Wakati haijafahamika nani aliyelipwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya IPTL, imebainika kuwa Bunge liliwahi kuagiza fedha hizo zisichukuliwe mpaka mitambo ya IPTL itakapokuwa chini ya Tanesco mwakani.
Hiyo imo katika taarifa ya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alithibitisha jana kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 Milioni (Sh195.2 bilioni) katika akaunti hiyo, lakini akakataa kutaja nani hasa aliyelipwa.
Mkataba wa miaka 20 baina ya IPTL na Tanesco ulisainiwa mwaka 1995 na ulitakiwa kuisha 2015 na mitambo hiyo kuwa mali ya Tanesco.
Hata hivyo, ukiwa umebaki mwaka mmoja kumalizika, imebainika kuwa mitambo hiyo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan African Power, ambayo inatarajiwa kuingia mkataba mwingine na Tanesco ili iwauzie umeme.
Ndulu alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Dola za Marekani 22 milioni na Sh161 bilioni za Tanzania ambazo zote kwa pamoja ndizo zilizofikisha jumla ya Sh195.2 bilioni.
Vyanzo vingine vilitoa takwimu mbili tofauti, kimoja kikisema kiasi cha fedha hizo kilifikia Dola za Marekani 270 milioni na kingine Dola 250 milioni. Kuhusu nani mwenye mamlaka ya kutoa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema kwa mujibu wa mkataba wa kufunguliwa kwa akaunti ya fedha hizo, ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na IPTL.
“Hakuna mtu mwingine anayeweza kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo zaidi ya hao, kwa hiyo hao ndiyo waliosaini kutolewa kwa hizo fedha na taratibu zote zilifuatwa,” alisema Profesa Ndulu.
Alipoulizwa ni nani aliyelipwa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema IPTL ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kusema ni nani alipwe na ilifanya hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alipoulizwa juu ya fedha hizo alisema: “Kwa kawaida huwa nina majibu mafupi sana, lakini kwa kuwa mmeamua kuandika uongo, endeleeni, siwezi kukujibu chochote wasiliana na hao IPTL wakujibu.”
Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata kiongozi wa IPTL kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari kampuni hiyo ni mufilisi.
Msimamo wa Bunge
Ripoti ya POAC inasema Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aliorodhesha matatizo ya mkataba kati ya Tanesco na IPTL na kuangalia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mipango ya kununua mitambo hiyo na kuibadilisha iwe inatumia gesi badala ya mafuta mazito.
“Mgogoro uliopo hivi sasa kati ya Tanesco na IPTL unahusu kiwango cha malipo ya uwekezaji yaani capacity charges ambacho IPTL walikuwa wanalipwa na Tanesco. Kwa mujibu wa mkataba huo, capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31.
Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa, ilikubalika kuwa mtaji uliowekezwa uwe ni Dola za Marekani 36 milioni.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika kuwa IPTL haikuwekeza fedha hizo, bali Sh50,000,” inasema ripoti hiyo.
Ilisema kuwa, mpaka kufikia Mei 2008, Tanesco ilikuwa imeilipa IPTL Sh221 bilioni tangu ilipoanza uzalishaji umeme Januari 2002.
Kamati iliagiza: “Wanasheria wa Tanesco na Serikali watumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow) ndicho hichohicho kitumike kumaliza madeni yaliyopo na vilevile kufanyia marekebisho mitambo hiyo ili itumie gesi,” inasema taarifa hiyo.
Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge huku POAC ikitoa maelekezo kwa Gavana Ndulu kuwa fedha zilizopo Escrow zisitumike kwa namna yoyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa na kutumia gesi asilia.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema ameshtushwa na taarifa za kutolewa kwa fedha hizo kinyemela.
“Tunaitaka Serikali kutoa taarifa kama kweli hizo fedha zimetolewa, kwa sasa siwezi kutoa msimamo wetu kwa kuwa hatujakaa kama kamati, tunatarajia kuitisha kikao cha dharura Dodoma kuzungumzia suala hili,” alisema Zitto.
CHANZO: Mwananchi