwa sahihi. Kadhalika katika hatua hii, dhana yenye/zenye mapungufu - kwa maana ya kwamba hazijitshelezi kueleza somo linalochunguzwa - yaweza/zaweza kuondolewa. Na katika somo hili la mauaji ya MKIRU, nimefikia hitimisho la kuondoa dhana mbili za 'mwisho' (nitaeleza maana ya 'mwisho' mbeleni) yaani "chuki za kisiasa" na "mauaji hayo ni uhalifu kama mwingine." Kwahiyo ninabakiwa na dhana mbili, yaani "ugaidi" na "hasira za wananchi."

Hatua ya tano ya ACH inatokana na hatua ya nne na imenipelekea kuwa na matrix yenye dhana mbili, ya ugaidi na hasira za wananchi.



Hatu ya saba ya ACH ni kuripoti matokeo ya uchambuzi. Najua hayo majedwali ya matrix yanaweza kumchanganya msomaji lakini nyenzo muhimu kufikia hitimisho la karibu zaidi na ukweli. Ikumbukwe kuwa intelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100 - kwa kimombo wanasema "intelligence is not exact science." Kwahiyo, dhana, ushahidi wake, na msaada mkubwa wa ACH unanipeleka kufikia hitimisho lifuatalo.

1. Kumekuwa na harakati za muda mrefu za kusambaza na hatimaye kuimarisha ugaidi nchini Tanzania. Katika uchambuzi huu, ushahidi uliotumika umeanzia mwaka 2013, miaka minne iliyopita. Hata hivyo, jitihada hizo za kusambaza/kuimarisha ugaidi zimekuwa kama za kulipuka na kufifia (sporadic), japo kama tukiamini kuwa mauaji ya MKURU ni sehemu ya harakati hizo, basi hitimisho linakuwa kwamba harakati hizo zimefanikiwa kujikita.

2. Chuki ya wakazi wa maeneo husika zinasaidia kufanikisha harakati hizo za magaidi hao. Katika matrix ya pili iliyobakiwa na dhana mbili badala ya nne za awali, kuna 'consistency' katika 'uhusiano' wa dhana ya ugaidi na chuki ya wananchi. Pengine hili limechangiwa na mamlaka husika kutofanyia kazi vilio vya wakazi wa eneo hilo (rejea taarifa ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi kuhusu maujai ya MKIRU).

3. Kauli ya IGP kuwa mauaji hayo yana mkono wa kutoka nje inapewa uzito na matukio mbalimbali yaliyotumika katika uchambuzi huu. Na  katika hitimisho langu, natafsiri kuwa mauaji yanayoendelea katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni ugaidi unaofanywa na kundi lenye asili ya nje ya Tanzania lakini lenye ufuasi wa kutosha nchini humo, na linapatiwa msaada na wakazi wa eneo hilo.

4. Kuhusu 'mashehe wa UAMHO,' hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kauli ya Rais Magufuli hivi karibuni iliyoashiria kuwa kuna uhusiano kati sare za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni, mashehe wa UAMSHO na mauaji ya MKIRU. Kinachowezekana ni wahusika (magaidi) wanaweza kutumia suala la mashehe hao kama sababu ya kufanya ugaidi wao. 

5. Tukiafikiana kuwa mauaji ya MKIRU yanafanywa na magaidi, na tukiafikiana pia kuwa magaidi hao wanaweza kutumia suala la 'mashehe wa UAMSHO' kama moja ya sababu zao, bado ni muhimu kuepuka kulifanya suala hilo kuwa linatokana na masuala ya kidini. Kama ambavyo kuna wanasiasa wanaotumia mauaji hayo kuendeleza chuki za kisiasa na hatusemi siasa ndio chanzo cha mauaji hayo, ndivyo ilivyo kwa wanaoweza kutumia dini kama kisingizio cha kufanya ugaidi. Hili ni muhimu sana kuzingatiwa kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa MKIRU ni Waislamu, na kuhusisha ugaidi huo na Uislamu/Waislamu sio tu itaathiri uwezekano wowote wa ushirikiano baina ya wakazi wa eneo hilo na vyombo vya dola/serikali bali pia inaweza kuzua balaa la machafuko ya kidini.

6. Tukiafikiana kuwa kinachoendelea huko MKIRU ni ugaidi basi itabidi pia tuafikiane kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji uwekezaji mkubwa kweli intelijensia kuliko matumizi ya nguvu. Taarifa kwamba baadhi ya wakazi wa maeneo ya MKIRU wamelazimika kuhama makazi yao kwa "kuhofia vipigo kutoka kwa Polisi" zinafanya uwezekano wa kupata ufumbuzi kuwa mgumu. 

7. Kwa wanaofahamu vema pwani ya mkoa wa Pwani sambamba na jiografia yake na mikoa ya jirani watatambua kuwa wingi wa "vipenyo" (ambavyo hadi hivi karibuni vilikuwa vikitumika kama 'njia za panya' kuingiza na kutoa bidhaa mbalimbali) na mtawanyiko wa makazi yaliyochanganyika na mashamba, mapori na misitu, vinaweza kuwa mazingira mwafaka kwa watu hao wenye nia mbaya. 

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kusisitiza kuwa intelijensia sio exact science. Nimejitahidi kadri nilivyoweza kuongozwa na ACH kufikia hitimisho husika. Lengo la kufanya uchambuzi huu sio kuonyesha mapungufu ya mtu au taasisi fulani. Nimekuwa nikitumia ACH kwa majukumu yangu binafsi, na nimeona sio vibaya kuitumia kwenye suala hili la MKIRU. Hakuna anayelazimishwa kuafikiana na uchambuzi huu.

20 Jun 2017

Katika Tanzania yetu ya zama hizi ambapo takriban kila jambo linaanglaiwa kwa jicho la kisiasa, ni vigumu sio tu kusimamia ukweli bali pia kukwepa lawama kutoka kwa pande mbili kuu za siasa zetu: CCM au Upinzani.

Sie tusio na vyama, tukikosoa masuala yanayoigusa CCM/serikali, akina Humphrey Polepole wanakurupuka na kutuita majina ya ajabu ajabu. Tukikosoa Upinzani, tunaambiwa "nafasi za Ukuu wa Wilaya zimeshajaa." Good news is, kuna watu - hata kama ni wachache - waliopo CCM, Upinzani na wasio na vyama ambao wanatusikiliza. Na wanatusikiliza kwa vile wanafahamu hatuelemei upande wowote isipokuwa kwenye ukweli.

Baada ya angalizo hilo, tugeukia big news iliyosikika jana, ghafla, na kutukuta wengi wetu tusiamini macho/masikio yetu. Baada ya miaka nenda miaka rudi, hatimaye mfanyabiashara James Rugemalira na mwenzie Singasinga Harbinder Seth Singh walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuhujumu uchumi.



Kwa tunaofahamu Rugemalira ameisumbua Tanzania yetu kiasi gani, na sambamba na 'usumbufu' wa huyu Singasinga, hatua hiyo tu ya kuwapindisha wawili hao kizimbani inastahili pongezi za kila Mtanzania. Na anayestahili pongezi hizo kwa wingi kabisa ni Rais John Magufuli.
Sawa, kuna watakaosema kuwa "lakini hiyo si ndio kazi ya Rais?" only if tukipuuzia ukweli kwamba Rugemalira alikuwa kama ameshindikana katika Awamu angalau mbili zilizopita, ya Mkapa na Kikwete, na ilikuwa kama huyu mtu kaachwa afanye apendacho katika kuihujumu nchi yetu.
Nimesoma angalizo la mwanasiasa wa Chadema na mwanasheria nguli, Tundu Lissu, akitahadharisha kuhusu Rugemalira na Singasinga, kwamba hao ni sehemu tu ya mtandao mkubwa wa ufisadi. Hata hivyo, japo angalizo hilo ni muhimu, haliondoi ukweli kwamba angalau JPM amethubutu, sio tu kuwapandisha Rugemalira na Singasinga kizimbani bali pia kuwalaza rumande.

Ni wazi kuwa vita hii ambayo Rais Magufuli ameivalia njuga sio rahisi. Sio tu kwa vile inahusisha watu wenye uwezo mkubwa kifedha bali pia kwa sababu pia inawagusa baadhi ya wanasiasa maarufu ndani ya chama chake cha CCM. 
Licha ya angalizo la Lissu, kuna baadhi ya wananchi wanaotoa tahadhari 'kushangilia mapema kabla ya dakika 90.' Hawa pia wana hoja ya msingi hasa kwa kuzingatia mfano kama wa kesi ya Balozi Mahalu. Hata hivyo, kuna haja ya kuwa na matumaini hasa ikizingatiwa kuwa JPM hafanyi anayofanya kwa shinikizo la mtu yeyote yule. Ni utashi wake tu. Angetaka kukaa kimya, kusingekuwa na maandamano ya kumshinikiza achukue hatua.

Kama ningekuwa na fursa ya kumshauri Rais Magufuli basi ningemwomba sana awekeze nguvu zaidi katika vita hii dhidi ya ufisadi ambayo kwa hakika inawaunganisha Watanzania wengi waliochoka kuona nchi yao ikigeuzwa shamba la bibi, badala ya 'uhasama na wanasiasa wa Upinzani.'

Kwa mfano, jana, kabla ya habari hiyo ya Rugemalira na Singasinga kufikishwa mahakamani na baadaye kutupwa rumande, zilizpatikana taarifa kuhusu serikali kupitia jeshi la polisi 'kuwabughudhi' wanasiasa kadhaa wa Chadema ikiwa ni pamoja na kuzuwia ziara ya Waziri Mkuu wa zamani na kiognozi wa ngazi za juu Chadema, Frederick Sumaye.
Katika kipindi hiki cha vita ngumu dhidi ya mafisadi na ufisadi, tunapaswa kuwa kitu kimoja. Si kwamba vyama vya upinzani viungane na CCM, bali angalau tofauti zisizo na msingi ziepukwe, na kubwa zaidi ni kupeuka uadui wa kisiasa.

Nihitimishe kwa pointi moja muhimu kwamba japo tuna historia isiyopendeza kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi, na japo ni kweli kuwa wanasheria wa serikali hawana rekodi nzuri kwenye kesi kubwa za serikali, na vilevile japo ni kweli kuwa mara nyingi ukada umekuwa kikwazo kwa serikali kuchukua hatua stahili dhidi ya mafisadi, wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni kumuunga mkono Rais Magufuli kwani angalau ameonyesha dhamira ya kuchukua hatua stahili. 

Vilevile ni muhimu kutambua kuwa vita hii sio dhidi ya watu tu bali ni dhidi ya mfumo uliojengeka muda mrefu. Kwa maana hiyo, japo tunatamani kuona watuhumiwa wote wakikamatwa na kupandishwa kizimbani, ni muhimu tuwe na subira, hasa ikizingatiwa kuwa kukurupusha mambo kunaweza kutupelekea kupoteza kesi dhidi ya 'maadui' wetu ambao kwa uweo wao mkubwa wa kifedha, wataajiri wanasheria bora kabisa kuwatetea.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

14 Jun 2017





Kwanza, bila kujali ukada wa CCM au Chadema au kutokuwa kada, ni muhimu kutambua kuwa katika Tanzania yetu ya sasa – na pengine katika nchi nyingi za Dunia ya Tatu – alichofanya Rais John Magufuli kinastahili pongezi.

Ofkoz, alichofanya ni kazi yake, tunamlipa mshahara kama Rais wetu ili atutumikie, na uamuzi wa kuunda tume mbili zakufuatilia kuhusu usafirishaji wa mchanga wa madini ni sehemu ya kazi tuliyomwajiri aifanye.

Hata hivyo, uzoefu watuonyesha kuwa katika Dunia ya Tatu, viongozi kuanzia viranja darasani to wakuu wa nchi, hugeukia kuwa viumbe wa ajabu kabisa, na kusahau kabisa watu waliowawezesha kupata madaraka husika.

Sote tumeshuhudia jinsi watu wanavyotumia ovyo madaraka yao, kuanzia viranja shuleni hadi wenyeviti wa vikao vya harusi, kutoka kwa “ma-admini” kwenye Whatsapp groups hadi kwa wazazi kwenye familia, kutoka wajumbe wa nyumba kumi hadi mabosi wetu makazini. Kwahiyo, katika mazingira tunayoishi, ni kama inatarajiwa kuwa “kiongozi atende kinyume na matarajio ya wananchi waliomwajiri kuwatumikia.”

Kwamba tumezowea kushuhudia vituko vya watawala wetu, wapole na wanyenyekevu wakati wanaomba kura, lakini maharamia pindi wakiingia madarakani.

Wakati mwingine tatizo sio viongozi hao as such bali wapambe, viumbe wanaonufaika kwa uwepo wa fulani madarakani. Mfano wa hivi karibuni kuhus hili ni jinsi kundi la “Mtandao” lililokuwa na mchango mkubwa kumwingiza madarakani Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, na likamfanya kuwa kama “mateka wao” kwa takriban miaka yote 10 ya utawala wake.

Kwahiyo, japo Magufuli amefanya kazi tuliyomwajiri kuifanya, anastahili pongezi kwa vile “ameamua tu” kufanya jambo zuri. Twampongeza kwa kuamua kufanya jambo zuri badala ya kufuata “utamaduni uliozoeleka” wa “bora liende.” Na kubwa zaidi, hata angeamua kutofanya lolote, asingeathiriwa na lolote lile. Kwa kiongozi kuamua kufanya kitu asichotegemewa kufanya, na ambacho hata kama asingekifanya kisingemsababishia matatizo yoyote, basi hatuna budi kumpongeza bila kujali itikadi zetu.

Baada ya pongezi hizo, tuelekee kwenye ripoti husika. Kwa vile ninaamini watu wengi wameshazisoma ripoti hizo, sintorudia kueleza yaliyomo kwenye ripoti hizo. Kama hujazisoma, fanya urafiki na Google, andika “ripoti ya mchanga” utakutana nazo.

Makala hii inaangalia maeneo makuu matatu: tulikotoka, tuliko na tuendako. Katika eneo la kwanza, ninawaomba ndugu zangu wa Chama Cha Mapindui CCM waturuhusu tu tuwalaumu kwa makosa yaliyopelekea Tanzania yetu kujikuta katika hali tuliyonayo.

Rafiki yangu Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM amekuwa akiniambia kuwa “nina chuki binafsi” (sijui chuki binafsi na nani, ikizingatiwa nilikuwa na mchango wangu japo kiduchu katika kampeni za Magufuli katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2015) kila ninapoishutumu CCM kwa mchango wake katika ufisadi kwenye sekta ya madini.

Simalumu Bwana Polepole kwa sababu ajira yake ni Msema Chochote (MC) wa chama tawala. Tunapolumbana nae kwenye mitandao ya kijamii, mnufaika ni yeye maana analipwa “kusema chochote.” Na kama nilivyoeleza hapo awali, madaraka huwabadili watu kuwa viumbe wa ajabu kabisa. Polepole, mmoja wa watu walionnekana kuwa wenye busara mno wakati wa mchakato wa Katiba mpya, leo anadiriki kutoa kauli zinazotubagua Watanzania tunaoishi Ughaibuni, kama kwamba si Watanzania kamili, kwa vile tu baadhi yetu tunaikosoa CCM.

Enewei, makala hii si kumhusu kada huyo. Hoja yangu ni kwamba katika kuangalia tulikotoka, hatuwezi kukwepa kuzungumzia Ilani za uchaguzi za CCM, miswaada mbalimbali ya sheria iliyoungwa mkono na wabunge wa CCM, upinzani mkali wa CCM kupitia kwa marais wake, mawaziri wake, wabunge wake na makada wake mbalimbali dhidi ya mashujaa kutoka kambi ya upinzani – akina Dkt Slaa, Zitto, Tundu Lissu, Lema, nk – waliopigana kufa na kupona kutetea raslimali zetu, na wakaishia kuadhibiwa na uongozi wa Bunge ambao siku zote umekuwa kama muhuri wa kuidhinisha matakwa ya awamu mbalimbali za serikali za CCM.

Kwa vile kwa kupitia Ripoti mbili za mchanga tumeweza kufahamu ni kwa jinsi gani tumefisadiwa, ili tuweze kusonga mbele na jitihada za kujiondoa kwenye ufisadi, hatuwezi kuepuka “kuwajua wabaya wetu.” Huwezi kutibu maradhi kwa kuepuka kuwafahamu bakteria au virusi waliosababisha madhara husika.

Kwahiyo, japo twafahamu inawauma, ndugu zetu wa CCM “wawe wapole tu” wakati Watanzania wanatoa hasira zao dhidi ya viongozi mbalimbali wa CCM walioshiriki kuwezesha ufisadi kwenye sekta ya madini.

Baada ya kuangalia tulikotoka, tunahamia kwenye tuliko muda huu. Ndio, tushasomewa ripoti mbili zinazoeleza jinsi ambavyo tunaibiwa kwenye sekta ya mdani. Lakini sidhani kama kuna Mtanzania anashangazwa na kilichomo kwenye ripoti hizo. Kama mikataba ya madini inafanyiwa usiri kuliko tendo la ndoa, basi ni wazi kuna masuala flani ambayo wananchi wa kawaida hawapaswi kuyajua. Na hawapaswi kuyajua kwa vile yanawapora raslimali zao.

Halafu hapa pia, CCM haiwezi kukwepa lawama kwa sababu kwa kiasi kikubwa – pamoja na mzuri mengi ya chama hicho tawala – kimekuwa kichaka cha ufisadi. Sio siri kwamba Watanzania wengi wanaiangalia CCM kwa jicho la mashaka linapokuja suala la kulinda raslimali za nchi yetu. Rekodi ya chama hicho kwenye ufisadi inatosha kabisa kukipatia OSCAR ya ufisadi: EPA, Kagoda,Richmond, Kiwira, Buzwagi, Escrow…orodha ni ndefu mno.

Lakini sote twajua lawama pekee hazijengi. Sawa, CCM haiwezi kukwepa lawama  kwa kutufikisha hapa, lakini hatuwezi kuendelea kulaumu milele bila kufanya jitihada za kusonga mbele. Na hata tukitaka kuendelea kulaumu, ni muhimu kukumbuka kuwa sio tu Magufuli aliyechukua hatua hizi ni mwana-CCM pia lakini vilevile angetaka kuendeleza kasumba ya CCM, angeweza kabisa kupuuzia suala hilo.

Kwa sasa, tunafahamu kiasi gani tumeibiwa. Hatua za kuchukua ni pamoja na
  • -      Makampuni ya madini ‘kukaliwa kooni’ yarejeshe tunachowaidai.
  • -      Watanzani wenzetu walioshiriki katika ufisadi huo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zao ili waturejeshee haki yetu
  • -      Tutengeneze mazingira ya kuepusha kujikuta tena katika hali kama hii huko mbeleni. Moja ya solutions ni Katiba Mpya (japo kwa bahati mbaya au makusudi, Rais Magufuli ameonyesha kuwa hiki sio kipaumbele chake)
  • -      Yanapokuja masuala la muhimu kwa nchi yetu, tusiangaliane kwa lesni ya “huyu wa CCM” AU “huyu mpinzani.” Ni wazi kuwa laiti tungesikiliza vilio vya akina Dkt Slaa, Zitto, Lissu, nk basi tusingefika hapa. Tofauti za kiitikadi sio uadui. Na hili pia ni fundisho kwa Bwana Polepole: akina Chahali kuwepo nje ya nchi hakumaanishi wanachopigia kelele kuhusu nchi yao ni “chuki binafsi.”
  • -      Pengine huu ni wakati mwafaka kuangalia uwezekano wa reforms kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwani ufisadi wote uliojiri katika sekta ya madini ulifanyika wakati ndugu zangu hao wakiwa ‘macho’ kazini.


Mapendekezo ni mengi lakini angalau kwa sasa tunaweza kuanza na hayo.

Lakini pengine kubwa zaidi ni kwamba kwa wakati huu tunapaswa kuwa kitu kimoja. Ni muhimu tukubaliane kwamba tunapokumbana na mwizi, kila mtu ata-react kwa namna yake. Kuna uwezekano mkubwa kwa wale waliowahi kutuambia “huyu mwizi” tukawapuuza, wakatunyooshe vidole na kutukumbusha “tuliwaambia.” Haina haja ya kuwachukua, Wanatukumbusha na kutuambia ukweli. Kama kina Lissu walinyanyaswa na kubughudhiwa kwa hayahaya tunayoyashangaa leo, kuna dhambi gani kwa wao kutukumbusha kuwa walishatutahadharisha huko nyuma?

Pamoja na pongezi kwa Magufuli kwa kuchukua hatua ya kuanzisha tume ya kuchunguza kuhusu mchanga wa madini, ninamlaumu kwa lugha yake ambayo haiwezi kutusaidia katika kipindi hiki tunachohitaji ushairikiano bila kujali itikadi zetu. Maagizo yake kwa Spika Ndugai (mtu ambaye hapaswi kuongea lolote kuhusu wizi wa madini yetu kwa sababu ‘kila Bunge la CCM’ limekuwa wawezeshaji wa wizi huo) yanajenga mfarakano tu badala ya umoja tunaohitaji kipindi hiki.

Sijui kwanini Rais Magufuli anapenda sana kutengenezea ‘bifu’ zisizo na umuhimu. Hivi akitoa wito kuwa Watanzania wote tushirikiane, na kuwakaribisha wapinzani katika mapambano haya, atapungukiwa nini? Mbona ‘kiongozi mkuu wa upinzani’ Edward Lowassa, kammwagia pongezi Magufuli kwa hatua alizochukua kuhusu suala hilo la madini? Ni muhimu kwa Rais wetu kukumbushwa kuwa siasa za uhasama sio tu hazina fursa katika Tanzania yetu bali pia hazina faida.

Kuhusu jinsi ya kuwashughulikia watu waliohusika katika ufisadi kwenye sekta ya madini, tuna njia mbili tu: aidha, kufumba macho na kumsomba kila aliyehusika, na hii itajumuisha marais wastaafu, au, tuendeshe mambo Kiswahili, tuchukue hatua kwa wale tu ‘wasio na madhara makubwa,’ na kuwastiri ‘watuhumiwa muhimu’ kama vile marais wastaafu.

Tatizo la hiyo approach ya pili ni kwamba hao ‘wasio na mdhara makubwa’ watajitetea kirahisi tu kuwa maamuzi yao yalitokana na ridhaaza ‘watuhumiwa muhimu.’

Je inawezekana suala hili ambalo linanapaswa kushughulikiwa na mkono mrefu wa sheria likafanywa bila kuingiza siasa? Yes, inawezekana lakini sio rahisi kwa Tanzania yetu hii. Ila ni mapema mno kutoa hukumu. Acha muda uongee.

Tunakolekea? Well, Sie kama Watanzania tunapaswa kuacha kuwa ‘wapole’ kupita kiasi. Muda huu tulipaswa kuandamana kulaani waliotuibia, lakini kama kutakuwa na maandamano basi ni ya kisiasa ya kumpongeza Magufuli kutueleza kile ambacho tunakifahamu muda mrefu tu. Ni lini Watanzania wataamka na kudai – kwa amani – haki zao za msingi? Hivi ni lini Watanzania watashinikiza viongozi wetu waweke mbele maslahi ya nchi yetu badala ya maslahi yao binafsi?

Na kufumbukiwa macho suala la mikataba ya madini kuwe mwanzo wa safari ndefu ya “kudai chetu.” Tunataka mikataba ya  gesi na mafuta sio tu iwekwe wazi bali itafsiriwe kwa Kiswahili ili kila Mtanzania aisome.

Tunataka pia mikataba ya ununzi wa Bombadier nayo iwekwe wazi, ili huko mbeleni tusijikute tukilazimika kuunda tume nyingine.

Tunataka mikataba ya utalii, iwekwe hadharani. Tujue nani anatorosha wanyamapori wetu, nani baada ya kupewa Ukatibu Mkuu ghafla biashara ya ujangili nayo ikaanza kupaa, tuambiwe watu waliondoka na magunia ya fedha kwenye utapeli wa Escrow ni akina nani (sio wale tulitajiwa kuhusu ‘benki ya waswahili’ bali Stanbic), tunataka kila kilichofichwa kiwekwe wazi.

Lakini ili hayo yote yawezekana, ni muhimu sote wenye uchungu wa nchi yetu tuwe kitu kimoja. Na nitumie fursa hii kumwomba tena Rais Magufuli ajaribu ku-embrace consensual politics (siasa za kufikia mwafaka) badala ya hizi za mifarakano (conflictual politics). Afterall, Haijalishi mtu ni CCM, Chadema, CUF au hana chama, sote ni Watanzania.


Uchambuzi huu ni endelevu. Kwa leo naomba kuishia hapa. Swaumu njema kwa ndugu zangu Waislamu. Asanteni

29 May 2017



Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka tisa iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana. Japo miaka tisa inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana. Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka. Kwa kifupi, mama mpendwa, kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minane iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa, ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu, kwa mumeo marehemu Baba Mzee Chahali (aliyeungana nawe huko peponi mwaka juzi) na kwa wanao wote na ndugu na jamaa. Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani, ulirukaruka kwa furaha, ukanikumbatia na kunipakata mwanao, ukaniandalia maji ya kuoga, ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga. Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani. Inaniuma sana.
Marehemu mama akicheza siku ya harusi ya mwanae wa nne. Yeye na marehemu baba walijaliwa kupata watoto tisa, mmojaalifariki  na tukabaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.
Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na marehemu Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu, ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha, ndoa, upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya. Kabla ya kifo chako, nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na  marehemu Baba, na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho. Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako na marehemu baba kwangu mwanenu. Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo, kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti. Nilikugusa mama, nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha. Hukuamka hadi leo hii.
Hospitali Teule ya Mtakatifu Fransisko ambapo marehemu mama alilazwa akiwa amepoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitatu hadi alipofariki siku kama ya leo miaka minane iliyopita
Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuguza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu. Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis, Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha. Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza, kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha. Nikategemea ungemka na kunieleza japo neno moja. Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote. Iliniuma sana, inaniuma sana na itaendelea kuniuma sana, mama.

Kabla marehemu baba hajaungana nawe huko uliko, nilikuwa na wakati mgumu sana kila nilipopiga simu nyumbani kwa wakati wa uhai wako, nilizowea kuwa nikimaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori. Na kila nilipoongea nawe nilijisikia kudeka kutokana na upendo wako usiomithilika. Baada ya kifo chako, na kabla marehemu baba hajafariki, kila nilipompigia simu mzee huwa nilijikuta najisahau na nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi. Sasa ndio imekuwa uchungu maradufu kwani kila nikipiga simu nyumbani, ninatamani kuongea nawe na marehemu baba kisha nakumbuka kuwa hampo nasi.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki wewe na baadaye marehemu baba. Siwalaumu, kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa hampo nasi na haiwezekani kuwarejesha. Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako na cha baba vinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.


Mama mpendwa, sijui nisemeje. Rafiki zako wakubwa, wanao vitinda-mimba, Kulwa na Doto, ndio wananitia uchungu zaidi, Wanawa-miss mno wewe na marehemu baba kwa sababu ndio uhusiano wenu ulikuwa zaidi ya kati ya wazazi na vitinda-mimba wao. Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka, mnataniana na kunipa kila aina ya faraja. Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu, na kila anayemjua anafahamu hilo. Japo mnaomboleza kifo chake, lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema, Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua. Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi, na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani. Nguvu nyingine niliyonanyo ni imani kuwa wewe na marehemu baba mnaendelea kutuombea huko mlipo.

Nyumba ya milele ya marehemu Adelina 

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE WEWE NA MAREHEMU BABA PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AWAANGAZIE, MPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.