10 Oct 2015

HATIMAYE tumebakiwa na takriban wiki mbili tu kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika hapo Oktoba 25. Wakati kampeni hizo zikielekea ukingoni, matukio mawili makubwa yamejitokeza Jumapili iliyopita.
Tukio la kwanza ni kifo cha mwanasiasa nguli, Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila. Tukio jingine lililotokea siku hiyo hiyo ni uamuzi wa mwanzilishi wa CCM na TANU, na mkongwe wa siasa za Tanzania, Kingunge Ngombale Mwiru. Nimeona ni vema kuyajadili matukio haya kwa sababu yote yanahusiana na Uchaguzi Mkuu, kwa namna moja au nyingine.
Tuanze na hilo la pili. Kwanza, tangazo la Kingunge kujiondoa uanachama wa CCM lilistahili liwe na mvuto mkubwa kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipotangaza kung’atuka. Lakini ukweli ‘mchungu’ ni kwamba tukio hilo limeonekana kama mwanachama wa kawaida tu wa CCM kuamua kujiondoa katika chama hicho.
Lakini, pili, uamuzi wa Kingunge kujiondoa CCM, haukuwa jambo la kushtua, kwa vile kwa muda mrefu sasa, kada huyo, rafiki wa karibu wa Baba wa Taifa, alikwishajitambulisha yupo upande gani katika siasa za uchaguzi. Kingunge, alipigana kwa hali na mali kuhakikisha mgombea ‘ chaguo lake,’ Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anashinda katika mchujo wa chama hicho tawala kupata mgombea wake.
Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa laiti busara ingemwongoza mzee huyo – hasa ikzingatiwa kuwa katika mila zetu za Kiafrika, wazee hutazamwa kama ‘visima’ vya busara na hekima – basi asingejiweka upande wa mgombea fulani au hata kama angefanya hivyo, licha ya kuwa ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba, basi labda angefanya kwa usiri.
 Nilitahadharisha hivyo kwa sababu, kwa kuegemea upande mmoja ilhali kuna pande nyingi katika jambo husika kuna matokeo ya aina mbili, kuwa sahihi au kukosea. Sasa, kama matokeo ya kuwa sahihi ni kudumisha hadhi na kukosea ni kupoteza hadhi, kila mwenye busara anatarajiwa kuwa makini katika jambo hilo.
Kitendo cha Kingunge kumuunga mkono Lowassa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, na hatimaye jina la kada huyo kukatwa katika mchujo, ilikuwa na athari kwa hadhi ya Kingunge kama mkongwe wa siasa. Bila kujali kuwa Lowassa alionewa au alistahili kukatwa, ukweli tu kwamba hakupitishwa ni sawa na kufeli kwa waliokuwa wakimuunga mkono, ikiwa ni pamoja na Kingunge.
Niliposoma tamko lake la kujiengua CCM nilibakiwa na maswali kadhaa, kubwa likiwa “...hivi huyu ndiye Kingunge yule yule wa zama za Nyerere au huyu ni toleo jipya? Na pengine bila hata kwenda mbali sana na kurejea zama za Nyerere, Kingunge huyu huyu alikuwa mstari wa mbele katika kampeni zilizomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2005. Yeye ni sehemu muhimu ya takriban kila analolaumu kuhusu CCM.
Matarajio ya wengi kwa Kingunge yalikuwa angekuwa mrithi wa Baba wa Taifa, si kwa sababu ya umri wake tu bali uumini wake katika Itikadi ya Ujamaa. Kingunge alikaa kimya wakati nguzo kuu ya itikadi hiyo, Azimio la Arusha ikizikwa katika kile kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar. Kada huyo licha ya kuwa kimya katika masuala mbalimbali yanayoifanya CCM kupoteza umaarufu, hususan suala la ufisadi, alijitokeza kuwa mtetezi mkubwa wa watu waliotuhumiwa katika orodha maarufu ya watu waliotuhumiwa na Chadema kuwa ndio ‘mapapa wa ufisadi,’ iliyojulikana kama ‘List of Shame.’
Kimsingi, Kingunge aliwananga Chadema na kuwaita waongo, wazushi na wanafiki, wanaosema uongo na hakuna ushahidi, hakuna kiongozi fisadi. Leo hii, mwanasiasa anayeamini kuwa ndio chaguo sahihi kuingoza Tanzania, yaani Lowassa, kajiunga na waongo, wazushi, na wanafiki hao.
Kingunge ni mwathirika wa makosa yake mwenyewe kimkakati. Alipaswa tangu awali, achague kuwa mtetezi wa wananchi kama Baba wa Taifa, au mtetezi wa tabaka tawala. Japo ninatambua madhara ya kuwa mtetezi wa wananchi, kwa maana ya kutengeneza maadui wengi kisiasa, lakini ukweli usiopingika ni kwamba heshima na hadhi ya mtu wa aina hiyo hudumu milele. Tunawakumbuka akina Nyerere na Sokoine si kwa vile tu walikuwa viongozi wetu bali kwa sababu walisimama upande wa wananchi tulio wengi kuliko kulinda tabaka la watawala walio wachache.
