24 May 2012




Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa

Evarist Chahali
Toleo la 240
23 May 2012
WIKI iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliingia kwenye vitabu vya historia ya taifa hilo kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja. Kwa muda mrefu Obama alikuwa aidha akipinga suala hilo nyeti au kuchelea kuweka wazi msimamo wake.
Tayari suala hilo la ndoa za jinsia moja limezua mgawanyiko mkubwa wa kimtizamo ingawa kura mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa msimamo huo ‘mpya’ wa Obama hautoathiri kwa kiasi kikubwa maamuzi ya wapigakura katika uchaguzi mkuu wa Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kura za maoni za hivi karibuni, takriban asilimia 60 ya Wamarekani wanasema kitendo cha Obama kuunga mkono ndoa za mashoga hakitowashawishi kumpigia au kutompigia kura.
Lakini moja ya makundi ambayo yanaonyesha kuguswa na suala hilo ni Wamarekani Weusi. Kama ilivyo kwetu Waafrika, Wamarekani Weusi wamekuwa wapinzani wakubwa si tu wa ndoa, bali hata uhusiano wa kawaida wa watu wa jinsia moja. Mara kadhaa wasanii wengi wa muziki wa kufokafoka (hip-hop/rap), ambao ni maarufu kwa Wamarekani Weusi, wamekuwa wakilaumiwa kwa tungo zao zenye kuonyesha bayana upinzani dhidi ya ushoga.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, baadhi ya viongozi wa makanisa ya Wamarekani Weusi wameeleza bayana kuwa hawamuuingi mkono Obama katika suala hilo, huku wengine wakitishia kutompigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Japo Obama anaendelea kuungwa mkono na kundi hilo (la Wamarekani Weusi) huku akionekana kuwa ni ‘mwenzao’, kura za maoni zinaonyesha kuwa asilimia 49 inampinga katika msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga kulinganisha na asilimia 43 ya Wamarekani Weupe.
Obama mwenyewe amekiri kuwa anafahamu bayana msimamo wake huo utawaudhi baadhi ya wanaomuunga mkono. Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha ABC cha Marekani, Rais huyo alieleza kuwa inamwia vigumu kuendelea na ‘sintofahaumu’ katika ‘ubaguzi’ dhidi ya mashoga ilhali Wamarekani kadhaa anaowaongoza wamo kwenye kundi hilo.
Alifafanua kuwa kama mzazi, alikuwa anapata wakati mgumu kutokuunga mkono ndoa za mashoga ilhali wanae Sasha na Malia wana  baadhi ya marafiki zao ambao wazazi wao ni mashoga.
Kadhalika, alieleza kuwa ilikuwa inamsumbua pia kuendelea kutokuunga mkono ndoa za mashoga huku baadhi ya makundi muhimu katika nchi hiyo, kwa mfano, wanajeshi wanaolitumikia taifa hilo kwa uadilifu mkubwa, yakijumuisha mashoga.
Lengo la makala hii si kumuunga mkono au kumpinga Obama katika msimamo wake huo kwa ndoa za mashoga bali kupigia mstari nafasi ya ujasiri katika uongozi.
Kama alivyokiri mwenyewe kuwa anafahamu bayana uamuzi wake wa kutangaza hadharani msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga utawakera wengi, na pengine kumgharimu katika uchaguzi mkuu ujao, lakini Obama ameweza kufanya ujasiri wa kusimamia kile anachokiamini.
Japokuwa kuna baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaotafsiri hatua hiyo ya Obama kama kigeugeu-kwa maana alishawahi kuwa mpinzani wa ushoga- huku wengine wakidai hatua hiyo ni ‘janja yake’ tu kusaka kura za mashoga, jambo la msingi hapa ni ukweli kwamba amediriki kuweka kando uoga (huku akijua madhara) na kuweka wazi wapi anasimamia katika suala hilo.
Kwa upande fulani, uamuzi huo unaweza kumnufaisha dhidi ya mpinzani wake mtarajiwa kutoka chama cha Republicans, Mitt Romney, ambaye kama ilivyo kwa wahafidhina wengi, suala la ushoga ni kama laana.
Sasa, kwa vile moja ya misingi muhimu ya taifa la Marekani ni uhuru wa mtu kufanya apendacho alimradi havunji sheria, sambamba na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Obama na wanaomuunga mkono wanaweza kuutumia upinzani wa Romney dhidi ya ndoa za mashoga kama mfano hai wa jinsi mgombea huyo (mtarajiwa) na chama chake cha Republicans walivyobobea kwenye ‘ubaguzi na kuminya uhuru’  wa Wamarekani.
Kwa mtizamo wangu, ujasiri alionyesha Obama (bila kujali kama naafikiana au ninapingana naye katika suala la ndoa za mashoga) ninaulinganisha na kauli za hivi karibuni za aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa sasa wa Monduli (CCM), Edward Lowassa. Naomba niweke wazi kuwa ninaamini wasomaji wengi wa makala hizi wanafahamu fika msimamo wangu dhidi ya Lowassa, hususan kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Lakini msimamo huo haumaanishi nichelee kumuunga mkono pale anapoonyesha ujasiri wa kisiasa.
Kwa muda mrefu sasa, Lowassa amejitokeza kuwa mmoja wa wanasiasa wachache ndani ya CCM wanaoeleza waziwazi mapungufu ya chama hicho na jinsi yanavyoliathiri taifa kwa ujumla. Lakini kama ilivyozoeleka, msimamo huo (ambao hapa ninauita ujasiri) umemfanya mwanasiasa huyo aonekane kama kiumbe hatari kabisa kwa ustawi na uhai wa chama hicho tawala.
Majuzi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alinukuliwa akimpinga Lowassa kutokana na kauli yake katika mkutano wa hadhara huko Mto wa Mbu, Arusha, kuwa tatizo la CCM ni uongozi kuacha kusimamia misingi. Katika majibu yake kwa Lowassa, Mukama alimtaka mbunge huyo wa Monduli kushughulikia matatizo jimboni kwake kwanza.
Kuna wanaotafsiri kuwa msimamo wa Lowassa kukikosoa chama chake ni sehemu tu ya mikakati yake ya kuwania urais mwaka 2015. Lakini wanaofikiria hivyo wanapaswa kumtendea haki mwanasiasa huyo hasa kwa vile hajatangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Kadhalika, ni muhimu kutanua upeo wetu na kuzichambua kauli za Lowassa pasipo kuzihusisha zaidi na malengo yake ya baadaye ya kisiasa.
Kimsingi, tukiweka kando hisia za ‘unafiki wa kisiasa’, anayoongea Lowassa kuhusu CCM ni ya kawaida sana kwa maana kwamba kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufikiri anaelewa ‘mchango wa CCM katika kukwaza maendeleo ya nchi yetu.’
Kama chama tawala, CCM haiwezi kujinusuru dhidi ya shutuma kwamba inachangia sana kukwaza jitihada za kulikwamua taifa kutoka kwenye lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na vitendo vya ufisadi.
Kwamba Lowassa ni mmoja wa wana-CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi si sababu ya kumfanya mwanasiasa huyo kutozungumzia suala hilo. Na hata hizo tuhuma dhidi yake zinaweza kukosa nguvu kwa vile CCM yenyewe imeshindwa kuchukua hatua zozote dhidi yake.
Makala hii haina maneno ya kuitia moyo CCM katika msimamo wa baadhi ya viongozi wake wanaokerwa na kauli za Lowassa, hasa ikizingatiwa kuwa anachofanya mwanasiasa huyo ni kuwakilisha tu mtizamo wa Watanzania wengi (ikiwa ni pamoja na wana-CCM) dhidi ya chama hicho tawala. CCM inaweza hata kumtimua Lowassa lakini isipojirekebisha, kuna kila dalili kuwa itang’olewa madarakani huko mbeleni.
Japo ninaelewa msimamo wa Mukama kwamba kama kiongozi wa CCM Lowassa anapaswa kuongelea matatizo ya chama hicho kwenye vikao vya ndani, kimsingi hilo ni moja ya vyanzo vya matatizo yanayosababisha watu kama Lowassa kuamua kuweka hadharani matatizo hayo.
Ni hivi, kama chama hicho kina matatizo, kisha yanazungumzwa kwenye vikao vya ndani na hayapatiwi ufumbuzi, kwa nini basi kiongozi asishawishike kuyaongelea matatizo hayo hadharani?
Halafu kuna suala la maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya chama. Kwa vile CCM ni chama tawala, kila inachofanya au kuzembea kufanya kinaligusa taifa moja kwa moja. Kwa mantiki hiyo, wakati Mukama anaweza kuyaona matatizo ya CCM kuwa ni suala la kichama, kiuhalisi matatizo hayo si tu yanaligusa taifa bali pia ni suala la kitaifa. Na kwa vile Tanzania ni yetu sote, basi ni sahihi na halali kwa kila Mtanzania, ikiwa ni pamoja na Lowassa, kuyaongelea matatizo yanayolisumbua taifa letu pasi uoga wa kumuudhi mtu flani.
Naomba kuhitimisha makala hii kwa kurejea kuweka bayana msimamo wangu kuwa lengo halikuwa kuunga mkono msimamo wa Obama kuhusu ndoa za mashoga wala kugeuka muungaji mkono wa Lowassa (japo vyote si dhambi).
Makala hii imelenga kuwapongeza wanasiasa hao kwa ujasiri wa kuweka wazi misimamo yao hata pale kufanya hivyo kunapoweza kuwaingiza matatizoni. Kinyume cha ujasiri ni uoga na unafiki, na sote tunafahamu kuwa kiongozi mwoga na/au mnafiki si tu hawezi kusimamia yale anayoamini lakini pia ni kikwazo katika jitihada za kuleta mabadiliko muhimu kwa anaowaongoza.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.