Showing posts with label OLE NAIKO. Show all posts
Showing posts with label OLE NAIKO. Show all posts

29 Jan 2009


HEBU SOMA KWANZA HABARI IFUATAYO KISHA TUIJADILI PAMOJA

MKURUGENZI wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel ole Naiko, amesema neno ufisadi linawatisha wawekezaji, hivyo kuwataka wananchi kulitumia kwa umakini huku
wakiweka uzalendo mbele.

Alisema wakati taratibu za kupambana na rushwa zikiendelea, kipaumbele kielekezwe kwenye uchumi na maendeleo kwa ujumla ili kulikwamua taifa, kwani kiwango cha rushwa kilichopo si kama kilichopo katika nchi zilizoendelea.

Naiko alisema hayo jana katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima, yaliyofanyika katika ofisi za TIC, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo alisema hakuna shaka kwamba rushwa na uwekezaji, haviendi pamoja lakini ni vema suala hili likachukuliwa kwa umakini na kutanguliza uzalendo kwa masilahi ya taifa.

“Tunatakiwa tuwe na uzalendo pale penye sifa mbaya, tulichukulie kwa umakini ili tusiendelee kulijengea sifa mbaya taifa letu. Tuziache taratibu na sheria zetu zifanye kazi, ikiwemo kuwapeleka mahakamani watuhumiwa,” alisema.

Alisema Tanzania haiongozi kwa rushwa lakini inaonekana hivyo kutokana na msimamo wa serikali kuweka wazi masuala ya rushwa. Akitolea mfano wa meya aliyeuza kiti cha useneta huko Illinois, nchini Marekani, Ole Naiko alisema hali hiyo inaashiria ni kwa jinsi gani kulivyo na rushwa katika nchi tajiri kuliko zile maskini.

“Sisi tuna rushwa ndogo ndogo, hatuwezi kuongoza kwa rushwa, nchi tajiri ndizo zinazoongoza kwa rushwa. Kwanza tuna taasisi za kupambana na rushwa na tunayaweka haya masuala wazi, wenyewe kamwe hawawezi, kwani hawataki nchi zao
zionekane mbaya,” alisisitiza. Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi aliwataka Watanzania kulifikiria taifa lao wakati likipambana na rushwa na kusisitiza kuwa wananchi wajadili jinsi ya kuliletea taifa maendeleo.

Akizungumzia mafanikio ya mkutano wa Sullivan uliofanyika mwaka jana, alisema huandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha Wamarekani na Waafrika katika kujadili mustakabali wa jinsi ya kuondokana na hali ya umaskini inayowakabili.

Pamoja na hilo, alikiri kwamba mafanikio yameonekana hasa kwa wawekezaji wa Kimarekani, kwani mkutano huo umeifanya Marekani itoke nafasi ya nane hadi ya nne kwa uwekezaji nchini, ikifuatiwa na nchi za Uingereza, Afrika Kusini na Kenya.

Kuhusu safari za Rais Jakaya Kikwete nchini Marekani, Naiko alisema zimewawezesha Wamarekani kuifahamu vema Tanzania, hivyo kuvutika kuwekeza zaidi. Alisema kwa sasa kituo chake kina mpango mahususi wa kutumia balozi zake katika kuitangaza Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuweka balozi zake katika nchi zenye uwezo wa kuwekeza nchini.


HIVI KIPI CHA BUSARA ZAIDI: KUTOPIGA KELELE KUHUSU UFISADI KWA VILE WAKIFANYA HIVYO WATAWATISHA WAWEKEZAJI AU KUPIGA KELELE KWA NGUVU ILI MAFISADI WATOKOMEE NA KISHA KUWAVUTIA WAWEKEZAJI WENGI ZAIDI? HIVI HUYU OLE NAIKO ANATAKA KUJIFANYA HAELEWI KWAMBA MASLAHI YA MTANZANIA YANA UMHIMU ZAIDI KULIKO HAO WAWEKEZAJI (AMBAO MIONGONI MWAO NI MAFISADI VILEVILE)?

