Pasipo
kutarajiwa, jana, Jumatatu ya Oktoba 30, 2017, anga za habari huko nyumbani
Tanzania zilitawaliwa na habari moja nzito: mmoja wa wana-CCM maarufu, Mbunge
kwa tiketi ya chama hicho tawala anayewakilisha jimbo la Singida Kaskazini, na
Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bwana Lazaro Nyalandu,
alitangaza kujivua uanachama wa CCM na kuomba kujiunga na chama kikuu cha
upinzani cha Chadema.
Tukio
hilo lilileta mshangao mkubwa kwa sababu kadhaa. Kwanza, licha ya matamshi ya
hivi karibuni ya Nyalandu kuhusu haja ya kurejeshwa mchakato wa Katiba mpya,
sambamba na kuwasihi wabunge wenzie wa CCM kupinga kwa nguvu zote jaribio la
kurefusha muda wa Rais madarakani, hakukuwa na dalili kubwa na za waziwazi iwapo kuna ‘kutofautiana’
kati ya Nyalandu na chama chake.
#Tanzania ex-Tourism Minister @LazaroNyalandu quits ruling party CCM. Been calling resuming constitutional reforms + no to term limit change pic.twitter.com/p9VQVEdRJp— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Na
hata kama kungekuwa na dalili hizo – kwa kificho au wazi – bado wananchi wengi
wangepokea habari hizo kwa mshtuko mkubwa.
Sababu
ya pili ya mshangao kuhusu tukio hilo ni ukweli kwamba mwanasiasa wa chama
tawala kuamua kujiunga na upinzani, tena miaka mitatu hivi kabla ya uchaguzi
mkuu, ni suala ambalo licha ya kuhitaji ujasiri mkubwa pia linaacha maswali
kadhaa ambayo pengine sio rahisi kuyapatia majibu.
Hadi
wakati ninaandika uchambuzi huu, kilicho bayana kuhusu sababu za Nyalandu kuchukua
uamuzi huo ni sababu alizotanabaisha mwenyewe katika tamko lake kwa umma.
Akizungumza
jana, mwanasiasa huyo alidai sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kutokuridhishwa
na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za
kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa Watanzania na
kutokuwepo kwa mipaka ya wazi ya mihimili ya dola yaani Serikali, Bunge na
Mahakama.
Lakini
hata kabla ya kuchukua uamuzi huo jana, Nyalandu alishaonyesha dalili ya
kutofautiana na wana-CCM wenzie, hasa kwa uamuzi wake wa kumtembelea Mbunge
Tundu Lissu wa Chadema aliyelazwa huko Nairobi, Kenya kufuatia jaribio la
kumuua. Hadi sasa, Nyalandu anabaki kuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CCM
kumtembelea Lissu huko Kenya.


Huku
kukiwa na tetesi kwamba uongozi wa juu wa CCM umewapiga marufuku viongozi wake
kujihusisha na suala la Lissu, uamuzi wa Nyalandu kwenye Kenya ‘kinyume na
maagizo ya chama chake’ ulihisiwa kuwa ungemwingiza matatizoni.
Dalili
nyingine kuwa mwanasiasa huyo hakuwa akipendezwa na baadhi ya mienendo ndani ya
CCM ni pale alipoibuka kuhamasisha haja ya kuanzisha upya mchakato wa
kupatikana Katiba mpya, sambamba na kuhamasisha wana-CCM wenzake dhidi ya
jitihada za chini chini kuongeza muda wa Rais madarakani.
Masuala
yote hayo mawili yalitarajiwa ‘kumsababishia matatizo’ mwanasiasa huyo.
Hata
hivyo, kuna ‘sababu mbadala’ kuhusu uamuzi wa Nyalandu kujiuzulu. Kuna taarifa
kwamba kuna uchunguzi unaofanyika dhidi ya mwanasiasa huyo kuhusiana na
utumishi wake kama Waziri wa zamani wa Maliasi na Utalii. Taarifa hizo ambazo
bado ni tetesi hadi muda huu, zinaweza kupewa uzito zaidi na ‘screenshot’
inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikidaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya kundi
la Whatsapp la viongozi wanawake wa CCM.
Katika
‘chat’ husika, mmoja wa makada wa kike wa CCM anadai kuwa kuna uchunguzi
unaofanyika dhidi ya Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na
kwamba uamuzi wa kujiondoa CCM na kuomba kujiunga na Chadema una lengo la
kugeuza suala hilo kuwa la kisiasa pindi akichukuliwa hatua.
