29 May 2017



Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka tisa iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana. Japo miaka tisa inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana. Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka. Kwa kifupi, mama mpendwa, kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minane iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa, ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu, kwa mumeo marehemu Baba Mzee Chahali (aliyeungana nawe huko peponi mwaka juzi) na kwa wanao wote na ndugu na jamaa. Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani, ulirukaruka kwa furaha, ukanikumbatia na kunipakata mwanao, ukaniandalia maji ya kuoga, ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga. Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani. Inaniuma sana.
Marehemu mama akicheza siku ya harusi ya mwanae wa nne. Yeye na marehemu baba walijaliwa kupata watoto tisa, mmojaalifariki  na tukabaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.
Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na marehemu Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu, ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha, ndoa, upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya. Kabla ya kifo chako, nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na  marehemu Baba, na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho. Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako na marehemu baba kwangu mwanenu. Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo, kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti. Nilikugusa mama, nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha. Hukuamka hadi leo hii.
Hospitali Teule ya Mtakatifu Fransisko ambapo marehemu mama alilazwa akiwa amepoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitatu hadi alipofariki siku kama ya leo miaka minane iliyopita
Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuguza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu. Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis, Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha. Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza, kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha. Nikategemea ungemka na kunieleza japo neno moja. Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote. Iliniuma sana, inaniuma sana na itaendelea kuniuma sana, mama.

Kabla marehemu baba hajaungana nawe huko uliko, nilikuwa na wakati mgumu sana kila nilipopiga simu nyumbani kwa wakati wa uhai wako, nilizowea kuwa nikimaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori. Na kila nilipoongea nawe nilijisikia kudeka kutokana na upendo wako usiomithilika. Baada ya kifo chako, na kabla marehemu baba hajafariki, kila nilipompigia simu mzee huwa nilijikuta najisahau na nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi. Sasa ndio imekuwa uchungu maradufu kwani kila nikipiga simu nyumbani, ninatamani kuongea nawe na marehemu baba kisha nakumbuka kuwa hampo nasi.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki wewe na baadaye marehemu baba. Siwalaumu, kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa hampo nasi na haiwezekani kuwarejesha. Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako na cha baba vinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.


Mama mpendwa, sijui nisemeje. Rafiki zako wakubwa, wanao vitinda-mimba, Kulwa na Doto, ndio wananitia uchungu zaidi, Wanawa-miss mno wewe na marehemu baba kwa sababu ndio uhusiano wenu ulikuwa zaidi ya kati ya wazazi na vitinda-mimba wao. Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka, mnataniana na kunipa kila aina ya faraja. Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu, na kila anayemjua anafahamu hilo. Japo mnaomboleza kifo chake, lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema, Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua. Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi, na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani. Nguvu nyingine niliyonanyo ni imani kuwa wewe na marehemu baba mnaendelea kutuombea huko mlipo.

Nyumba ya milele ya marehemu Adelina 

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE WEWE NA MAREHEMU BABA PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AWAANGAZIE, MPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.


26 May 2017



Juzi tumesikia ripoti kuhusu mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya Tanzania yetu (well, kuna jina la kitaalamu lakini sio la muhimu kulinganisha na athari kubwa za usafirishwaji wa mchanga huo).

Kwa baadhi ya wenzetu, taarifa hiyo imewashtua mno, na kuwapandisha hasira kubwa. Ndio Tanzania yetu hiyo, wengi wa raia wake hawana habari kuhusu yanayoisibu nchi yetu. Ukiwauliza watu, "hivi mustakabali wa Tanzania mwakani utakuwaje?" nina hakika watu kadhaa watajiumauma kutoa jibu la kueleweka.

Watanzania wengi aidha hawaelewi au wamesahau nchi yetu ilivyochukua mwelekeo mpya - na usiopendeza - baada ya kung'atuka kwa Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Hatua ya kwanza kabisa ya kubadili mwelekeo ilikuwa kitu kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar. Hili lilifanyika katika utawala wa Mzee Ruksa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Kimsingi, Azimio la Zanzibar liliua Azimio la Arusha na kulizika mubashara. Ukitafuta nyaraka kuhusu Azimio hilo la Zanzibar hutozipata kirahisi kwa sababu lilifanyika katika mkusanyiko uliokuwa kama "mkutano haramu."

Mzee wetu Mwinyi hakuitwa Mzee Ruksa kama utani. Utawala wake ulitawaliwa na kile Waingereza wanaita 'laissez faire', labda kwa Kiswahili chepesi tuseme 'bora liende' au 'liwalo na liwe.' 

Lakini kumtendea haki 'Mzee Ruksa,' asili hasa ya ufisadi haikuanza katika utawala wake bali ilianza katika utawala uliomtangulia, wa Baba wa Taifa. 

Tofauti kati ya tawala hizo mbili ilikuwa bayana: Wakati baadhi ya waliomzunguka Baba wa Taifa walikuwa 'mafisadi wa chinichini' au 'waliokuwa wakisubiri atokea madarakani ili waanze kutafuna keki ya taifa,' katika utawala wa Rais Mwinyi, ilikuwa ni mwanzo wa 'kula kadri unavyoweza,' Waingereza wanaita 'open season.'

Kwamba labda Baba wa Taifa alifahamu watu hao au walikuwa mahiri kuficha tabia zao, sina jibu la hakika. Lakini huhitaji kuwa mchambuzi mahiri wa siasa kubaini kwamba mara baada ya Nyerere kung'atuka na hatimaye kufariki, ghafla watu walewale waliokuwa wakiimba kuhusu Ujamaa na kulaani Ubepari wakageuka matajiri wa kupindukia, mabepari. Ninachofahamu ni kwamba kulikuwa na idadi kubwa tu ya wanasiasa waliomhadaa Baba wa Taifa kuwa ni waumini wa Ujamaa lakini walimudu kuhifadhi fedha huku nje wakisubiri 'Nyerere aondoke.' 

Kwahiyo, Awamu ya Pili ya Mzee Ruksa ni kama iliyotoa ruksa kwa walafi waliokuwa wakimendea keki ya taifa, lakini walishindwa kuitafuna wakati wa utawala wa Nyerere. Kwa kifupi, utawala wa Mzee Ruksa ulitoa rasmi ruksa kulifisadi taifa letu, hasa kupitia Azimio la Zanzibar. 