MASLAHI YA TAIFA YATALINDWA TU ENDAPO KELELE DHIDI YA MAFISADI ZITAENDELEA KWA NGUVU KUBWA NA KUWASHIRIKISHA WATU KAMA OLE NAIKO NA WALA SIO KWA KUONGEA CHINICHINI KWA KUHOFIA KUWATISHA WAWEKEZAJI.HIVI MAFISADI WAKISHAIFILISI TANZANIA HAO WAWEKEZAJI WATAKUJA KUWEKEZA KWENYE NINI?

TUANGALIE KWA MTIZAMO MWINGINE.HIVI SI KWELI KWAMBA NI VITENDO VYA UFISADI,NA SIO KELELE ZA WANANCHI KUHUSU MATENDO YAO,YANAYOCHAFUA SIFA YA TANZANIA NA HIVYO KUWATISHA WAWEKEZAJI?HUYU JAMAA VIPI?LAKINI SIMSAHNGAI SANA KWA VILE ALISHAWAHI KUCHEMKA HUKO NYUMA ALIPOHUSISHWA NA TUHUMA ZA MATAPELI WA RICHMOND NA AKAKIMBILIA KUDAI KWAMBA ANAFANYIWA HIVYO (KUHUSISHWA) KWA VILE YEYE NI MTU WA MONDULI (KAMA LOWASSA).
MFANO WAKE KWAMBA GAVANA (NA SIO MEYA KAMA ALIVYODAI) WA ILLINOIS,ROD BLAGOJEVICH,KUKABILIWA NA TUHUMA ZA "KUUZA KITI" CHA USENETA INAASHIRIA KUWA RUSHWA NI KUBWA KATIKA NCHI TAJIRI KULIKO MASIKINI UNASHINDWA KUZINGATIA UKWELI KWAMBA RUSHWA NI RUSHWA,IWE MAREKANI AU TANZANIA,TENA PENGINE RUSHWA KATIKA NCHI TAJIRI INAWEZA KUWA NA ATHARI NDOGO KULINGANISHA NA NCHI ZA MASIKINI KWA VILE ANGALAU WENZETU WANA MECHANISM KADHAA ZINAZOWEZA KUM-BANA MTU ALIYEPATA MADARAKA KWA NJIA YA RUSHWA.LA MUHIMU HAPO SIO GAVANA HUYO KUWA KISHIRIO KWAMBA RUSHWA IPO MAREKANI BALI NAMNA WENZETU WANAVYOJITAHIDI KUPAMBANA NAYO.SIJUI SIE TUNA AKINA BLAGO WANGAPI...KUBWA ZAIDI NI KILE WAINGEREZA WANACHOSEMA TWO WRONGS DO NOT MAKE A RIGHT.KUWEPO KWA RUSHWA MAREKANI,AU KWINGINEKO KOKOTE KULE HAKUWEZI KUHALALISHA RUSHWA WALA KUWA SABABU YA SIE KUPUNGUZA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA ETI KWA VILE TU "MBONA HATA KWA WENZETU IPO"!

WAKATI OLE NAIKO ANASEMA (NAMNUKUU) "Sisi tuna rushwa ndogo ndogo....nchi tajiri ndizo zinazoongoza kwa rushwa....wenyewe kamwe hawawezi, kwani hawataki nchi zao zionekane mbaya..." INAELEKEA ANASAHAU KWAMBA HIYO ANAYOITA RUSHWA NDOGO NDOGO (SIJUI KAPATA WAPI KIPIMO CHA KUJUA RUSHWA KUBWA NA NDOGO) INA MADHARA MAKUBWA SANA KWA NCHI MASIKINI KAMA AMBAVYO HIZO RUSHWA KUBWA ZINAVYOWEZA KUWA NA MADHARA KATIKA NCHI TAJIRI.HALAFU MBAONA ANAJICHANGANYA ANAPODAI KUWA NCHI TAJIRI "ZINAZOONGOZA KWA RUSHWA" (KWA MUJIBU WAKE) HAZIWEZI KUWEKA RUSHWA HADHARANI KWA VILE HAZITAKI ZIONEKANE MBAYA LAKINI HAPO HAPO AMETOA MFANO WA HUYO GAVANA WA ILLINOIS!?JE WANGEKUWA HAWATAKI HAYO YAONEKANE YEYE OLE NAIKO NA SIE TULIO NJE YA MAREKANI TUNGEJUAJE?