Katika hitimisho langu baada ya kupokea taarifa za Kingunge kujiuzulu uanachama wa CCM, niliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Kingunge aliwahi kuwa kama Muhmmad Ali wa siasa za Tanzania. Lakini tangazo lake la kujiuzulu CCM leo ni kama Ali angetangaza sasa kuwa anajiuzulu masumbwi. Alikwikushajiuzulu miaka kadhaa iliyopita. Nilichomaanisha ni kuwa, umuhimu wa mkongwe huyo wa siasa za nchi yetu ulisha- expire (kwisha muda wa matumizi) kitambo, na kubaki au kuondoka kwake CCM hakukuwa na faida kwa yeyote zaidi yake mwenyewe. Ninamsikitikia kwa sababu alipaswa kukumbukwa kwa mazuri mengi ya zama za Nyerere lakini dalili ni kwamba ataishi kukumbukwa zaidi kwa jithada za kumbeba Lowassa kwa gharama ya hadhi yake.
Tukiweka hilo kando, taarifa za kifo cha Mchungaji Mtikila kimeonekana kuwashtua Watanzania wengi. Binafsi, nilipopata taarifa hizo, kwanza nilidhani ni utani tu, lakini nilipogundua kuwa zina ukweli, hisia zangu zikaanza kupatwa na wasiwasi fulani.
Wakati tayari kuna taarifa zisizo rasmi mbalimbali zinazosambaa kwa kasi mtandaoni kuhusu chanzo halisi cha kifo cha Mchungaji Mtikila, licha ya taarifa za polisi kuwa chanzo cha ajali iliyosababisha kifo chake ni mwendo kasi wa gari alilokuwa akitumia huku akiwa hajavaa mkanda wa kiti cha gari, ukweli kwamba mwanasiasa huyo machachari alikuwa na ‘mabomu’ kuhusu mmoja wa wagombea urais, ilitosha kuniongezea wasiwasi huo.
Ni muhimu, katika hatua hii kukumbushia kuwa miongoni mwa sababu za umaarufu wa Mtikila ni kile ambacho wengi walikitafsiri kama ‘conspiracy theories,’ yaani hoja zinazoonyesha kubeba ukweli, zikiambatana na aina fulani ya ushahidi, lakini zinabaki vigumu kuzithibitisha.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa mtandaoni, Mtikila alikuwa akijipanga kuzuia ugombea wa mmoja wa wagombea urais, kwa hoja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madai yake kuwa mgombea huyo ni sehemu ya mkakati wa kimataifa kuihujumu nchi yetu. Kadhalika, Mchungaji huyo alinukuliwa akiongea kwenye kituo kimoja cha televisheni huko nyumbani (Tanzania) akisisitiza kwa nini anaamini mgombea huyo ni janga kwa taifa.
Sasa, japo kifo ni mapenzi ya Mola, lakini katika mazingira ya kawaida tu, kama anajitokeza mtu kumpinga mwanasiasa hadharani huku akipania kumwekea vikwazo katika safari yake ya Ikulu, kisha mtu huyo akafariki kwa ajali siku chache kabla ya uchaguzi, hisia za kibinadamu zinaweza kuhisi kuna namna hapo.
Kwa bahati mbaya, au pengine makusudi, jeshi la polisi limeonekana kuwa na haraka mno kutangaza chanzo cha ajali iliyosababisha kifo cha mwanasiasa huyo. Iwapo uchunguzi wa vyanzo vya ajali katika nchi zilizoendelea huchukua siku kadhaa licha ya taasisi zao za uchunguzi kuwa na nyezo za hali ya juu, iweje jeshi letu la polisi linalosifika kwa uchunguzi wa mwendo wa konokono lipate uwezo wa ghafla wa hali ya juu kuweza kutambua chanzo cha ajali hiyo siku moja tu baadaye?
Kwa mtizamo wangu, na ili kuwaridhisha Watanzania kuwa kifo cha mwanasiasa huyo hakina mkono wa mtu, polisi walipaswa kufanya uchunguzi wa kina, ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya uchunguzi wa kitabibu kuhusu chanzo cha ajali kabla ya kukurupuka na sababu ambazo ni rahisi kuhisi kuwa ni za kufikirika.
Kwa bahati mbaya, kifo cha Mtikila kilitokea siku moja na tukio la Kingunge kujivua uanachama wa CCM, suala lililosababisha baadhi ya watu kuyahusisha matukio hayo mawili. Pengine ni ‘coincidence’ tu lakini ni nadra kwa Tanzania yetu kukumbwa na matukio makubwa ya kisiasa ndani ya siku moja.
Nimalizie makala hii kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kufanya sala na dua kuombea Uchaguzi Mkuu ufanyike na kuhitimishwa kwa amani na usalama.
Kauli zinazoashiria kuchochea machafuko sio tu ziepukwe bali pia zikemewe vikali. 
Tukumbuke kuwa, wakati uchaguzi utafanyika na kupita, Tanzania yetu ni lazima ibaki kuwa nchi moja na yenye usalama kwa kila raia wake. Waingereza wanasema; there is life after election (maisha yetu yataendelea baada ya uchaguzi), kwa hiyo ni muhimu kutotumia fito za kujengea nchi yetu kuchapana wenyewe.
Mungu ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube