14 Feb 2008

KATIKA TOLEO LA WIKI HII LA GAZETI LA RAIA MWEMA,MAKALA YANGU INAZUNGUMZIA YALIYOJIRI KUTOKANA NA SAKATA LA RICHMOND.KWA SABABU ZILIZO NJE YA UWEZO WANGU,MAKALA HIYO HAIKO KWENYE ONLINE VERSION YA GAZETI HILO.PIA KWA VILE VICHWA VYA MAKALA ZANGU HUWEKWA NA MHARIRI KUNA UWEZEKANO KICHWA CHA HABARI KILICHOPO KWENYE PRINTED VERSION YA GAZETI NI TOFAUTI NA CHA HAPO JUU.

Nianze makala hii kwa kutoa pongezi tatu muhimu. Kwanza, kwa Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.CV yake katika utumishi wa umma “imetulia”.

Pili, nampongeza “mwana wa pakaya” ("mtoto wa nyumbani" kwa Kindamba), Jaji Kiongozi mpya Salum Masati, mzaliwa wa Ifakara, ambaye kuteuliwa kwake kumeuweka mji huo katika ramani ya uongozi wa kitaifa (angalau sasa Ifakara inaweza kujulikana kitaifa kwa jambo zaidi ya mchele na mafuriko ya Mto Kilombero.) 

Tatu, ni pongezi kwa mashujaa wote “walioshikia bango” suala la Richmond.Mungu awazidishie ujasiri zaidi na kuwapa ulinzi wake dhidi ya hujuma za mafisadi. Kwa kelele za kizalendo kama za akina Mheshimiwa Anne Kilango, tunaamini kuwa maslahi ya taifa yatawekwa mbele katika mjadala wa ufisadi wa BoT

Binafsi, sakata la Richmond liliniingiza kwenye msukosuko mkubwa baada ya “kupiga ngumi chini ya mkanda”. Novemba mwaka 2006,niliandika makala katika gazeti flani la huko nyumbani. Makala hiyo ilitokana na habari kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, angefanya kikao na wabunge wa CCM kuandaa mkakati wa kuzima mjadala bungeni kuhusu suala la Richmond. 

Katika makala yangu, nilikosoa utaratibu uliozoeleka wa viongozi wa CCM kuitisha vikao “vya kuwaziba midomo” wabunge wake kila linapojiri jambo linalogusa hisia za wengi. Sikuona mantiki ya Lowassa kuwaita wabunge wa chama chake kuwaweka sawa kwani tatizo la umeme lilikuwa mwiba mkali kwa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa. Kikao kilifanyika na agizo la kuweka mbele maslahi ya chama lilizingatiwa,na hatimaye ishu ya Richmond haikujadiliwa.

Kilichopuuzwa wakati huo ni hekima kwamba kuficha ugonjwa hakusaidii kuponya maradhi. Pengine suala hilo lingejadiliwa muda huo wala tusingefika hapa tulipo sasa. Waingereza wana msemo “sehemu mbaya ya uamuzi mbovu ni pale inapofika hatua ya kuujutia”. 

Pamoja na kushutumu mtindo huo wa kuwekana sawa ambao naamini unatumiwa kuficha maovu, makala yangu pia iligusia staili ya uongozi wa Lowassa ya kuwaumbua hadharani baadhi ya watendaji kwa madai ya utendaji wao mbovu wa kazi. 

Japo alikuwa sahihi kukemea viongozi wasiowajibika ipasavyo, kuwaumbua hadharani ulikuwa mkakati dhaifu wa kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Nilieleza kwamba zilikuwapo fursa mbalimbali kwa Lowassa kuwakaripia, kuwakosoa au hata kuwaumbua viongozi hao (kwa mfano kuwaita ofisini kwake, kuwaandikia maonyo au hata kuwapigia simu) pasipo haja ya kufanya hivyo kwenye mikutano ya hadhara. Nilihofia kwamba licha ya kuwashushia hadhi watendaji walioumbuliwa hadharani, staili hiyo ya Lowassa ingeweza kutafsiriwa kuwa ni mbinu ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa machoni mwa wananchi ilhali tatizo liko kwenye mfumo wa uongozi. 

Siku chache baadaye, Mwandishi wa Habari wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Saidi Nguba, alijibu makala yangu gazetini (na baadaye kunitumia barua pepe na comments kwenye blogu yangu) kumtetea bosi wake huku akidai suala la CCM kuitisha vikao vya ndani ni utaratibu walijiwekea wao wenyewe na haulengi kuwaziba midomo wabunge kwa vile “wabunge tulionao si watu wa kuzibwa midomo.” 

Mwanahabari huyo alitoa orodha ndefu ya “mafanikio” ya Lowassa ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi waliopata nafasi za kuendelea na masomo (japo hakugusia upungufu wa walimu, madawati, nk.) Alimalizia kwa kunikumbusha kuwa kama mwanafunzi niliyeko nje ya nchi nikisomeshwa kwa fedha za Watanzania masikini ninapaswa kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kukosoa “mambo nisiyoyajua.”

Nilimjibu kwa kumfahamisha kwamba kuwa mwanafunzi ninayesomeshwa kwa fedha za walipa kodi masikini ni sababu tosha ya kukemea mambo mabovu ili kuhalalisha kwamba fedha inayotumika kunisomesha haipotei bure.

Pia nilimfahamisha kwamba wazazi wangu ni miongoni mwa Watanzania hao walipa kodi masikini, na kama masikini na walipa kodi wengine, wana haki ya kufahamu na kukosoa utendaji wa serikali waliyoiweka madarakani. Kuhoji utendaji wa serikali sio upinzani, na hata kama ungekuwa ni upinzani basi ni kwa manufaa ya Taifa letu.

Kusomeshwa kwa fedha za masikini haimaanishi anayesomeshwa asitoe mawazo yake (usahihi au upotofu wa mawazo hayo ni suala jingine). Nilipingana na utetezi wake kuhusu “mafanikio” ya staili ya Lowassa kuwaumbua baadhi ya watendaji hadharani na kumkumbusha kuwa hata Rais akitaka kumkosoa Waziri Mkuu wake hatofanya hivyo hadharani bali atamwita chemba. 

Mwandishi huyo mkongwe atakubaliana nami kwamba wakati Lowassa alituaminisha majukwaani kuwa ni “Sokoine mpya” (kwa kuwabana viongozi wazembe papo kwa hapo), “nyuma ya pazia” hakuwa tofauti na hao aliokuwa akiwaumbua hadharani kwani uoza wa Richmond umetokea ofisini kwake.

Naamini (mwandishi huyo) alikuwa akitekeleza tu majukumu yake ya kazi. Pengine moyoni aliafikiana na hoja zangu lakini ulikuwa ni wajibu wake kumtetea bosi wake. Natamani kusikia maoni yake sasa yake kuhusu sakata zima la Richmond.Naamini kwamba wengi wa watetezi wa mkataba huo sasa wataona mantiki za makelele yetu.

Hatimaye Lowassa amejiuzulu huku akijitetea kwamba suala zima la Richmond lilikuwa njama za watu waliokuwa wanataka Uwaziri Mkuu. Kuna msemo wa kiingereza kwamba “hukumu ya umma ni mbaya zaidi ya ile inayotolewa mahakamani.”

Wakati Lowassa anailamu Kamati ya “Kamati ya Mwakyembe” kwa kutompatia nafasi ya kujitetea, kelele zilizosikika mitaani kusherehekea kujiuzulu kwake ndio “hukumu ya umma” huku wengine wakidai kuwa Mzimu wa Nyerere “umemrudi.” 

Hivi mwongozo wa Bunge unasemaje pindi Mbunge anapoituhumu Tume Teule ya Bunge kuwa imesema uongo (kama alivyodai Lowassa)? Wakati nakerwa na UNAFIKI wa kupongeza “ushujaa wa Lowassa kujiuzulu”, ni muhimu Lowassa athibitishe uongo wa tuhuma dhidi yake kwani kama hoja ni kutoitwa kujitetea basi hata Zitto Kabwe alisimamishwa ubunge bila kupewa fursa ya kujitetea. 

Na kwanini alikimbilia kujiuzulu badala ya kudai haki yake, kama kweli aliamini ameonewa? Iweje Kazaura na Msabaha na wengineo wakati walipohojiwa nje ya kiapo waashirie mhusika ni Lowassa na sio mtu mwingine katika kabineti lenye mawaziri 60?Naamini kilio cha Lowassa kimesikika kwa vyombo vya dola. Niandike kwa herufi kubwa: LOWASSA ANAHITAJI KUHOJIWA.

Apewe haki hiyo anayodai kunyimwa na Kamati ya Bunge, lakini pia umma pia unahitaji hivyo kuhusu hizo shs milioni 152 kwa siku za Richmond. Wote waliohusika katika skandali hilo wana uhaba mkubwa wa uzalendo. Walithamini zaidi matumbo yao (na pengine “nyumba ndogo” zao) kuliko maisha ya Watanzania wenzao.

Hakuna haja ya kuwapeleka jela kwani watatuongezea tu gharama ya kuwahudumia chakula gerezani. La muhimu ni kuwafilisi kila walichovuna kwenye “dili” hilo. Katika hili, tuweke pembeni sheria za mapatano (laws of reconciliation) za Agano Jipya na kurejea kwenye sheria za kisasi (laws of retaliation) za Agano la Kale, yaani jino kwa jino na jicho kwa jicho. Wametufilisi nasi lazima tuwafilisi.

KUNA MWANANCHI AMENITUMIA E-MAIL YENYE UJUMBE WA KUFURAHISHA KWA NAMNA FLANI.IKO KWENYE POWERPOINT FORMAT.

2 comments:

 1. ufisadi upo hata leo kupitia makaburu kam De Deers. Wanamakampuni makubwa huko afrika kusini ambayo yanivest kwa ukubwa na kunyonya rasilimali zetu, wanannunua ardhi, makampuni ya ummma na kudhulumu uchumi wetu leo. Ni walanguzi wakuu.
  Mwalinmu Nyerere aliona hili akafunga kabisa rasilimali zetu kwa mabeberu wa kijeuri. Lazima ifaamike huko afrika kusina kuna wayahudi wengi matajiri, including the de beers impire.
  Angalia ukweli huu.

  ReplyDelete
 2. ni video hii iangalie.
  http://khanverse.blogspot.com/2008/02/diamonds-are-4eva.html

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2020

Powered by Blogger.

Nisapoti

Podcast

Chaneli Ya YouTube