HALAFU ARGUEMENTS ZA HUYU MHESHIMIWA ZINAWEZA KUWA NA MADHARA KULIKO HICHO ANACHOJARIBU KUTUELEZA.HIVI TUMWELEWEJE ANAPODAI KUWA NCHI TAJIRI ZINAONGOZA KWA RUSHWA,HALAFU WAWEKEZAJI ANAOTAKA TUSIWATISHE KWA NENO UFISADI WANATOKA KWENYE NCHI HIZOHIZO ANAZODAI ZINAONGOZA KWA RUSHWA!!!!ANATAKA TUSIWATISHE ILI WAJE KUENDELEZA RUSHWA TANZANIA?

HOJA YENYE UZITO NI KWAMBA UFISADI SIO TU UNAATHIRI SEKTA YA UWEKEZAJI BALI PIA UNAATHIRI TAIFA LENYEWE AMBALO TUNATAKA KUWAVUTIA WAWEKEZAJI HAO.KWA MWENYE BUSARA ZA KUTOSHA HOJA YA MSINGI NI KUZIDISHA MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI NA WALA SIO HOFU KWAMBA NENO MAFISADI LITAWATISHA WAWEKEZAJI.JINGINE LA MUHIMU NI KILE ALICHOSEMA MWENYEKITI MAO KWAMBA NO RESEARCH NO RIGHT TO SPEAK.KUTUHUMU MATAIFA TAJIRI KUWA YANAONGOZA KWA RUSHWA PASIPO KUTOA TAKWIMU ZA KUSAPOTI HOJA HIYO,SIO TU INAWEZA KUWACHUKIZA HAO WAWEKEZAJI KWA VILE WANAWEZA KUDAI WANATUHUMIWA PASIPO SUPPORTING EVIDENCE,BALI PIA KUNAMPUNGUZIA CREDIBILITY MTOA HOJA HASA IKIZINGATIWA KUWA ENEO ANALOZUNGUMZIA NDILO ALILOKABIDHIWA DHAMANA NA TAIFA KULISIMAMIA KWA UMAKINI.

2 Mar 2008

MTANZANIA UGHAIBUNI

Sakata la mkataba wa Kampuni ya Richmond linaelekea kuchukua mwelekeo mpya kila kukicha. Ni rahisi kutafsiri kwamba suala hili lisipopatiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kuwa na madhara makubwa kwa nchi na kwa chama tawala, CCM.

Tangu ripoti ya “Tume ya Mwakyembe” ilipowekwa hadharani katika kikao kilichopita cha Bunge la Jamhuri ya Muungano, kumejitokeza kauli kadhaa za utatanishi ambazo japo zinaweza kuwa ni za kawaida tu, tafsiri ya ndani inaashiria matatizo makubwa huko tuendako.

Naomba niwe muwazi zaidi katika makala hii, na ningependa kutamka bayana kwamba sina nia ya kumshushia heshima yeyote nitakayemtaja. Lengo kuu la makala hii ni kuikumbusha kila pande inayoguswa na sakata hilo kutambua kwamba taifa letu ni muhimu zaidi kuliko maslahi ya mtu mmoja.

Naikumbuka sana siku taifa lilipotangaziwa kifo cha Baba wa Taifa.Watanzania wengi walitokwa na machozi sio tu kwa vile hawangemwona tena Mwalimu bali pia ni ile hali ya kutokuwa na uhakika taifa letu lingekuwaje bila Nyerere.Naamini kwamba laiti Mwalimu angekuwepo, baadhi ya upuuzi kama huo wa mkataba wa Richmond wala usingetokea, lakini ndio hivyo tena, hatuko naye duniani.

