Sakata la mkataba wa Kampuni ya
Richmond linaelekea kuchukua mwelekeo mpya kila kukicha. Ni rahisi kutafsiri kwamba suala hili lisipopatiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kuwa na madhara makubwa kwa nchi na kwa chama tawala, CCM.
Tangu ripoti ya “
Tume ya Mwakyembe” ilipowekwa hadharani katika kikao kilichopita cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, kumejitokeza kauli kadhaa za utatanishi ambazo japo zinaweza kuwa ni za kawaida tu, tafsiri ya ndani inaashiria matatizo makubwa huko tuendako.
Naomba niwe muwazi zaidi katika makala hii, na ningependa kutamka bayana kwamba sina nia ya kumshushia heshima yeyote nitakayemtaja. Lengo kuu la makala hii ni kuikumbusha kila pande inayoguswa na sakata hilo kutambua kwamba taifa letu ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya mtu mmoja.
Naikumbuka sana siku taifa lilipotangaziwa kifo cha Baba wa Taifa.Watanzania wengi walitokwa na machozi sio tu kwa vile hawangemwona tena Mwalimu bali pia ni ile hali ya kutokuwa na uhakika taifa letu lingekuwaje bila
Nyerere.Naamini kwamba laiti Mwalimu angekuwepo, baadhi ya upuuzi kama huo wa mkataba wa
Richmond wala usingetokea, lakini ndio hivyo tena, hatuko naye duniani.
Wanaoilaumu “
Tume ya Mwakyembe” kuwa imewaonea wanasahau kwamba tume hiyo haikuundwa baada ya
Mwakyembe na wenzake kutuma maombi ya kuwa kwenye tume hiyo.Inashangaza wanaolalamika sasa kwamba ripoti ya tume hiyo ilikuwa na ajenda za kumalizana kisiasa,ilhali hawakuipinga wakati inaundwa na pale ilipokuwa ikitimiza majukumu yake.Ina maana ajenda hizo za kisiasa zilianza baada ya akina Mwakyembe kuwa wajumbe wa tume au zilikuwapo kabla.Kama zilikuwapo kabla,kwanini basi waliotajwa kuhusika na kuliingiza taifa katika hasara kubwa kwa mkataba huo wa kizembe hawakulalamika?
Na iwapo ajenda hizo zilianza baada baada ya wajumbe hao kuingia kwenye tume,kwanini basi watajwa walikimbilia kujiuzulu (huku wengine wakigoma waziwazi kujiuzulu kwa kuendelea kung’ang’ania madaraka) badala ya kudai haki itendeke?Ni rahisi kuhitimisha kuwa kelele zinazoendelea hivi sasa ni za mfa maji.
Nakumbuka kwenye miaka ya tisini nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari ya wavulana ya Tabora (
Tabora Boys) tulibahatika kutembelewa na Komandoo
Salmin Amour.Nayakumbuka baadhi ya maneno yake ambayo kimsingi yalikuwa na lengo la kutupa changamoto ya mafanikio ya kielimu na hatimaye kufanikiwa maishani (japo sio kila mara kufanikiwa kielimu ni tiketi ya moja kwa moja ya kufanikiwa kimaisha).Alitueleza kwamba madaraka ni mazuri na kutupa mifano ya namna yeye kama rais alivyokuwa na wasaidizi kibao wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vema.
Nilikubaliana na Komando wakati huo,na nakubaliana nae sasa,kwamba madaraka ni mazuri na matamu,na ndio maana tunashuhudia hizi kelele zinazoendelea kutoka kwa waliokumbwa na zahma ya kisiasa baada ya skandali ya mkataba wa kampeni ya
Richmond.Hakuna dhambi kwa madaraka kuwa matamu kwani hata njia ya kuyafikia sio nyepesi.Inahitaji jitihada na juhudi za kutosha kufikia hatua ya kuongoza watu wenye akili timamu.Na inatarajiwa kwamba mtu akishapata bahati ya kuwa kiongozi atatambua kwamba wengi,kama sio wote,wa aliokuwa akiwaongoza ni watu wenye akili timamu,uwezo wa kufanya maamuzi na wanaostahili heshima.
Waziri Mkuu aliyepita,
Edward Lowassa,ameendelea kuonyesha kwamba japo aliamua kubwaga manyanga kwa hiari yake,alifanya hivyo huku roho ikimuuma.Nasema hivyo kwa sababu kauli zake za hivi karibuni zinaashiria wazi kwamba bado ana kinyongo kikubwa na matokeo ya uchunguzi wa “
Tume ya Mwakyembe.”
Lowassa anaamini kwamba atarejea tena kwenye ulingo wa juu wa kisiasa kama Rais mstaafu
Ali Hassan Mwinyi ambaye alipokuwa Waziri alilazimika kujiuzulu kutokana na skandali iliyoikumba Wizara yake.Tofauti ya msingi kati ya
Mwinyi na
Lowassa ni ukweli kwamba wakati
Mwinyi alijiuzulu kutokana na tukio lililotokea mbali kabisa na mahala alipokuwa akifanyia kazi (lilitokea Shinyanga wakati ofisi ya
Mwinyi ilikuwa Dar es Salaam),
Lowassa alijikuta akikumbwa na shutuma kuhusu mkataba huo kwa vile katika hatua flani ulipita machoni mwake na akaamua “kusikiliza maamuzi ya wataalamu.”
