11 Dec 2008

Na Simon Mhina
Kada machachari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema kauli ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kwamba mjadala juu ya mafisadi wa Akauti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ufungwe, inaashiria kuwakumbatia mafisadi. 

Mwanasiasa huyo chipukizi ambaye yupo katika kipindi cha mapambano na makada wenzake ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kutokana na kuvuliwa uanachama kwa kupinga mradi wa Jengo Jipya la Umoja huo, alisema hatua ya Makamba kuweka mizengwe mapambano dhidi ya ufisadi inawavunja moyo watendaji wa serikali ambao wapo mstari wa mbele kushughulikia tatizo hilo. 

Nape ambaye bado ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alisema kauli ya Makamba ni sawa na ya mtu anayeogopa kivuli chake. 

Hata hivyo, Nape katika mazungumzo na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, alisema kimsingi Makamba hana uwezo wala madaraka ya kuzuia mjadala juu ya mafisadi. 

Nape alisema ingawa hana uhusiano wowote na watu wanaopiga makelele juu ya ufisadi, lakini anafikiri wanafanya hivyo kutokana na machungu makubwa ya umasikini wanayopata Watanzania kutokana na mafisadi. 
Alihoji: ``Hivi Mzee Makamba mafisadi wakisemwa vibaya yeye anakerwa na nini? 

Hivi kinachomkera ni kipi, mafisadi waliopora fedha za wavuja jasho au wavuja jasho wanaopiga makelele juu ya mafisadi kuwaibia?`` 

Alisisitiza kuwa katika hali ya kawaida, hakuna Mtanzania ambaye atanyamazia ufisadi kutokana na uzito wake. 

Nape alihoji tena: ``Ina maana Mzee Makamba anajua idadi ya mafisadi wote nchini?`` 

Akifafanua, alisema kazi ya kuwashughulikia wahalifu hao ipo chini ya serikali na vyombo vyake vya dola na sio jambo la kisiasa. 

Wakati huo huo, Mbunge wa Moshi Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philimon Ndesamburo, amesema chama chake `kitafunga mdomo` kuhusu ufisadi, iwapo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, atakamatwa na kufikishwa mahakamani. 

Alisema Mkapa ni hazina kubwa ya mafisadi nchini na siku akifikishwa kortini janga hilo litakuwa limefikia tamati. 

``Chadema hatutaacha kupiga kelele juu ya ufisadi kama anavyosema Makamba hadi hapo Mkapa ambaye ni hazina ya mafisadi atakapopelekwa kortini, mambo yote yaliyofanyika yalikuwa chini ya utawala wake na alikuwa anayajua na alishiriki, lazima akamatwe,``alisema Ndesamburo. 

Mbunge huyo alisema mafisadi ndani ya CCM na serikali yake, hawajamalizika hivyo lazima waendelee kusakwa. 
Alisema asilimia 10 tu ya mafisadi wote nchini ndio wamekamatwa, lakini asilimia 90 akiwemo `baba lao` bado wapo mitaani. 

Ndesamburo alisema japokuwa Makamba amelenga kuwasaidia baadhi ya mafisadi, lakini kwa hili anatakiwa aone aibu. 

``Yaani wakati huu ambao Rais Jakaya Kikwete ameridhia watu waliokuwa mawaziri wafikishwe Mahakamani yeye anasimama kutetea ufisadi, namuomba angalau aone aibu, hata kama amelambishwa asali,`` alisema. 

Kuhusu Operesheni Sangara, Ndesamburo alisema itaendelea kwa nguvu zote licha ya Makamba kuibeza, kwa vile inalenga kuwafumbua macho Watanzania. 

Alisema operesheni hiyo si uchochezi wala nguvu ya soda, bali Makamba ametoa shutuma hizo, baada ya kushindwa kujibu hoja zinazotolewa na Chadema. 

Makamba alinukuliwa katika vyombo vya habari jana akisema kwamba mjadala wa EPA kwa sasa umefungwa kwa kuwa watuhumiwa wote wamefikishwa kortini. 

Hata hivyo, ukweli ni kwamba bado watuhumiwa wengine wakiwamo wamiliki wa Kagoda Agriculture Ltd hawajafikishwa kortini. 

CHANZO: Nipashe

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.