Wanaoilaumu “Tume ya Mwakyembe” kuwa imewaonea wanasahau kwamba tume hiyo haikuundwa baada ya Mwakyembe na wenzake kutuma maombi ya kuwa kwenye tume hiyo.Inashangaza wanaolalamika sasa kwamba ripoti ya tume hiyo ilikuwa na ajenda za kumalizana kisiasa,ilhali hawakuipinga wakati inaundwa na pale ilipokuwa ikitimiza majukumu yake.Ina maana ajenda hizo za kisiasa zilianza baada ya akina Mwakyembe kuwa wajumbe wa tume au zilikuwapo kabla.Kama zilikuwapo kabla,kwanini basi waliotajwa kuhusika na kuliingiza taifa katika hasara kubwa kwa mkataba huo wa kizembe hawakulalamika?

Na iwapo ajenda hizo zilianza baada baada ya wajumbe hao kuingia kwenye tume,kwanini basi watajwa walikimbilia kujiuzulu (huku wengine wakigoma waziwazi kujiuzulu kwa kuendelea kung’ang’ania madaraka) badala ya kudai haki itendeke?Ni rahisi kuhitimisha kuwa kelele zinazoendelea hivi sasa ni za mfa maji.

Nakumbuka kwenye miaka ya tisini nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys) tulibahatika kutembelewa na Komandoo Salmin Amour.Nayakumbuka baadhi ya maneno yake ambayo kimsingi yalikuwa na lengo la kutupa changamoto ya mafanikio ya kielimu na hatimaye kufanikiwa maishani (japo sio kila mara kufanikiwa kielimu ni tiketi ya moja kwa moja ya kufanikiwa kimaisha).Alitueleza kwamba madaraka ni mazuri na kutupa mifano ya namna yeye kama rais alivyokuwa na wasaidizi kibao wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vema.

Nilikubaliana na Komando wakati huo,na nakubaliana nae sasa,kwamba madaraka ni mazuri na matamu,na ndio maana tunashuhudia hizi kelele zinazoendelea kutoka kwa waliokumbwa na zahma ya kisiasa baada ya skandali ya mkataba wa kampeni ya Richmond.Hakuna dhambi kwa madaraka kuwa matamu kwani hata njia ya kuyafikia sio nyepesi.Inahitaji jitihada na juhudi za kutosha kufikia hatua ya kuongoza watu wenye akili timamu.Na inatarajiwa kwamba mtu akishapata bahati ya kuwa kiongozi atatambua kwamba wengi,kama sio wote,wa aliokuwa akiwaongoza ni watu wenye akili timamu,uwezo wa kufanya maamuzi na wanaostahili heshima.

Waziri Mkuu aliyepita,Edward Lowassa,ameendelea kuonyesha kwamba japo aliamua kubwaga manyanga kwa hiari yake,alifanya hivyo huku roho ikimuuma.Nasema hivyo kwa sababu kauli zake za hivi karibuni zinaashiria wazi kwamba bado ana kinyongo kikubwa na matokeo ya uchunguzi wa “Tume ya Mwakyembe.”

Lowassa anaamini kwamba atarejea tena kwenye ulingo wa juu wa kisiasa kama Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye alipokuwa Waziri alilazimika kujiuzulu kutokana na skandali iliyoikumba Wizara yake.Tofauti ya msingi kati ya Mwinyi na Lowassa ni ukweli kwamba wakati Mwinyi alijiuzulu kutokana na tukio lililotokea mbali kabisa na mahala alipokuwa akifanyia kazi (lilitokea Shinyanga wakati ofisi ya Mwinyi ilikuwa Dar es Salaam),Lowassa alijikuta akikumbwa na shutuma kuhusu mkataba huo kwa vile katika hatua flani ulipita machoni mwake na akaamua “kusikiliza maamuzi ya wataalamu.”

Uongozi ni pamoja na kuwa na maamuzi ya haraka na yanayoangalia athari zinazoweza kujitokeza mbeleni iwapo yatafanyika maamuzi potofu.Haiyumkiniki kwamba Waziri Mkuu mzima anaweza kusikiliza ushauri mbovu na kuafikiana nao pasipo kujiridhisha iwapo ushauri huo ni wa manufaa kwa taifa.Hilo pekee linamvua sifa ya uongozi mtu yeyote aliye katika nafasi ya juu kitaifa.

Hivi kama mkataba wa Richmond ungekuwa na madhara ya moja kwa moja kwa familia ya Lowassa,kiongozi huyo angeendelea kusikiliza ushauri asio na uhakika na matokeo yake au angetaka kujiridhisha kwamba kilichokuwa kikifanyika hakingekuwa na madhara kwa familia yake?

Tukimweka kando Lowassa kwa muda,tumeshuhudia vituko vingine kutoka kwa Mkurugenzi wa TIC Emmanuel Ole Naiko ambaye anadai kuna dalili za “mauaji ya halaiki” dhidi ya watu wenye asili ya wilaya ya Monduli.Hizi ni hoja mufilisi ambazo kama zitaachwa bila kudhibitiwa zinaweza kuliingiza taifa kwenye matatizo yasiyo na msingi.


Hivi Ole Naiko amefanya utafiti wa kutosha kiasi gani kuthibitisha kwamba kuna mpango wa “ethnic cleansing” dhidi ya watu wa Monduli?Kwa hakika serikali inapswa kumhoji kwa undani mtu huyu mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na matamshi hayo ambayo yanaweza kabisa kuathiri hata utendaji wa ofisi yake (hakuna mwekezaji aliye tayari kuwekeza kwenye nchi inayoelekea kwenye “ethnic cleansing.”)

Kuna tetesi kwamba upo mkakati mkubwa wa “kujibu mashambulizi” dhidi ya ripoti ya “Tume ya Mwakyembe.” CCM imekuwa ikituaminisha kila siku kwamba vikao nje ya chama ni majungu,sasa basi inapaswa kuhakikisha kwamba wote wenye kudhani hawakutendewa haki wawasilishe malalamiko yao kwa ngazi hsuika katika chama hicho au hata bungeni.

Kama taarifa tunazozisoma katika vyanzo mbalimbali kwamba kuna mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM kutokana na skandali la Richmond zina ukweli, basi ni muhimu kwa uongozi wa juu wa chama hicho kuachana na itifaki zake za kawaida za kuwasifia hata wanaostahili kukemewa na badala yake kuwawekwa “kiti moto” waeleze malalamiko yao mbele ya vikao halali badala ya kuendeleza mbinu za chini chini ambazo zinaweza kabisa kuathiri hali ya usalama wa nchi yetu.

Tusirejee makosa yaliyojitokeza katika mkataba wa Richmond ambapo baadhi ya watu walitahadharisha mapema kuhusu uhalali wa kampuni hiyo lakini wakapuuzwa.Kuna watu wanataka urais kwa kutimia njia yoyote ile hata kama kwa kufanya hivyo wanahatarisha uhai wa chama.

Lakini wakati tunawalaumu wanaolalamika kwamba wameonewa na “Tume ya Mwakyembe” tunapaswa pia kujiuliza kama hawapati jeuri hiyo kutokana na uzembe unaendelea wa kutowachukulia hatua wahusika.Pengine jeuri waliyonayo inatokana na ukweli kwamba wanaamini kuwa hakuna mwenye jeuri ya kuwachukulia hatua hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao wameishia kupongezwa kwa “ushujaa wao” badala ya kushutumiwa kwa hasara waliyoisababisha kwa taifa.

Nadhani anachopaswa kufanya Lowassa,Ole Naiko na wengine wote waliohusishwa na mkataba wa Richmond ni kutafuta msaada wa kisheria kuona haki inatendeka upande wao iwapo wanaamini kuwa hawakutendewa haki,badala ya kuendeleza hizi porojo ambazo kwa hakika zinaweza kuua kabisa ndoto zao za kurejea kwenye ulingo wa juu wa siasa za nchi yetu.Mahakama zipo,vikao vya chama vipo,sasa kwanini kelele za kuonewa zisipelekwe huko?TANZANIA NI MUHIMU ZAIDI KULIKO MASLAHI YA MTU BINAFSI.

BAADA YA KUMALIZA KUSOMA MAKALA HII,UNAWEZA KUANGALIA VITUKO VYA SIASA ZA URUSI AMBAVYO VIMEZAA TERM MPYA YA NANO PRESIDENT (as in iPod Nano).BONYEZA HAPA

HALAFU KWA WALE AKINA DADA "WENYE ULIMI MZITO",CLIP IFUATAYO INAWEZA KUWA YA MSAADA WA INA FLANI



Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.