Showing posts with label Lazaro Nyalandu. Show all posts
Showing posts with label Lazaro Nyalandu. Show all posts

31 Oct 2017



Pasipo kutarajiwa, jana, Jumatatu ya Oktoba 30, 2017, anga za habari huko nyumbani Tanzania zilitawaliwa na habari moja nzito: mmoja wa wana-CCM maarufu, Mbunge kwa tiketi ya chama hicho tawala anayewakilisha jimbo la Singida Kaskazini, na Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bwana Lazaro Nyalandu, alitangaza kujivua uanachama wa CCM na kuomba kujiunga na chama kikuu cha upinzani cha Chadema.


Tukio hilo lilileta mshangao mkubwa kwa sababu kadhaa. Kwanza, licha ya matamshi ya hivi karibuni ya Nyalandu kuhusu haja ya kurejeshwa mchakato wa Katiba mpya, sambamba na kuwasihi wabunge wenzie wa CCM kupinga kwa nguvu zote jaribio la kurefusha muda wa Rais madarakani, hakukuwa na dalili kubwa na za waziwazi iwapo kuna ‘kutofautiana’ kati ya Nyalandu na chama chake.


Na hata kama kungekuwa na dalili hizo – kwa kificho au wazi – bado wananchi wengi wangepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa.

Sababu ya pili ya mshangao kuhusu tukio hilo ni ukweli kwamba mwanasiasa wa chama tawala kuamua kujiunga na upinzani, tena miaka mitatu hivi kabla ya uchaguzi mkuu, ni suala ambalo licha ya kuhitaji ujasiri mkubwa pia linaacha maswali kadhaa ambayo pengine sio rahisi kuyapatia majibu.

Hadi wakati ninaandika uchambuzi huu, kilicho bayana kuhusu sababu za Nyalandu kuchukua uamuzi huo ni sababu alizotanabaisha mwenyewe katika tamko lake kwa umma.

Akizungumza jana, mwanasiasa huyo alidai sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kutokuridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Lakini hata kabla ya kuchukua uamuzi huo jana, Nyalandu alishaonyesha dalili ya kutofautiana na wana-CCM wenzie, hasa kwa uamuzi wake wa kumtembelea Mbunge Tundu Lissu wa Chadema aliyelazwa huko Nairobi, Kenya kufuatia jaribio la kumuua. Hadi sasa, Nyalandu anabaki kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CCM kumtembelea Lissu huko Kenya.


Huku kukiwa na tetesi kwamba uongozi wa juu wa CCM umewapiga marufuku viongozi wake kujihusisha na suala la Lissu, uamuzi wa Nyalandu kwenye Kenya ‘kinyume na maagizo ya chama chake’ ulihisiwa kuwa ungemwingiza matatizoni.

Dalili nyingine kuwa mwanasiasa huyo hakuwa akipendezwa na baadhi ya mienendo ndani ya CCM ni pale alipoibuka kuhamasisha haja ya kuanzisha upya mchakato wa kupatikana Katiba mpya, sambamba na kuhamasisha wana-CCM wenzake dhidi ya jitihada za chini chini kuongeza muda wa Rais madarakani.

Masuala yote hayo mawili yalitarajiwa ‘kumsababishia matatizo’ mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, kuna ‘sababu mbadala’ kuhusu uamuzi wa Nyalandu kujiuzulu. Kuna taarifa kwamba kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya mwanasiasa huyo kuhusiana na utumishi wake kama Waziri wa zamani wa Maliasi na Utalii. Taarifa hizo ambazo bado ni tetesi hadi muda huu, zinaweza kupewa uzito zaidi na ‘screenshot’ inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikidaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya kundi la Whatsapp la viongozi wanawake wa CCM.

Katika ‘chat’ husika, mmoja wa makada wa kike wa CCM anadai kuwa kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na kwamba uamuzi wa kujiondoa CCM na kuomba kujiunga na Chadema una lengo la kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa pindi akichukuliwa hatua.

Pengine swali muhimu linaloendelea kutawala vichwa ni “kwanini HASWA Nyalandu amejiuzulu?” Kuna sababu alizotoa yeye mwenyewe, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaleta mantiki, lakini pia kuna hiyo tetesi kuwa amechukua uamuzi huo kama tahadhari pindi akianzishiwa tuhuma za ufisadi.

Tuchambue sababu zote mbili, yaani alizotoa mwenyewe na hizo tetesi. Kwa vile hatuna maelezo yenye uhakika yaliyo kinyume na sababu alizotoa Nyalandu, nadhani kwa kuzingatia busara tu, itakuwa sio sahihi kudhani anaongopa. Unapopinga kauli ya mtu basi shurti uwe na kauli mbadala yenye uthibitisho. Kwahiyo, angalau kwa muda huu, hakuna sababu za msingi za kupinga sababu alizotoa mwanasiasa huyo.

Kuhusu tetesi za kuwepo kwa mchakato wa ‘kumshughulikia kutokana na tuhuma za ufisadi,’ kuna mantiki kwa mbali, na utata kwa mbali pia. Sio siri kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa kama ‘makao makuu’ ya ufisadi. Wizara hiyo ilikuwa kama ile ya Nishati na Madini, ambapo mawaziri lukuki walihamishwa au kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi.

Kwamba Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kulikuwa na tuhuma za ufisadi, hilo halina mjadala. Lakini kwa kuzingatia kanuni ya asili ya haki, tuhuma hizo zinabaki tuhuma tu mpaka zitakapothibitishwa.

Kwahiyo, hadi hapa, mantiki ya mbali kuhusu uwezekano wa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi dhidi ya Nyalandu ipo. Hata hivyo, utata wa mbali ni kwamba katika mazingira ya kawaida tu, na tukijifanya kuamini (angalau kwa minajili ya uchambuzi huu) kwa Nyalandu anafahamu kuhusu uchunguzi huo, je isingekuwa mwafaka kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa CCM kuliko nje ya chama hicho tawala?

Sawa, kuna hiyo hoja ya “amehama CCM na anataka kuhamia Chadema ili pindi akichukuliwa hatua, suala hilo lionekane la kisiasa,” lakini ikumbukwe kuwa suala la muhimu sio “suala lionekane la kisiasa” bali “lisitokee kabisa.” Na katika mazingira ya kawaida, huo uamuzi wa tu Nyalandu kuhama CCM na kuikosoa hadharani unatosha kuipa serikali ya chama hicho tawala na taasisi zake “hasira” dhidi ya mwanasiasa huyo. Na hapo hatujagusia uwezekano wa mwanasiasa huyo kujiunga na “adui nambari moja wa CCM” yaani Chadema.

Kwa mtazamo wangu, kama ni kweli kuna uchunguzi unaoendelea au unaotarajiwa kufanyika kuhusu Nyalandu basi yayumkinika kuhisi kwamba ingekuwa rahisi zaidi kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa ndani ya CCM kuliko nje ya chama hicho chenye historia ya siasa za kinyongo, visasi na majitaka.

Lakini kuna ‘angle’ kubwa zaidi katika uamuzi huo wa Nyalandu. Yawezekana amesoma vema upepo wa kisiasa huko nyumbani chini ya utawala wa Rais Magufuli, na kubaini vitu kadhaa. Moja laweza kuwa kinachoonekana kama wananchi wengi kutoridhishwa na utawala wa Magufuli, ndani na nje ya CCM. Keyword hapa ni ‘kinachoonekana,’ nikimaanisha pengine ni hisia tu kuwa kuna wananchi wengi wasioridhishwa ilhali ukweli ni kinyume na hisia hiyo.

Kwa minajili ya uchambuzi huu, tufanye kuwa hisia hizo zipo kweli. Kwahiyo, kwa vile Nyalandu alikuwa miongoni mwa makada wa CCM walioomba ridhaa ya chama hicho kuwa wagombea wa urais mwaka 2015 lakini haukufanikiwa, basi pengine anataka kutupa kete yake kupitia upande wa upinzani.

Lakini sio tu kusukumwa na nia ya kuwania urais, lakini yayumkinika kuhisi kuwa mazingira yaliyopo muda huu yanampatia mwana-CCM yeyote nafasi nzuri ya kukikimbia chama hicho. Sio siri kuwa hisia kwamba Magufuli ana dalili za udikteta zinazidi kushika hatamu. Kwa maana hiyo, hata mtu mwenye sababu zake binafsi akikurupuka na kutamka “ninahama CCM kwa sababu utawala wa Magufuli ni wa kidikteta” ataeleweka kirahisi, na anaweza kuungwa mkono kirahisi pia.

Kwamba Nyalandu anaweza “kuruka kutoka kwenye ngalawa na kuingia majini kwenye bahari yenye papa na nyangumi” sio suala dogo. Kama kuikosoa CCM ukiwa ndani ya chama hicho ni hatari, sote twafahamu nini kinachoweza kumkumba anayediriki sio kukosoa tu bali pia kuhama chama hicho tawala. Kwa mantiki hiyo, kwa sababu yoyote ile – iwe hizo alizotaja mwenyewe au tetesi za uchunguzi wa ufisadi – mwanasiasa huyo amefanya maamuzi magumu, na yayumkinika kuamini kuwa amejiridhisha vya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Kuna mambo matatu yanayoweza kutoa mwangaza kidogo. Kwanza, hivi karibuni, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangallah alinukuliwa akisema kwamba anayo orodha ya watu mashuhuri, viongozi wastaafu na wabunge wanaojihusisha na ujangili, na atahakikisha anawashughulikia.

Pili, jana katika hotuba yake akiwa huko Mwanza, Rais Magufuli alikumbushia kuhusu Mahakama Maalum ya Ufisadi, ambayo pasi kuuma maneno, imekuwa kama kichekesho kutokana na kukosa kesi. Rais kuitaja mahakama hiyo ‘isiyo na ufanisi angalau hadi sasa’ inaweza kumaanisha kilekile alichokigusia Waziri Kigwangallah kuhusu ujangili.

Na tatu, ‘vijana wa Lumumba’ (makada wa CCM kwenye mitandao ya kijamii) walishaanza kuzungumzia ‘ufisadi wa Nyalandu’ mara tu alipoenda Nairobi kumjulia hali Lissu. Na kasi yao ya mashambulizi dhidi ya Nyalandu imepamba moto zaidi jana baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kujiondoa katika chama hicho tawala.

Lakini pia kuna tamko la Humprey Polepole, ‘katibu Mwenezi’ wa CCM kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Binafsi nilitarajia tamko kali na pengine lililosheheni kebehi kama sio kashfa (na Polepole ni hodari sana kwenye maeneo hayo), lakini reaction ya msemaji huyo wa CCM imekuwa ‘muted.’ Sana sana ameishia kudai kuwa Nyalandu amejiondoa kwa sababu ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano. Pia amejaribu kuonyesha kuwa mwanasiasa huyo sio ‘mtu mkubwa’ ndani ya chama hicho tawala. Huyu si Polepole tunayemfahamu kwa umahiri wake wa ‘kusema ovyo.’ Huenda ‘upole’ wake una sababu flani.

Japo kauli ya Kigwangallah na ya Rais Magufuli, sambamba na ‘vijana wa Lumumba’ kumwandama Nyalandu, na ‘upole’ wa Polepole yanaweza kuwa mambo ya kawaida tu, lakini pia yanaweza kutoa mwangaza kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Hata hivyo, kama nilivyotanabaisha awali, sidhani kama mazingira hayo yangetosha kumfanya Nyalandu kuchukua uamuzi huo mzito.

Kwamba Nyalandu ataandamwa baada ya kuchukua uamuzi huo, hilo halina mjadala. Kama asipoandamwa na ngazi za juu za CCM au kupitia taasisi za dola/umma basi ‘vijana wa Lumumba’ watakesha mitandaoni kumchafua. Pamoja na ukongwe wake katika siasa si Tanzania tu bali barani Afrika kwa ujumla, kwa kiasi kikubwa CCM inaendekeza mno siasa za kisasi, kinyongo na adui mkubwa wa ukweli. Kuikosoa CCM au serikali yake ni kama kusaini ruhusa ya kusumbuliwa kwa kila namna.



Na ni muhimu kutambua kuwa Nyalandu alikuwa akifahamu kuhusu ‘mabalaa’ yanayomsubiri baada ya kuchukua uamuzi huo mzito. Angalia yanayomsibu Yusuph Manji, mtu aliyemwaga mamilioni ya fedha kuifadhili CCM lakini amebaki kuwa ‘kielelezo cha hasira za CCM.’

Je CCM wakiamua kulipa kisasi kwa Nyalandu watafanikiwa? Inategemea sana busara za Magufuli. Yote yanayoelezwa kuwa ‘ufisadi wa Nyalandu’ yailikuwa na baraka za mtangulizi wa Magufuli, yaani Rais Kikwete. Kwahiyo, kama ambavyo jitihada zozote za kumbana Lowassa zilivyoshindikana kwa vile zingeishia kumchafua pia Kikwete, ndivyo jaribio la ‘kulipiza kisasi kwa Nyalandu’ linavyoweza kumtia matatani JK.


Licha ya kuelezwa kuwa Nyalandu alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa JK, pia ni muhimu kutambua kuwa mmoja wa watu wake wa karibu ni mke wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Mama Anna. Mara baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani, Nyalandu alikuwa miongoni mwa washauri Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Kwa maana hiyo, jaribio lolote la ‘kumwandama Nyalandu’ linaweza kuzua kile Waingereza wanaita ‘unintended consequences,’ au ‘matokeo yasiyokusudiwa kwa Kiswahili.

Pia ni muhimu kutambua u-kimataifa wa Nyalandu. Mwanasiasa huyo ana mahusiano mazuri na wanasiasa wenye nguvu kubwa hususan nchini Marekani. Japo ‘nguvu’ zao zinaweza kutofua dafu kwa Magufuli, lakini sote twafahamu kuwa ni vigumu kwa Tanzania yetu kuwa na ‘jeuri’ katika umasikini wetu.


Hatma ya Nyalandu akifanikiwa kuhamia Chadema ikoje? Binafsi, ninahisi mambo makuu mawili. Kwanza, ujio wake katika chama hicho kikuu cha upinzani unaweza kuamsha msisimko mpya wa siasa za ndani na nje ya chama hicho, na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande mmoja, anaweza kuendeleza hoja zake kama hiyo ya kudai kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya, suala ambalo Chadema na washirika wake wa UKAWA ni kama wamelitelekeza.

Lakini pengine kubwa zaidi ni uwezekano mkubwa wa Nyalandu kuwa mmoja wa wagombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwamba amejiondoa CCM kwa hiari yake (angalau kwa mujibu tunachofahamu hadi muda huu) na kujiunga na Chadema kwa hiari yake, anaweza kuwa na faida ya ziada kuliko majina mengine mawili yanayotajwa kuhusu urais mwaka 2020 kupitia Chadema, Mawaziri Wakuu wa zamani, Lowassa na Sumaye.


Kwamba Nyalandu ni ‘mwana-CCM pekee aliyemjali Lissu kwa kumtembelea huko Nairobi,’ na ukweli kuwa yeye na Lissu wanatoka mkoa mmoja, wanaweza kujenga ‘dream team’ inayoweza kuirejesha Chadema enzi za kina Dkt Slaa, Zitto na Mbowe.

Lakini pia katika mazingira yaliyopo sasa, Chadema imekuwa kama haina mpango wa kushiriki uchaguzi mkuu ujao. Maandalizi yanayopaswa kufanyika sasa – miezi 36 tu kabla ya uchaguzi huo – ni kama hayapo. Ndiyo, Magufuli kapiga marufuku shughuli za kisiasa, lakini ni lini Rais kutoka CCM aliwahi kuridhika shughuli za wapinzani?

Kwa maana hiyo, ujio wa Nyalandu unaweza kuamsha matumaini kwa chama hicho kikuu cha upinzani kuhusu nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, kuna vikwazo vikuu viwili. Cha kwanza, ni lile lililojiri baada ya Lowassa kujiunga na CCM, Kwa minajili ya kumbukumbu tu, Chadema ilimwandama Lowassa kuwa ni ‘baba wa ufisadi’ kwa takriban miaka 9 mfululizo, kisha ghafla wakampokea na kumfanya mgombea wao wa Urais katika uchaguzi mkuu uliopita. Kwa busara za kawaida tu, huwezi kumchafua mtu kwa muda wote huo kisha ukategemea kumsafisha ndani ya miezi mitatu. Japo makada wa chama hicho hawataafiki, athari za kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wao zinaendelea kukisumbua chama hicho.

Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, baadhi ya viongozi wa Chadema walishawahi ‘kumpaka’ Nyalandu wakimwita fisadi, hali inayoweza kutumiwa na CCM kudai kuwa ‘Chadema ni kimbilio la mafisadi.’ Hata hivyo ni rahisi kwa chama hicho cha upinzani kuwauliza CCM, “mpaka mwanasiasa awakimbie na kujiunga nasi ndio mnaanza kumwita fisadi?” Ni hoja inayoingilia akilini.


Je Nyalandu atapata mapokezi mazuri huko Chadema? Kama kauli ya Lowassa jana kuwa Chadema itakuwa ‘imelamba dume’ pindi Nyalandu akijiunga na chama hicho inaashiria chochote basi kuna uwezekano mkubwa wa mafanikio makubwa kwa mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, ukweli kwamba Nyalandu ni miongoni mwa watu wenye sifa na uwezo wa kuwa wagombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 unaweza kupelekea mgongano dhidi yake na majina mengine yanayotarajiwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro hicho, yaani Lowassa, Sumaye na Lissu.

Hili sio tatizo kubwa sana iwapo maslahi ya Chadema – badala ya maslahi ya mtu au kikundi binafsi – yakiwekwa mbele. Kwamba kufanyike tathmini ya kutosha kufahamu nani anayeweza kukiwezesha chama hicho kuing’oa CCM madarakani hapo mwaka 2020.

Kwamba Nyalandu anaweza kuleta hamasa kwa wana-CCM wengine (Membe?) kujiunga na Chadema, na kama ujio wake huko Chadema utaleta matokeo chanya, ni suala la muda. Lililo bayana hadi muda huu, uamuzi wake huo wa ghafla umetushtua wengi ikiwa ni pamoja na CCM na makada wake. Na yayumkinika kuamini kuwa uamuzi huo utaleta msisimko mpya katika siasa za Tanzania.

Mwisho, uchambuzi huu umetokana na uelewa wangu wa siasa za Tanzania, na unaweza kuwa sio sahihi kulingana na mitazamo tofauti. Jiskie huru kuchangia maoni, kunikosoa au hata pongezi zinaruhusiwa. Siku zote ninajitahidi kwenda mbali zaidi ya kuripoti tu matukio badala ya kuyachambua kwa undani zaidi. Asanteni na siku njema



31 Jul 2013

WARAKA MZITO WA PAPII KOCHA KWA JK

Na Mwandishi Wetu
ULE waraka wa mwanamuziki aliyefungwa gerezani kifungo cha maisha sambamba na baba yake mzazi, Nguza Viking ‘Babu Seya’, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ umeibua mjadala tena huku Naibu Waziri wa Mali Asili na Utalii, Lazaro Nyalandu akiombwa na kukubali kuufikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ (kushoto) akiwa na baba yake Nguza Viking ‘Babu Seya’.
MIAKA 10 GEREZANI
Hivi karibuni wasanii hao walitimiza miaka kumi tangu walipofungwa katika Gereza la Ukonga, Dar mwaka 2003 hivyo kusababisha waraka huo aliouandika Papii Kocha Februari mwaka 2010 kusababisha mjadala upya.
Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Julai 21, mwaka huu waraka huo ulikuwa gumzo kubwa juu ya ombi la Papii Kocha kwa Rais Kikwete kuwa amhurumie atoke gerezani kwa kuwa bado ni kijana mdogo huku nyuma yake watu wakituhumiana bila ushahidi.
Waraka alioandika Papii Kocha kwa Mhe rais Kikwete.
OMBI KWA WAZIRI NYALANDU
Mwandishi Mtanzania aishie Uskochi, Evarist Chahali aliutundika waraka huo katika ukurasa wake wa Twitter na kusababisha msigano wa kimawazo.
Chahali aliusindikiza waraka huo na maneno akimuomba Waziri Nyalandu kwa kuwa ni mmoja wa ‘memba’ wake mtandaoni aufikishe kwa Rais Kikwete kwa kuwa ulimlenga yeye moja kwa zote.
Alimwandikia Waziri Nyalandu: “Nina imani sana kwako, mheshimiwa waziri na kwa vile Rais Kikwete yupo katika swaumu, natumaini kilio hicho kitasikilizwa.”
Kukawa mchana, kukawa usiku, siku hiyo ikaisha.
Waziri Nyalandu.
WAZIRI NYALANDU AKUBALI
Kesho yake, yaani Julai 22, mwaka huu, Waziri Nyalandu alimjibu Chahali kwa kumwandikia: “Chahali copy that (nimepokea), asante kaka.”

SEHEMU YA MANENO YA KUCHOMA YA WARAKA WA PAPII KOCHA
Baada ya salamu kwa mkuu huyo wa nchi, Papii Kocha aliyekuwa nyota wa Bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ aliandika: “Naanguka na kushika miguu yako mitukufu mheshimiwa rais.
“Nakuomba msaada (msamaha) kwako mheshimiwa rais kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu (Kisutu).
“Mhe. Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mhe. Rais.
“Naomba huruma yako mheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninayehitaji huruma yako wewe mzazi.
“Natumaini kauli yako ya mwisho ndiyo itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu.
“Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu. Mungu akubariki.”
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
WAKIKUBALIWA WATAREJEA URAIANI?
Baada ya Waziri Nyalandu kukubali kuupeleka waraka huo ikulu na habari hiyo ikasambaa mitandaoni, baadhi ya watoa maoni walikwenda mbele zaidi wakidai huenda ombi lake litakubaliwa na kumfanya Papii Kocha na baba yake kurudi kula bata uraiani.
Wanamuziki hao walifungwa gerezani kwa tuhuma za kunajisi watoto 10 wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza jijini Dar.
Mbali na kuachiwa kwa baadhi ya watoto wa familia ya Babu Seya waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha, Papii na baba yake bado wanaendelea kutumikia kifungo hicho hadi sasa.

24 Jul 2013


WAKATI taifa likiwa katika maombolezo ya vifo vya mashujaa wetu saba waliouawa huko Darfur, Sudan, wakitumikia kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini humo, Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilifanya tukio linalostahili pongezi nyingi, japo huenda ni wananchi wachache tu wenye taarifa nalo.
Jumapili iliyopita jeshi hilo lilianza kutumia rasmi mtandao wa kijamii wa twitter likitumia ‘handle’ @jw_tz. Hatua hiyo ni ya kimaendeleo na inaonyesha kuwa jeshi letu limedhamiria kwenda na kukumbatia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Mtandao wa twitter na pengine mitandao ya jamii kwa ujumla, bado ni suala geni kwa Watanzania wengi. Na licha ya ugeni huo, ukweli kwamba umiliki na upatikanaji wa huduma ya kompyuta bado ni ‘anasa’ wanayomudu watu wachache unafanya matumizi ya twitter (na mitandao mingine ya kijamii) kutokuwa suala muhimu au maarufu kwa jamii yetu.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii hivi sasa imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano; huku ikibadili kwa kiasi kikubwa upatikanaji na kupashana habari. Wakati kwa muda mrefu mawasiliano kati ya mtu na mtu yamekuwa yakitegemea aidha neno la mdomo (kwa maana ya watu kukutana au kwa njia ya barua) au magazeti na redio, na kwa kiasi fulani runinga, mitandao ya jamii na teknolojia ya mawasiliano kwa ujumla imetokea kuwa njia ya haraka ya mawasiliano katika jamii.
Ukitaka kupata mfano wa umuhimu wa teknolojia hiyo ya mawasiliano, ni jinsi ziara ya kihistoria ya Rais wa Marekani Barack Obama huko nyumbani Tanzania, hivi karibuni, ilivyoripotiwa in real time (kadri matukio yalivyokuwa yakitokea) badala ya kusubiri gazeti la kesho au ripoti za redioni au kwenye runinga.
Kadhalika, kwa kutumia mtandao wa twitter, wananchi wamekuwa wakiendesha kampeni mbalimbali, na ya hivi karibuni kabisa ni ile inayohamasisha kupinga kodi ya sim card ambapo inatumia hashtag #NoSIMcardTax.
Iwapo Serikali itasikiliza kilio cha wananchi na kusitisha au kufuta kodi hiyo, basi kampeni hiyo ya mtandaoni (hususan huko twitter) itastahili pongezi kubwa.
Pamoja na pongezi zangu kwa hatua hiyo ya JWTZ kujiunga na mtandao wa twitter, bado taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa; hususan kutumia ipasavyo mtandao huo kama nafasi kwa jeshi hilo kuupasha umma habari stahili.
Kwa mfano, juzi Rais Jakaya Kikwete aliwaongoza Watanzania kutoa heshima zao za mwisho kwa miili ya wanajeshi wetu waliouawa Darfur, na katika mazingira mwafaka, tungetegemea akaunti ya twitter ya JWTZ ingetulea tukio hilo ‘live’ lakini haikuwa hivyo. Siwalaumu kwa vile pengine ni ugeni tu katika matumizi ya teknolojia hiyo.
Licha ya ujio huo wa JWTZ huko twitter, mtandao huo wa kijamii unatumiwa pia na baadhi ya viongozi wetu wa serikali na wanasiasa, japo idadi yao ni ndogo. Rais Kikwete ni miongoni mwa viongozi hao; huku akiweka historia ya kuwa mmoja wa marais wachache wa Afrika wanaotumia mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa mawaziri wachache wanaotumia mtandao wa twitter ni Mheshimiwa Lazaro Nyalandu (@LazaroNyalandu), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Uwepo wake katika mtandao huo umenisaidia kumfahamu katika namna ambayo pengine Watanzania wengi hawaifahamu.
Nyalandu amekuwa mfano bora wa jinsi inavyostahili na inavyowezekana kuweka maslahi ya nchi mbele ya maslahi ya kiitikadi. Lilipotokea tukio la milipuko ya mabomu jijini Arusha, Waziri Nyalandu alishiriki kikamilifu kuufahamisha umma kuhusu hatua mbalimbali zilizokuwa zikifanyika kuwasaidia majeruhi.
Na japo Nyalandu ni Mbunge wa CCM, kamwe hajawahi ku-tweet mambo ya kiitikadi, na badala yake tweets zake zimekuwa zikihusu masuala ya Tanzania na Watanzania, badala ya masuala ya CCM.
Kingine kinachopendeza kuhusu Naibu Waziri huyo ni usikivu kwa hoja mbalimbali zinazowasilishwa kwake kupitia mtandao huo. Kama ilivyo kwa Naibu Waziri mwingine, Januari Makamba (@JMakamba), Nyalandu huwasiliana na wananchi waliopo twitter kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, kiasi yaweza kuwa vigumu kudhani ni mtu mwenye dhamana kubwa serikalini.
Ni kwa sababu hiyo, kupitia mtandao wa twitter Jumapili iliyopita nilimtumia ombi Waziri Nyalandu kumsihi awasilishe kilio cha msanii Johnson Nguza (Papii Kocha) ambaye, pamoja na baba yake Nguza Viking na kaka zake wawili, wanatumikia kifungo kirefu jela kwa kosa la kubaka.
Mwishoni wa wiki, blog mbalimbali zilichapisha barua iliyoandikwa na msanii huyo (Papii Kocha) kwenda kwa Rais Kikwete akiomba msamaha kwa yeye na familia yake, na kumwomba Rais awatoe gerezani.
Nina sababu mbili za msingi za kuguswa na suala la ‘Babu Seya’ na wanae ambao wamekuwa gerezani kwa takriban miaka 10 sasa. Kwanza, japo kuna msemo maarufu kwenye kila jela kuwa ‘kila mfungwa hana hatia’ (yaani amefungwa kwa kuonewa), tangu Nguza na wanae walipokamatwa na hatimaye kufungwa nimebaki na hisia kuwa sheria ilipindishwa dhidi yao.
Mengi yameshasemwa huko mitaani kwamba kesi hiyo ilisababishwa na visasi binafsi dhidi ya msanii huyo na wanae. Ikumbukwe kuwa katika nchi zetu masikini kuna ‘haki za aina mbili,’ kwa wanyonge ambao wanaweza kwenda jela kwa kusingiziwa tu, na kwa vigogo ambao ni kama wana kinga ya kudumu ya kisheria.
Sababu ya pili ya kumwomba Waziri Nyalandu amfikishie Rais Kikwete ujumbe wa Papii Kocha ni ya kibinadamu zaidi. Tuweke kando hisia kuwa kifungo cha Nguza na wanae ni sheria kufuata mkondo au kupindishwa.
Kama binadamu, na hasa katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, unajiskiaje ukisoma barua ya kutoa majonzi kutoka kwa kijana mfungwa anayezeekea jela akiomba msamaha kuhusu hukumu ambayo tangu mwanzo wafungwa hao wamekuwa wakidai ni ya uonevu tu dhidi yao?
Ndio, huko jela ‘kila mfungwa hana hatia’ (yaani wafungwa wengi hudai wamefungwa kwa kuonewa hata kama walikamatwa red-handed wakifanya makosa).Lakini katika mazingira ya kawaida, ni wafungwa wangapi waliopo jela kwa takriban miaka 10 na wanaendelea kusisitiza kuwa walifungwa kwa uonevu na wanaomba hukumu dhidi yao ziangaliwe upya au wasamehewe?
Laiti ukisoma barua hiyo ya Papii Kocha (na amekuwa akiandika barua kama hiyo mara kadhaa) usipolengwa na machozi basi utakuwa na ‘moyo mgumu’ kweli.
Lakini hata tukiweka kando huruma ambayo baadhi yetu tunayo kwa Nguza na wanae, katika ubinadamu tu, msanii huyo na wanae wameshatumikia adhabu ndefu (bila kujali walitenda kosa au la), na adhabu waliyokwishapata inatosha kutoa fundisho kwao na kwa jamii kwa ujumla. Hivi sisi kama jamii tutaathirika vipi iwapo Nguza na wanawe wakisamehewa?
Kama nilivyotarajia, ‘mtu wa watu’ Naibu Waziri Nyalandu alinijibu juzi akisema kwa tweet (namnukuu) “copy that...” akimaanisha amesikia ombi langu na atalifanyia kazi.
Licha ya imani yangu kwa Nyalandu, nina imani pia kuwa Rais Kikwete atasikiliza ujumbe huo kutoka kwa mteuliwa wake. Vilevile ukweli kuwa huu ni Mwezi Mtukufu, na nina hakika Rais amefunga pia, roho ya huruma itamsukuma kusikiliza kilio cha mara kwa mara kutoka kwa Papii Kocha, kaka zake na baba yao.
Mwisho, ninaomba kila Mtanzania mwenye kuamini katika kuwasamehe waliotukosea (ikiwa ni pamoja na wanaotajwa kuwa wahanga wa makosa yaliyofanywa na ‘Babu Seya na wanawe) atajumuika nami kuwaombea msamaha wasanii hao.
Maandiko Matakatifu katika Surat Al I’mran 155 ya Kurani Tukufu na Marko 11:25 ya Biblia Takatifu ni baadhi za aya lukuki zinazotusisitiza kuhusu msamaha.



23 Jul 2013



MF/NA: 836'04 Johnson Nguza
(Papii Kocha) Gereza Kuu Ukonga
S.L.P 9091
Dar es SalaamMh. Rais Jamuhuri ya Muungano Tanzania


YAH: MAOMBI YA KUPEWA MSAADA (MSAMAHA) WA KUFUTIWA ADHABU YA KIFUNGO NILIYOPEWA NA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU.
Husika na somo hilo hapo juu. Mimi ni mfungwa katika gereza kuu Ukonga. Kwa heshma na taadhima na kwa kutambua utu na huruma yako ya kiMUNGU ulionayo dhidi ya binadamu wenzako pamoja na mamlaka uliokabidhiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Naanguka na kushika miguu yako mitukufu muheshimiwa rais....Nakuomba msaada (msamaha) kwako muheshimiwa rais, kwa njia hii ya maandishi kusudi niweze kuondolewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani, niliyohukumiwa na mahakama tajwa hapo juu. Mh.Rais mimi nimefungwa nikiwa bado kijana mwenye umri mdogo, na ukweli kutoka moyoni sikufanya kosa hilo.
Si mimi, baba yangu Nguza wala ndugu yangu yeyote aliyefanya kitendo kile. Lakini wenye mamlaka wakatuona tuna hatia na kuamua kuteketeza kizazi chetu gerezani.

Natamani kiama ifike ili mwenyezi Mungu aweke wazi ukweli wote uliojificha nyuma ya pazia. Mpaka sasa natambua wazi hatima pamoja na dhamana ya maisha yangu ipo katika mikono yako mitukufu Mh. Rais Naomba huruma yako muheshimiwa Rais maana mimi ni mtoto wako ninaehitaji huruma yako wewe mzazi. Lakini pia sisi ni binadamu wenye nafsi na miili kama wengine. Waliotumia mamlaka yao kutuweka gerezani nao ni binadamu pia, wenye miili na nafsi.


Ipo siku nafsi zetu zitapaswa kutoa hesabu ya tuliyoyafanya hapa duniani. wakati huo miili yetu tunayoitumia kunyanyasa wanyonge itakuwa imeoza mavumbini.


Natumaini kauli yako ya mwisho ndio itakayoleta pumzi ya uhai nafsini mwangu. Nakutakia kazi njema, afya njema na maisha marefu. Mungu akubariki. Wako mtiifu


Mfungwa NO:836'04 JOHNSON NGUZA (PAPII KOCHA)

Nimemwomba Mheshimiwa LAZARO NYALANDU, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,kupitia mtandao wa Twitter, afikishe ujumbe huu kwa Rais Jakaya Kikwete. So far, amenijibu kuwa 'ame-copy that...' na nina matumaini atasaidia katika suala hili

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.