Showing posts with label KINGUNGE. Show all posts
Showing posts with label KINGUNGE. Show all posts

10 Oct 2015

HATIMAYE tumebakiwa na takriban wiki mbili tu kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika hapo Oktoba 25. Wakati kampeni hizo zikielekea ukingoni, matukio mawili makubwa yamejitokeza Jumapili iliyopita.
Tukio la kwanza ni kifo cha mwanasiasa nguli, Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila. Tukio jingine lililotokea siku hiyo hiyo ni uamuzi wa mwanzilishi wa CCM na TANU, na mkongwe wa siasa za Tanzania, Kingunge Ngombale Mwiru. Nimeona ni vema kuyajadili matukio haya kwa sababu yote yanahusiana na Uchaguzi Mkuu, kwa namna moja au nyingine.
Tuanze na hilo la pili. Kwanza, tangazo la Kingunge kujiondoa uanachama wa CCM lilistahili liwe na mvuto mkubwa kama Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipotangaza kung’atuka. Lakini ukweli ‘mchungu’ ni kwamba tukio hilo limeonekana kama mwanachama wa kawaida tu wa CCM kuamua kujiondoa katika chama hicho.
Lakini, pili, uamuzi wa Kingunge kujiondoa CCM, haukuwa jambo la kushtua, kwa vile kwa muda mrefu sasa, kada huyo, rafiki wa karibu wa Baba wa Taifa, alikwishajitambulisha yupo upande gani katika siasa za uchaguzi. Kingunge, alipigana kwa hali na mali kuhakikisha mgombea ‘ chaguo lake,’ Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anashinda katika mchujo wa chama hicho tawala kupata mgombea wake.
Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa laiti busara ingemwongoza mzee huyo – hasa ikzingatiwa kuwa katika mila zetu za Kiafrika, wazee hutazamwa kama ‘visima’ vya busara na hekima – basi asingejiweka upande wa mgombea fulani au hata kama angefanya hivyo, licha ya kuwa ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba, basi labda angefanya kwa usiri.
 Nilitahadharisha hivyo kwa sababu, kwa kuegemea upande mmoja ilhali kuna pande nyingi katika jambo husika kuna matokeo ya aina mbili, kuwa sahihi au kukosea. Sasa, kama matokeo ya kuwa sahihi ni kudumisha hadhi na kukosea ni kupoteza hadhi, kila mwenye busara anatarajiwa kuwa makini katika jambo hilo.
Kitendo cha Kingunge kumuunga mkono Lowassa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, na hatimaye jina la kada huyo kukatwa katika mchujo, ilikuwa na athari kwa hadhi ya Kingunge kama mkongwe wa siasa. Bila kujali kuwa Lowassa alionewa au alistahili kukatwa, ukweli tu kwamba hakupitishwa ni sawa na kufeli kwa waliokuwa wakimuunga mkono, ikiwa ni pamoja na Kingunge.
Niliposoma tamko lake la kujiengua CCM nilibakiwa na maswali kadhaa, kubwa likiwa “...hivi huyu ndiye Kingunge yule yule wa zama za Nyerere au huyu ni toleo jipya? Na pengine bila hata kwenda mbali sana na kurejea zama za Nyerere, Kingunge huyu huyu alikuwa mstari wa mbele katika kampeni zilizomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2005. Yeye ni sehemu muhimu ya takriban kila analolaumu kuhusu CCM.
Matarajio ya wengi kwa Kingunge yalikuwa angekuwa mrithi wa Baba wa Taifa, si kwa sababu ya umri wake tu bali uumini wake katika Itikadi ya Ujamaa. Kingunge alikaa kimya wakati nguzo kuu ya itikadi hiyo, Azimio la Arusha ikizikwa katika kile kinachofahamika kama Azimio la Zanzibar. Kada huyo licha ya kuwa kimya katika masuala mbalimbali yanayoifanya CCM kupoteza umaarufu, hususan suala la ufisadi, alijitokeza kuwa mtetezi mkubwa wa watu waliotuhumiwa katika orodha maarufu ya watu waliotuhumiwa na Chadema kuwa ndio ‘mapapa wa ufisadi,’ iliyojulikana kama ‘List of Shame.’
Kimsingi, Kingunge aliwananga Chadema na kuwaita waongo, wazushi na wanafiki, wanaosema uongo na hakuna ushahidi, hakuna kiongozi fisadi. Leo hii, mwanasiasa anayeamini kuwa ndio chaguo sahihi kuingoza Tanzania, yaani Lowassa, kajiunga na waongo, wazushi, na wanafiki hao.
Kingunge ni mwathirika wa makosa yake mwenyewe kimkakati. Alipaswa tangu awali, achague kuwa mtetezi wa wananchi kama Baba wa Taifa, au mtetezi wa tabaka tawala. Japo ninatambua madhara ya kuwa mtetezi wa wananchi, kwa maana ya kutengeneza maadui wengi kisiasa, lakini ukweli usiopingika ni kwamba heshima na hadhi ya mtu wa aina hiyo hudumu milele. Tunawakumbuka akina Nyerere na Sokoine si kwa vile tu walikuwa viongozi wetu bali kwa sababu walisimama upande wa wananchi tulio wengi kuliko kulinda tabaka la watawala walio wachache.
Katika hitimisho langu baada ya kupokea taarifa za Kingunge kujiuzulu uanachama wa CCM, niliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Kingunge aliwahi kuwa kama Muhmmad Ali wa siasa za Tanzania. Lakini tangazo lake la kujiuzulu CCM leo ni kama Ali angetangaza sasa kuwa anajiuzulu masumbwi. Alikwikushajiuzulu miaka kadhaa iliyopita. Nilichomaanisha ni kuwa, umuhimu wa mkongwe huyo wa siasa za nchi yetu ulisha- expire (kwisha muda wa matumizi) kitambo, na kubaki au kuondoka kwake CCM hakukuwa na faida kwa yeyote zaidi yake mwenyewe. Ninamsikitikia kwa sababu alipaswa kukumbukwa kwa mazuri mengi ya zama za Nyerere lakini dalili ni kwamba ataishi kukumbukwa zaidi kwa jithada za kumbeba Lowassa kwa gharama ya hadhi yake.
Tukiweka hilo kando, taarifa za kifo cha Mchungaji Mtikila kimeonekana kuwashtua Watanzania wengi. Binafsi, nilipopata taarifa hizo, kwanza nilidhani ni utani tu, lakini nilipogundua kuwa zina ukweli, hisia zangu zikaanza kupatwa na wasiwasi fulani.
Wakati tayari kuna taarifa zisizo rasmi mbalimbali zinazosambaa kwa kasi mtandaoni kuhusu chanzo halisi cha kifo cha Mchungaji Mtikila, licha ya taarifa za polisi kuwa chanzo cha ajali iliyosababisha kifo chake ni mwendo kasi wa gari alilokuwa akitumia huku akiwa hajavaa mkanda wa kiti cha gari, ukweli kwamba mwanasiasa huyo machachari alikuwa na ‘mabomu’ kuhusu mmoja wa wagombea urais, ilitosha kuniongezea wasiwasi huo.
Ni muhimu, katika hatua hii kukumbushia kuwa miongoni mwa sababu za umaarufu wa Mtikila ni kile ambacho wengi walikitafsiri kama ‘conspiracy theories,’ yaani hoja zinazoonyesha kubeba ukweli, zikiambatana na aina fulani ya ushahidi, lakini zinabaki vigumu kuzithibitisha.
Kwa mujibu wa taarifa zinazosambaa mtandaoni, Mtikila alikuwa akijipanga kuzuia ugombea wa mmoja wa wagombea urais, kwa hoja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na madai yake kuwa mgombea huyo ni sehemu ya mkakati wa kimataifa kuihujumu nchi yetu. Kadhalika, Mchungaji huyo alinukuliwa akiongea kwenye kituo kimoja cha televisheni huko nyumbani (Tanzania) akisisitiza kwa nini anaamini mgombea huyo ni janga kwa taifa.
Sasa, japo kifo ni mapenzi ya Mola, lakini katika mazingira ya kawaida tu, kama anajitokeza mtu kumpinga mwanasiasa hadharani huku akipania kumwekea vikwazo katika safari yake ya Ikulu, kisha mtu huyo akafariki kwa ajali siku chache kabla ya uchaguzi, hisia za kibinadamu zinaweza kuhisi kuna namna hapo.
Kwa bahati mbaya, au pengine makusudi, jeshi la polisi limeonekana kuwa na haraka mno kutangaza chanzo cha ajali iliyosababisha kifo cha mwanasiasa huyo. Iwapo uchunguzi wa vyanzo vya ajali katika nchi zilizoendelea huchukua siku kadhaa licha ya taasisi zao za uchunguzi kuwa na nyezo za hali ya juu, iweje jeshi letu la polisi linalosifika kwa uchunguzi wa mwendo wa konokono lipate uwezo wa ghafla wa hali ya juu kuweza kutambua chanzo cha ajali hiyo siku moja tu baadaye?
Kwa mtizamo wangu, na ili kuwaridhisha Watanzania kuwa kifo cha mwanasiasa huyo hakina mkono wa mtu, polisi walipaswa kufanya uchunguzi wa kina, ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya uchunguzi wa kitabibu kuhusu chanzo cha ajali kabla ya kukurupuka na sababu ambazo ni rahisi kuhisi kuwa ni za kufikirika.
Kwa bahati mbaya, kifo cha Mtikila kilitokea siku moja na tukio la Kingunge kujivua uanachama wa CCM, suala lililosababisha baadhi ya watu kuyahusisha matukio hayo mawili. Pengine ni ‘coincidence’ tu lakini ni nadra kwa Tanzania yetu kukumbwa na matukio makubwa ya kisiasa ndani ya siku moja.
Nimalizie makala hii kwa kuwasihi Watanzania wenzangu kufanya sala na dua kuombea Uchaguzi Mkuu ufanyike na kuhitimishwa kwa amani na usalama.
Kauli zinazoashiria kuchochea machafuko sio tu ziepukwe bali pia zikemewe vikali. 
Tukumbuke kuwa, wakati uchaguzi utafanyika na kupita, Tanzania yetu ni lazima ibaki kuwa nchi moja na yenye usalama kwa kila raia wake. Waingereza wanasema; there is life after election (maisha yetu yataendelea baada ya uchaguzi), kwa hiyo ni muhimu kutotumia fito za kujengea nchi yetu kuchapana wenyewe.
Mungu ibariki Tanzania

19 Aug 2010

I came across an article below in The Moscow Times of today (“Financial Investigator's Son Handles Cash for Aeroflot”) and thought it would be appropriate to rekindle the discussion on Nepotism in Tanzania we had with you a while ago, see my email of Aug. 11th herein under. Before that, in July this year, I made similar comments about the son of the former Russian prime minister {Mr. Mikhail Fradkov - now Head of the Russia’s Foreign Intelligence Service (SVR)}, Mr. Peter Fradkov, who is currently the deputy chairman of Vnesheconombank (Russia’s State Bank for Foreign Economic Relations) and also the deputy chairman of the African Coordinating Committee for Economic Cooperation with African Countries (AfroCom). See in the Aeroflot article mentioned above (read the yellow-shaded part below) on how other senior Russian government officials place their off-springs in honey places, a similar trend currently appearing in Tanzania, albeit at times we see off-springs of our officials involved in fraudulent crimes as you may read in the article below on the son (Tony) of CCM stalwart Kingunge Ngombale Mwiru (“Kingunge relative in the dock for forgery, 242 million/- theft”). As I wrote earlier, I don’t think putting kids and relatives of bigwigs in high places based on kinship only and not merit is a wise thing to do. Indeed, it is very dangerous and speaks a lot of the unhealthy political situation in a country as well as the existence of an incompetent and ineffective government .

Best regards,

Shaaban

Moscow, Russia

29 Jul 2009

(Picha kwa hisani ya MJENGWA)

Wenzetu wa huku Magharibi wanasifika kwa kuwajali watoto. Licha ya serikali zao kutunga sheria zenye kulenga kuzuia na kukomesha uonevu, unyanyasaji, ukatili na unyama mwingine dhidi ya watoto, kuna mlolongo wa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazojihusisha na suala hilo. Hiyo sio kusema watoto wote wako salama.Ni vigumu katika ubinadamu wetu kufanya kitu kiwe absolutely perfect.

Pamoja na sifa hiyo ni shutuma kwamba upendeleo huo wa hali ya juu kwa watoto unachangia “kuwaharibu” watoto hao. Yayumkinika kusema kwamba miongoni mwa time bombs katika jamii za Magharibi ni watoto wanaodekezwa kupita kiasi. Kama ilivyo kwenye nyanja nyingine, uhuru usipokuwa na mipaka unaweza kupelekea matokeo yasiyopendeza.Hatahivyo, katika hili, uzuri (kuwajali watoto) unazidi ubaya (kuwadekeza).

Ni katika minajili hiyo kunajitokeza hofu kwa baadhi ya watu kutoa misaada kwa watoto kwa kuhofia misaada hiyo inaweza kutafsiriwa tofauti. Hivi karibuni niliona kwenye runinga mtunzi mmoja wa vitabu akilalamikia utaratibu wa kufanyiwa background checks (uchunguzi wa kiusalama,kwa tafsiri isiyo rasmi) kila anapokwenda kwenye shule za watoto kuwasomea vitabu anavyotunga.Mtunzi huyo analalamika kwamba kitendo hicho kinamfanya ajisikie kama mhalifu licha ya ukweli amekuwa akijihusisha na usomaji vitabu kwa watoto kwa miaka kadhaa sasa. Mamlaka husika zinajitetea kwamba utaratibu huo unalenga kuwalinda watoto.

Zamani kidogo niliwahi kukutana na simulizi moja kwamba jamaa flani (mwanaume) alimwona mtoto wa kike anakaribia kuzama kwenye bwawa la kuogelea.Kwa huruma, akajitosa majini kumwokoa mtoto huyo ambaye kwa bahati mbaya chupi yake ilimvuka katika hekaheka hiyo ya kukaribia kuzama.Alipomwokoa na kumpeleka mtoto huyo kwa mama yake akapigwa swali la kutatanisha: “Chupi ya mtoto iko wapi?”Kabla hajatafakari jibu akatandikwa kigongo kingine, “Hivi lini mibaba kama wewe mtaacha kunyemelea watoto wetu kwenye sehemu za kuogelea huku mkisubiri wakumbwe na matatizo kisha muwatomasetomase kwa kisingizio cha kuwaokoa? Hebu nipe chupi ya mwanangu kabla sijakuripoti kwa polisi”.Sijui ungekuwa wewe ungefanyaje!

Tafiti zisizo rasmi zinadokeza kwamba wanaume wengi wamekuwa waoga kusaidia watoto, hususan wa kike, kwa kuhofia kwamba ukarimu na msaada wao usije kuwaingiza matatizoni kwa tuhuma za child molestation.

Nadhani kufikia hapa unajiuliza naelekea wapi! Well, nataka kuzungumzia namna mamlaka zetu zinavyowadekeza mafisadi, lakini nataka kwanza nikupe mifano ya kuiweka akili yako vema kabla hatujaivaa hoja ya ufisadi.Twende kwenye mfano mwingine. Katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya watu wanaoporwa na vibaka wameishia kupata vipigo kutoka kwa raia baada ya washirika wa kibaka aliyepora kupiga ukelele wa “mwiz,mwizi...” dhidi ya aliyeporwa.Na kama kanuni za mob justice zilivyozoeleka,hakuna muda wa kuhakiki iwapo aliyepigiwa ukelele ni kibaka halisi au victim.

Back to hoja kuhusu mafisadi. Inaelekea mamlaka husika huko nyumbani zimeamua kuwalinda mafisadi mithili jamii za Magharibi zinavyowalinda watoto dhidi ya suspected/potential/career child molesters.Na anayediriki kupiga kelele dhidi ya mafisadi anakumbana na yaleyale ya anayeporwa na kibaka na kisha kupigiwa ukelele wa “mwizi,mwizi...” na washirika wa kibaka mhusika, na kuishia kupewa kipigo cha haja katika mtindo wa mob justice.

Wachunga kondoo wa Bwana walipobaini kwamba kondoo wao wanakamuliwa hadi damu baada ya maziwa kumalizika miilini mwao wakaamua kuja na kinachoitwa roughly muongozo wa kanisa kuhusu elimu ya uraia hususan uchaguzi wa viongozi. Tuliyekuwa tukimwamini kuwa swahiba wa karibu wa Baba wa Taifa, Kingunge Ngombale Mwiru,akatuthibitishia his true colours kwa kuwakemea wachunga kondoo wa Bwana.Hata kama Kingunge aliasi Nyumba ya Bwana (tukiaminishwa kuwa ni matokeo ya kuamini Ujamaa kupitiliza hadi kuufanya kuwa dini yake) tunapaswa kumshangaa babu huyu ambaye hivi karibuni ameibuka kuwa mtetezi mahiri wa mafisadi. Gazeti la Taifa Letu limemnukuu mtumishi mmoja wa Mungu akim-describe Kingunge kama BABA WA TAIFA WA MAFISADI.

Walioliibia taifa kwa kununua mgodi wa Kiwira kwa bei ya kutupa kana kwamba wanachonunua ni kifusi wameishia sio tu kusafishwa bali kufidiwa kwa wizi wao. This is more than crazy! Yaani tunawafidia majambazi!?Tunalipeleka wapi taifa letu? Wakati hatujui hizo milioni kadhaa walizotumia kununulia mgodi huo walizitoa wapi (lakini kwa vile hawakuwa wafanyabiashara basi yayumkinika kuhisi ni fedha za kifisadi),tuna uhakika wa asilimia zaidi ya 1000 kwamba hayo mabilioni watakayolipwa kama “fidia za kutufisadi” ni fedha zangu, zako na zetu walalahoi,walalawima,walala kichwa-chini miguu-juu, na wanyonge wengineo.

Kinachosikitisha ni kwamba kuna waungwana wanalipwa mishahara minono kuzuia upuuzi wa namna hii lakini badala ya kutumia nguvu za kikatiba walizonazo kustopisha ujambazi wa aina hii, wanakuwa bize zaidi na wale wanaowasaidia (waungwana hao) kupiga kelele dhidi ya ufisadi na mafisadi. Kama hufahamu basi naomba nikujulishe kwamba shughuli ya hatari kabisa kwa Mtanzania ni kudiriki kukemea ufisadi.Utaandamwa,utatishwa,utafanywa ujione mhaini,na kufanyiwa kila anachopaswa kufanyiwa Osama bin Laden pindi akikamatwa!Na shughuli yenye uhakika wa kipato, heshima na ulinzi kuliko zote ni ufisadi. Correct me if I’m wrong!

Siku zote nimekuwa nafahamu kwamba kimbelembele changu (according to how those in the know describe it) dhidi ya mafisadi ni kujiingiza kwenye kundi la dead men walking. I know, you’re thinking I’m scared of my own shadow. Kwa vile hapa si mahala mwafaka kutoa ushuhuda wangu, then ni bora tuliache hilo kwa sasa. Hata hivyo, naamini kwa nguvu zote kwamba ukimya sio suluhisho la matatizo yetu. Silence is not an option at all.

Kinachonisikitisha zaidi ni namna baadhi ya wenzetu wenye nguvu, uwezo na sababu wanapokosa nia au ujasiri wa kuendeleza kelele hizi. Inasikitisha zaidi unapoona wasomi wenye uwezo mkubwa wa uchambuzi wanageuka vibaraka wa kusifia pasipo kugeuza upande wa pili wa shilingi kukemea mwenendo tete wa taifa letu.Hate me or love me, ninachofanya ni kinachopaswa kufanywa na kila Mtanzania mwenye uchungu wa dhati wa taifa letu, na anayefahamu kwamba it’s no use crying over spilled milk. Imani kwamba “hata tukipiga kelele hatuwezi kubadili kitu” ni hatari sana kwa vile japo Ukimwi umekuwepo kwa miongo kadhaa sasa bado jamii inaendelea kuhamasisha vita dhidi ya gonjwa hilo hatari.

Kinachopaswa kuwaamsha wanaochelewa kujiunga kwenye mapambano dhidi ya ufisadi ni ukweli ufuatao.Katika utafiti wangu wa kitaaluma unaoelekea ukiongoni,kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba vurugu za kidini (utafiti wangu unahusu dini) na nyinginezo katika jamii zinachangiwa sana na jamii kukatishwa tamaa na mwenendo wa watawala kushughulikia matatizo yanayozikabili jamii hizo.Na kwa vile watawala wa aina hiyo hufanya kila wawezalo kuzuia “sauti zisizopendeza masikioni mwao”,kimbilio pekee hubaki kwa nyumba za ibada na dini kwa ujumla.

Tatizo ni kwamba masuala ya dini yanaelemea zaidi kwenye hisia kuliko reasoning. Sote tunafahamu, kwa mfano, kuwa piga ua huwezi ku-reason na Mkatoliki kuhusu ishu “ngumu kuelezeka” kama Utatu Mtakatifu, namna Bikira Maria alivyomzaa Yesu pasipo “kukutana” na Josefu, na maswali mengine kama hayo.Na katika masuala ya dini, ambapo mara nyingi emotions tend to come in front of common sense, hakuna taratibu kama za jeshini kwamba amri ya jenerali lazima iheshimiwe na brigedia, au ya kanali iheshimiwe na meja, au ya kapteni kwa lance corporal. Kwenye dini, kauli ya askofu au shehe haina nguvu sana katika kutuliza hamasa za waumini pindi wanapoamua kupambana na mamlaka za kidunia kwa jina la Mungu.

Kinachoniogopesha zaidi ni vuguvugu linaloendelea huko nyumbani ambapo ishu kama ahadi hewa za CCM kuanzisha mahakama ya kadhi,mwongozo wa Kanisa kuhusu uchuguzi wa viongozi waadilifu,mwendelezo wa madai kuwa Wakristo wanapendelewa na Waislam wanaonewa,nk zimetawala anga za habari. Kibaya zaidi, hayo yanatokea katika kipindi ambacho mafisadi wako tayari kufanya lolote alimradi wafanikiwe kuendelea kutufisadi. Yayumkinika kuamini kwamba hawawezi kusita kutumia fursa hii ya “kuwachanganya Watanzania” kwa misingi ya dini na hivyo ku-deflect attention yao (Watanzania) kuhusu ufisadi na mafisadi kwa vile watakuwa bize zaidi kunyoosheana vidole kwa misingi ya udini.

Tukiunyamazia ufisadi, utatumaliza!

It can be done if you play your part.

It’s now or never!

27 Jun 2008

Katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema nazungumzia dalili zakutimia kwa utabiri wa Mwalimu Nyerere kwamba upinzani wa kweli unaweza kutoka ndani ya CCM.Kwa namna mambo yanavyokwenda mramba ndani ya chama hicho nidhahiri kwamba kuna tofauti kubwa za kiimani na kimtazamo miongoni mwa viongozi wake.Ili kutokukunyima uhondo zaidi,bingirika na makala hiyo,pamoja na nyinginezo zilizopanda vidato,kwa KUBONYEZA HAPA

20 Jan 2008

Makala hii ilitoka kwenye gazeti la Mtanzania siku ya Alhamisi 17Jan 2008.

Hatimaye ugavana wa Dkt Daudi Ballali katika Benki Kuu ya Tanzania umetenguliwa.Sijui kama utenguzi huo ni sawa na tunachosoma,kuona na kusikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba Balali amefukuzwa kazi.Pengine la muhimu kwa sasa ni kwamba mtu huyo ametolewa katika wadhifa huo japo la muhimu zaidi ni kuweka rekodi vizuri kwa minajili ya kuondoa utata uliojitokeza hasa katika neno “KUTENGUA”.

Kuna wanaosema kwamba Ballali ametolewa kafara hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba sio rahisi wizi mkubwa namna hiyo uwe umefanywa na mtu mmoja tu.Ni vigumu pia kuamini kwamba uamuzi wa gavana huyo wa zamani kuyazawadia makampuni yaliyotajwa kwenye ufujaji wa fedha hizo ulifanywa na mtu mmoja pekee (Balalli).

Sakata hili lilisabaisha,linasababisha na litaendela kusababisha maswali mengi zaidi kuliko majibu.Sijui kuna wazalendo wangapi hapo Benki Kuu, lakini nashawishika kuhoji uzalendo wao kwani japo si kila mtumishi angeweza kufahamu alichokuwa akifanya Balali na washirika wake,ni dhahiri wapo waliokuwa katika nafasi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika lakini wakaamua kukaa kimya.

Nadhani kuna waliojua kinachoendela lakini wakaa kimya kwa vile nao walikuwa washiriki katika ufisadi huo.Hawa hawana cha kujitetea kwani hawana tofauti na Balalli na wanachostahili ni adhabu tu.Kikwazo kikubwa kinachojitokeza katika uwezekano wa kuwaadhibu waungwana hawa ni ukweli kuwa baadhi yao wamepewa nafasi ya kujichunguza wenyewe (kwa vile bado wako madarakani) na sote tunaelewa kwamba hawawezi kujihukumu.Sanasana wataishia kuharibu ushahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa ufisadi huo.

Kundi la pili ni wale waliokuwa wakifahamu kinachoendelea lakini hawakuchukua hatua kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kauli za utetezi zilizokuwa zikitolewa na watu mbalimbali pindi tuhuma za ufisadi huo zilipoanza kuibuka.Tunakumbuka kwamba kuna wakati huko bungeni lilitolewa tishio la kumfikisha Dr Slaa mbele ya vyombo vya sheria akituhumiwa kwamba ameghushi nyaraka zinazohusiana na sakata hilo.Yayumkinika kusema kwamba kauli kama hizo zinaweza kuwa ziliwakwaza baadhi ya watumishi wa Benki Kuu (waliokuwa na ufahamu wa ufisadi huo) kuripoti kuhusu uhuni uliokuwa ukiendelea hapo.
Imeripotiwa pia kwamba moja ya makampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya benki hiyo iliripoti kuhusu kasoro zilizokuwepo lakini ikaishia kuona mkataba wake na benki hiyo ukisitishwa.Ni rahisi kukubaliana na “busara” hii kwamba kama kampuni iliyolipwa kuchunguza mahesabu imepuuzwa je “nani atanisikiliza mie niliyeajiriwa kufanya majukumu mengine katika Benki Kuu”.

Miongoni mwa madhara ya kulea ubadhirifu ni kujengeka kwa imani (miongoni mwa wasiojihusisha na ubadhirifu huo) kwamba ubadhirifu sio dhambi kwani ingekuwa haukubaliki basi wahusika wasingeendelea nao pasipo kuchukuliwa hatua.Yeyote aliyehusika na skandali hiyo lakini bado yuko madarakani ni sawa na kansa ambayo isipodhibitiwa inasambaa katika mwili mzima.Ni kama katika familia yenye watoto kadhaa na baadhi yao wanajihusisha na tabia zisizofaa.Ni dhahiri wale wanaoepuka tabia hizo (ilhali wenzao wanaendelea nazo) wanaweza kushawishika kuiga tabia hizo hususan kama wanaona wenzao wananufaika kwa namna flani.

Nakumbuka hivi karibuni,mkongwe wa siasa Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alinukuliwa na gazeti moja akieleza masikitiko yake kuhusu namna uzalendo unavyopungua miongoni mwa Watanzania.Ni kweli uzalendo umepungua sana na tusipokuwa makini utapotea kabisa lakini kuwa na wasiwasi au kulalamika pekee hakuwezi kusaidia kurekebisha mambo.Ni dhahiri kwamba moja ya mambo yanayochangia kupungua uzalendo ni pamoja na ufisadi kama huo uliofanyika hapo Benki Kuu.

Hivi mtu atakuwaje mzalendo iwapo wakati yeye anahangaika kutafuta fedha za kumwezesha kupata angalau mlo mmoja wa siku kuna wajanja wanatumbukiziwa mamilioni ya shilingi kwenye makampuni yao pasipo kuvuja tone moja la jasho.Kibaya zaidi na pengine katika kuwaringia walipa kodi wanaoibiwa,mafisadi hawaogopi kuonyesha namna wizi wao “unavyolipa” kwa kuporomosha mahekalu ya gharama kubwa,magari ya thamani ya kutisha na vimbwanga vingine chungu mbovu.Ni kama mtu anakupora mke halafu kesho yake unamwona anatamba nae mtaani.Hii inaongeza chuki na hasira kwa aliyeibiwa.

Kila zinapojitokeza tuhuma za ufisadi huwa nashindwa kujizuia kuhoji uwezo wa TAKUKURU katika jukumu lake la kuzuia na kupambana na rushwa.Taasisi hii imekuwepo kwa muda mrefu sasa lakini bado ni legelege licha ya jitihada kadhaa zilizokwishafanywa iwe na ufanisi zaidi.Naafikiana na baadhi ya hoja kwamba matendo mengi ya ulaji fedha za umma hayafanyiki hadharani,hivyo kusababisha ugumu katika kuyabaini.Hata hivyo,katika sakata hili la ufisadi hapo BoT,tetesi zilikuwepo mtaani na magazetini kwa muda mrefu.Kama ilivyozeleka,kauli za TAKUKURU zilikuwa “taarifa hizo tunazo na tunazifanyia uchunguzi”.Ikumbukwe kwamba katika mazingira ambayo matatizo yanazaliana kila kukicha,kuchelewa kutatua tatizo moja ni sawa na kutengeneza mlima wa matatizo hayo ambapo mwisho wake itakuwa ni suala lisilowezekana kabisa kuyaondoa.

Pengine umefika wakati mwafaka kwa wawakilishi wetu huko bungeni kuhoji uhalali wa kuendelea kuwa na taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa.Kanuni ya haki katika sheria inatamka waziwazi kwamba haki sio tu itendeke bali pia ionekane imetendeka.Tunaweza kuitumia kanuni hiyo kwa TAKUKURU pia kwamba mapambano dhidi ya rushwa yasiishie tu kuwa ya dhamira bali yaonekane hadharani kuwa yapo na yana ufanisi unaotarajiwa.

Naweza kuonekana mtu wa ajabu iwapo nitashauri kuvunjwa kwa TAKUKURU lakini nina hoja ya msingi napofikiri hivyo.Mamilioni ya fedha yanayoelekezwa kwa taasisi hiyo kupambana na rushwa hayajasaidia lolote katika kupunguza tatizo hilo.Mabadiliko mbalimbali ya kisheria yaliyolenga kuipa meno taasisi hiyo nayo yameshindwa kuifanya iwajibike ipasavyo.Binafsi sioni cha ziada kinachoweza kubadili ulegelege wa taasisi hiyo zaidi ya kuivunjilia mbali na kasha majukumu yake kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine kama vile kitengo cha upelelezi katika jeshi la polisi (CID).

Kwa kuzingatia rekodi ya TAKUKURU katika uendeshaji wa kesi inazopeleka mahakamani,sintoshangaa iwapo wanaotajwa kwenye sakata hilo wataishia kuibuka washindi kwenye kesi hizo.Tumeshuhudia namna taasisi hiyo ilivyokuwa “ikipelekeshwa” kwenye kesi dhidi ya Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.Kama kesi ya mtu mmoja imekuwa ngoma nzito namna hiyo,tutarajie nini kwenye lundo la kesi linalowahusu watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha?

Wengi wanatafsiri vurugu zinazoendelea nchini Kenya kuwa ni matokeo ya ukabila.Lakini baadhi ya wachambuzi wa uchumi wananyumbulisha kwamba vurugu hizo ni sehemu tu ya mapambano ya kiuchumi kati ya wenye nacho na wasio nacho.Migongano ya kidini au kikabila hujichomoza zaidi kwenye jamii isiyo na uwiano wa kimapato kwani mara nyingi washiriki kwenye vurugu hizo huamini kwamba pindi zikifanikiwa zitarekebisha maisha yao ya kila siku.Tuna kila sababu ya kuzuia nchi yetu inayosifika kwa amani na utulivu isiingie kwenye machafuko yanayoweza kusababishwa na wengi wanaoona wachache wakinufaika kwa “ulafi wa kula keki ya taifa” huku wao (wengi hao) wakiendelea kutaabika.Kinachowezekana leo kisingoje kesho.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.