Ni muhimu kukumbuka Utawala wa Mzee Ruksa ulikuwa wa Chama Cha Mapenduzi, CCM.

Kuingia kwa Rais Benjamin Mkapa mwaka 1995 kuliingiza zama mpya kuhusiana na ufisadi. Miaka 10 ya Mzee wa Uwazi na Ukweli ilitawaliwa na Watanzania kuhadaiwa kuwa ufumbuzi wa matatizo yao upo mikononi mwa wawekezaji, ilhali wengi wa hao walioitwa wawekezaji walikuwa in fact majambazi waliokuwa wakiwinda raslimali zetu. 

Miaka 10 ya Mkapa ilileta matumaini ya kitakwimu, tukiambiwa kuwa sijui GDP, sijui Pato la Taifa, sijui vipimo gnai vya kiuchumi, kuwa vyote vilionyesha uchumi wa Tanzania ukifanya vizuri. Kama kuna kitu kinanichukiza mno kuhusu hizi takwimu za uchumi ni kuwaangalia watu kama bidhaa au namba na sio binadamu. Haiingii akilini kusema uchumi unakua ilhali watu wanazidi kuwa masikini. Uchumi unakua kimazingaombwe?

Tofauti kati ya utawala wa Mwinyi na Mkapa ni ya wazi: nimeshaeleza kuwa katika zama za Mwinyi ilikuwa 'ruksa' kufanya lolote lile. Zama za Mkapa zilituaminisha kuwa kila kitu kinafanyika kwa uwazi na ukweli, na kwenye uwazi na ukweli hakupaswi kuwa na ufisadi. 

Yaliyojiri katika utawala wa Mwinyi yalikuwa yakionekana mubashara. Hiki kilikuwa kipindi cha mtu tu kuamua kuwa tajiri kwa njia halali au zisizo halali, maana ilikuwa ruksa. Lakini katika zama za 'uwazi na ukweli,' watu pekee walioonekana kuwa na ruksa ya kufanya wapendayo ni wawekezaji.Mkapa aliwathamini wawekezaji kuliko Watanzania wenzake.

Lakini ni baada ya Mkapa kutoka madarakani ndio tukafahamu kilichokuwa kikijiri 'behind the scene.' Kumbe wakati anatuhubiria kuhusu uwazi na ukweli, yeye akaigeuza Ikulu kuwa soko la Kariakoo, akawa anafanya biashara. 

Na Mkapa, mwanafunzi mtiifu wa Mwalimu Nyerere, ni mfano sahihi wa watu ambao Nyerere aliwaamini sana lakini alipoondoka nao wakapuuza misingi aliyoijenga Mwalimu. 

Zama za Mkapa ndio haswa zilizowavutia wawekezaji kujazana nchini mwetu. Wengi wao walikuja na brifukesi tupu, wakaondoka na mamilioni ya dola. Baadhi ya wawekezaji hao, walipoona bado wanahitaji kuchuma wasichopanda, walibadili majina na kuongezewa likizo ya kulipa kodi.

Ni muhimu kukumbuka kuwa Mkapa alikuwa Rais kwa tiketi ya CCM.

Baada ya Mkapa akaingia Kikwete. Ili kuorodhesha madudu yote yaliyofanywa katika utawala wa Kikwete inahitaji kitabu kizima. Wakati mwingine unaweza kupatwa na kizunguzungu kuona sasa Watanzania wengi wanamlilia JK, mwanasiasa ambaye hakuwa makini kabisa kuhusu mustakabali wa Tanzania yetu.

Ni hivi, kuna mengi hayawekwi wazi kuhusu yaliyojiri kati ya 2005 na 2015, na siku yakiwekwa hadharani itakuwa balaa. Bwana Magufuli aliposema 'tusifukue makaburi' alitumia busara tu ili kuepusha aibu ambayo kimsingi isingekuwa kuhusu utawala wa JK tu bali mwendelezo wa CCM kuwa janga kwa taifa letu.

Kutoka EPA hadi Kagoda hadi Richmond hadi Escrow, utawala wa JK ulitawaliwa na skandali mfululizo. Pengine JK hakuwa mwanasiasa mwenye mapungufu lakini kosa lake kubwa lilikuwa maandalizi yake kuwania urais from 1995 to 2005, ambapo alikusanya sapoti ya kila kundi, ikiwa ni pamoja na mafisadi. lipopata urais, JK alikuwa na deni kubwa kwa watu hawa, na hii ilipeleka awaruhusu kutafuna keki ya taifa kama asante yake kwao.

Sihitaji kukumbusha kuwa JK alikuwa Rais kwa tiketi ya CCM.

Magufuli pia ni Rais kwa tiketi ya CCM, lakini wakati tunapongeza jitihada zake binafsi ni muhimu kutambua kuwa chama chake kina mchango mkubwa katika matatizo mengi yanayotukabili leo, ikiwa ni pamoja na hilo la utoroshaji wa mchanga wa dhahabu.

Lakini Magufuli hawezi kukwepa lawama kwa uamuzi wake kumteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, nafasi aliyolazimika kujiuzulu katika utawala wa JK kutokana na kashfa ya Escrow. Hivi Magufuli alikuwa anategemea miujiza kutoka kwa Prof Muhongo? 

Kwa waliosoma kitabu changu cha 'Dokta John Magufuli: Sa fari ya Urais, Mafanikio na Changamoto Katika Urais Wake' watakumbuka nilichoandika ukurasa wa 74 kuhusu uamuzi wa Magufuli kumteua Profesa Muhongo. 



Niliandika


Hata hivyo, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Angalau Magufuli amejitahidi kufanya jitihada binafsi kukabiliana na majambazi wanaobaka uchumi wetu. Ile tu kuchukua hatua inapaswa kupongezwa hasa ikizingatiwa kuwa watangulizi wake watatu -Mwinyi,Mkapa na JK - waliishia kutupatia matumaini hewa huku ufisadi ukizidi kushamiri.