Pengine
swali muhimu linaloendelea kutawala vichwa ni “kwanini HASWA Nyalandu
amejiuzulu?” Kuna sababu alizotoa yeye mwenyewe, ambazo kwa kiasi kikubwa
zinaleta mantiki, lakini pia kuna hiyo tetesi kuwa amechukua uamuzi huo kama
tahadhari pindi akianzishiwa tuhuma za ufisadi.
Tuchambue
sababu zote mbili, yaani alizotoa mwenyewe na hizo tetesi. Kwa vile hatuna
maelezo yenye uhakika yaliyo kinyume na sababu alizotoa Nyalandu, nadhani kwa
kuzingatia busara tu, itakuwa sio sahihi kudhani anaongopa. Unapopinga kauli ya
mtu basi shurti uwe na kauli mbadala yenye uthibitisho. Kwahiyo, angalau kwa
muda huu, hakuna sababu za msingi za kupinga sababu alizotoa mwanasiasa huyo.
Kuhusu
tetesi za kuwepo kwa mchakato wa ‘kumshughulikia kutokana na tuhuma za ufisadi,’
kuna mantiki kwa mbali, na utata kwa mbali pia. Sio siri kwamba Wizara ya
Maliasili na Utalii ilikuwa kama ‘makao makuu’ ya ufisadi. Wizara hiyo ilikuwa
kama ile ya Nishati na Madini, ambapo mawaziri lukuki walihamishwa au
kuondolewa madarakani kutokana na tuhuma za ufisadi.
Kwamba
Nyalandu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kulikuwa na tuhuma za ufisadi,
hilo halina mjadala. Lakini kwa kuzingatia kanuni ya asili ya haki, tuhuma hizo
zinabaki tuhuma tu mpaka zitakapothibitishwa.
Kwahiyo,
hadi hapa, mantiki ya mbali kuhusu uwezekano wa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi
dhidi ya Nyalandu ipo. Hata hivyo, utata wa mbali ni kwamba katika mazingira ya
kawaida tu, na tukijifanya kuamini (angalau kwa minajili ya uchambuzi huu) kwa
Nyalandu anafahamu kuhusu uchunguzi huo, je isingekuwa mwafaka kwa yeye
kupambana na suala hilo akiwa CCM kuliko nje ya chama hicho tawala?
Sawa,
kuna hiyo hoja ya “amehama CCM na anataka kuhamia Chadema ili pindi akichukuliwa
hatua, suala hilo lionekane la kisiasa,” lakini ikumbukwe kuwa suala la muhimu
sio “suala lionekane la kisiasa” bali “lisitokee kabisa.” Na katika mazingira
ya kawaida, huo uamuzi wa tu Nyalandu kuhama CCM na kuikosoa hadharani unatosha
kuipa serikali ya chama hicho tawala na taasisi zake “hasira” dhidi ya
mwanasiasa huyo. Na hapo hatujagusia uwezekano wa mwanasiasa huyo kujiunga na “adui
nambari moja wa CCM” yaani Chadema.
Kwa
mtazamo wangu, kama ni kweli kuna uchunguzi unaoendelea au unaotarajiwa
kufanyika kuhusu Nyalandu basi yayumkinika kuhisi kwamba ingekuwa rahisi zaidi
kwa yeye kupambana na suala hilo akiwa ndani ya CCM kuliko nje ya chama hicho
chenye historia ya siasa za kinyongo, visasi na majitaka.
Lakini
kuna ‘angle’ kubwa zaidi katika uamuzi huo wa Nyalandu. Yawezekana amesoma vema
upepo wa kisiasa huko nyumbani chini ya utawala wa Rais Magufuli, na kubaini
vitu kadhaa. Moja laweza kuwa kinachoonekana kama wananchi wengi kutoridhishwa
na utawala wa Magufuli, ndani na nje ya CCM. Keyword hapa ni ‘kinachoonekana,’
nikimaanisha pengine ni hisia tu kuwa kuna wananchi wengi wasioridhishwa ilhali
ukweli ni kinyume na hisia hiyo.
Kwa
minajili ya uchambuzi huu, tufanye kuwa hisia hizo zipo kweli. Kwahiyo, kwa
vile Nyalandu alikuwa miongoni mwa makada wa CCM walioomba ridhaa ya chama
hicho kuwa wagombea wa urais mwaka 2015 lakini haukufanikiwa, basi pengine
anataka kutupa kete yake kupitia upande wa upinzani.
