Rostam Aziz |
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005,mfanyabiashara controversial Rostam Aziz alitumia raslimali zake nyingi kuhakikisha mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM,Jakaya Kikwete,anashinda kwa gharama yoyote ile.Na kutokana na utajiri mkubwa alionao pamoja na mbinu zake mbalimbali,mchango wake ulimsaidia sana Kikwete kuingia Ikulu,na sasa ni Rais wetu anayeomba tena ridhaa ya kutuongoza kwa miaka mitano ijayo.
Kati ya mwaka 2005 (baada ya Kikwete kuingia Ikulu) na sasa,Rostam ameibuka kuwa kiumbe mwenye nguvu za kutisha sio tu ndani ya CCM bali kwenye siasa za Tanzania kwa ujumla.Lakini kubwa zaidi katika kipindi hicho ni kwa mfanyabiashara huyo kuhusishwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi na Kikwete na serikali yake kushindwa kuwaridhisha Watanzania kwamba "hamkumbatii swahiba wake huyo".Haihitaji kurejea namna Rostam alivyohusishwa na ufisadi wa EPA (Kagoda) na ujambazi wa Richmond.
Jakaya Kikwete |
Mwaka 2010,yaani mwaka huu,Rostam anaelekea kurejea tena ulingoni japo si kwa wazi sana.Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuhusika kwa mfanyabiashara huyo katika kampeni za Kikwete.Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Rostam vimekuwa vikiendesha kampeni ya chuki dhidi ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dokta Wilbroad Slaa,mwanasiasa anayeonekana kuwa tishio kwa mfanyabiashara huyo na vitendo vyake dhidi ya maslahi ya taifa.
Magazeti yanayomilikiwa na Rostam |
Na kama hilo la vyombo vya habari vya Rostam kumuandama Dkt Slaa halitoi mwangaza wa kutosha basi taarifa kwamba mwandishi mwandamizi wa kampuni ya Habari Corporation (inayomilikiwa na Rostam),Muhingo Rweyemamu,anatajwa kuwa mratibu wa kampeni za Kikwete.Itakumbukwa kuwa mwaka 2005,waliokuwa waandishi waandamizi wa Habari Corporation,Salva Rweyemamu na Dokta Gideon Shoo walitumika sana kwenye kampeni hizo.Baada ya kuingia Ikulu,Kikwete "alimzawadia" Salva ukurugenzi wa habari wa Ikulu,nafasi anayoshikilia hadi sasa.
Muhingo Rweyemamu |
Kama alivyo Salva,Muhingo anasifika kwa uwezo wake wa hali ya juu wa kujenga hoja.Kwa bahati mbaya au makusudi,uwezo huo pia unatumika ipasavyo kutengeneza fitna.Wengi watakumbuka namna Dokta Salim Ahmed Salim,mmoja wa wana-CCM waliokuwa wanawania kuchuana na Kikwete,alivyoundiwa zengwe kubwa na kumhusisha na kundi la Hizbu la huko Zanzibar.Inaelekea kuwa mbinu hizohizo zimeanza kutumika dhidi ya Dokta Slaa,na kuna kila sababu ya kuamini kuwa kuna mengi yatakayoibuliwa dhidi yake.
Salva Rweyemamu (kushoto) na Gideon Shoo |
Yayumkinika kuamini kuwa waandishi wa habari wanaotumiwa kumchafua Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla wanafanya hivyo kwa minajili ya "kupeleka mkono kinywani".Kubwa zaidi ni sapoti ya Rostam kwa Kikwete.Wakati mwaka 2005 alijibidiisha ili kufanikisha maslahi yake binafsi ya kibiashara (na amenufaika kweli-kwa kuangalia ishu za Kagoda na Richmond/Dowans) safari hii Rostam anahaha kumzuia Dokta Slaa kwa vile anafahamu fika kwamba laiti mwanasiasa huyo wa Chadema anayesifika kwa msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi akiingia Ikulu,zama za mafisadi kutumia jeuri yao ya fedha "kuendesha serikali kwa remote control" itakuwa imefikia kikomo.
Kwahiyo,Dokta Slaa na Chadema kwa ujumla wanapaswa kuelewa kuwa safari hii Rostam ana "special mission" ya kuhakikisha "survival (kusalimika) yake.Atatumia kila raslimali aliyonayo kuhakikisha Dokta Slaa haingii Ikulu.Anafanya hivyo akifahamu wazi kuwa rais yeyote mwenye kujali maslahi ya nchi yake "atamkalia kooni" mfanyabisahara huyo na washirika wake.
Hata hivyo,kwa vile si fedha za Rostam au wanahabari wake zitakazopiga kura kwenye uchaguzi mkuu,bali mimi na wewe pamoja na kila Mtanzania aliyechoshwa kuona nchi yetu ikigeuzwa "shamba la bibi",ni muhimu kwa wapiga kura kusema HAPANA.Tusitoe fursa kwa watu wenye maslahi binafsi kuipeleka nchi yetu kwenye maangamizi.Na ni muhimu zaidi kutambua kuwa baadhi ya watu hao wana utata wa kutosha tu kuhusu asili ya mahali walipozaliwa.Hiyo inamaanisha kuwa "wakishaiingiza Tanzania kwenye mtaro",watakuwa na sehemu ya kukimbilia.
KILA MTANZANIA MWENYE KUITAKIA MEMA NCHI YETU ANAPASWA KUPAMBANA NA WAHUNI WA KISIASA WANAOTAKA KUTUWEKEA MADARAKANI VIONGOZI WANAOWAMUDU NA HIVYO KUENDELEA KUTUFISADI KAMA ILIVYOKUWA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO ILIYOPITA.
INAWEZEKANA,TIMIZA WAJIBU WAKO