Jana nilimwangalia Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Poplepole akitoa maneno mazito kuhusiana na suala la mchanga wa dhahabu. Nikaandika tweet kwamba Bwana Polepole anaongea kana kwamba CCM haihusiki na kuwezesha ujambazi uliopelekea mchanga wa madini kusafirisha. Akaleta uzushi kuwa sijui mie nipo ughaibuni, sijui sina uhalali. Baadhi ya watu wakamshutumu kuwa ni mbaguzi (kuwa ughaibuni  hakuninyimi uhuru wa kuzungumzia mustakabali wa taifa letu) lakini mie siamini kabisa kuwa huyu Polepole ni mbaguzi. Ni siasa tu.

Mwisho, makala hii haitokamilika ipasavyo bila kuwatupia neno ndugu zangu wa kitengo. Hebu fanyeni kuona aibu japo kidogo. Hivi inawezekanaje taifa kuibiwa zaidi ya shilingi trilioni moja ilhali ninyi mkifaidi mishahara minono na posho nzuri inayotakana na jasho la Watanzania masikini lakini mnawaangusha kiasi hicho? Tatizo la kitengo ni vipaumbele fyongo, kuandama watu wasiohusika badala ya kukwekeza nguvu dhidi ya wahalifu halisi/matishi halisi kwa usalama wa taifa letu.

Hata hivyo, kwa vile lawama hazijengi, ni matumaini yangu makubwa kuwa suala hilo la mchanga wa dhahabu litatufungua mcho kama taifa na kukabiliana na ujambazi wa aina hii. Sina uhakika sana kuhusu mbinu mwafaka, lakini pengine kwa kuanzia, CCM hata kama inaona aibu kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwa kichaka cha ufisadi, hali iliyowezesha ujambazi wa mchanga huo wenye madini, basi angalau imuunge mkono mwenyekiti wao, si kwa porojo za kina Polepole bali kwa vitendo halisi. Wingi wa wabunge wa chama hicho tawala uwe na faida kwa wananchi na taifa na sio mhuri wa kupitisha kila kitu kama ilivyokuwa kwa miswada iliyopeleka sheria za madini zinazowapa fursa wawekezaji wasio waaminifu kutorosha kila wanachotaka ilhali sie tukizidi kuwa masikini.

Mungu ibariki Tanzania

21 May 2017


Baada ya safari ya muda mrefu iliyodumu takriban miaka 20 sasa, ya uandishi wa makala magazetini, hatimaye nimeamua kutundika daluga (kustaafu)

Nilianza rasmi uandishi mwaka 1998, nilipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani. Aliyenishawishi kuingia kwenye fani hiyo ni aliyekuwa mwandishi mkongwe, Albert Memba, ambaye alidai kuwa nina kipaji cha asili cha kuandika.

Nilianza uandishi katika gazeti la kwanza kabisa la udaku, lililokuwa linajulikana kwa jina la "Sanifu." Gazeti hili lilikuwa maarufu sana, na mpaka leo sijui kwanini halikudumu muda mrefu. 

Wakati nikiwa 'Sanifu' sikuwa nikiandika makala as such bali nilikuwa na safu yangu iliyohusu unajimu, well sio kama ule wa Marehemu Sheikh Yahya lakini karibu kidogo. Ulikuwa utani wa aina flani ambao baadhi ya watu waliuchukulia serious. Na kama 'kachumbari,' ninajipa jina la 'Ustaadh Bonge.' Na hadi leo baadhi ya marafiki zangu wa enzi za Mlimani (UDSM) wananiita jina hilo.

Baadaye nikapata kolamu katika gazeti jipya la 'Kasheshe.' Hili lilikuwa gazeti la pili nchini Tanzania lililohusu udaku. Na huko nako nilikuwa na safu inayohusu unajimu, nikiendelea na jina la 'Ustaadh Bonge.' Nilikuwa nikifarijika kila nilipomsikia marehemu Julius Nyaisanga akieleza wasomaji watarajie nini kwenye toleo la wiki husika la gazeti la Kasheshe huku akiwakumbusha "bila kusahau safu ya unajimu ya Ustaadh Bonge." Sema enzi hizo hata neno "kiki" lilikuwa halijazaliwa.

Na kuna watu ambao baada ya mie kujitambulisha walipatwa na mshangao na kusema, "ah mie nilijua Ustaadh Bonge ni mzee flani wa pwani..." na mie nikiishia kucheka tu. 

Baadaye tena nikapata safu kwenye gazeti-dada la 'Kasheshe' lililoitwa 'Komesha,' ambako pia niliendelea na 'unajimu' wangu nikitumia jina lilelile la Ustaadh Bonge.

Hatimaye likaanzishwa gazeti jipya la habari na makala lililojulikana kwa jina la 'Kulikoni.' Na hili ndilo hasa lililopelekea kuzaliwa kwa jina la blogu hii yaani 'Kulikoni Ughaibuni.' Blogu hii ilianzishwa kwa lengo la kuwa sehemua mabyo Watanzania walio nje ya nchi wangeweza kusoma makala zangu zilizochapaishwa katika gazeti la 'Kulikoni' lakini hazikuwepo mtandaoni kwa vile gazeti hilo halikuwa na tovuti. 

Kumbuka wakati huko kulikuwa hakuna Facebook, wala Twitter, wala Instagram, wala selfie...hizo zilikuwa zama za Hi5, Myspace, na kwa Tanzania kulikuwa na blogu chache tu na mtandao maarufu wa DarHotWire. 

Anyway, kwa vile nilikuwa nakabiliwa na majukumu mbalimbali, ilibidi niachane na uandishi katika magazeti ya udaku na kukazania uandishi wa makala. Safu yangu katika gazeti la 'Kulikoni'  ilikuwa ikijulikana kama 'Kulikoni Ughaibuni.'

Baadaye kidogo nikapata safu kwenye gazeti la Mtanzania, nikaipa jina 'Mtanzania Ughaibuni,' kabla ya kuanzishwa kwa gazeti la Raia Mwema ambako nilikuwa miongoni mwa wana-makala wa awali kabisa, na safu yangu ikijulikana kama 'Raia Mwema Ughaibuni.'

Moja ya matukio ambayo sintoyasahu katika uandishi wa makala ni uamuzi wangu wa kuvalia njuga sakata la Richmond. Licha ya kujivunia kama mwana-makala pekee niliyevalia njuga suala hilo vya kutosha, athari zake zilikuwa kubwa mno. Kilichotokea wakati huo ndio kilichonisukuma kumuunga mkono mgombea wa CCM kwenye nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, John Magufuli. 

Uandishi wa makala ulinikuta nikikumbana na 'msala' mwingine mwaka 2013, ambapo mwanzoni mwa mwezi Februari (mwaka huo) nilijulishwa na vyombo vya dola hapa Uingereza kuwa kulikuwa maisha yangu yalikuwa hatarini.

Kwahiyo hadi kufikia uamuzi wa kustaafu uandishi wa makala magazetini ni takriban miaka 20 sasa (actually ni miaka 19, yaani 2017 kutoa 1998).

Nikipima 'faida' na 'hasara' za uandishi wa makala hizo, jibu ni rahisi kabisa: faida zilizidi hasara. Ndio, uandishi wa makala hizo umenigharimu mno kimaisha, lakini ndani kabisa ya nafsi yangu ninaamini kuwa uamuzi wangu kuwasemea wasio na sauti (to be the voice of the voiceless) ulikuwa uamuzi sahihi.

Ninaamini ilikuwa sahihi kusimama kidete kuhusu skandali ya Richmond, tangu mwanzo hadi mwisho, licha ya gharama kubwa kimaisha kwa upande wangu.

Ninaamini nilikuwa sahihi kwa safu zangu kuwa sauti adimu iliyopigania haja ya mageuzi katika Idara ya Usalama wa Taifa, kwa minajili ya kuondoa siasa katika utendaji kazi wa taasisi hiyo muhimu, kuhamasisha uzalendo na kwa ujumla kubaki kuwa chombo muhimu kwa ustawi wa Tanzania yetu.

Uandishi wa makala umenitengenezea marafiki wengi mno, japo pia umenitengenezea maadui wachache wenye nguvu kisiasa au kijamii. Na jana nilipotoa taarifa rasmi huko Facebook nilipata fursa adimu ya kufahamu kuwa kumbe kuna idadi kubwa tu ya watu waliovutiwa na makala zangu.

Uamuzi wangu kustaafu uandishi wa makala magazetini hauhusiani na 'yaliyonikumba wiki hii inayoisha leo.' Kwa upande mmoja nilipewa taarifa na ushahidi kuwa Rais Magufuli hakupendezwa na makala yangu ya mwisho katika gazeti la Raia Mwema, ambayo ndani yake nilimkosoa kuwa "yeye kama Amiri Jeshi mkuu ni mfariji mkuu pia na anapaswa kuhudhuria misiba ya kitaifa.

Japo kumkosoa kwangu hakukuwa tofauti na kauli ya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambapo kiongozi huyo wa Chadema alieleza bayana kushangazwa kwake na hatua ya Rais kutohudhuria msiba wa wanafunzi 32 wa shule ya Lucky Vncent ya Arusha, akisisitiza kwamba ni msiba mzito kitaifa ambao ilipaswa Rais kuhudhuria.

Wakati kauli ya Lowassa ilijibiwa na Ikulu, mie makala yangu imepelekea msala ambao nitauelezea siku nyingine.

Kwa upande mwingine, kuna watu waliohojiwa kuhusiana na tweet ya utani niliyoandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Ni kwamba, katika 'mila na desturi' za Twitter, kuna kitu kinaitwa 'future tweet,' ambacho huandikwa kama alama ya reli #FutureTweet. Kitu hicho hutumika kama utani unaoashirika kuwa 'sikuzijazo kutakuwa na tweet ya aina hii baada ya kitu hiki kutokea.' 

Ni UTANI usiopaswa kuipotezea muda serikali sio tu kuandika taarifa rasmi za kuukanusha na kuahidi kuchukua hatua bali pia kuhoji watu kadhaa kuhusu mie mwandishi wa #FutureTweet hiyo. Huu ni UTOTO. Serikali ilioingia madarakani kwa mbwembwe za #HapaNiKaziTu inaonekana kioja kwa sio tu kushindwa kuelewa #FutureTweet ni kitu gani bali pia kituko kwa kufikia hatua ya kukanusha #FutureTweet na hatimaye kuhoji watu kuhusu mie mwandishi wa #FutureTweet hiyo. 

Niwe mkweli, sikupendezwa na gazeti la Raia Mwema kutonijulisha kuwa walihojiwa kuhusu mie na kisha kutonambia kuhusu suala hilo. Kama walifanya hivyo kwa sababu ya uoga wao au waliamriwa kunificha, binafsi nimetafsiri kama 'wameninyima ushirikiano,' na sioni umuhimu wa kuendelea kuwa mwana-makala katika gazeti hilo. 

Lakini kubwa zaidi, sitaki kuwasababishia usumbufu wasiostahili. Ungetegemea gazeti kubwa kama hilo lingepata ujasiri kuzungumzia kadhi hiyo ya kubughudhiwa na serikali kwa ajili yangu lakini ni wazi kuwa vyombo vyetu vya habari vimetishwa na tishio la Rais Magufuli kuwa "visidhani vina uhuru kiasi hicho." 

Nihitimishe makala hii kwa kuwashukuru nyote mliosoma makala zangu mbalimbali katika miaka hii takriban 20 ya utumishi wangu kwenu. Naomba ifahamike kuwa kustaafu kuandika makala magazetini hakumaanishi kuwa nimestaafu pia katika kublogu. Hapana. Na pia haimaanishi nimestaafu kuwa muumini wa #SharingIsCaring. Nitaendelea kutumia mitandao ya kijamii kuelimisha, kuhabarisha, kukosoa...na pengine kuburudisha.

Nimeitumikia Tanzania yangu vya kutosha. Licha ya takriban miaka 20 ya uandishi wa makala, niliitumia Tanzania yangu kwa uadilifu mkubwa kama mtumishi wa serikali, na pia kupitia #SharingAndCaring na kublogu na uandishi wa vitabu.Lakini kubwa zaidi ni kwa kuwa raia mwema, ambaye licha ya kuwa mbali na nchi yangu, nimejitahidi kuwatumikia Watanzania wenzangu angalau kwa kushiriki mijadala muhimu kuhusu mustakabali wa taifa letu.

Licha ya kuwa nitaendelea kublogu, kuandika vitabu na kudumisha #SharingAndCaring kwenye mitandao ya kijamii, kustaafu uandishi wa makala magazetini kunanipa fursa ya kuanza safari mpya ya maisha yangu: kuzalisha 'waleta mabadiliko wa kesho' (future change makers) kupitia ujasiriamali jamii (social entreprenuership). 




11 May 2017


NIANZE makala hii kwa salamu za pole na rambirambi kwa ndugu, jamaa, na marafiki wa wanafunzi zaidi ya 30 waliopoteza maisha kufuatia ajali ya basi dogo la abiria, huko Karatu Arusha.
Nimeandika “zaidi ya mara 30” kwa sababu wakati ninaandika makala hii, zimepatikana taarifa kuwa inawezekana idadi ya abiria kwenye basi lililopata ajali ilikuwa kubwa kuliko iliyoripotiwa. Taarifa rasmi zinatajwa idadi ya waliofariki kuwa ni wanafunzi 33, walimu wawili na dereva mmoja.
Mungu awapatie marehemu wote pumziko la milele, na mwanga wa milele awaangazie, wapumzike kwa amani. Amina. Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Wenzetu wametutangulia tu, lakini sote tupo safari moja, kwani kila nafsi huonja mauti.
Salamu nyingi za pole kwa wafiwa, maana uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Wanafunzi hao wamekumbwa na mauti wakati wanaelekea kwenye mitihani yao. Kwa hiyo, tunaomboleza sio kifo tu bali pia kukatishwa kwa ndoto za kielimu za wanafunzi hao. Hili ni pigo kubwa sio kwa ndugu, jamaa na marafiki tu wa wanafunzi hao, bali taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa mila na desturi zetu, si vema kuanza kulaumiana kuhusu msiba kabla hata mazishi hayajafanyika. Lakini kama kuna kasumba mbaya inayojitokeza katika kila majanga makubwa kitaifa, basi binafsi sioni haja ya kuwa na subira.
Kama kuna kitu kinanisumbua mno kila yanapojiri majanga ya kitaifa kama ajali hii ya Karatu ni ile hali kwamba “wenzetu huku nilipo wanathamini mno uhai uliopotea, pengine kuliko sisi. Hili nimekwishaliongelea mara kadhaa, na kuna mifano lukuki ya kuthibitisha hisia hizo zisizopendeza.
Nashindwa “kupata picha” hali ingekuwaje hapa Uingereza laiti kungetokea ajali kama hiyo ya Karatu. Naandika hivyo kwa sababu “ajali ndogo tu” kwa maana ya idadi ya vifo au majeruhi, hupewa uzito mkubwa mno kiasi kwamba takriban kila mkazi wa nchi hii anaguswa na janga husika.
Nabaki ninajiuliza, “je wenzetu wanathamini mno uhai kuliko sisi?” Sipati jawabu. Najiuliza tena, “labda wenzetu ni ‘wazima’ lakini sisi tumerogwa?” Siambulii jibu. Lakini kilicho wazi ni kwamba tuna upungufu mkubwa katika kuguswa kwetu na majanga makubwa kitaifa.
Mifano ya karibuni zaidi ni janga la tetemeko la ardhi lililoyakumba maeneo ya Kanda ya Ziwa, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa na uharibifu mkubwa wa mali; mauaji dhidi ya askari polisi wanane huko Kibiti, mkoani Pwani, na sasa janga hili ambalo limeripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari duniani.
Kitu kimoja kisichopendeza katika matukio yote hayo matatu ni kwamba serikali haikuona haja ya kutangaza maombolezo ya kitaifa. Katika udadisi wangu, nimesikia utetezi usio na mashiko kuwa “ili kuwe na maombolezo ya kitaifa, na bendera ipepe nusu mlingoti basi msiba husika shurti uwe wa kiongozi wa kitaifa.” Maana yake kwamba uhai wa viongozi wetu una thamani zaidi ya uhai wa wananchi wa kawaida. Ama?
Kitu kingine ambacho sio tu hakipendezi lakini pia kinashangaza ni Rais wetu, John Magufuli kutoungana na waombolezaji wakati wa kuaga miili ya marehemu. Hakuwepo katika tukio la kuaga miili ya waliofariki kwenye ‘Tetemeko la Kagera,’ hakuwepo kwenye tukio la kuaga miili ya askari polisi wanane waliouawa huko mkoani Pwani. Na hadi wakati naandika makala hii, mgeni rasmi kwenye kuaga miili ya wanafunzi hao wa Karatu ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Kuna wanaoweza kusema “kwani rais akiwepo atarejesha uhai wa waliofariki?” Hoja hiyo ni ya kukosa ubinadamu. Ni muhimu kutambua kuwa licha ya kuwa “commander-in-chief” wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama, Rais pia ni “comforter-in-chief.” Rais ni kama baba, mlezi, na mtu ambaye taifa zima linamuangalia katika nyakati kama hizi.
Tukiweka kando ‘sintofahamu’ hiyo, Shirika la Utangazaji la taifa TBC, limeonyesha kasoro kwa kuendelea na ratiba za vipindi vyake badala ya kuongoza vyombo vingine vya habari katika maombolezo ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo ya Karatu.
Nitumie fursa hii kuipongeza Clouds Media Group kwa uzalendo na ubinadamu wao mkubwa uliowasukuma kubadili ratiba za vipindi vyao ili kuungana na wafiwa na Watanzania kwa ujumla kuomboleza vifo hivyo.
Mwisho, japo ajali haina kinga, uzoefu unaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotokea huko nyumbani huchangiwa na uzembe wa madereva ikiwa ni pamoja na kukiuka kwa makusudi kanuni za usalama barabarani, sambamba na ubovu wa vyombo vya usafiri wa abiria.
Japo sina maana kuwa sababu hizo ndio zilizochangia ajali hiyo ya Karatu, lakini ni muhimu sasa kama taifa kuliangalia balaa la ajali kama janga la kitaifa. Kwa kiasi kikubwa, madereva wazembe wapo barabarani huku wengine wakiendesha magari yasiyopaswa kuwa barabarani kwa sababu moja kuu, ugonjwa sugu wa rushwa kwenye kitengo cha polisi wa usalama barabarani. Pasipo kukabili rushwa kwenye kitengo hicho, uhai wetu utazidi kuwa mashakani kwa janga la ajali.
Poleni sana wafiwa, poleni Watanzania kwa ujumla. Njia mwafaka ya kuomboleza msiba huu mkubwa ni kwa kuwakumbuka marehemu katika dua/sala zetu

