10 Apr 2015NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kwa makala zangu ‘kupotea’ kwa wiki mbili mfululizo. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.
Pia ningependa kutoa salamu za pole na rambirambi kwa ndugu zetu wa Kenya kufuatia shambulio kubwa la kigaidi lililotokea huko Garissa na kuuwa watu kadhaa.Ugaidi umeendelea kuwa moja ya matishio makubwa kwa usalama wa binadamu.
Wakati tukiungana na majirani zetu wa Kenya katika kipindi hiki kigumu, kuna dalili na sababu kadhaa za kiintelijensia na kimazingira zinazonipa wasiwasi kwamba Tanzania yetu inaweza kukumbwa na shambulio la kigaidi huko mbeleni (Mola aepushie). Hapa chini, ninabainisha dalili/ sababu hizo.
Tukio la ugaidi Garissa, nchini Kenya:
Wiki iliyopita, magaidi wa Al-Shabaab walifanya shambulio kubwa la ugaidi katika mji wa Garissa, uliopo mpakani mwa Kenya na Somalia.Shambulio hilo limepelekea vifo vya watu takriban 150 huku taarifa mbalimbali zikionyesha uwezekano wa kuwepo idadi kubwa zaidi ya waliouawa.
Awali, nilikuwa upande wa watetezi wa serikali ya Kenya na vyombo vya usalama vya nchi hiyo katika lawama kwamba walizembea kuchukua tahadhari. Hoja yangu kuu ilikuwa kwamba kupewa taarifa kuhusu ugaidi ni kitu kimoja, kuweza kuzifanyia kazi taarifa hizo na kuweza kuzuwia ugaidi ni kitu kingine kabisa.
Hata hivyo, utetezi huo umepungua baada ya kupatikana taarifa mbalimbali zinazoashiria mapungufu makubwa ya serikali ya Kenya na taasisi za Usalama nchini humo kukabiliana na tetesi walizopewa kuhusu uwezekano wa shambulio hilo la kigaidi.
Tukiweka kando kilichojiri nchini Kenya lakini tukitilia maanani ukweli kuwa nchi hiyo ilitahadharishwa kabla ya tukio hilo, kwa Tanzania hali ni tofauti. Hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya uwezekano wa kutokea shambulio la ugaidi.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa Kenya ina ushirikiano mkubwa zaidi na taasisi za kiusalama za mataifa makubwa zaidi ya Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa Marekani, kwa mfano, ina kituo chake cha kijeshi nchini humo (Manda Bay)
Kwa maana hiyo, tahadhari ya Wamarekani kwa Kenya sio tu kwa maslahi ya Kenya bali ya Wamarekani pia.
Hitimisho: Kwa kufanikiwa kufanya shambulio kubwa kabisa nchi Kenya, ikiwa ni takriban mwaka na nusu baada ya kufanya shambulio jingine la ugaidi kwenye supamaketi ya Westgate jijini Nairobi, magaidi wa Al-Qaeda wanaweza kushawishika kupanua kampeni yao ya uharamia hadi Uganda (ambako tayari kuna tishio kama ninavyoeleza hapo chini) na hata Tanzania (kwa sababu nitazobainisha mbeleni katika makala hii)
Uwezekano wa shambulio la kigaidi Uganda:
Machi 25 mwaka huu, Marekani ilitoa tahadhari kwa Uganda kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi nchini humo. Kama ilivyo kwa Kenya, Marekani ina maslahi yake nchini Uganda ambako inarusha ndege zake za upelelezi (PC 12) kutoka Entebbe, Kwa hiyo usalama kwa Uganda una maslahi kwa Marekani pia.
Hitimisho: Iwapo Al-Shabaab watafanikiwa kutimiza uovu wao kuishambulia Uganda (Mungu aepushe hili), wanaweza kupata motisha wa kutanua zaidi kampeni yao hadi Tanzania hasa kwa kuzingatia kuwa kundi hilo la kigaidi linaziona nchi hizi tatu kama kikwazo kikubwa kwa uhai wake.
Shaka ya ugaidi nchini Tanzania:
Moja ya matatizo makubwa ya kufahamu ukubwa au udogo wa tishio la ugaidi nchini Tanzania ni siasa. Kwa muda mrefu, chama tawala CCM kimekuwa kikiutumia ugaidi kama kisingizio cha kudhibiti vyama vya upinzani na baadhi ya viongozi wake. Kwa minajili hiyo, hata serikali ikitoa taarifa sahihi kuhusu uwezekano wa tishio la ugaidi, kuna uwezekano wa wananchi wengi kudhani hiyo ni siasa tu.