Lakini
sio tu kusukumwa na nia ya kuwania urais, lakini yayumkinika kuhisi kuwa
mazingira yaliyopo muda huu yanampatia mwana-CCM yeyote nafasi nzuri ya
kukikimbia chama hicho. Sio siri kuwa hisia kwamba Magufuli ana dalili za
udikteta zinazidi kushika hatamu. Kwa maana hiyo, hata mtu mwenye sababu zake
binafsi akikurupuka na kutamka “ninahama CCM kwa sababu utawala wa Magufuli ni
wa kidikteta” ataeleweka kirahisi, na anaweza kuungwa mkono kirahisi pia.
Kwamba
Nyalandu anaweza “kuruka kutoka kwenye ngalawa na kuingia majini kwenye bahari
yenye papa na nyangumi” sio suala dogo. Kama kuikosoa CCM ukiwa ndani ya chama
hicho ni hatari, sote twafahamu nini kinachoweza kumkumba anayediriki sio
kukosoa tu bali pia kuhama chama hicho tawala. Kwa mantiki hiyo, kwa sababu
yoyote ile – iwe hizo alizotaja mwenyewe au tetesi za uchunguzi wa ufisadi –
mwanasiasa huyo amefanya maamuzi magumu, na yayumkinika kuamini kuwa amejiridhisha
vya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Kuna
mambo matatu yanayoweza kutoa mwangaza kidogo. Kwanza, hivi karibuni, Waziri
mpya wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangallah alinukuliwa akisema
kwamba anayo orodha ya watu mashuhuri, viongozi wastaafu na wabunge
wanaojihusisha na ujangili, na atahakikisha anawashughulikia.
Pili,
jana katika hotuba yake akiwa huko Mwanza, Rais Magufuli alikumbushia kuhusu
Mahakama Maalum ya Ufisadi, ambayo pasi kuuma maneno, imekuwa kama kichekesho
kutokana na kukosa kesi. Rais kuitaja mahakama hiyo ‘isiyo na ufanisi angalau
hadi sasa’ inaweza kumaanisha kilekile alichokigusia Waziri Kigwangallah kuhusu
ujangili.
Na
tatu, ‘vijana wa Lumumba’ (makada wa CCM kwenye mitandao ya kijamii)
walishaanza kuzungumzia ‘ufisadi wa Nyalandu’ mara tu alipoenda Nairobi
kumjulia hali Lissu. Na kasi yao ya mashambulizi dhidi ya Nyalandu imepamba
moto zaidi jana baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kujiondoa katika chama hicho
tawala.
Lakini
pia kuna tamko la Humprey Polepole, ‘katibu Mwenezi’ wa CCM kuhusu uamuzi huo
wa Nyalandu. Binafsi nilitarajia tamko kali na pengine lililosheheni kebehi
kama sio kashfa (na Polepole ni hodari sana kwenye maeneo hayo), lakini
reaction ya msemaji huyo wa CCM imekuwa ‘muted.’ Sana sana ameishia kudai kuwa
Nyalandu amejiondoa kwa sababu ameshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano.
Pia amejaribu kuonyesha kuwa mwanasiasa huyo sio ‘mtu mkubwa’ ndani ya chama
hicho tawala. Huyu si Polepole tunayemfahamu kwa umahiri wake wa ‘kusema ovyo.’
Huenda ‘upole’ wake una sababu flani.
Japo
kauli ya Kigwangallah na ya Rais Magufuli, sambamba na ‘vijana wa Lumumba’
kumwandama Nyalandu, na ‘upole’ wa Polepole yanaweza kuwa mambo ya kawaida tu,
lakini pia yanaweza kutoa mwangaza kuhusu uamuzi huo wa Nyalandu. Hata hivyo,
kama nilivyotanabaisha awali, sidhani kama mazingira hayo yangetosha kumfanya
Nyalandu kuchukua uamuzi huo mzito.
Kwamba
Nyalandu ataandamwa baada ya kuchukua uamuzi huo, hilo halina mjadala. Kama
asipoandamwa na ngazi za juu za CCM au kupitia taasisi za dola/umma basi ‘vijana
wa Lumumba’ watakesha mitandaoni kumchafua. Pamoja na ukongwe wake katika siasa
si Tanzania tu bali barani Afrika kwa ujumla, kwa kiasi kikubwa CCM inaendekeza
mno siasa za kisasi, kinyongo na adui mkubwa wa ukweli. Kuikosoa CCM au
serikali yake ni kama kusaini ruhusa ya kusumbuliwa kwa kila namna.
Almost certainly CCM's "gutter politics machinery" would get into full attack mode vs @LazaroNyalandu. We'll be hearing a lot #MarkThisTweet pic.twitter.com/xsJL6rVJsu— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
On other hand,as a key minister in exceedingly corrupt 4th phase govt under Kikwete, he seemingly is readymade target of attacks from CCM— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Na
ni muhimu kutambua kuwa Nyalandu alikuwa akifahamu kuhusu ‘mabalaa’
yanayomsubiri baada ya kuchukua uamuzi huo mzito. Angalia yanayomsibu Yusuph
Manji, mtu aliyemwaga mamilioni ya fedha kuifadhili CCM lakini amebaki kuwa ‘kielelezo
cha hasira za CCM.’
Je
CCM wakiamua kulipa kisasi kwa Nyalandu watafanikiwa? Inategemea sana busara za
Magufuli. Yote yanayoelezwa kuwa ‘ufisadi wa Nyalandu’ yailikuwa na baraka za
mtangulizi wa Magufuli, yaani Rais Kikwete. Kwahiyo, kama ambavyo jitihada
zozote za kumbana Lowassa zilivyoshindikana kwa vile zingeishia kumchafua pia
Kikwete, ndivyo jaribio la ‘kulipiza kisasi kwa Nyalandu’ linavyoweza kumtia
matatani JK.
That he, allegedly, was among former President Kikwete's trusted allies might make any CCM's attempt to tarnish Nyalandu backfire.— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Licha
ya kuelezwa kuwa Nyalandu alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa JK, pia ni muhimu
kutambua kuwa mmoja wa watu wake wa karibu ni mke wa Rais mstaafu Benjamin
Mkapa, Mama Anna. Mara baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani, Nyalandu
alikuwa miongoni mwa washauri Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya
Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).
Kwa
maana hiyo, jaribio lolote la ‘kumwandama Nyalandu’ linaweza kuzua kile
Waingereza wanaita ‘unintended consequences,’ au ‘matokeo yasiyokusudiwa kwa
Kiswahili.
Pia
ni muhimu kutambua u-kimataifa wa Nyalandu. Mwanasiasa huyo ana mahusiano
mazuri na wanasiasa wenye nguvu kubwa hususan nchini Marekani. Japo ‘nguvu’ zao
zinaweza kutofua dafu kwa Magufuli, lakini sote twafahamu kuwa ni vigumu kwa
Tanzania yetu kuwa na ‘jeuri’ katika umasikini wetu.
So wht would Nyalandu bring to Chadema's table?Well, has powerful pals in US who might raise voice vs "ongoing political persecution" by JPM pic.twitter.com/DPFTE56luw— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Hatma
ya Nyalandu akifanikiwa kuhamia Chadema ikoje? Binafsi, ninahisi mambo makuu
mawili. Kwanza, ujio wake katika chama hicho kikuu cha upinzani unaweza kuamsha
msisimko mpya wa siasa za ndani na nje ya chama hicho, na Tanzania kwa ujumla.
Kwa
upande mmoja, anaweza kuendeleza hoja zake kama hiyo ya kudai kurejeshwa kwa
mchakato wa Katiba mpya, suala ambalo Chadema na washirika wake wa UKAWA ni
kama wamelitelekeza.
Lakini
pengine kubwa zaidi ni uwezekano mkubwa wa Nyalandu kuwa mmoja wa wagombea wa
Urais kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwamba
amejiondoa CCM kwa hiari yake (angalau kwa mujibu tunachofahamu hadi muda huu)
na kujiunga na Chadema kwa hiari yake, anaweza kuwa na faida ya ziada kuliko
majina mengine mawili yanayotajwa kuhusu urais mwaka 2020 kupitia Chadema,
Mawaziri Wakuu wa zamani, Lowassa na Sumaye.
He (Nyalandu) is likely to become potential presidential candidate for Chadema in 2020 General election.Other names are Lowassa,Sumaye+Lissu pic.twitter.com/ct25FP7jiw— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Kwamba
Nyalandu ni ‘mwana-CCM pekee aliyemjali Lissu kwa kumtembelea huko Nairobi,’ na
ukweli kuwa yeye na Lissu wanatoka mkoa mmoja, wanaweza kujenga ‘dream team’
inayoweza kuirejesha Chadema enzi za kina Dkt Slaa, Zitto na Mbowe.
Lakini
pia katika mazingira yaliyopo sasa, Chadema imekuwa kama haina mpango wa
kushiriki uchaguzi mkuu ujao. Maandalizi yanayopaswa kufanyika sasa – miezi 36
tu kabla ya uchaguzi huo – ni kama hayapo. Ndiyo, Magufuli kapiga marufuku
shughuli za kisiasa, lakini ni lini Rais kutoka CCM aliwahi kuridhika shughuli za
wapinzani?
Kwa
maana hiyo, ujio wa Nyalandu unaweza kuamsha matumaini kwa chama hicho kikuu
cha upinzani kuhusu nafasi yake katika uchaguzi mkuu ujao.
Hata
hivyo, kuna vikwazo vikuu viwili. Cha kwanza, ni lile lililojiri baada ya
Lowassa kujiunga na CCM, Kwa minajili ya kumbukumbu tu, Chadema ilimwandama
Lowassa kuwa ni ‘baba wa ufisadi’ kwa takriban miaka 9 mfululizo, kisha ghafla
wakampokea na kumfanya mgombea wao wa Urais katika uchaguzi mkuu uliopita. Kwa
busara za kawaida tu, huwezi kumchafua mtu kwa muda wote huo kisha ukategemea
kumsafisha ndani ya miezi mitatu. Japo makada wa chama hicho hawataafiki,
athari za kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wao zinaendelea kukisumbua chama
hicho.
Kama
ilivyokuwa kwa Lowassa, baadhi ya viongozi wa Chadema walishawahi ‘kumpaka’
Nyalandu wakimwita fisadi, hali inayoweza kutumiwa na CCM kudai kuwa ‘Chadema
ni kimbilio la mafisadi.’ Hata hivyo ni rahisi kwa chama hicho cha upinzani
kuwauliza CCM, “mpaka mwanasiasa awakimbie na kujiunga nasi ndio mnaanza
kumwita fisadi?” Ni hoja inayoingilia akilini.
Reminds me of "Lowassa's corrupt" tale but when told to prove it or take him to the court,was clear such move would open can of worms re: JK pic.twitter.com/B7RU5cQ2vG— Evarist Chahali (@Chahali) October 30, 2017
Je
Nyalandu atapata mapokezi mazuri huko Chadema? Kama kauli ya Lowassa jana kuwa
Chadema itakuwa ‘imelamba dume’ pindi Nyalandu akijiunga na chama hicho
inaashiria chochote basi kuna uwezekano mkubwa wa mafanikio makubwa kwa
mwanasiasa huyo.
Hata
hivyo, ukweli kwamba Nyalandu ni miongoni mwa watu wenye sifa na uwezo wa kuwa
wagombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020 unaweza kupelekea mgongano
dhidi yake na majina mengine yanayotarajiwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro hicho,
yaani Lowassa, Sumaye na Lissu.
Hili
sio tatizo kubwa sana iwapo maslahi ya Chadema – badala ya maslahi ya mtu au
kikundi binafsi – yakiwekwa mbele. Kwamba kufanyike tathmini ya kutosha
kufahamu nani anayeweza kukiwezesha chama hicho kuing’oa CCM madarakani hapo
mwaka 2020.
Kwamba
Nyalandu anaweza kuleta hamasa kwa wana-CCM wengine (Membe?) kujiunga na
Chadema, na kama ujio wake huko Chadema utaleta matokeo chanya, ni suala la
muda. Lililo bayana hadi muda huu, uamuzi wake huo wa ghafla umetushtua wengi
ikiwa ni pamoja na CCM na makada wake. Na yayumkinika kuamini kuwa uamuzi huo
utaleta msisimko mpya katika siasa za Tanzania.
Mwisho,
uchambuzi huu umetokana na uelewa wangu wa siasa za Tanzania, na unaweza kuwa
sio sahihi kulingana na mitazamo tofauti. Jiskie huru kuchangia maoni,
kunikosoa au hata pongezi zinaruhusiwa. Siku zote ninajitahidi kwenda mbali
zaidi ya kuripoti tu matukio badala ya kuyachambua kwa undani zaidi. Asanteni
na siku njema