4 May 2017

MAKALA yangu wiki hii inahusu maoni yangu kuhusu hatua ya serikali ya Rais John Magufuli kufukuza watumishi wa umma takriban 10,000 kwa tuhuma za kugushi sifa zao kielimu/ujuzi.
Kwanza, nitanabaishe mapema kuwa sisi ambao tumetumia sehemu kubwa ya uhai wetu kusaka elimu – na tunaendelea kuisaka – hatua yoyote dhidi ya ‘wahalifu wa kielimu’ inastahili pongezi.
Kwa hiyo, hatua ya serikali dhidi ya watumishi wake walioghushi vyeti/ujuzi ni ya kupongezwa. Haipendezi kuona wadogo zetu wanahitimu kihalali katika ngazi mbalimbali lakini wanakosa ajira kwa vile baadhi ya nafasi za kazi zimekaliwa na watu walioghushi vyeti.
Hata hivyo, licha ya hatua hiyo inayostahili pongezi, kuna kasoro kadhaa. Kwanza, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi kadhaa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao sio tu walikatishwa masomo yao lakini pia waliiitwa "vilaza" kwa kosa lisilo lao la kuingizwa katika kozi ya ualimu, japo alama za ufaulu za baadhi yao zilikuwa za chini.
Lengo la serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kuwachukua wanafunzi hao lilikuwa zuri, kwa maana ya mkakati wa kukabiliana na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, lakini pia kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi hao baada ya matokeo yao kutowaruhusu kuendelea na masomo ya kidato cha tano
Kama ambavyo wanafunzi hao hawakujichagua wenyewe, ndivyo ilivyokuwa kwa watumishi wa umma waliofukuzwa kwa ‘kufoji vyeti.’ Hawakujiajiri wenyewe. Waliajiriwa. Tumepasua jipu kwa kuwafukuza kazi lakini hatujashughulikia kiini cha jipu hilo. Na kwa kiasi kikubwa, kiini ni wanasiasa, ambao kama mzaha vile, hawakuguswa na zoezi la uhakiki wa vyeti vyao/elimu zao.
Uzoefu wangu katika utumishi wa serikali unaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa, ajira serikalini zimekuwa zikitolewa sio kwa kuzingatia elimu au uzoefu bali kujuana.
Nimeandika kuhusu hilo katika kitabu changu cha #Shushushu (kinachozungumzia kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa) kuwa moja ya changamoto kubwa kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ni mfumo mbovu wa ajira unaotoa fursa ya ajira za kujuana/kubebana. Utumishi katika taasisi kama hiyo unahitaji utiifu kwa taifa, lakini ukiajiri mtu kwa vile ni mtoto wa fulani, sio tu anakuwa na utiifu zaidi kwa huyo "fulani" kuliko taifa, bali pia kunakuwa na dharau ya "ah watanifanya nini wakati fulani aliyeniingiza kazini yupo?"
Sasa tumeanza kuwafahamu kwa majina baadhi ya watumishi hao waliofukuzwa kazi. Hata hivyo, ni mapema mno kufahamu iwapo hatua hiyo iliwahusu watumishi wote wa umma au wale tu "wasio ndugu, jamaa au marafiki wa akina fulani"?
Je, wale watoto wa vigogo pale Benki Kuu nao waliguswa na zoezi hilo? Je, ndugu, jamaa na marafiki wa watawala wetu waliojazana kwenye balozi zetu za nje nao waliguswa? "Kitengo" je?
Ila jambo moja ninalohisi linaweza kuwa "matokeo yasiyotarajiwa" (unintended consequences) ni uwezekano wa baadhi ya waliofukuzwa kazi kufungua kesi dhidi ya serikali. Kuna kasoro kadhaa za kisheria katika utekelezaji wa amri hiyo ya rais lakini hapa sio mahala pake kuyajadili.
Japo siwezi kubashiri matokeo ya kesi hiyo iwapo itafunguliwa, vitu viwili vinavyoweza kuongeza uzito wa hoja za watumishi hao ni pamoja na kauli ya Rais Magufuli kwamba "wafungwe miaka saba." Ni kazi ya mahakama kutoa hukumu, sio Rais. Na kwa Rais katamka hivyo, ni kama anaiamuru mahakama itekeleze matakwa yake badala ya kufuata sheria.
Pili, ni wazi kuwa serikali imefanya ubaguzi kwa kuendesha zoezi hili kwa kuangalia “watumishi wasio vigogo” huku ikifumbia macho viongozi mbalimbali, ambao baadhi yao wanaendelea kuandamwa na tuhuma sio za kughushi vyeti vya elimu tu bali hata majina (ni nani asiyejua kuhusu suala la “Bashite”?)
Yayumkinika kuituhumu serikali kuwa imekwepa kwa makusudi kuhakiki sio elimu tu bali hata uraia wa viongozi wa kisiasa. Tuna wanasiasa wengi tu wenye elimu au uraia tata.
Kwa hiyo japo hatua ya kuhakiki elimu ya watumishi wa umma inastahili pongezi, ubaguzi wa makusudi uliofanyika katika zoezi hilo unapaswa kulaaniwa vikali. Lengo halikuwa kumnusuru ‘Bashite’ pekee bali pia baadhi ya wabunge, Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, na viongozi wengine wa kisiasa ambao baadhi yao sio tu wana walakini kielimu bali pia uraia wao ni tete.

20 Apr 2017


NIANZE makala hii kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia za askari wanane wa Jeshi la Polisi waliouawa kinyama wiki iliyopita, wilayani Kibiti, mkoani Pwani.
Huu ni msiba wa kitaifa, japo hakuna maombolezo ya kitaifa – sijui kwa vile hatuthamini uhai wa Watanzania wenzetu au tumekwishazoea sana vifo kama vile vya ajali.
Katika moja ya vitu nilivyojifunza katika miaka yangu kadhaa ya kuishi hapa Uingereza ni jinsi wenzetu wanavyothamini uhai. Laiti tukio hili la kuuawa polisi wanane huko Kibiti ndio lingekuwa limetokea hapa, basi huenda kila kitu kingesimama.
Na si hapa Uingereza pekee. Kwa hali ilivyo sasa katika baadhi ya mataifa ya Ulaya Magharibi sasa ni kama "tumekwishaanza kuzoea” matukio ya kigaidi, maana yanatuandama mno, hasa Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, na majuzi hapa Uingereza.
Katika kila tukio, bila kujali idadi ya waathirika, takriban ndani ya saa moja tangu kutokea tukio husika, Rais au Waziri Mkuu wa nchi husika huongea na wananchi katika runinga mubashara, kutoa pole kwa waathirika, kuwahakikishia usalama wananchi, na kuwaonya wahusika kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Huu ndio uongozi.
Je, sisi hali ikoje? Sana sana ni taarifa ya salamu za rambirambi kutoka kwa Rais, matamko ya hapa na pale ya Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, na kauli za vitisho za IGP Ernest Mangu – sio kwa “majambazi” bali “wananchi wanaochekelea vifo vya polisi hao waliouawa.”
Japo sio busara kwa mtu yeyote kufurahia kifo cha mtu mwingine – hata kama sio polisi – lakini hilo sio kosa la jinai. Kadhalika, ni vema nguvu ikaelekezwa kwenye tatizo halisi, ambalo Jeshi la Polisi chini ya uongozi wa IGP Mangu haliwezi kukwepa lawama, kwa sababu tishio la usalama mkoani Pwani limedumu kitambo sasa bila kupatiwa ufumbuzi, kuliko ‘tatizo la kufikirika’ (kuwa kuna watu wanafurahia vifo vya polisi hao)
Saa kadhaa baada ya kupatikana taarifa za mauaji hayo, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, alizungumza na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kuwa jeshi hilo "halitokuwa na mzaha wala msamaha" katika operesheni maalumu kuhusiana na tukio hilo. Je, kulikuwa na mzaha na msamaha kabla ya tukio hilo, ambao sasa hautakuwepo wakati wa operesheni husika?
Tukiweka kando kasoro hizo, jambo moja lililonigusa mno ni kukosekana kwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwenye tukio la kuaga miili ya polisi hao. Badala ya kujumuika na wafiwa, Rais alihudhuria hafla mbili (ambazo zingeweza kabisa kusogezwa mbele) za uzinduzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na makazi katika kitongoji cha Magomeni.
Sambamba na hilo, tukilinganisha na matukio makubwa mawili ya hivi karibuni – uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha Clouds na "kutekwa" kwa msanii wa bongofleva, Roma Mkatoliki – mauaji hayo ya polisi hao wanane yalipewa uzito mdogo na Watanzania wengi, angalau huko mtandaoni.
Hali hiyo inasikitisha lakini haishangazi. Sababu moja kuu ya "wananchi wengi kutoonekana kuguswa na mauaji hayo ya polisi wanane" ni ukweli kwamba uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi wengi sio mzuri. Polisi wetu kwa kiasi Fulani wamekuwa wakisifika kwa unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia.
Na kama kuna kitengo cha polisi wetu "kinachochukiwa mno" ni hicho cha FFU (Kikosi cha Kuzuia Ghasia) ambacho askari hao wanane walikuwamo. Japo siungi mkono "chuki" hiyo, lakini naelewa jinsi gani Watanzania wengi wasivyopendezwa na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
Kwa upande mwingine, jeshi hilo limekuwa likionekana kama "adui wa kudumu" dhidi ya vyama vya upinzani, huku likifanya upendeleo wa wazi kwa chama tawala CCM.
Kwa hiyo, wakati tunaomboleza vifo hivyo vya polisi hao wanane, ni muhimu mno kwa wahusika kuchukua hatua za makusudi kuondoa "uhusiano wa chuki na shaka" uliopo kati ya Jeshi la Polisi na asilimia kubwa ya Watanzania.
Kana kwamba uhusiano bora kati ya Jeshi la Polisi na wananchi sio muhimu ‘sana,’ moja ya nyenzo muhimu ya kujenga na kuimarisha ushirikiano huo, mpango wa Polisi Jamii, ulifutwa kwa sababu wanazozijua wahusika. Polisi jamii ilikuwa kiungo muhimu kati ya polisi wetu na jamii.
Kioperesheni, japo tukio hilo la mauaji ya polisi wanane linaelezwa kuwa ni la kijambazi, binafsi ninahisi kuwa kuna tatizo zaidi ya ujambazi. Na kwa tafsiri ninayoelewa kuhusu ugaidi, basi tukio hilo linastahili kabisa kuitwa la kigaidi. Ni majambazi gani wenye ujasiri wa kuwavizia polisi na kuwaua kwa namna hiyo ya uvamizi wa kushitukiza?
Halafu, hilo sio tukio la kwanza. Na hao polisi wanane sio polisi wa kwanza kuuawa katika eneo hilo, sambamba na wakazi wengine. Yayumkinika kuhitimisha kuwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani hawawezi kukwepa lawama, kwa kushindwa kukabili kushamiri kwa mauaji katika eneo hilo.
Sijui Rais Magufuli ameishiwa na zile sindano zake za kutumbulia majipu, au kaishiwa pumzi ya “TumbuaMajipu” lakini ni wazi kuna matatizo ya msingi katika uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Ukimya wa polisi katika uvamizi huko Clouds, na "kutekwa" kwa Roma, na sasa hili la Kibiti, vilipaswa kumfanya Rais Magufuli achukue hatua.
Moja ya sababu maarufu ya polisi wetu wanapozuia mikutano au maandamano ya vyama vya upinzani huwa "intelijensia." Sasa kama intelijensia ipo kwenye kudhibiti shughuli halali za vyama vya siasa, kwa nini intelijensia hiyo isitumike kwenye kukabiliana na "magaidi" hao wanaotikisa Mkoa wa Pwani?
Nihitimishe makala hii kwa kurejea salamu zangu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa kinyama. Pamoja na upungufu wote nilioutanabaisha katika makala hii, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha unyama waliofanyiwa askari hao.
Lakini pia wakati tunaomboleza vifo vyao, ni vema tukatafakari kama taifa kuhusu uhusiano kati ya Jeshi la Polisi (na vyombo vyote vya dola kwa ujumla) na raia, ambao ukiwa bora, unaweza kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na taifa kwa ujumla

15 Apr 2017



Nianze makala hii kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia za askari wanane wa Jeshi letu la Polisi waliouawa kinyama wilayani Kibiti, Mkoani Pwani. 

Huu ni msiba wa kitaifa, japo hakuna maombolezo ya kitaifa - sijui kwa vile hatuthamini uhai wa Watanzania wenzetu au tushazowea sana vifo kama vile vya ajali, nk.

Jambo moja lililonikera mno jana ni ukimya wa wahusika, na mpaka wakati ninaandika makala hii sijasikia kauli yoyote kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi. Labda kuna watakaosema "aanasubiri taarifa kamili." Hapana. Uongozi hauko hivyo. Sie huku Ulaya sasa ni kama "tumeshaanza kuzowea"  matukio ya kigaidi, maana yanatuandama mno, hasa Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, na majuzi hapa Uingereza.

Katika kila tukio, bila kujali idadi ya waathirika, takriban ndani ya saa moja tangu kutokea tukio husika, Rais au Waziri Mkuu wa nchi husika huongea na wananchi katika runinga mubashara, kutoa pole kwa waathirika, kuwahakikishia usalama wananchi, na kuwaonya wahusika kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Huu ndio uongozi.

Je sie hali ikoje? Sana sana ni taarifa ya salamu za rambirambi kutoka kwa Rais, kama inavyoonekana hapa chini



Hadi wakati salamu hizo za rambirambi zinatolewa, hakukuwa na tamko lolote kutoka kwa uongozi wa jeshi la polisi. Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alithibitisha kutokea kwa tukio hilolakina akadai "hana taarifa" kuhusu tukio hilo hadi atakapowasiliana na IGP. 


Baadaye, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, aliongea na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kuwa jeshi hilo "halitokuwa na mzaha wala msamaha" katika operesheni maalum kuhusiana na tukio hilo


Je, kulikuwa na mzaha na msamaha kabla ya tukio hilo, ambao sasa hautokuwepo wakati wa operesheni husika?

Tukiweka kando kasoro hizo, jambo moja lililonigusa mno ni ukweli kwamba matukio makubwa mawili ya hivi karibuni - uvamizi uliofanywa na RC Makonda kwenye kituo cha Clouds na "kutekwa" kwa msanii wa bongofleva, Roma Mkatoliki - yalipewa uzito mkubwa na Watanzania kuliko mauaji hayo ya polisi hao wanane.

Inasikitisha lakini haishangazi. Sababu moja kuu ya "wananchi wengi kutoonekana kuguswa na mauaji hayo ya polisi wanane" ni ukweli kwamba mahusiano katika ya Jeshi la Polisi na wananchi wengi sio mazuri. Polisi wetu wamekuwa wakisifika kwa unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia. 

Na kama kuna kitengo cha Polisi wetu "kinachochukiwa mno" ni hicho cha FFU (Kikosi cha Kuzuwia Ghasia) ambacho askari hao wanane walikuwamo.

Japo siungo "chuki" hiyo, lakini naelewa jinsi gani Watanzania wengi wasivyopendezwa na utendaji kazi wa jeshi la polisi. 

Kwa upande mwingine, Jeshi hilo limekuwa likionekana kama "adui wa kudumu" dhidi ya vyama vya upinzani, huku likifanya upendeleo wa wazi kwa chama tawala CCM.

Kwahiyo, wakati tunaomboleza vifo hivyo vya polisi hao wanane, ni muhimu mno kwa wahusika kuchukua hatua za makusudi kuondoa "uhusiano wa chuki na mashaka" uliopo kati ya jeshi la polisi na asilimia kubwa ya Watanzania.

Kana kwamba uhusiano bora kati ya jeshi la polisi na wananchi sio muhimu "kihivyo," moja ya nyenzo muhimu ya kujenga na kuimarisha ushirikiano huo, mpango wa 'Polisi Jamii,' ulifutwa kwa sababu wanazozijua wahusika. Polisi jamii ilikuwa kiungo muhimu kati ya polisi wetu na jamii.

Kioperesheni, japo tukio hilo la mauaji ya polisi wanane linaelezwa kuwa ni la kijambazi, binafsi ninahisi kuwa kuna tatizo zaidi ya ujambazi. Na kwa tafsiri ninayoelewa kuhusu ugaidi, basi tukio hilo linastahili kabisa kuitwa la kigaidi. Ni majambazi gani wenye ujasiri wa kuwavizia polisi na kuwaua kufuatia 'ambush' kama hiyo iliyotokea eneo la tukio?

Halafu, hilo sio tukio la kwanza. Na hao polisi wanane sio polisi wa kwanza kuuawa katika eneo hilo, sambamba na wakazi wengine. Yayumkinika kuhitimisha kuwa jeshi la polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani hawawezi kukwepa lawama, kwa kushindwa kukabili kushamiri kwa mauaji katika eneo hilo. Sijui Rais Magufuli ameishiwa na zile sindano zake za kutumbulia majipu, au kaishiwa pumzi ya #TumbuaMajipu lakini ni wazi kuna matatizo ya msingi katika uongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani na jeshi la polisi kwa ujumla. Ukimya wa polisi katika uvamizi huko Clouds, na "kutekwa" kwa Roma, na sasa hili la Kibiti, vilipaswa kumfanya Rais Magufuli achukue hatua.

Moja ya sababu maarufu ya polisi wetu wanapozuwia mikutano au maandamani ya vyama vya upinzani huwa "intelijensia." Sasa kama intelijensia ipo kwenye kudhibiti shughuli halali za vyama vya siasa, kwanini intelijensia hiyo isitumike kwenye kukabiliana na "magaidi" hao wanaotikisa Mkoa wa Pwani?

Nihitimishe makala hii kwa kurejea salamu zangu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa kinyama. Pamoja na mapungufu yote niliyotanabaisha katika makala hii, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha unyama waliofanyiwa askari hao.

Lakini pia wakati tunaomboleza vifo vyao, ni vema tukatafakari kama Taifa kuhusu mahusiano kati ya jeshi la polisi (na vyombo vyote vya dola kwa ujumla) na raia, ambayo yakiwa bora, yanaweza kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na taifa kwa ujumla

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.