Showing posts with label BAKWATA. Show all posts
Showing posts with label BAKWATA. Show all posts

13 Mar 2009


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limeibua upya hoja za kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu Duniani (OIC), kwa kuitaka serikali kutafakari kwa kina na hekima juu ya kuridhia kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

Kuibuka tena kwa hoja hizo kumekuja miezi michache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufunga mijadala hiyo iliyokuwa ikielekea kuwagawa wananchi kwa misingi ya kidini.

Hoja hizo zimeibuliwa juzi kwenye Baraza la Maulid na Naibu Katibu Mkuu wa Utawala wa Bakwata, Suleiman Lolila, ambaye aliitaka serikali iangalie upya na kwa hekima na kama inawezekana iharakishe masuala hayo mawili.

“Tunaipongeza serikali kwa hekima kubwa na jitihada inayoitumia katika kushughulikia masuala ya Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, Waislamu wanangoja kwa hamu na shauku kubwa ridhaa ya serikali, Inshallah, tunaiombea serikali ipate wepesi katika masuala haya maridhawa.

“Tunawaomba Waislamu wadhamirie kwa dhati katika suala hili la OIC na mahakama ya kadhi kwa kutokuruhusu mwanya wowote wa mifarakano miongoni mwetu, kwani mifarakano itakaribisha mgawanyiko na utengano miongoni mwa jamii,” alisema Lolila.

Naibu Katibu Mkuu huyo, akisoma risala ya Bakwata mbele ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alisema ili kuridhiwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na OIC kuna hitaji utulivu wa hali ya juu miongoni mwa waumini wa dini zote mbili (Waislamu na Wakristo) ili kuipa serikali nafasi ya kufanya maamuzi ya busara kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa miongoni mwa jamii.

Suala la uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, mwishoni mwa mwaka jana lilizua mjadala mpya nchini, baada ya kufika bungeni na kutishia kuwagawa wabunge kwa itikadi za kidini.

Oktoba mwaka jana katika hotuba yake, Rais Kikwete, hakutaka kuweka wazi ni lini Tanzania itaridhia kujiunga na OIC pamoja na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, na badala yake aliwatuliza wananchi kwa kuwaambia wavute subira wakati serikali ikilifanyia kazi suala hilo kwa masilahi ya umma.

Rais Kikwete aliweka bayana kuwa ni mapema mno kuanza kutoa uamuzi wa masuala hayo, kwa kuwa bado utafiti haujakamilika pamoja na serikali kutotoa uamuzi wa mwisho, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kulumbana.

13 Jan 2009

Venance George, Morogoro
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kauli iliyotolewa juzi na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kupinga oparesheni Sangara inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si kauli ya waislamu wote.
Akizungumza mjini Morogoro kwa niaba ya Kaimu Mufti wa Tanzania,
Shekhe Suleiman Gorogosi, mratibu wa habari wa Bakwata, ustadhi Issa Mkalinga alisema kauli hiyo ni ya waislamu wachache ambao wamekuwa wakitumiwa na viongozi wa kisiasa kwa manufaa binafsi.
Ustadhi Mkalinga pamoja na Mkurugenzi wa Utawala, ustadhi Karim Mataliwa, aakizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kaimu mufti huyo ya kutembelea mikoani kuhamasisha uhai wa baraza, alisema baraza halitambui kauli hiyo na wala halijihusishi na mambo ya siasa.
"Ujue tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu hapo mwakani, hivyo wako baadhi ya wanasiasa wanatumia mwanya wa majukwaa ya dini kupeleka ujumbe wao," alisema.
Akizungumzia ziara ya kaimu mufti mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Utawala alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu aliyojiwekea kaimu mufti ya kutembelea baraza katika mikoa yote Tanzania na kwamba kaimu mufti ametembelea Dodoma na Morogoro na atatembelea mikoa mingine.
Ustadhi Mataliwa alisema lengo la ziara hizo ni kutaka kujua uhai wa baraza na matatizo yanayolikabili baraza katika ngazi hizo ikiwa ni pamoja na kuhimiza kufanya maandalizi ya uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi ya msikiti hadi taifa utakaoanza kufanyika mwezi April mwaka huu.
Wakati huo huo, katika mahojiano na baadhi ya waumini wa dhehebu hilo, mkoani Morogoro wameunga mkono kauli ya Bakwata na kudai kuwa viongozi wa dini ni vema wakafanya shughuli zao za kiroho na kuwaacha wanasiasa kufanya kazi zao za siasa.
Mmoja wa waumini hao, Ismael Rashid, alisema tamko lililotolewa na waislamu katika kongamano la jijini Dar es Salaam la kudai kuwa Chadema haina manufaa na msaada wowote kwa uislamu si maneno ya kiungwaana na si vema kukipakazia chama hicho kwamba ni kikabila na cha kibinafsi.
Rashid ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Jahazi asilia mkoani Morogoro alisema hatua iliyochukuliwa na Chadema ya kuacha kuunga mkono vyama vya CUF na Sauti ya Umma (SAU) ilikuwa ni sahihi kwa sababu chadema walisimamisha mgombea ubunge katika jimbo la Mbeya vijijini lakini vyama hivyo vilimwekea pingamizi mgombea huyo na kuenguliwa.
"Pingamizi hilo lilisababisha mgombea ubunge wa Chadema akaenguliwa kugombea
nafasi hiyo, sasa iweje chadema iwaunge mkono?" alihoji Rashid .
Alisema chama cha Chadema hakiungi mkono kampeni za mgombea wa CUF kwa mdai kuwa chama hicho, mwakani inakusudia kusimamisha mgombea wake katika jimbo hilo kwa hiyo kama Chadema ikiunga mkono CUF itashindwa kusimamisha mgombea wake hapo mwakani.


CHANZO:Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.