Kana kwamba hiyo haitoshi, mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge hapo Oktoba. Japo haijazoeleka sana, historia inaonyesha kuwa angalau katika uchaguzi mkuu mmoja uliopita zilisikika taarifa za 'tishio la usalama' kutoka kwa nchi jirani. Mbinu hii hutumiwa na vyama tawala kujenga hofu ya kiusalama kwa wapigakura, na kuwaunganisha chini ya mwavuli wa chama kilichopo madarakani. Kwa mantiki hiyo, iwapo kutakuwa na taarifa za tishio la ugaidi, yayumkinika kuhisi baadhi ya wananchi wakatafrisi kuwa ni mbinu tu ya CCM kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Lakini tatizo kubwa zaidi kwa sasa ni imani ndogo ya wananchi kwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete na nyingi ya taasisi za serikali yake. Uhaba huo wa imani unatokana na mchanganyiko wa hisia za ushahidi wa matukio yaliyopita. Kutokana na kuandamwa mno na kashfa za ufisadi, kumeanza kujengeka imani miongoni mwa Watanzania kuwa serikali yao ni ya kifisadi pia.
Matumizi mabaya ya 'taarifa za kiintelijensia' yamewafanya Watanzania wengi kuwa na hisia kuwa 'taarifa za intelijensia' ni mbinu ya serikali kuwadhibiti. Mara kadhaa, Jeshi la Polisi limekuwa likipiga marufuku maandamano ya kisiasa au kijamii kwa kisingizio cha 'taarifa za kiintelijensia'.
Hivi karibuni, zilipatikana taarifa za mapigano makali kati ya jeshi la polisi wakishirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya 'magaidi' kwenye mapango ya Amboni mjini Tanga. Mchanganyiko wa taarifa za kukanganya na imani haba ya wananchi kwa jeshi hilo vilipelekea tukio hilo kuonekana kama 'mchezo wa kuigiza'.
Lakini licha ya kasoro hizo zinazoihusu serikali na taasisi zake, kuna tatizo jingine linalohusu vyombo vya habari vya nchini. Utitiri wa magazeti ya udaku na uhaba wa uandishi wa kiuchunguzi katika 'magazeti makini' umekuwa ukichangia mkanganyiko katika kubaini ukweli na porojo. Mfano mzuri ni tukio hilo la Amboni ambalo kwa kiasi flani liligeuka kama mfululizo 'series' ya mchezo wa kuigiza, huku magazeti ya udaku yakiwa na 'habari' nyingi zaidi ya 'magazeti makini.'
Hali hiyo yaweza kuwa inachangiwa na mahusiano hafifu kati ya taasisi za dola na vyombo vya habari, sambamba na mazoea ya taasisi hizo kutoa tu taarifa pasipo kuruhusu maswali kutoka kwa wanahabari. Ukosefu wa taarifa sahihi, sambamba na ugumu wa kupata taarifa hizo huchangia 'udaku' kuziba ombwe husika.
Tukiweka kando kasoro hizo hapo juu, hadi sasa kuna mambo yafuatayo ambayo yanaweza kuwashawishi magaidi kuvamia Tanzania.
1. Mgogoro wa muda mrefu kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi
Japo hadi muda huu suala hili limeendelea kuwagawa Watanzania kwa njia za mijadala na kwa amani, yayumkinika kuhisi kuwa magaidi wanaweza kulitumia kama kisingizio cha kuishambulia Tanzania.
Cha kutia hofu ni ukweli kwamba si tu suala hili limedumu kwa muda mrefu, hasa baada ya chama tawala CCM kuahidi katika ilani yake ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2005 kuwa itaanzisha mahakama hiyo lakini imeshindwa kufanya hivyo hadi leo, bali pia uamuzi usio wa busara wa kuupeleka bungeni Muswada wa Uanzishwaji Mahakama ya Kadhi kisha kuuondoa.
Kana kwamba hiyo haitoshi, majuzi Rais Kikwete alikaririwa akidai kuwa serikali haina mpango wa kuanzisha mahakama hiyo, na badala yake jukumu hilo linabaki kwa Waislamu wenyewe. Haihitaji uelewa wa sheria kujiuliza kwamba kama suala hilo lilikuwa la Waislamu wenyewe, lilipelekwa bungeni kwa minajili gani?