Uongozi ni pamoja na kuwa na maamuzi ya haraka na yanayoangalia athari zinazoweza kujitokeza mbeleni iwapo yatafanyika maamuzi potofu.Haiyumkiniki kwamba Waziri Mkuu mzima anaweza kusikiliza ushauri mbovu na kuafikiana nao pasipo kujiridhisha iwapo ushauri huo ni wa manufaa kwa taifa.Hilo pekee linamvua sifa ya uongozi mtu yeyote aliye katika nafasi ya juu kitaifa.
Hivi kama mkataba wa
Richmond ungekuwa na madhara ya moja kwa moja kwa familia ya
Lowassa,kiongozi huyo angeendelea kusikiliza ushauri asio na uhakika na matokeo yake au angetaka kujiridhisha kwamba kilichokuwa kikifanyika hakingekuwa na madhara kwa familia yake?
Tukimweka kando Lowassa kwa muda,tumeshuhudia vituko vingine kutoka kwa Mkurugenzi wa
TIC Emmanuel Ole Naiko ambaye anadai kuna dalili za “mauaji ya halaiki” dhidi ya watu wenye asili ya wilaya ya Monduli.Hizi ni hoja mufilisi ambazo kama zitaachwa bila kudhibitiwa zinaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo yasiyo na msingi.
Hivi
Ole Naiko amefanya utafiti wa kutosha kiasi gani kuthibitisha kwamba kuna mpango wa “ethnic cleansing” dhidi ya watu wa Monduli?Kwa hakika serikali inapswa kumhoji kwa undani mtu huyu mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na matamshi hayo ambayo yanaweza kabisa kuathiri hata utendaji wa ofisi yake (hakuna mwekezaji aliye tayari kuwekeza kwenye nchi inayoelekea kwenye “
ethnic cleansing.”)
Kuna tetesi kwamba upo mkakati mkubwa wa “kujibu mashambulizi” dhidi ya ripoti ya “
Tume ya Mwakyembe.” CCM imekuwa ikituaminisha kila siku kwamba vikao nje ya chama ni majungu,sasa basi inapaswa kuhakikisha kwamba wote wenye kudhani hawakutendewa haki wawasilishe malalamiko yao kwa ngazi hsuika katika chama hicho au hata bungeni.
Kama taarifa tunazozisoma katika vyanzo mbalimbali kwamba kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM kutokana na skandali la
Richmond zina ukweli, basi ni muhimu kwa uongozi wa juu wa chama hicho kuachana na itifaki zake za kawaida za kuwasifia hata wanaostahili kukemewa na badala yake kuwawekwa “kiti moto” waeleze malalamiko yao mbele ya vikao halali badala ya kuendeleza mbinu za chini chini ambazo zinaweza kabisa kuathiri hali ya usalama wa nchi yetu.
Tusirejee makosa yaliyojitokeza katika mkataba wa Richmond ambapo baadhi ya watu walitahadharisha mapema kuhusu uhalali wa kampuni hiyo lakini wakapuuzwa.Kuna watu wanataka urais kwa kutimia njia yoyote ile hata kama kwa kufanya hivyo wanahatarisha uhai wa chama.
Lakini wakati tunawalaumu wanaolalamika kwamba wameonewa na “
Tume ya Mwakyembe” tunapaswa pia kujiuliza kama hawapati jeuri hiyo kutokana na uzembe unaendelea wa kutowachukulia hatua wahusika.Pengine jeuri waliyonayo inatokana na ukweli kwamba wanaamini kuwa hakuna mwenye jeuri ya kuwachukulia hatua hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao wameishia kupongezwa kwa “ushujaa wao” badala ya kushutumiwa kwa hasara waliyoisababisha kwa taifa.
Nadhani anachopaswa kufanya
Lowassa,Ole Naiko na wengine wote waliohusishwa na mkataba wa
Richmond ni kutafuta msaada wa kisheria kuona haki inatendeka upande wao iwapo wanaamini kuwa hawakutendewa haki,badala ya kuendeleza hizi porojo ambazo kwa hakika zinaweza kuua kabisa ndoto zao za kurejea kwenye ulingo wa juu wa siasa za nchi yetu.Mahakama zipo,vikao vya chama vipo,sasa kwanini kelele za kuonewa zisipelekwe huko?TANZANIA NI MUHIMU ZAIDI KULIKO MASLAHI YA MTU BINAFSI.
BAADA YA KUMALIZA KUSOMA MAKALA HII,UNAWEZA KUANGALIA VITUKO VYA SIASA ZA URUSI AMBAVYO VIMEZAA TERM MPYA YA NANO PRESIDENT (as in iPod Nano).BONYEZA HAPAHALAFU KWA WALE AKINA DADA "WENYE ULIMI MZITO",CLIP IFUATAYO INAWEZA KUWA YA MSAADA WA INA FLANI