Showing posts with label EU REFERENDUM. Show all posts
Showing posts with label EU REFERENDUM. Show all posts

24 Jun 2016

Leo nilishiriki katika mahojiano mawili kuhusu kura ya maoni iliyopigwa hapa Uingereza juzi kuhusu hatma ya uanachama wa taifa hilo kwenye Umoja wa Ulaya, ambapo matokeo yalikuwa kwa Uingereza kujitoa. Mahojiano hayo yalikuwa kati yangu na kipindi cha radio cha  Dira ya Dunia ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC na baadaye kipindi cha televisheni cha Dira ya Dunia cha kituo hicho.

Hapa chini ni video na audio ya mahojiano hayo. KaribuniJUMATANO hii, wakazi wa hapa Uingereza watapiga kura kuamua hatma ya nchi hii kwenye Umoja wa Ulaya. Katika kura hiyo, Waingereza wanaulizwa iwapo wanataka nchi yao ibaki kuwa mwanachama wa umoja huo au wanataka nchi yao ijitoe.


Hadi wakati ninaandika makala hii, kura za maoni (opinion polls) zinaashiria matokeo yanayokaribiana kabisa, kwa maana kwamba upande wowote utakaoshinda, utafanya hivyo kwa tofauti ndogo tu ya ushindi.Kampeni za kura hiyo zilisimamishwa wiki iliyopita baada ya mauaji ya kwanza katika historia ya nchi dhidi ya mbunge aliyepo madarakani, ambapo mbunge wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Joanne ‘Jo’ Cox aliuawa Alhamisi iliyopita, kwa kupigwa risasi na kuchomwa kisu.Tayari mtu mmoja amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya mauaji. Wakati mtu huyo akifanya unyama huo, alisikika akisema ‘Britain first!’ (Uingereza kwanza), pengine kuonyesha upinzani wake dhidi ya mbunge huyo ambaye alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia ‘wanyonge’ sehemu mbalimbali duniani na hapa Uingereza.Licha ya kauli hiyo ya muuaji huyo kuwa jina la chama cha kibaguzi cha Britain First, uchunguzi wa awali wa polisi umegundua nyaraka kadhaa zinazoashiria mawasiliano kati ya mtu huyo na vikundi vyenye mrengo mkali wa kulia, vya kibaguzi.Kadhalika, kabla ya kukutwa na mauti, mbunge huyo alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wapige kura ya hapana, kupinga wazo la Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Ni muhimu kuelezea katika hatua hii kwamba iwapo kambi inayotaka Uingereza ibaki kwenye umoja huo wa Ulaya itashinda, basi tukio hilo la kusikitisha la mauaji ya mbunge huyo, aliyekuwa akiunga mkono nchi hii isijitoe, linaweza kuwa limechangia kwa namna fulani.Huu ni mtizamo wangu binafsi, kwamba kwa namna fulani tukio hilo linaweza kuwaogopesha baadhi ya wapigakura kuwa Uingereza nje ya Umoja wa Ulaya yaweza kutawaliwa na siasa za mrengo mkali au za kibaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa vikundi vya aina hiyo vinaunga mkono nchi hii kujitoa kwenye umoja huo.Kabla ya mauaji hayo, kura za maoni zilikuwa zinaonyesha kambi inayotaka Uingereza ijitoe ilikuwa ikiongoza kwa takriban asilimia tano. Hata hivyo, kura kadhaa za maoni zilizotolewa juzi, zikiwa ni za kwanza baada ya kifo cha mbunge huyo, zinaonyesha kambi inayotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya ikiongoza kwa asilimia chache kidogo. Hii ni mara ya kwanza kwa siku za hivi karibuni kwa kambi hiyo kuongoza katika kura hizo za maoni.Laiti ningeandika makala hii miezi michache tu iliyopita, basi wala nisingepata shida kubashiri kuwa Uingereza ingeendelea kubaki mwanachama wa Umoja huo. Awali, ilionekana kuwa kambi ya wanaotaka Uingereza ijitoe ilikuwa haina hoja za msingi zaidi ya kulalamika kuwa umoja huo unaikandamiza nchi hii, sambamba na kudai kuwa mamlaka ya utawala katika taifa hili kubwa duniani imeporwa na umoja huo.Moja ya masuala muhimu kuhusu hoja nzima ya kujitoa au kubaki kwenye umoja huo ni pamoja na suala la uhamiaji na wahamiaji. Siku zote suala hili limekuwa nyeti sana kisiasa. Wapinzani wa uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya wanadai kuwa nchi hii imekuwa ikibanwa na sheria za umoja huo hususan katika masuala ya uhamiaji na wahamiaji. Sheria zilizopo zinaruhusu ‘uhuru wa matembezi’ (freedom of movement) kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa wakazi wa nchi wanachama, kitu ambacho wapinzani wanadai kinachochea uhamiaji haramu.Kadhalika, baadhi ya wahamiaji haramu waliotaka kufukuzwa Uingereza waliweza kukwamisha uamuzi huo kwa kukata rufaa kwenye Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya.Vile vile, sheria za umoja huo zinatoa ruhusa kwa wahamiaji kutoka nchi zilizo ndani ya umoja huo kupata haki mbalimbali kama vile huduma za bure za afya, fedha za kujikimu na za makazi zinazotolewa kwa watu wasio na kazi au wenye kipato duni.Pia, kama mwanachama wa umoja huo, Uingereza imekuwa ikilipa mamilioni ya pauni kila wiki kama mchango wake kwa umoja huo, suala ambalo wanaotaka nchi hii ijitoe wamekuwa wakililamikia mno, wakidai linaathiri uwezo wa nchi hii kuhudumia wananchi wake kwa ufanisi.Kwa upande mwingine, hoja kuu ya upande unaotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya ni uchumi. Na kambi hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata watetezi mbalimbali, kuanzia Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela Angela Markel wa Ujerumani hadi taasisi kama Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia.Hoja kuu ni kwamba laiti Uingereza ikijitoa kwenye umoja huo, uchumi wake utaathirika vibaya. Na pengine katika kile kinachoweza kuwa kinaashiria ukweli wa tishio hilo, thamani ya sarafu ya nchi hii – Pauni ya Kiingereza – imejikuta ikishuka thamani kulinganisha na Dola ya Marekani. Hata gavana wa benki kuu ya hapa, ambaye haruhusiwi kujihusisha na siasa, ameonya kuwa uchumi wa nchi hii utayumba iwapo itajitoa kwenye umoja huo.Kambi ya wanaotaka Uingereza ibaki kwenye umoja huo imepata nguvu pia kutoka kwa taasisi mbalimbali za kibiashara na uchumi ndani na nje ya nchi hii, sambamba na uungwaji mkono kutoka kwa wakuu wa zamani wa taasisi za kiintelijensia za MI5 (idara ya ushushushu wa ndani ya nchi) na MI6 (idara ya ushushushu wa nje ya nchi, yaani ujasusi). Mashushushu hao wastaafu wametahadharisha kuwa kwa Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya itahatarisha ushirikiano uliopo dhidi ya matishio ya kiusalama kwa nchi wanachama wa umoja huo.Ni vigumu kueleza kwa hakika ni suala gani lililoweza kubadili mwelekeo wa kampeni ambapo awali ilionekana kama wazo tu la Uingereza kujitoa kwenye umoja huo ni kama mzaha. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa kosa la kambi inayotaka nchi hii isijitoe ni kutegemea zaidi vitisho kutoka kwa wataalamu mbalimbali.Mbinu hiyo, inayoelezwa kwa kimombo kama “fear factor” ilikuwa na ufanisi mkubwa katika kura iliyopigwa hapa Uskochi mwaka juzi kuamua kama taifa hili lijitoe katika muungano wa Uingereza au liendelee kuwemo. Kwa kutumia wataalamu mbalimbali hususan wa uchumi, serikali kuu chini ya Waziri Mkuu David Cameron ilifanikiwa kuwatisha Waskochi kuhusu hatma yao nje ya muungano wa Uingereza.Kwa kifupi, ilikuwa ni hadithi ya zimwi likujualo, kwamba angalau Waskochi wanafahamu mazuri na mabaya ya muungano wa Uingereza na wanaweza kuenzi mazuri hayo na kuyarekebisha mabaya, kinyume na kuchukua uamuzi wa kujitoa ambao faida na hasara zake zilikuwa kama za kufikirika (kwa maana kwamba ni kitu ambacho kilikuwa bado hakijatokea).Ni hivi, hata kwenye chaguzi za huko nyumbani (Tanzania), moja ya turufu ya chama tawala CCM huwa kwenye hoja ya angalau mnafahamu mazuri na mabaya ya CCM. Je, mnataka kufanya majaribio na vyama vya upinzani? Itakuwaje iwapo majaribio hayo yatakwenda kombo?Hoja hiyo pia inatumiwa na kundi linalotaka Uingereza ibaki kwenye Umoja wa Ulaya lakini tofauti na ilivyokuwa kwenye kura ya uhuru wa Uskochi, safari hii hoja hiyo imekumbana na hoja mbadala kama sisi ni Waingereza, tumemudu mambo mengi katika historia ya taifa letu. Tukiwa nje ya Umoja wa Ulaya tutamudu kusimama wenyewe.Kwa kuwategemea sana wataalamu na taasisi mbalimbali kuonyesha madhara ya nchi hii kujitoa kwenye umoja huo, kambi inayofahamika kama Remain (kubaki) imejikuta kwenye wakati mgumu pale inapotuhumiwa kuwa hao wataalamu wenyewe sio watu wanaoishi maisha ya kawaida. Yaani ni kama vigogo ambao hawaathiriwi na adha wanazokumbana nazo wananchi wa kawaida kutokana na Uingereza kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kwa siasa za wenzetu huku, serikali au wanasiasa kuwa karibu na watu – wenyewe wanaita kuongea lugha ya mtu wa kawaida – ni turufu muhimu. Na huo umekuwa mtaji muhimu wa watu kama Boris Johnson, Meya wa zamani wa Jiji la London, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kambi inayotaka nchi hii ijitoe kwenye umoja huo, inayofahamika kwa kifupi kama Leave (Ondoka).Mwanasiasa huyo machachari na mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuongea “lugha ya watu wa kawaida” kueleza kwa nini nchi hii itakuwa bora zaidi nje ya Umoja wa Ulaya.Upinzani mwingine dhidi ya Umoja huo ni tishio la mpango wa umoja huo kuiingiza Uturuki kuwa mwanachama. Licha ya kuwa nchi ya Ulaya, Uturuki inaangaliwa kama taifa la Kiislamu, wapinzani wa uanachama wa Uingereza kwenye umoja huo wanadai kuwa huko mbele Uturuki itaruhusiwa kuwa mwanachama, na hali hiyo itatishia usalama wa nchi hii. Ukweli mchungu tunaoishi nao hapa ni mtizamo wa kibaguzi wa kuhusisha Uislamu na ugaidi.Kichekesho cha suala lote hili la Uingereza kubaki au kujitoa katika Umoja wa Ulaya ni kwamba Waziri Mkuu Cameron alitumia hoja ya kura hii kuomba ridhaa kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Aliahidi kuwa chama chake cha wahafidhina (Conservatives) kikishinda, kitaitisha kura hii ili wananchi waamue kama wanataka kubaki kwenye umoja huo au la. Kwa wakati huo, hoja hiyo ilimsaidia sana Cameron na chama chake kushinda katika uchaguzi huo.Je, nini kitatokea iwapo Waingereza wataamua kubaki kwenye umoja huo? Hadi muda huu, nchi hii tayari imepewa hadhi maalumu kwenye maeneo mbalimbali ya umoja huo. Kwa hiyo, iwapo kambi ya Remain inayoongozwa na Waziri Mkuu Cameron, akiungwa mkono na kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, itashinda, hakutakuwa na mabadiliko makubwa katika uanachama wa nchi hii kwa sababu tayari imekwishapatiwa hadhi maalumu kwenye umoja huo.Je, nini kitatokea iwapo Uingereza itajitoa kwenye Umoja huo? Kwa kimombo wanasema “that’s a million-dollar question” (hilo ni swali la dola milioni moja). Kimsingi, hakuna anayejua kwa hakika hali itakuwaje. Hata hivyo, kuna kitu kama mwafaka miongoni mwa wataalamu wa uchumi wa dunia kwamba kwa nchi hii kujitoa kwenye umoja huo, uchumi wake utayumba. Hoja hiyo inapangwa na kambi ya Leave kwa kubainisha ‘hesabu’ zao mbalimbali, kubwa ikiwa mchango wa Uingereza kwenye umoja huo, ambapo kambi hiyo inadai kuwa fedha hizo zikitumika nchini hapa zitafidia pengo lolote litakalojitokeza.Kadhalika, kambi hiyo ya Leave inadai kuwa hata kama nchi hii itatakiwa kujiunga upya na mikataba mbalimbali ya kimataifa, ukweli kwamba taifa hili ni kubwa na lenye mvuto kwa nchi nyingine, basi hawaoni uwezekano wa nchi hii kususiwa.Moja ya madhara yanayoweza kujitokeza iwapo Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya ni kile kinachofahamika kama ‘domino effect,’ yaani kama kwenye mchezo wa goroli au ‘pool’, ukiipiga moja inaipiga nyingine, nayo inaipiga nyingine, na kadhalika. Kwamba, iwapo Uingereza ikijitoa, baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo nazo zinaweza kuitisha kura za kujadili uanachama wao, suala linaloweza kusababisha kuvunjika kwa umoja huo muhimu.Tishio jingine kubwa linahusu muungano wa Uingereza. Nchi hii inaundwa na muungano wa mataifa manne, ambayo ni England, Wales, Uskochi na Ireland ya Kaskazini (Jina kamili la nchi hii ni The United Kingdom of Great Britain – yaani England, Wales na Uskochi – and Northern Ireland). Tayari chama tawala cha hapa Uskochi, SNP (Scottish National Party), ambacho huko nyuma ndicho kilipigania kura ya uhuru wa Uskochi, kimekwishatamka kuwa kama Uingereza itajitoa kwenye Umoja wa Ulaya, basi nacho kitaitisha kura nyingine ya kudai uhuru.Ningetamani mno kuhitimisha makala hii kwa kujifunga na kutabiri matokeo ya kura hiyo hapo kesho (Juni 23, 2016) lakini ninachelea kufanya hivyo kwa sababu, kwanza kura za maoni zinaonyesha kambi zote mbili zina nafasi zinazokaribiana kitakwimu, lakini pili, kura za maoni katika uchaguzi mkuu uliopita nchini hapa zilitoa mshangao mkubwa baada ya matokeo ya uchaguzi huo kuwa kinyume kabisa na takriban kura zote za maoni. Wajuzi wanasema kura za maoni sio “exact science” (sayansi ya uhakika kabisa).’Ninachoweza kuahidi katika hitimisho la makala hii ni kuzungumzia zaidi kuhusu Uingereza kabla na baada ya kura hiyo katika makala ijayo.

23 Jun 2016


Leo tarehe 23.06.2016 Uingereza itapiga kura ya maoni kuamua kuhusu hatma ya uanachama wake katika Umoja wa Ulaya (EU). Jana, nilipata fursa ya kushiriki katika mjadala mkali katika kipindi cha Dira ya Dunia cha Idhaa ya Kiswahili ya BBC Radio.

Sikiliza kwenye audio hapo chini mjadala huo (unaojiri baada ya taarifa ya habari). Karibuni


 
Check this out on Chirbit

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.