Licha ya mjadala huo wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kuendelea kwa amani, mjadala kuhusu suala hilo umewagawa viongozi wa dini (Wakristo na Waislamu) na kwa kiasi flani umerejesha mgogoro kati ya baadhi ya viongozi wa Kiislam na serikali, sambamba na kuleta sintofahamu miongoni mwa baadhi ya wanasiasa.
Yayumkinika kuhisi kuwa magaidi wanaweza kutumia ‘mgogoro’ huo kama kisingizio cha kufanya uovu wao. Na hii ni juu ya malalamiko ya muda mrefu kuwa Waislam wamekuwa wakibaguliwa na serikali huku Wakristo wakionekana kupendelewa. Uzoefu unaonyesha kuwa vikundi vya kigaidi vya kimataifa vina kasumba ya kuteka hoja za ndani ya nchi na kuigeuza yao, kwa kisingizio cha kupigania Uislam.
2. Vitisho bayana kutoka kwa watu wanaodai ni magaidi.
Hivi karibuni ilipatikana video huko nyumbani ambapo mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kaisi Bin Abdallah alidai kuwa kundi lao limekuwa na mafanikio katika ugaidi wa kudhuru polisi na vituo vya polisi.
Licha ya 'mapungufu kadhaa' katika video hiyo, ambayo yanaweza kutupa imani kuwa ni porojo tu, yawezekana tishio lililo kwenye video hiyo ni la kweli. Na hili ni moja ya matatizo ya kukabiliana na tishio la ugaidi: kuchukulia taarifa kuwa ni za kweli au za kupuuza.
Hofu kuhusu uwezekano wa matukio ya ugaidi nchini Tanzania ilithibitishwa na kauli ya hivi karibuni ya Rais Kikwete kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini humo yana uhusiano na ugaidi, japo hakubainisha iwapo kuna uhusika wa makundi ya kigaidi ya kimataifa au la.
3. Taarifa za kimataifa:
Hadi muda huu hakuna taarifa za moja kwa moja zinazoashiria uwezekano wa tukio la ugaidi nchini Tanzania. Hata hivyo, bado kuna hali ya tahadhari ya wastani kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi.
Wakati serikali ya Canada inaeleza kuwa haina 'ushauri unaohusu taifa (Tanzania) zima, inawashauri raia wake kuchukua tahadhari kubwa kuhusiana na ugaidi.
Kwa upande wake, serikali ya Uingereza inatoa angalizo la jumla tu japo inatahadharisha kuhusu tishio la ugaidi wa Al-Shabaab kwa eneo la Afrika Mashariki (ikiwa ni pamoja na Tanzania). Serikali ya Marekani inatoa ushauri wa jumla tu kwa kurejea matukio ya uvunjifu wa amani huko nyuma.
Hata hivyo, ripoti iliyotolewa Jumamosi iliyopita na taasisi ya HTH Worldwide kuhusu ‘hatari’ (risks) zinazoikabili Tanzania, ugaidi unatajwa kuwa ni tishio la kuaminika, japo uwezekano wa kutokea shambulizi la ugaidi ni wa wastani.
Pengine taarifa ya kuogofya zaidi ni ile iliyobainisha uwepo wa jitihada za kundi la kigaidi la ISIS kutaka kujiimarisha katika eneo la Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ISIS inajaribu kujenga ushirikiano na Al-Shabaab kwa minajili ya kuwa na influence katika eneo la Afrika Mashariki.
Taarifa zaidi za kiintelijensia zinabainisha uwepo wa kikundi cha Al-Hijra nchini Tanzania, ambacho kinatajwa kama ‘tawi’ la Al-Shabaab nchini Kenya. Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikundi hicho kinakadiriwa kuwa na wafuasi takriban 1,000.
Inaelezwa kuwa kikundi hicho kinafadhiliwa na Waislamu wa nje wa madhehebu ya Wasalafi (Salafist). Habari zaidi zinabainisha kuwa malengo ya kikundi hicho ni kuanzisha jihadi nchini Kenya na Tanzania. Uwepo wa kikundi hicho unadaiwa kusaidiwa na kikundi kingine cha Al-Muhajiroun ambacho kinatajwa kuwa na mahusiano na kikundi kingine cha kigaidi cha Al-Qaeda.
Kadhalika, majuzi zimepatikana taarifa kutoka Kenya kuhusu mwanamke mmoja wa Kitanzania aliyekamatwa na wenzie wawili Wakenya wakijaribu kwenda Somalia kuwa wenza wa magaidi wa Al-Shabaab.
Tukio hilo linaakisi kinachotokea katika nchi mbalimbali za huku Magharibi ambapo mabinti kadhaa wamekuwa wakitorokea Syria kwenda kuwa 'wenza' wa magaidi wa ISIS.
Vilevile, taarifa zilizopatikana muda mfupi kabla sijaandika makala hii zinaeleza kuwa mmoja wa wahusika wa shambulio hilo la kigaidi nchini Kenya ni Mtanzania. Haihitaji uelewa mkubwa wa intelijensia kutambua kuwa kama baadhi ya Watanzania wenzetu wanaweza kwenda kufanya ugaidi nje ya nchi, wanaweza pia kufanya ugaidi ndani ya nchi.
Hitimisho:
Ni vigumu kwa kuwa na hakika ya asilimia 100 iwapo magaidi watafanya shambulio au la. Kwa upande mmoja, magaidi wana muda wote wanaohitaji kabla ya kutimiza azma yao, yaani wanaweza kusubiri kwa muda mrefu, ilhali vyombo vya dola havina faida hiyo kwani vinatakiwa kuwa makini muda wote.
Kuna msemo maarufu kuhusu ugaidi, kwamba wakati magaidi wanahitaji DAKIKA MOJA TU kutimiza uovu wao, vyombo vya usalama vinahitaji KILA SEKUNDE YA DAKIKA kuwazuia magaidi husika.
Na japo uwepo wa taarifa za uhakika kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi unaweza kusaidia jitihada za kukabiliana na magaidi husika, ukweli mchungu ni kwamba, kuwa na taarifa ni kitu kimoja, uwezo wa kuzitumia taarifa hizo ni kitu kingine.
Wakati huu tunaungana na wenzetu wa Kenya kulaani unyama wa Al-Shabaab, ni muhimu kuchukua tahadhari mahususi ili kuweza kukabiliana na uwezekano wa magaidi hao kushambulia Tanzania.
La muhimu zaidi ni umoja na mshikamano, ambao kwa hakika unapotea kwa kasi, na haja ya haraka kwa serikali kurejejesha imani ya wananchi kwake. Kingine ni umuhimu wa kuweka kando siasa katika masuala nyeti kama haya..
Kubwa zaidi ya yote ni la kitaalamu zaidi. Wakati serikali ya Tanzania imekuwa ikitegemea zaidi misaada ya kimataifa katika kuiimarisha kiuwezo Idara ya Usalama wa Taifa, ni muhimu jitihada za ndani pia zielekezwe katika kuijengea uwezo wa kukabiliana na matishio mbalimbali ya usalama wa taifa letu, ikiwa ni pamoja na hilo la ugaidi.
Kwa uelewa wangu, uwezo wa vitengo vya kuzuwia ugaidi na kitengo cha kupambana na ujasusi unaathiriwa na mapungufu ya kimfumo na kisera, sambamba na nafasi ya maafisa wa Idara hiyo kwenye balozi mbalimbali za Tanzania nje ya nchi 'kubweteka' na hisia ya teuzi zinazodaiwa kufanywa kwa misingi ya undugu, urafiki au kujuana.
Lakini changamoto kubwa zaidi kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ni kurejesha imani kwa Watanzania. Nimeshawahi kuandika mara kadhaa kwamba kushamiri kwa ufisadi huko nyumbani kunachangiwa na udhaifu wa taasisi hiyo nyeti.
Zama za Idara hiyo ‘kuogopwa’ zimegeuka na kwa kiasi kikubwa taasisi hiyo, ambayo moja ya mafanikio yake makubwa huko nyuma yalikuwa kusimama imara dhidi ya njama na hujuma za utawala wa Makaburu, kwa sasa inaonekana kama sehemu ya mfumo wa kifisadi. Ili Idara yetu ya Usalama wa Taifa iweze kukabiliana na tishio hili la ugaidi inabidi iaminike kwa wananchi.
Mwisho, tishio hili la ugaidi sio la kufikirika. Lipo, na kwa bahati mbaya, mazingira ya kulirutubisha yapo pia. Japo si rahisi kuzuia ugaidi kwa asilimia 100, mikakati madhubuti ya kiintelijensia hususani katika kukabili ugaidi (counterterrorism) inaweza kuwakwaza magaidi kufikiria kuivamia nchi yetu

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube