15 Aug 2014

Rais Obama na watawala wa Afrika
WIKI iliyopita, viongozi kadhaa wa Afrika walikutana nchini Marekani kuhudhuria ‘Mkutano kati ya Marekani na Afrika’ (US Africa Summit).
Tukiweka kando maelezo ya kisiasa au kidiplomasia kuhusu mkutano huo, lengo halisi lilikuwa kupromoti uwekezaji wa kibiashara wa Marekani barani Afrika.
Kwa hiyo kimsingi, tukio hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kwa Wamarekani kuliko Waafrika, kwani laiti yaliyoafikiwa yakitimia, basi wao ndio watakaonufaika zaidi.
Lakini kabla ya kujadili kwa undani kuhusu mkutano huo ni vema kuangalia mambo mawili ya msingi. Kwanza, mkutano huo unashabihiana na tukio kubwa la kihistoria lililotokea miaka 130 iliyopita huko Berlin, Ujerumani.
Ninarejea ‘Mkutano wa Berlin’ (The Berlin Conference) kati ya mwaka 1884 na 1885. Mkutano huo uliligawanya Bara letu miongoni mwa mataifa ya Magharibi na hatimaye kutuletea ukoloni.
Tofauti ya msingi kati ya Berlin Conference na US Africa Summit ni kwamba wakati huo wa kwanza uliwakutanisha ‘wakoloni watarajiwa’ pekee, huu wa wiki iliyopita umewahusisha watawala wa Afrika.
Kufanana kwa mikutano hiyo miwili ya kihistoria kupo katika ukweli kwamba yote ililenga kuchuma rasilimali za Bara letu, japo Berlin Conference ilikuwa ni kwa manufaa ya wakoloni pekee ilhali huu wa Marekani unaelezwa kuwa utalinufaisha Bara la Afrika pia (angalau kwa mujibu wa maelezo ya Wamarekani na watawala wetu).
Pili, moja ya sababu kubwa zilizofanya Marekani kuitisha mkutano huo ni kukabiliana na kasi ya China kutumia fursa mbalimbali zilizopo barani Afrika. Mataifa yote hayo mawili, China na Marekani, yanaongoza kiuchumi duniani, na kwa kutambua ‘urahisi wa kuvuna utajiri’ kutoka Afrika ambao kwa lugha ya kistaarabu unaitwa uwekezaji, imekuwa muhimu kwao ‘kuwaweka karibu’ watawala wetu ili kunufaika na utajiri mkubwa tuliojaliwa kuwa nao japo hatuutumii ipasavyo.
Kwa upande mwingine, mkutano huo kati ya Marekani na Afrika unawaweka watawala wetu katika wakati mgumu wa kuchagua ‘nani wa kumtumainia’ wakati wa shida (na kimsingi shida ni sehemu ya maisha ya kawaida katika bara letu: umasikini, maradhi, nk).
Wakati China inafahamika kwa kuweka mbele maslahi yake ya kiuchumi pasi kujali masuala muhimu kama utawala bora na haki za binadamu, Marekani imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha masuala hayo mawili (japo tafsiri halisi yaweza kuleta maana tofauti, mifano hai ikiwa ni pamoja na sapoti yake kwa Israel dhidi ya Palestina na ‘majanga’ iliyosababisha huko Iraki, Afghanistan na Libya).
Pengine ni kwa kutambua kuwa China haina muda na masuala ya haki za binadamu na utawala bora, Rais Barack Obama ameonekana kutoyapa kipaumbele masuala hayo.
Lakini kwa kuangalia sera za nje za Marekani ni rahisi kutambua kwamba taifa hilo linafahamu bayana kwamba litapoteza ‘marafiki wengi’ kwa maana ya watawala wetu likiwekea mkazo ajenda hizo hasa ikizingatiwa kuwa tawala nyingi za Afrika ‘zina uhasama wa muda mrefu’ na haki za binadamu na utawala bora.
Lakini wakati Obama na watawala wetu wanausifia mkutano huo kama fursa ya ‘kuikuza Afrika,’ baadhi ya wachambuzi wanaonya kwamba huo ni mwendelezo wa sera zilezile zilizochangia kulifikisha Bara letu hapa tulipo: mafukara wa kupindukia licha ya utajiri mkubwa tulionao, ambao sana unawanufaisha watawala wetu na washiriki wao.
“Angalia waliopo mezani kuelewa kinachoendelea: baadhi ya watawala wa Afrika wenye rekodi mbaya kabisa wakiwa pamoja na waandamizi wa makampuni makubwa ya Marekani,” anaeleza Emira Woods, mtaalam wa sera za nje za Marekani.
Ni vigumu kuikuza Afrika kwa ushirikiano kati ya watu walewale wanaokwaza maendeleo yake – baadhi ya watawala katika Bara hilo wanaoendekeza rushwa na kusigina haki za binadamu – na makampuni makubwa ya kimataifa ambayo baadhi yake yana rekodi chafu linapokuja suala la kusaka faida, na yanathibitisha kauli ya Marehemu Baba wa Taifa kuwa ‘ubepari ni unyama’ (kwa maana ya kujali faida kuliko utu).
Mwandishi mmoja wa Jarida la Foreign Policy anabainisha kwamba kimsingi mkutano huo wa Marekani na Afrika ni marudio ya tukio la kihistoria linalofahamika kama ‘Scramble for Africa,’ ambapo mataifa ya Magharibi yalikuwa ‘yakifukuzana’ kuja kuchuma raslimali katika Bara hilo.
Anaeleza kwamba mkutano huo umefungua milango kwa Marekani kwenda kuvuna mafuta na madini barani Afrika na kupata soko la bidhaa zake.
Hivi msomaji, unafahamu kwamba sentensi iliyopita ndiyo inafanana kabisa na sababu kuu mbili za ujio wa ukoloni barani Afrika: kupata fursa za rasilimali kwa ajili ya mahitaji ya viwanda katika nchi za wakoloni na masoko ya bidhaa za viwanda vyao?
Licha ya Wamarekani wenyewe, inaelezwa kuwa wanufaika wakubwa wa mkutano huo ni tabaka tawala barani Afrika ambalo kwa namna moja au nyingine litatumia fursa hizo za uwekezaji wa Wamarekani kujinufaisha wao wenyewe na washirika wao, na hiyo inatajwa kama moja ya sababu kubwa za watawala wetu kuuona mkutano huo kama ‘fursa muhimu kwa Afrika.’
Lakini kama kuna mtu aliyeelezea vema kuhusu mkutano huo ni mfanyabiashara tajiri wa Kiafrika, Mo Ibrahim. Kauli yake yaweza kuwafanya watawala wetu waliokusanywa na Obama huko Marekani waone aibu.
Anasema Mo Ibrahim,
“Popote uendapo barani Afrika kuna wafanyabiashara wa Kichina, kuna wafanyabiashara wa Kibrazili. Hakuna miongoni mwetu (Waafrika) aliyekwenda Brazil au India au China kuwaambiwa waje wawekeze Afrika. Walijibidiisha wenyewe na wakaja kuwekeza.  Kwanini sasa tuje kuwashawishi ‘Wamarekani wenye umbumbumbu kuhusu bara la Afrika’? Nyie (Wamarekani) ndio mliovumbua Google (tovuti ya kutafuta habari kupitia mtandao wa kompyuta), kwanini msiitumie?”
Afrika tuliyonayo si ile iliyokuwa na jeuri ya kumtimua mkoloni. Yayumkinika kubashiri kuwa laiti tungekuwa na akina Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na wenzake wenye msimamo kama Kenneth Kaunda, Samora Machel, na kadhalika, wangemwambia bayana Obama aje yeye Afrika na si kukusanya viongozi wetu kama kundi la wanafunzi waliopewa  nafasi za masomo nchi za nje.
Naam, kama Wamarekani ni kama mtu anayetaka kuchumbia, sharti yeye aende nyumbani kwa anayetaka kumchumbia. Lakini viongozi wa kizazi hiki hawajali ‘kuuza utu/Uafrika wao’ alimradi kuna ‘faida za uwekezaji’.
Mo anaukosoa mkutano huo katika maeneo makuu mawili: kwanza, ‘jeuri’ ya Obama kukataa mikutano na viongozi mmoja mmoja (bilateral meetings)  licha ya wito kutoka Nigeria, Kenya na Afrika Kusini, na pili, ukweli kwamba  Obama amebakiwa na miaka miwili tu ya urais wake wa Marekani, na hivyo pengine mikakati yake ya ‘kuisaidia’ Afrika ikaishia njiani baada ya yeye kutoka madarakani mwaka 2016.
Sidhani kama mkutano huu utakuwa na manufaa yoyote ya maana kwa mamilioni ya walalahoi wa Afrika. Wakati Rais Kikwete akieleza katika mkutano huo  kuwa moja ya sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo makubwa zaidi na ya haraka zaidi ya Afrika ni uzalishaji mdogo na matumizi ya chini mno ya umeme, ukweli wa wazi ni kwamba kikwazo kikubwa ni rushwa inayozidi kuota mizizi na kutapakaa, sambamba na kupuuzia utawala bora na haki za binadamu.
Ni muhimu kwa Kikwete na viongozi wengine wa Afrika kutambua kuwa maendeleo ya kweli katika nchi zao hayataletwa na Wamarekani au Wachina bali wananchi wenyewe. Laiti watawala wetu wangewekeza nguvu katika kuwawezesha wawekezaji wa ndani badala ya kutarajia miujiza kutoka kwa wawekezaji wa nje basi kwa hakika wasingekusanywa na Obama huko Washington DC. Angewafuata kuwaomba nchi yake ipatiwe nafasi za uwekezaji.
Nimalizie makala hii kwa kupongeza uamuzi wa busara wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kufikia hoteli yenye gharama nafuu wakati wa mkutano huo kati ya Marekani na Afrika. Uhuru alifikia hoteli ya JW Warriot inayotoza Dola za Kimarekani 339 (takriban sh 560,000) kwa usiku mmoja. Kadhalika, aliwaagiza maafisa alioambatana nao katika msafara wake kuweka makazi katika hoteli za gharama nafuu. 
Sina taarifa kuhusu hoteli aliyofikia Rais wetu Kikwete ila ninachofahamu ni kuwa aliambatana na msafara mkubwa (siku hizi hawaoni umuhimu wa kutufahamisha akina nani wanaambatana na Rais katika ziara zake mfululizo nje ya nchi).0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube