25 Mar 2017


Kuna wanaotusimanga tuliompigia kampeni Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Kwamba sie ndo tumemleta Magufuli. Kwamba bila sie kumnadi, Tanzania isingeshuhudia kipindi hiki cha 'maajabu' ambapo kwa mara ya kwanza tumeshuhudia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam'anayebebwa na Magufuli' akiwa na uhuru wa kuvunja sheria, na yeyote atakayemkemea atakuwa amenunua ugomvi na Magufuli.

Wanaotusimanga wanasahau kitu kimoja. Laiti Upinzani ungekuwa na mgombea imara katika uchaguzi mkuu uliopita, kazi ya kuiangusha CCM ilikuwa rahisi kuliko wakati mwingine wowote ule.

Nakumbuka kada mmoja mwandamizi wa CCM alinieleza wakati wa kampeni kuwa "laiti Wapinzani walivyoungana na kumsimamisha mtu asiye na rekodi yenye mawaa, kwa mfano Dokta Slaa hivi, basi uchaguzi huu ungekuwa mgumu sana kwetu." Alieleza kuwa UKAWA uliirahisishia CCM kampeni ya kumnadi mgombea wake kwa vile, pamoja na sababu nyingine, mgombea wa UKAWA -Lowassa- alikuwa akijulikana vizuri mno huko CCM, kitu kilichowarahisishia kumshinda 'kirahisi.'

Kwahiyo, kabla ya kuachana na suala la lawama hizo, niseme hivi: sie tuliomnadi Magufuli hatukujua kuwa angekuja kubadilika kiasi hiki, lakini laiti Upinzani ungesimamisha mgombea bora, sie wengine wala tusingekimbia, tungefanya kampeni kama mwaka 2010, na kwa vile kwa kiasi kikubwa Upinzani auliamia kuweka kando tofauti zao, basi uwezekano wa kuiangusha CCM ulikuwa mkubwa. Ila hayo yameshapita sasa, tugange yaliyopo na yajayo.

Na yaliyopo tunayaganga vipi? Ni kwamba wakati tunaendelea kukuna vichwa kufahamu kitu gani kilichomsibu Rais Magufuli, aliyeingia kwa kishindo kikubwa sio Tanzania tu bali kimataifa pia, na hadi kutawala dunia na alama ya reli #WhatWouldMagufuliDo hadi kufikia hatua aliyofikia sasa ya kutawala kwa vitisho, jazba, ubabe na kutetea waziwazi uvunjifu wa sheria uliofanywa na RC Makonda, ni vema basi tujipange imara kuzuwia jitihada zozote za kiongozi huyu kuwa wa kutumia mabavu tu.

Kuna mwanafalsafa mmoja aliusia huko nyuma kuwa "ili maovu yashamiri, yahitaji tu watu wema kutofanya lolote." Wenye uwezo wa kupiga sauti dhidi ya maovu tukikaa kimya, labda kwa vile tu tuliwahi kumpigia kampeni Magufuli, au kwa vile "yatapita tu," kuna kila dalili kuwa tunakoelekea sio kuzuri.

Moja ya mambo yanayotatiza sana kuhusu Rais Magufuli ni kile kinachoonekana kama kupenda ugomvi usio wa muhimu. Hilo nimelieleza kwa kirefu katika makala ninayoiambatanisha hapo chini ambayo ilipaswa kuchapishwa na gazeti la Raia Mwema toleo la wiki hii lakini ninahisi haikuchapishwa (njia pekee ya mie kufahamu imechapishwa au la ni kuona makala husika kwenye tovuti ya gazeti hilo, na wiki hii haipo).

Kati ya nilipoandika makala hiyo na leo, kuna matukio makubwa manne yaliyojitokeza. Kwanza ni Waziri wa Habari (na masuala mengine)  Bwana Nape Nnauye kusimamia vema wajibu wake kama waziri husika, kufuatilia uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha redio na televisheni cha Clouds. Nape alipokea ripoti ya Tume aliyounda, na licha ya msimamo wa Magufulikujulikana mapema kuwa "anambeba Makonda," Nape alionyesha ujasiri na kuiweka hadharani ripoti hiyo ambayo awali baadhi yetu tulidhani ingekuwa 'changa la macho.'

Tukio la pili ni uamuzi wa Rais Magufuli kumfukuza kazi Nape kwa kufanya mabadiliko kwenye kabineti yake, na nafasi ya Nape kukabidhiwa Dkt Harrison Mwakyembe, ambaye majuzi tu 'alilikoroga' kwa kupiga marufuku kufunga ndoa bila cheti cha kuzaliwa. Amri hiyo ya kizembe ilitenguliwa na Magufuli siku chache baadaye.

Tukio la tatu ni mkutano wa Nape na waandishi wa habari, ambao tukiweka kando aliyoyasema mwanasiasa huyo, kubwa zaidi lilikuwa kitendo cha afisa mmoja wa usalama (haijulikani kwa hakika kama alikuwa polisi au taasisi nyingine ya dola) kumtolea bastola Nape hadharani. Tukio hilo la kutisha, na lile na Makonda kuvamia Clouds, yatabaki kuwa historia isiyopendeza kwa taifa letu kwani hayajawahi kutokea...labda zama za ukoloni.

Tukio la nne ni 'mafuriko' ya maneno yasiyopendeza kutoka kwa Rais Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa jana wakati anawaapisha Mwakyemba na Profesa Kabudi, aliyerithi nafasi ya Mwakyembe. 

Sitaki kurudia vitisho alivyotoa Rais Magufuli lakini nachoweza kutahadharisha ni kuwa tunakoelekea sio kuzuri. Unapoona Rais anakerwa kwa vile habari zinazomhusu hazijapewa kipaumbele kwenye vyombo vya habari vingi, basi ujue tuna tatizo kubwa. Unapoona Rais anaamini kuwa habari za maandamano ya wafugaji na wakulima kuhusu migogoro ya ardhi ni "habari mbaya mbaya" basi ni wazi huyu si yule tuliyedhani ni tetezi wa wanyonge.

Tulipasw akuona dalili hizo mapema, kupitia baadhi ya kauli zake kama "I wish I could be Jaji Mkuu" na "I wish I could be IGP." Ukiona Rais anatamani madaraka zaidi ya aliyonayo, hiyo ni hali ya hatari.

Nihitimishe makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli asikilize ushauri anaopewa na "wataalamu kuhusu hali ilivyo huko mtaani." Kadhalika, ninamsihi Rais wangu apunguze jazba. Hazitamfikisha popote. Aache kasumba ya kutafuta 'mabifu' yasiyo na msingi. Lakini jingine ni ukweli kwamba hatoweza 'kumbeba Makonda' milele, na kuendelea kumkumbatia kijana huyo kunaweza kumgharimu yeye Magufuli binafsi. 

SOMA MAKALA ILIYOPASWA KUTOKA KATIKA RAIA MWEMA TOLEO LA WIKI HII (JUMATANO 23/03/2017) LAKINI HAIKUTOKA (KWA SABABU WANAZOJUA WAMILIKI WA GAZETI HILO)


MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA MACHI 22, 2017

Disemba 31 mwaka juzi, siku ya mkesha wa ‘mwaka mpya 2016, nilichapisha kitabu cha kielektroniki kilichobeba jina “Dokta John Magufuli: Safari ya Urais, Mafanikio na Changamoto Katika Urais Wake.”

Pamoja na watu wengi waliokisoma kitabu hicho kukipongeza, wapo pia walionikosoa, hoja yao kuu ikiwa “ni mapema mno kutathmini Urais wa Magufuli katika muda huu mfupi aliokaa madarakani.”
Kwa wakati huo, sikuafikiana na ukosoaji huo, hasa kwa vile tathmini ya uongozi ni kama maadhimisho ya siku ya kuzaliwa: yanaweza kufanywa siku 40 baada ya kuzaliwa, kila mwezi, na kila mwaka kama wote tunavyofanya.

Kwahiyo, sikuona tatizo katika kufanya tathmini ya urais wa Dokta Magufuli, hasa ikizingatiwa kuwa aliingia na “kasi ya kutisha.” Kati ya siku aliyopishwa, Novemba 5, 2015 hadi nilipochapisha kitabu hicho – takriban miezi miwili hivi – Rais Magufuli alimudu kukonga nyoyo, sio za Watanzania tu, bali dunia nzima kwa ujumla kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya uzembe, rushwa, ufisadi, sambamba na ari yake kubwa ya kubana matumizi.

Naamini sote tunakumbuka alama ya reli (hashtag) ‘iliyotikisa’ dunia nzima ya #WhatWouldMagufuliDo ambayo watumiaji mbalimbali wa mtandao wa kijamii wa Twitter katika kila kona ya dunia walijaribu kuonyesha jinsi gani Dokta Magufuli alivyo bora zaidi ya viongozi wengine duniani.

Lakini sababu nyingine ya kuandika kitabu hicho ilikuwa ushiriki wangu binafsi kwenye kampeni za kumnadi Dokta Magufuli kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Pamoja na sababu nyingine, niliamua kumnadi kutokana na sababu zangu binafsi dhidi ya mpinzani wake mkuu.

Na haikuwa kazi rahisi kumnadi mwanasiasa huyu, kwa sababu baadhi ya watu walishindwa kabisa kunielewa, huku wengine wakihoji “kwanini unaweza kutusaliti wapinzani na kumpigia debe mgombea wa chama tawala, ambacho wewe binafsi ni mhanga wa unyanyasaji unaofanywa na serikali yake dhidi ya wanaoikosoa?” Na kilichoambatana na kauli hizo ni matusi mazito, udhalilishaji usiomithilika, na mengineyo yasiyostahili kukumbukwa.

Takriban miaka miwili baadaye, nimeshikwa na bumbuwazi baada ya kumsikia Rais Magufuli “akimkingia kifua” Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye majuzi ameandika historia ya matukio ya kisiasa nchini Tanzania kwa kuvamia ofisi za kituo cha habari cha Clouds, akiambatana na askari wenye silaha nzito.

Niweke rekodi sahihi. Awali nilimtetea RC Makonda katika nilichoamini kuwa ni jitihada zake dhidi ya biashara haramu ya madawa ya kulevya. Niliamini kuwa suala la ‘utata wa elimu yake’ ni sehemu tu ya mikakati za kumwondoa kwenye ajenda hiyo muhimu.

Hata hivyo, baada ya mawasiliano na “wenye uelewa wa yanayojiri nyuma ya pazia la siasa za Tanzania,” nilithibitishiwa kuwa tuhuma dhidi ya kiongozi huyo zina ukweli, na nikaelezwa kuwa “hata Dokta Magufuli anafahamu hilo.” Na kimsingi, awali nilipanga makala hii iwe ya ushauri kwa Rais kuchukua hatua stahili dhidi ya mteuliwa wake huyo “ili kuwatendea haki wanaomshauri.”

Lakini kabla sijawasilisha makala hiyo, ambayo ililenga zaidi kwenye kusisitiza haja kwa viongozi wetu kuzingatia ushauri wa kitaalamu badala ya kuendekeza ajenda binafsi, kukajitokeza tukio la RC Makonda kuvamia huko Clouds.

Nitumie fursa hii kuupongeza uongozi wa kampuni ya Clouds, hususan Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga, kuwa kufanya kile kilichotamaniwa na Watanzania wengi waliokuwa wakisubiri tamko la kampuni hiyo kuhusu tukio hilo la uvamizi wa Makonda, kwamba wasimamie ukweli.

Na kwa hakika, Ruge na Kusaga hawakuwaangusha watumishi wenzao wa Clouds na Watanzania kwa ujumla, wakaeleza “A hadi Z” ya kilichotokea wakati wa uvamizi huo ambao, kwa kumbukum bu zangu, ni wa kwanza kabisa kutokea nchini mwetu.

Ingeweza kuwa rahisi tu kwa viongozi hao wa Clouds “kuweka mbele maslahi yao binafsi” na kubadili maelezo, hasa ikizingatiwa kuwa lolote ambalo wangesema lingeweza kuaminika, lakini wakaamua kuhatarisha uhusiano wao na Makonda pamoja na shabiki mkubwa wa kituo hicho, yaani Rais Magufuli mwenyewe.

Akiongea kwenye uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za juu, pamoja na mambo mengine Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kujielekeza kwenye vitu vya maendeleo badala ya kujielekeza zaidi kwenye udaku. Ikumbukwe kuwa siku chache tu zilizopita, Rais alipiga simu kwenye kituo cha televisheni cha Clouds na kueleza kuwa yeye pia ni shabiki wa kipindi cha Shilawadu, ambacho ni cha “udaku” huo huo anaokemea Rais.

Suala hapa sio tu “kama ni sahihi kwa Rais kuwa shabiki wa kipindi cha udaku, basi isiwe dhambi kwa wananchi kupenda udaku” bali “kitendo cha Makonda kuvamia Clouds sio kujielekeza kwenye maendeleo.”

Dokta Magufuli alikumbusha pia kuwa “kampeni zimekwisha, ulie lakini Rais ni Magufuli, mimi kwangu hapa ni kazi tu, maendeleo.” Hivi kweli Rais anaamini kelele za kutaka Makonda achukuliwe hatua kutokana na uvamizi huko Clouds ni mwendelezo wa kampeni? Au ni “kelele za wasiojua kuwa Rais ni Magufuli”? Na sitaki kabisa kuamini kuwa Rais anaamini kitendo cha uvamizi wa Makonda huko Clouds ni sehemu ya “hapa ni kazi tu.”

Kilichonisikitisha zaidi ni kauli ya Dokta Magufuli kwamba “mnahangaika na viposti vyenu mara hili mara lile, mpaka wengine wanaingilia uhuru wangu kwamba nifanye hivi, ukiniingilia ndio unapoteza kabisa.”

Kwangu binafsi, nimeoiona kauli hiyo ya Rais kuwa kama dhihaka dhidi ya baadhi yetu tulioshiriki kikamilifu kumpigia kampeni mwaka 2015 kwa kutumia “viposti” hivyo hivyo anavyovidharau. Na sio sahihi kwa Rais kudai tunamwingililia uhuru wake. Yeye ni mtumishi wetu, na tuna haki ya kumweleza matakwa yetu. Huko sio kumwingilia uhuru wake bali kudai stahili yetu kutoka kwake.

Rais alitukumbusha pia kuwa yeye hapangiwi mambo, anajiamini, na ndio maana siku ya kuchukua fomu alikwenda peke yake. Kumtaka amwajibishe mteule wake aliyevamia kituo cha habari sio kumpangia mambo bali kumkumbusha wajibu wake kama kiongozi. Na kupangiwa mambo kama “mwajiriwa wa Watanzania” sio kosa, isipokuwa tu pale “kumpangia mambo” huko kunalenga kuidhuru nchi yetu.

Sawa, Dokta Magufuli alikwenda peke yake kuchukua fomu za kuwania urais, lakini hakufanya kampeni peke yake. Na kwenda kwake pepe yake kuchukua fomu hakumpi ruhusa ya kutuongoza peke yake, bali kwa ushirikiano kati yetu waongozwa na yeye kiongozi. Hivi, sio Dokta Magufuli huyuhuyu ambaye kila mara anatusihi tumwombee, lakini leo anatuona tunamwingilia?

Kadhalika, Rais alimuunga mkono RC Makonda kwa kumwambia kuwa yeye (Rais) ndio anayepanga nani akae wapi na afanye nini…kwahiyo RC Paul Makonda achape kazi. Hivi Rais amesahau kuwa sio yeye kama Magufuli bali taasisi ya Urais ndiyo inayompa nguvu kufanya maamuzi kwa maslahi ya Watanzania wote?

Na je Dokta Magufuli anataka kutuaminisha kuwa ameridhia kitendo cha Makonda kuvamia kituo cha habari akiwa na askari wenye silaha, kiasi cha kumtaka Mkuu huyo wa mkoa “aendelee tu kuchapa kazi”? Je hiyo haitompa jeuri Makonda, na hata wengineo, kufanya “abuse of power” kwa vile “Rais kuruhusu”?

Nimalizie makala hii kwa ushauri huu kwa Dokta Magufuli: kwanza, hakuna tija katika kusaka ugomvi usio na umuhimu (picking up cheap fights). Uamuzi wa kuzuwia kurushwa matangazo ya bunge mubashara, kuzuwia mikutano ya vyama vya siasa vya upinzani, kuwaambia wahanga wa tetemeko Kagera kuwa “serikali haikuleta tetemeko hilo” na “kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe”, kuwaambia wananchi wanaolalamikia njaa kuwa “wewe Rais huwezi kuwapikia,” nk sio tu ni “kusaka ugomvi usio wa lazima” lakini haziendani na matarajio ya Watanzania kwako Rais wetu.

Vilevile ninaomba sana kumshauri Rais kuzingatia ushauri wa kitaalamu anaopatiwa na wasaidizi wake. Ni vigumu kufafanua katika hili, lakini ninaamini “nimeeleweka.” Taifa litakuwa katika hali mbaya itapofika mahala “washauri watakapotumia njia mbadala kukufikishia ujumbe.” Na ndicho kinachotokea kuhusu “viposti.”

Mwisho, siku zote Rais wetu umekuwa ukimtanguliza Mungu katika hotuba zako mbalimbali na kuwasihi Watanzania wakuombee. Wewe ni Mkristo, na hii ni Kwaresma. Ni kipindi cha maungamo, kusamehe waliotukosea, kuangalia tulikotoka, tulipo na tuendako. Penye Mungu pana upendo, na penye upendo pana haki. Japo hupangiwi cha kufanya, naomba kukushauri uwapatie haki Watanzania kwa kumwajibisha RC Makonda kwa kuvunja haki za Clouds kutokana na uvamizi aliofanya.
Mungu Ibariki Tanzania


Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @cha



21 Mar 2017



Baada ya tukio la Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kuvamia ofisi za Kampuni ya Clouds jijini Dar, Ijumaa usiku, na kuahidiwa na uongozi wa Kampuni hiyo kuwa ungetoa taarifa rasmi jana, watu wengi - ikiwa ni pamoja nami- walihisi kuwa "sio rahisi kwa Clouds kumtosa Makonda, kwa vile ni mshkaji wao."

Sie hapa Uingereza tupo masaa matatu nyuma ya masaa ya Tanzania (japo Jumapili ijayo masaa yatabadilika), na jana nilipoamka, tayari uongozi wa Clouds chini ya Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga ulikuwa umeshatoa taarifa kuhusu kilichojiri Ijumaa iliyopita kuhusu Makonda.

Awali, nilitaka kupuuzia kufuatilia habari hiyo nikihofia "kuharibu siku yangu kwa kuianza na habari mbaya" nikidhani kuwa Ruge na Kusaga "wamemsafisha Makonda."

Hata hivyo, baada ya kutupia macho tweets za Millard Ayo aliyerusha press conference ya uongozi wa Clouds mubashara, nilibaini kuwa Ruge, Kusaga na Clouds kwa ujumla wamefanya kile ambacho kimekuwa kigumu mno kufanywa na Watanzania wengi: kuwa wakweli. Kuwa tayari kupoteza rafiki kuliko kupoteza ukweli.

Kwa wengi hilo linaweza kuwa suala dogo lakini kwa hakika lina umuhimu wa kipekee. Sote twafahamu ukaribu wa Makonda na Clouds, na hata Ruge amekiri kuwa yeye binafsi ni rafiki na Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwahiyo, kama ilivyotarajiwa na wengi, ingekuwa rahisi zaidi kwa Clouds "kumbemba Makonda" (kama alivyobebwa na Rais Magufuli) na pengine "stori ingeishia hapo" kuliko kuamua kusimamia kwenye haki na ukweli.

Jana niliwapa angalizo ndugu zangu wa Clouds kuhusu "kukubali kutumika." Nili-tweet hivi


Lakini japo ni rahisi kulaumu kuliko kujihangaisha kujua kwanini flani kafanya kitu tunachomlaumu kukifanya, mazingira ya media zetu yanalazilazimisha kutumika. Kwahiyo, wakati ni rahisi kuwalaumu Clouds "wanapotumika" kuinadi CCM na serikali yake, ni muhimu twenda mbali na kufahamu kwanini wanafanya hivyo.

Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, uhuru wa habari Tanzania bado ni fadhila kutoka kwa watawala. Kwa kiasi kikubwa, chanzo kikuu cha mapato ya vyombo vya habari ni matangazo kutoka serikalini. Kwahiyo, chombo cha habari "kitakachoiudhi serikali" kinaweza kujikuta kinanyimwa matangazo. Hiyo inalazimisha "urafiki" kati ya vyombo hivyo na serikali.

Lakini licha ya matangazo, vyombo vyetu vya habari vinafanya kazi katika mazingira kandamizi, na kwa ridhaa ya watawala badala ya kanuni stahili. Ndio maana, kama tulivyoshuhudia jana, Waziri Nape anapigania "sheria" huku Bosi wake Magufuli anakumbatia ridhaa yake kama mtawala.

Kingine kinachohusiana na tukio hilo ni ukweli kwamba Rais wetu Dokta John Magufuli anaelewa kasoro za wasifu wa elimu ya Makonda...kwa sababu alishajulishwa ukweli huo na "wahusika." Laiti angefanyia kazi ushauri aliopewa, tusingefika hapa. 

Kuna tatizo pia katika jinsi Rais wetu alivyojitahidi kutuonyesha kuwa ni rafiki wa Clouds, na ameshapiga simu mara kadhaa na kurushwa hewani, 

na kusifiwa na watu kibao kuwa "ni mtu wa watu" lakini swahiba wake, Paul Makonda, alipovunja sheria kwa kuvamia ofisi za Clouds, akapuuza "urafiki wake na Clouds" na "kumbeba swahiba wake Makonda." 
Kasoro nyingine ni kudai kuwa yeye Rais anapenda kipindi cha "udaku" cha Shilawadu cha Clouds lakini jana anatuchamba kuwa "Watanzania tunaendekeza udaku." Je ni Rais pekee anayestahili kupenda udaku, lakini ni jinai kwa raia wa kawaida?


Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Magufuli aache kupenda ugomvi usio na maana, Waingereza wanaita "cheap fights." Alizuwia "matangazo ya bunge mubashara," na majuzi kajisifu kwa hatua hiyo; lilipotokea tetemeko Kagera, akakaa muda mrefu bila kwenda kuwapa pole wahanga, na alipokwenda akawasemea ovyo, eti "yeye hakuleta tetemeko hilo" na "hakuna serikali duniani inayosaidia wahanga wa tetemeko" (kitu ambacho sio kweli).


Kana kwamba hayo hayakutosha kutibua watu, alipokuwa ziarani mikoani, wananchi walisikika wakimwambia "njaa baba!" akawasemea ovyo "njaa mnataka mie niingie jikoni kuwapikia?" Na jana, amejigamba kuwa anajiamini, ndio maana alikwenda kuchukua fomu ya kuwania urais peke yake. Anajifanya kusahau kuwa hakujipigia kampeni peke yake, na kuna tuliotukanwa mtandaoni tukihangaika kumpigia kampeni.

Nilishaandika kwenye jarida la Raia Mwema kumsihi Rais Magufuli azingatie umuhimu wa kutumia lugha ya kidiplomasia badala ya kuendekeza ukali usio na maana, hasa katika mazingira kama ya jana ambapo hakupaswa kumlinda Makonda kwa uhuni aliofanya huko Clouds. Kusema "hapa ni kazi tu" kwa minajili ya kumlinda Makonda kinatufanya tuliosapoti kauli mbiu hiyo ya "hapa ni kazi tu" kujiskia kichefuchefu. Yaani "hapa ni kazi tu" kwa Mkuu wa Mkoa kuvamia kituo cha habari akiwa na askari wenye silaha?


Lakini kosa kubwa alilofanya Magufuli jana sio kumtetea Makonda bali kutupa jawabu la wazi kuwa jeuri ya Makonda inatoka kwa bsoi wake, yaani Magufuli. Kwanini Magufuli anamlinda Makonda kiasi hicho? Baadhi yetu twaelewa lakini huu sio muda mwafaka kuyaongelea hayo. Ila tu Rais wetu afahamu kuwa sapoti ya baadhi ya watu kwake ina ukomo, itafika mahala "akimwaga mboga, watamwaga ugali." I hope hatutofika huko. I hope Rais wetu atatumia busara, kufanyia kazi mapungufu yake eg kuwabwatukia watu ovyo huku anawalea watu kama Makonda, na kuepuka kusaka ugomvi usio na maana.

Historia ina mafundisho mengi kuhusu viongozi walioendekeza jeuri, kiburi, ubabe, dharau na kujiona majabali, na hatma yao haikuwa nzuri.

Waingereza wanasema WRONG IS JUST THAT, WRONG (Kitu kisicho sahihi kiko hivyo tu, hakiko sahihi). Alichofanya Makonda was wrong. Utetezi wa Rais Magufuli kwa Makonda was wrong too. Huo ni ukweli hata kama utamchukiza Mheshimiwa Rais.





16 Mar 2017


MAJUZI, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifanya Mkutano wake Mkuu Maalum huko Dodoma, ambao pamoja na mambo mengine ulikuwa na ajenda kuu ya "kujadili na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama hicho na jumuiya zake."
Nimeyawekea msisitizo maneno "kujadili na kupitisha" kwa sababu inaonekana kuwa wazi kuwa majadiliano yaliyofanyika hayakupaswa kutoyapitisha marekebisho hayo.
Ni rahisi kutafsiri hatua hiyo kama ya kuminya demokrasia (kwa maana kwamba kujadili pekee hakutoshi bali pia kuwepo uhuru wa kuyakubali au kuyakataa mapendekezo husika) lakini pengine ni rahisi pia kutambua kwanini CCM "ilijihami" mapema.
Mabadiliko hayo ya katiba ya chama hicho yamepelekea kupungua idadi ya wajumbe wa vikao vya ngazi za juu vya chama hicho na kupunguza 'kofia mbili' kwa viongozi wenye vyeo ndani ya chama, serikalini au bungeni.
Kutokana na mabadiliko hayo, mwanachama anatakiwa kushika nafasi moja tu ya uongozi, katika ngazi za Mwenyekiti wa Tawi, Kijiji, Mtaa, Kata, Wadi, Jimbo, Wilaya na Mkoa. Wengine ni Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote, Diwani na Mbunge/Mwakilishi.
Kwa hiyo ni wazi kuwa mabadiliko hayo yanawaathiri 'vigogo' kadhaa wa chama hicho, na pengine ndio maana ikaamuliwa kuwe na "mjadala na kupitisha mabadiliko hayo" badala ya "mjadala na kupitisha au kutopitisha mabadiliko husika."
Kadhalika, mabadiliko hayo yatapelekea kupungua kwa idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, kutoka 34 hadi 24.
Vilevile, idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho imepungua zaidi ya nusu, kutoka 388 hadi 168.
Miongoni mwa 'vigogo' waliotarajiwa kuathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na kushika nyadhifa zaidi ya moja ni pamoja na William Lukuvi, Makame Mbarawa, Dk. Hussein Mwinyi, na Shamsi Vuai Nahodha.
'Kigogo' mwingine ni Mama Salma Kikwete, ambaye licha ya kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Lindi, hivi karibuni aliteuliwa na Rais  Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.
Wengine ni wenyeviti wa CCM mikoa ambao pia ni wabunge, kama vile Joseph Musukuma, Martha Mlata na Deo Simba, ilhali Godfrey Zambi ni mbunge na mkuu wa mkoa, Adam Kimbisa ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma.
Kuna usemi mmoja, kwamba sio kila kitu sahihi ni kizuri, na sio kila kitu kizuri ni sahihi. Uamuzi wa CCM kuwapunguzia wanachama wake kofia zaidi ya moja kwenye uongozi ni sahihi lakini sio mzuri kwa watakaoathiriwa nao.
Jicho la uchambuzi litaelekezwa kwa 'wahanga' hao kadri chama hicho kinavyoingia kwenye mchakato wake wa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, na kwenye kinyang'anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2020.
Siku moja kabla ya Mkutano huo Mkuu Maalum, chama hicho tawala kilitangaza adhabu kwa viongozi wake kadhaa, kubwa zaidi ikiwa kuwavua uanachama viongozi 12 akiwemo Sophia Simba, kada mkongwe wa chama hicho na ambaye hadi anapewa adhabu hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge.
Hatua hizo kali zilizochukuliwa na CCM chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli, sambamba na mabadiliko niliyoyaongelea awali, yana tafsiri kuu mbili.
Kwanza, hatua kali za kinidhamu zinapeleka ujumbe kwa wana-CCM wa kada mbalimbali kuwa Rais Magufuli amepania kwa dhati kukisafisha chama hicho tawala.
Pili, mabadiliko kusudiwa, sambamba na hatua kali zilizochukuliwa dhidi ya viongozi kadhaa wa chama hicho, ni mtihani mkubwa, kwa Mwenyekiti Magufuli na CCM kwa ujumla.
Kwa Mwenyekiti Magufuli, hatua hizo zimemwongezea idadi ya maadui zaidi ya wale ambao tayari ni waathirika wa msimamo wake dhidi ya ufisadi na rushwa, ambapo watendaji kadhaa wa serikali wametumbuliwa huku wakwepa kodi wakidhibitiwa, na majangili na 'wauza unga' wakibanwa.
Japo ni mapema mno kufanya tathmini timilifu kwa hatua hizo, ile kuzichukua tu sio tu kwaonyesha dhamira lakini pia ni wazi zimetengeneza maadui wa kutosha dhidi ya Dk. Magufuli.
Katika hili, ni muhimu kutambua kuwa ni bora kuwa na kiongozi atakayechukiwa na kwa kutenda vitu sahihi kuliko atakayependwa kwa kufanya madudu.
Siku moja kabla ya Mkutano huo Mkuu Maalum zilipatikana taarifa za kukamatwa kwa makada watatu wa chama hicho, Msukuma, Hussein Bashe na Adam Malima.
Kilichonisikitisha ni maelezo kuwa "walikamatwa na kuhojiwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa CCM."
Katika mazingira ya kawaida, sio rahisi kwa makada hao watatu kupanga kuvuruga mkutano mkubwa kama huo ila yayumkinika kuhisi kuwa kilichofanyika ni kuzuwia kile nilichogusia awali, yaani "sio kujadili na kupitisha tu mabadiliko husika" bali pia "kujadili na kupitisha au kutopitisha mabadiliko hayo."
Hili la kuminya fursa ya upinzani kwa mabadiliko hayo linaweza kuwa na athari kwa chama hicho huko mbeleni. Sauti za manung'uniko ni kitu cha kawaida lakini sauti hizo zikiakisi mtazamo wa watu wengi, zinaweza kuathiri mshikamano wa chama hicho.
Hata hivyo, kwa wanaotarajia kuwa "CCM itakufa kutokana na mabadiliko haya" wanapaswa wazielewe vema siasa za Tanzania yetu.
Si kwamba CCM itatawala milele, lakini kwa mazingira tuliyonayo hivi sasa, hakuna chama mbadala. Huo ndio ukweli mchungu.
CCM wanaweza kukandamiza upinzani dhidi ya mabadiliko ya Katiba yao lakini angalau wameitisha mkutano mkuu, wamejadiliana na kupitisha mabadiliko ya katiba yao, sambamba na wameadhibu waliokiuka taratibu za chama hicho.
Sio kamili, lakini hiyo yaakisi demokrasia kwa kiasi fulani. Kwa takriban vyama vyetu vyote vya upinzani, jaribio la kufanya kilichofanywa na CCM wiki iliyopita linaweza kutishia “kukiuwa” chama husika.
Ukiangalia wapinzani wakuu wa CCM, yaani Chadema, sio tu "wamegoma kabisa" kufanya tathmini ya kilichowaangusha katika uchaguzi mkuu uliopita bali pia wametelekeza turufu yao kubwa na iliyowajengea imani kubwa kwa Watanzania, yaani mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi, yaliyoibua 'List of Shame,' skandali nzito kama Richmond, EPA, Kiwira, nk.
Cha kusikitisha ni kwamba vyama vyetu vya upinzani sasa vimekuwa kama vinachezeshwa ngoma na CCM. Wafuasi wa vyama hivyo "wapo bize" kujadili matukio yanayoihusu CCM badala ya kuwekeza nguvu kwenye mustakabali wa vyama hivyo.
Jiulize, hivi ajenda kuu ya Chadema, au CUF au ACT- Wazalendo ni ipi muda huu?
Ni katika mazingira hayo, baadhi ya viongozi wa CCM watavumilia mabadiliko yanayoendelea ndani ya chama chao kwa sababu hakuna mbadala wa chama hicho tawala kwa sasa. Tumebaki na miaka mitatu na miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu ujao lakini wapinzani wetu wapo bize kuijadili CCM na serikali yake badala ya kujipanga vyema kwa uchaguzi ujao.
Moja kati ya vitu vilivyoiangusha UKAWA katika uchaguzi mkuu uliopita ni "kusubiri makapi ya CCM" badala ya kutangaza mgombea wao mapema na kisha kumnadi kwa nguvu zote, kipindi ambacho CCM ilikuwa na shika-nikushike ya makada wake 40+ waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho tawala.
Nihitimishe makala hii kwa kupigia mstari uwezekano wa aina mbili
Kwanza, CCM kuibuka imara zaidi baada ya Mkutano huo Mkuu Maalum pamoja na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya makada kadhaa, kwa sababu nidhamu katika taasisi yoyote ile ni nguzo ya mafanikio, na pia, ili maendeleo yafikiwe shurti kuwepo na mabadiliko, na mabadiliko hukumbana na vikwazo ambavyo vyaweza kurukwa iwapo kuna nidhamu bora.
Japo yaweza kuwa mapema mno kuhitimisha hili, yayumkinika kusema kuwa “mahesabu ya Magufuli yamelipa” kwa maana ya uamuzi wake wa kumteua Mama Salma kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri hivi karibuni unaweza kuwa umesaidia “kumweka karibu” Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Taifa, na mwenye ushawishi mkubwa katika chama hicho kuliko Dk. Magufuli mwenyewe.
Pili, mambo mawili – hatua dhidi ya makada walioadhibiwa na mabadiliko yaliyopelekea baadhi ya viongozi kupunguziwa nyadhifa – yanaweza kuzua manung’uniko ndani ya chama hicho. Ni wazi kuwa waliochukuliwa hatua za kinidhamu na walioathirika wa kuvuliwa kofia zaidi ya moja za uongozi hawatofurahishwa na hatua hizo. Hata hivyo, je wana pa kukimbilia? Na hapo ndipo utapobaini kuwa siasa za nchi yetu "zingechangamka sana" laiti tungekuwa na upinzani imara.
Na upinzani imara sio lazima upewe ruhusa na serikali kufanya mikutano/maandamano bali kama ule ulioibua 'List of Shame,' Richmond, EPA, nk…hawakuwa na ruhusa ya kufanya hivyo, na pia wanasiasa kama Dk. Willibrord Slaa na Zitto Kabwe walinusurika kwenda jela kwa ajili ya kuwapigania Watanzania.

12 Mar 2017

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafanya Mkutano wake Mkuu Maalum huko Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ni ajenda kuu ya "kujadili na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama hicho na jumuiya zake."

Nimeyawekea msisitizo maneno "kujadili na kupitisha" kwa sababu inaonekana kuwa wazi kuwa majadiliano yatakayofanyika hayapaswi kutoyapitisha marekebisho hayo. 

Ni rahisi kutafsiri hatua hiyo kama ya kunyima demokrasia (kwa maana kwamba kujadili pekee hakutoshi bali pia kuwepo uhuru wa kuyakubali au kuyakataa mapendekezo husika) lakini pengine ni rahisi pia kutambua kwanini CCM "imejihami" mapema.

Sijui ni watu wangapi wanaofahamu kwa hakika mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika kwenye katiba hiyo ni yapi, lakini nitakurahisishia msomaji kwa kuyaorodhesha baadhi:
  • Kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao vya ngazi za juu vya chama hicho
  • Kupunguza 'kofia mbili' kwa viongozi wenye vyeo ndani ya chama, serikalini au bungeni.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, mwanachama anatakiwa kushika nafasi moja tuya uongozi, katika ngazi za Mwenyekiti wa Tawi, Kijiji, Mtaa, Kata, Wadi, Jimbo, Wilaya na Mkoa. Wengine ni Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote, Diwani na Mbunge/Mwakilishi.

Kwahiyo ni wazi kuwa mabadiliko hayo yatawaathiri 'vigogo' kadhaa wa chama hicho, na pengine ndio maana ikaamuliwa kuwe na "mjadala na kupitisha mabadiliko hayo" badala ya "mjadala na kupitisha au kutopitisha mabadiliko husika."

Kadhalika, mabadiliko hayo yatapelekea kupungua kwa idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, kutoka 34 hadi 24.

Vilevile, idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho itapungua zaidi ya nusu, kutoka 388 hadi 158.

Miongoni mwa 'vigogo' watakaoathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na kushika nyadhifa zaidi ya moja ni pamoja na William Lukuvi, Makame Mbarawa, Dkt Hussein Mwinyi, na Shamsi Vuai Nahodha.

'Kigogo' mwingine ni Mama Salma Kikwete, ambaye licha ya kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Lindi, majuzi ameteuliwa na Rais Dkt John Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.

Wengine ni wenyeviti wa CCM mikoa ambao pia ni wabunge, kama vile Joseph Musukuma, Martha Mlata na Deo Simba, ilhali Godfrey Zambi ni mbunge na mkuu wa mkoa, Adam Kimbisa ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma.

Kuna usemi mmoja, kwamba sio kila kitu sahihi ni kizuri, na sio kila kitu kizuri ni sahihi. Uamuzi wa CCM kuwapunguzia wanachama wake kofia zaidi ya moja kwenye uongozi ni sahihi lakini sio mzuri kwa watakaoathiriwa nao. Jicho la uchambuzi litaelekezwa kwa 'wahanga' hao kadri chama hicho kinavyoingia kwenye mchakato wake wa uchaguzi mkuu baadaye  mwaka huu, na kwenye kinyang'anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2020.

Kuna tetesi zisizothibitishwa kuwa miongoni mwa mabadiliko yatayofanyika katika Mkutano huo Mkuu Maalum ni pamoja na kumwezesha Rais aliyepo madarakani kuwa mgombea pekee kwenye mchakato wa chama hicho kumpata mgombea wake. Siwezi kujadili kitu ambacho sina uhakika nacho. Hata hivyo, tutalijadili suala hilo iwapo litajitokeza kwenye Mkutano huo.

Kufuatia vikao vya awali vilivyofanyika jana, chama hicho tawala kilitangaza adhabu kwa viongozi wake kadhaa, kubwa zaidi ikiwa kuvuliwa uanachama kwa Sophia Simba, kada mkongwe wa chama hicho na ambaye hadi jna alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa  jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge.

Orodha kamili ya viongozi walioadhibiwa ni hiyo pichani chini

 




Hatua hizo kali zilizochukuliwa na CCM chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli, sambamba na mabadiliko niliyoyaongelea awali, yana tafsiri kuu mbili. Kwanza, hatua kali za kinidhamu zinapeleka ujumbe kwa wana-CCM wa kada mbalimbali kuwa Rais Magufuli amepania kwa dhati kukisafisha chama hicho tawala. Ifahamike tu kuwa kilichojiri jana kinaingia moja kwa moja kwenye vitabu vya historia ya chama hicho na siasa za Tanzania kwa ujumla.

Pili, mabadiliko kusudiwa - na yakipita salama - sambamba na hatu kali zilizochukuliwa dhidi ya viongozi kadhaa wa chama hicho ni mtihani mkubwa, kwa Mwenyekiti Magufuli na CCM kwa ujumla.

Kwa Mwenyekiti Magufuli, hatua hizo zimemwongezea idadi ya maadui zaidi ya wale ambao tayari ni waathirika wa msimamo wake dhidi ya ufisadi na rushwa, ambapo watendaji kadhaa wa serikali wametumbuliwa huku wakwepakodi wakidhibitiwa, na majangili na 'wauza unga' wakibanwa. Japo ni mapema mno kufanya tathmini timilifu kwa hatua hizo, ile kuzichukua tu sio tu kwaonyesha dhamira lakini pia ni wazi zimetengeneza maadui wa kutosha dhidi ya Dkt Magufuli.

Katika hili, ni muhimu kutambua kuwa ni bora kuwa na kiongozi atakayechukiwa na kwa kutenda vitu sahihi kuliko atakayependwa kwa kufanya madudu.

Jana pia zilipatikana taarifa za kukamatwa kwa makada watatu wa Chama hicho, Msukuma, Hussein Bashe na Adam Malima. Sintoshangaa iwapo miongoni mwao akatimuliwa mtu uanachama. Kilichonisikitisha ni maelezo kuwa "walikamatwa na kuhojiwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa CCM."

Katika mazingira ya kawaida, sio rahisi kwa makada hao watatu kupanga kuvuruga mkutano mkubwa kama huo ila yayumkinika kuhisi kuwa kilichofanyika ni kuzuwia kile nilichogusia awali, yaani "sio kujadili na kupitisha tu mabadiliko husika" bali pia "kujadili na kupitisha au kutopitisha mabadiliko hayo."

Hili la kuminya fursa ya upinzani kwa mabadiliko hayo linaweza kuwa na athari kwa chama hicho huko mbeleni. Sauti za manung'uniko ni kitu cha kawaida lakini sauti hizo zikiakisi mtazamo wa watu wengi, zinaweza kuathiri mshikamano wa chama hicho.

Hata hivyo, kwa wanaotegemea kuwa "CCM itakufa kutokana na mabadiliko haya" wanapaswa wazielewe vema siasa za Tanzania yetu. Si kwamba CCM itatawala milele, lakini kwa mazingira tuliyonayo, hakuna chama mbadala. Huo ni ukweli mchungu.

CCM wanaweza kukandamiza upinzani dhidi ya mabadiliko ya Katiba yao lakini angalau wamefanya mkutano mkuu, na wameadhibu waliokiuka taratibu za chama hicho. Je katika vyama vya upinzani kuna ujasiri wa aina hiyo? 

Ukiangalia wapinzani wakuu wa CCM, yaani Chadema, sio tu "wamegoma kabisa" kufanya tathmini ya kilichowaangusha katika uchaguzi mkuu uliopita bali pia wametelekeza turufu yao kubwa na iliyowajengea imani kubwa kwa Watanzania, yaani mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi, yaliyoibua 'List of Shame,' skandali nzito kama Richmond, EPA, Kiwira,nk. 

Cha kusikitisha ni kwamba vyama vyetu vya upinzani sasa vimekuwa kama vinachezeshwa ngoma na CCM. Wafuasi wa vyama hivyo "wapo bize" kujadili matukio yanayoihusu CCM badala ya kuwekeza nguvu kwenye mustakabali wa vyama hivyo. Jiulize, hivi ajenda kuu ya Chadema, au CUF au ACT- Wazalendo ni ipi muda huu?

Ni katika mazingira hayo, baadhi ya viongozi wa CCM watavumilia mabadiliko yanayoendelea ndani ya chama chao kwa sababu hakuna mbadala wa chama hicho tawala kwa sasa. Tumebaki na miaka mitatu na miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu ujao lakini wapinzani wetu wapo bize kuijadili CCM na serikali yake badala ya kujipanga vyema kwa uchaguzi ujao.

Unajua moja kati ya vitu vilivyoiangusha UKAWA katika uchaguzi mkuu uliopita ni "kusubiri makapi ya CCM" badala ya kutangaza mgombea wao mapema na kisha kumnadi kwa nguvu zote, kipindi ambacho CCM ilikuwa na shika-nikushike ya makada wake 40+ waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho tawala.

Nihitimishe makala hii kwa kupigia mstari uwezekano wa aina mbili: 

kwanza, CCM kuibuka imara zaidi baada ya Mkutano huo Mkuu Maalum pamoja na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya makada kadhaa, kwa sababu nidhamu katika taasisi yoyote ile ni nguzo ya mafanikio, na pia, ili maendeleo yafikiwe shurti kuwepo na mabadiliko, na mabadiliko hukumbana na vikwazo ambavyo vyaweza kurukwa iwapo kuna nidhamu bora. 

Pili, mabadiliko hayo na hatua dhidi ya makada hao zinaweza kuzua mgogoro ndani ya chama hicho. Ni wazi kuwa waathirika wa kuvuliwa kofia zaidi ya moja za uongozi na hao waliochukuliwa hatua za kinidhamu hawatoridhishwa na hatua hizo. Hata hivyo, je wana pa kukimbilia? Na hapo ndipo utapobaini kuwa siasa za nchi yetu "zingechangamka sana" laiti tungekuwa na upinzani imara.

Na upinzani imara sio lazima upewe ruhusa na serikali kufanya mikutano/maandamano bali kama ule ulioibua 'List of Shame,' Richmond, EPA,nk...hawakuwa na ruhusa ya kufanya hivyo, na pia wanasiasa kama Dkt Willbrord Slaa na Zitto Kabwe walinusurika kwenda jela kwa ajili ya kuwapigani Watanzania. 

Kwa uchambuzi kamili kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa CCM na hatua za nidhamu zilizochukuliwa na chama hicho dhidi ya baadhi ya makada wake, ungana nami kwenye toleo la wiki hii la gazeti bora kabisa Tanzania la Raia Mwema hapo Jumatano panapo majaliwa.


9 Mar 2017


KATIKA hitimisho la makala yangu katika safu hii wiki iliyopita niliahidi kuwaletea uchambuzi kuhusu mivutano ya kugombea madaraka (power struggles) ndani ya chama tawala CCM.Kwa bahati nzuri, kati ya makala hiyo na hii, kumejitokeza tukio ambalo linaweza kuhusishwa na mada hiyo ninayoiongelea katika makala hii.
Wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli alimteua Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.Uteuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti, na kuzua mjadala unaoendelea hadi wakati ninaandika makala hii.
Kwa upande mmoja, inaonekana kama kuna mwafaka wa kutosha kwamba Rais ametumia madaraka yake kikatiba kufanya uteuzi huo.
Kwa upande mwingine, pengine kutokana na ukweli kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kumteua mke wa mtangulizi wake kuwa mbunge, kuna hisia za hapa na pale kwamba uteuzi huo hauleti picha nzuri.
Kwamba, labda kwa vile Salma alikwishakaa Ikulu kwa miaka 10 kama mke wa Rais basi pengine nafasi hiyo ya ubunge wa kuteuliwa ingeenda kwa mtu mwingine.
Hata hivyo, licha ya kuwa Rais ameshaeleza kwa nini alifanya uteuzi huo, ukweli unabaki kuwa Katiba inamruhusu kufanya hivyo, na Salma Kikwete kama Mtanzania mwingine ana haki ya kuteuliwa kushika wadhifa wowote ule bila kujali historia yake kama mke wa rais mstaafu.
Lakini licha ya kuruhusiwa na Katiba kufanya uteuzi, kwa sisi tunaofuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, tunauona uteuzi huo kama wa kimkakati, kwa maana ya Dk. Magufuli kujipanga vyema kwa ajili ya mitihani miwili ya kisiasa inayomkabili:  uchaguzi mkuu wa CCM baadaye mwaka huu, na kubwa zaidi, kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Ni hivi, katika nchi zetu zinazoendeshwa kwa mazoea, ni dhahiri kuwa kiongozi wa aina ya Magufuli hawezi kuwa maarufu miongoni mwa waliozoea kuona mambo yakiendeshwa sio yanavyopaswa kuwa, au kwa njia sahihi, bali kwa mazoea, hata kama mazoea hayo yana matokeo hasi.
Viongozi wa aina ya Magufuli wanaominya mianya ya ulaji, wanaozuia safari za ‘matanuzi’ ughaibuni, na wanaojaribu kuwa upande wa wananchi wanyonge badala ya kuendelea kutetea masilahi ya tabaka tawala, hawawezi kuwa na marafiki wengi.
Na ukweli kuhusu Dk. Magufuli ni kwamba kwa muda mfupi aliokaa madarakani ametengeneza maadui wengi tu serikalini na ndani ya chama chake. Kwa serikalini, maadui hao sio tishio kwake kwa sababu mfumo wa utawala sio tu unamwezesha kuwadhibiti kirahisi maadui hao bali pia hata kufahamu dhamira zao ovu mapema.
Changamoto kubwa zaidi kwake ipo ndani ya chama chake. Sio siri kwamba CCM aliyoirithi Magufuli imekuwa, kwa muda mrefu, kichaka cha mafisadi, sehemu ambayo watu waliohitaji kinga dhidi ya mkono mrefu wa sheria walikimbilia huko. Hii haimaanishi kuwa CCM nzima imesheheni watu wa aina hiyo.
Kwa vile licha ya kuwa Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, Magufuli ni kama mgeni kwenye medani za uongozi wa juu wa chama hicho, maadui zake ndani ya chama wanaweza kutumia fursa walizonazo – kama vile ushawishi wao au kukubalika kwao – kumhujumu kiongozi huyo.
Lakini kama ilivyo serikalini, Magufuli ametengeneza maadui ndani ya chama chake kwa sababu ile ile ya kuanzisha zama mpya za kuachana na siasa za/uongozi wa mazoea.
Katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho, kuna viongozi waliozoea kujiona kama wanaendesha kampuni binafsi, huku wakitumia fursa zao kufanya ufisadi. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuiona alama ya jembe na nyundo kwenye bendera ya CCM ikigeuka kuwa umma na bunduki kuashiria ulaji.
Uadui mkubwa ni kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo, kuna jitihada za chinichini ndani ya chama hicho tawala kuangalia uwezekano wa kumfanya Magufuli awe rais wa awamu moja.
Angalau hadi muda huu hakuna dalili kuwa uchaguzi mkuu wa CCM unaweza kuwa na athari zozote katika uenyekiti wa Magufuli japo ni wazi maadui zake watatumia kujipanga kwa ajili ya kinyang’anyiro cha mwaka 2020.
Kwa kumteua Salma Kikwete, Magufuli amemleta karibu mtu muhimu katika siasa za CCM, na pengine kujenga ngome imara ya kumwezesha sio tu kushinda uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CCM bali pia kumrahisishia kazi ngumu ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho tawala.
Nimalizie kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika makala zijazo
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

2 Mar 2017


MWAKA 1990 nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuliibuka mgomo mkubwa uliodumu kwa siku kadhaa. Kwangu, mgomo huo ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwani sikuwa ‘mwanafunzi’ wa kawaida, bali nilikuwa kamanda wa wanafunzi au chifu.
Shule hiyo, pamoja na Sekondari ya Wasichana Tabora, zilikuwa shule pekee nchini zilizokuwa na mchepuo wa kijeshi. Hata sare zetu zilikuwa ‘magwanda,’ na baadhi ya walimu wetu wakiwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Huo wadhifa wa kuwa chifu ulikuwa ni ukiranja mkuu. Kwa hiyo mgomo huo ulitokea wakati nikiwa kiranja mkuu katika shule hiyo yenye historia ya kipekee. Chanzo kikuu cha mgomo huo kilikuwa madai ya wanafunzi kuwa chakula kilikuwa duni.
Nimesema kuwa mgomo huo ulikuwa mtihani kwangu kwa sababu kwa upande mmoja nilikuwa mwanafunzi kama wenzangu waliogoma, na upande mwingine, nilikuwa sehemu ya uongozi wa shule hiyo. Na kwa hakika, nilikuwa kiungo kati ya utawala na wanafunzi.
Hatimaye mgomo huo ulimalizika na kwa vile sikuwa nimeelemea upande wowote wakati wa mgomo huo, kumalizika kwake kuliniacha nikiwa ‘sijauudhi’ upande wowote – wa utawala wa shule na wa wanafunzi wenzangu. Na nyenzo yangu muhimu ilikuwa kusimamia kwenye kanuni na sheria, sambamba na kushawishi matumizi ya busara ili kufikia mwafaka. Mara nyingi huwa vigumu kuziridhisha pande zote za mgogoro husika.
Nimelikumbuka tukio hilo muhimu baada ya kutupia jicho baadhi ya mambo yanayoendelea kwenye Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli. Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, baadhi ya mawaziri wameonyesha bayana kuwa aidha hawaendani na kasi ya Dk. Magufuli au wanamhujumu kwa makusudi.
Baadhi yetu tunaofuatilia siasa za Tanzania tulikwishahisi mapema kuwa uamuzi wa Dk. Magufuli kuzileta baadhi ya sura zile zile ambazo zilikuwa mzigo kwa taifa huko nyuma, ungeweza kusababisha matatizo mbele ya safari.
Kwa kurejea tukio la mgomo nililolielezea hapo juu, Rais anajikuta kwenye ‘mtihani’ kwa sababu kwa upande mmoja anapaswa kuwa upande wa watendaji wake aliowateua kwa umakini mkubwa (ndio maana ilichukua wiki kadhaa kabla Rais hajatangaza Baraza lake la Mawaziri) na kwa upande mwingine yeye sio rais wa mawaziri wake pekee bali Watanzania wote.
Sakata la vita dhidi ya dawa za kulevya lililoibuliwa upya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, limechangia kwa kiasi kikubwa kuonyesha kukosekana ‘visheni’ ya pamoja miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.
Kwa mtazamo wangu, pengine ingekuwa vema kama Rais alipounda Baraza lake la Mawaziri angeepuka kuwaingiza makada wengi wa chama chake kwenye baraza hilo. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho tawala kimeshika hatamu za uongozi wa taifa na ukada unawapa jeuri baadhi ya watendaji wa serikali. Na si kosa lao kwa sababu ukada umekuwa nyenzo muhimu katika uongozi wa Tanzania huku baadhi ya wakosaji wakiepuka adhabu kwa vile tu ni makada muhimu.
Wakati wa sakata la dawa za kulevya lililoibuliwa na RC Makonda, angalau waziri mmoja alijitokeza waziwazi kupingana na uamuzi wa kutangaza majina ya watuhumiwa, akidai hatua hiyo ingeathiri chapa (brands) za wasanii waliotajwa katika orodha ya watumiaji au wauzaji wa dawa za kulevya.
Kanuni muhimu ya uongozi ni uwajibikaji wa pamoja, na pindi mtendaji mmoja akikosea, basi kuna fursa ya kuongea tofauti za kimtazamo faragha badala ya kuitisha mikutano na waandishi wa habari kuonyesha mpasuko.
Naomba ieleweke kuwa sio ninakemea uhuru wa kujieleza miongoni mwa watendaji wa serikali, ikiwa pamoja na mawaziri, lakini uhuru huo sharti uzingatie kanuni.
Hata tukiweka kando hali tata iliyotokana na sakata hilo la dawa za kulevya, haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli ni mzigo kwake. Ni mzigo kwa vile aidha hawaendani na kasi yake au wanafanya makusudi kwa minajili ya kumkwamisha.
Ndio maana, picha inayopatikana mtaani ni kwamba mara kadhaa ni mpaka rais aingilie kati ndio hiki au kile kifanyike. Swali linalojitokeza ni je, rais haoni hali hiyo? Je, washauri wake (kwa mfano ndugu zetu wa Idara ya Usalama wa Taifa) nao hawaoni hali hiyo?
Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Dk. Magufuli kuwa pengine imefika wakati mwafaka kufanya utumbuaji kwa watu baadhi ya aliowakabidhi dhamana ya uwaziri kwenye kabineti yake. Asipochukua hatua mapema, inaweza kugharimu urais wake.
Nitaendelea na makala hii wakati mwingine kujadili kile Waingereza wanaita ‘power struggles’ zinazoendelea ndani ya CCM na ambazo kwa kiasi fulani zinachangia utendaji duni wa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli (kwa maana ya utendaji duni kama mkakati wa makusudi).

Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.