Showing posts with label SIASA NA DINI TANZANIA. Show all posts
Showing posts with label SIASA NA DINI TANZANIA. Show all posts

4 Jul 2009



KWANZA Merged

Picha kwa hisani ya KENNEDY

Wanasema siasa ni mchazo mchafu.Lakini siasa katika bara letu la Afrika ni zaidi ya mchezo mchafu.Ni mchanganyiko wa kanyaboya,songombingo,mbinde,usanii,ufisadi na what have you.Hiyo sio kumaanisha kuwa siasa katika maeneo mengine,kama Ulaya na kwingineko ni safi kihivyo.Lakini angalau hawa wenzetu check-and-balance mechanism zinafanya kazi kwa kiasi kikubwa.Sie tunazo lakini aidha wenye majukumu ya kuzitumia wako bize sana na posho au nyumba ndogo au hawajui kwa nini wapo mahala panapopaswa kufanya hiyo check na balance.

Hivi CCM walikuwa wanafikiri nini mwaka 2005 kuahidi kuwa wangeshughulikia uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi?Binafsi sina tatizo na uanzishwaji wa mahakama hiyo as long as suala hilo linafanywa kwa uangalifu.Sio priority kwa sasa lakini kwa vile ni haki kwa Waislamu,then hakuna budi kuangalia uwezekano huo.Kwahiyo,CCM hawakufanya kosa "kukubali" kuanzisha Mahakama ya aina hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa 2005.Hawakufanya kosa kwa vile wazo hilo sio baya au la hatari kama baadhi ya watu wanavyofikiria.Nitatafuta wasaa mwafaka siku nyingine kuelezea kwanini Waislam wako sahihi kudai mahakama hiyo na kwanini uanzishwaji wake hauna madhara kwa wasio waislam.In fact,suala sio "kuanzisha" bali "kurejesha" kwa vile mahakama za aina hiyo zilikuwepo wakati wa ukoloni na muda mfupi baada ya uhuru.

Kosa la jinai (yes,ni jinai) la CCM ni kutoa ahadi nyeti kama hiyo wakati inafahamu fika kwamba haina muda wa kuishughulikia.Ni kosa pia kwa vile pamoja na ahadi hiyo ya kuanzisha mahakama ya kadhi tayari chama hicho kilikuwa kimeshatoa ahadi nyingine lukuki kana kwamba kinaomba kutawala kwa miaka 100 na sio mitano (2005-2010)!Kulikuwa na ahadi za kuwakalia kooni wala rushwa,kushughulikia kero za Muungano,kuboresha maisha ya Watanzania,na ahadi nyingine kedekede.Si tu kwamba wakati tunaelekea mwishoni mwa miaka hiyo mitano rushwa imeshamiri na ku-mutate into ufisadi (kumbuka,neno hili limejitokeza katika kipindi hiki),kero za Muungano sio tu kuwa bado zipo ila tumeshuhudia "kibiriti kikitikiswa mpaka kinataka kulipuka",na hayo maisha bora kwa kila Mtanzania sanasana yamewezekana kwa mafisadi na washirika zao....

Hili la kuahidi kushughulikia masuala yanayogusa imani (ya kiroho) ilhali hakuna dhamira au uwezo wa kufanya hivyo ni jambo hatari mno.Dini ni hatari zaidi ya ukabila kwani inahusisha uhai na kifo (mtu akifa kwa ajili ya dini ni martyr,at least dini nyingi zinaamini hivyo).

Kauli za viongozi kuhusu suala hili sio tu zimekuwa za kujichanganya bali zimechangia kukuza tatizo hilo.Mara mchakato unaendelea,mara sheria za kiislam zitaingizwa kwenye sheria za mahakama za sasa (hicho tayari kinafanyika),mara hili,mara lile.Kama kawaida,wahusika wanasubiri lilipuke ndio watafute chanzo cha mlipuko.Unfortunately,milipuko mingine ikianza hata huo muda wa kutafuta chanzo hautokuwepo.Waulize Nigeria!

Tuiombee nchi yetu.

3 Jul 2009


Mufti Simba aagiza Waislamu waikatae CCM

Mufti Issa bin Shaaban Simba, amekasilishwa na uamuzi wa serikali kuhusu Mahakama ya Kadhi.

Na Ummy Muya

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kutokana na serikali kutupilia mbali ombi la kunzisha Mahakama ya Kadhi, Waislamu hawataipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika taarifa yake, Bakwata ilifikia hatua ya kusema Waislamu wasimchague Rais Jakaya Kikwete iwapo atasimamishwa na CCM kugombea urais, ikiwa ni pamoja na wabunge na madiwani watakaosimamishwa na chama hicho tawala kutokana na kitendo cha serikali kutupilia mbali hoja ya Mahakama ya Kadhi.

Kauli hiyo imetolewa jana wakati Mufti Issa bin Shaaban Simba alipokuwa akitoa tamko kupinga uamuzi wa serikali kutaka kutumia sheria za dini ya Kiislamu katika mahakama za kawaida badala ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi, kitu ambacho alisema anaamini kitawanyima haki Waislamu.

Alisema serikali imedhihirisha kuwa inaendeshwa na Wakristo na si kweli kama serikali haina dini na akamtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kubatilisha kauli hiyo kwa kuwa inamchafua Rais Jakaya Kikwete mbele ya umma wa Waislamu.

Waziri ametuthibitishia kama Rais Kikwete alikuwa akitulaghai ili tumpigie kura kwa kigezo kuwa suala hilo litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi na sio kuchanganywa kama ilivyokuwa mwaka 1970 katika Sheria ya Ndoa na kuwanyima haki Waislamu,alisema.

Alisema kwa muda mrefu sana Waislamu wamekuwa kimya wakitumia hekima na busara kudai haki zao, lakini katika hatua hii ambayo serikali imefikia hawapo tayari kuendelea kudhalilishwa na kuwa kitendo hicho ni dhalimu.

Mufti alisema wamekuwa wakiiomba Mahakama ya Kadhi kwa zaidi ya miaka 20 na hivyo hawezi kuendelea kuwa kimya na kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kuwa mahakama hiyo ni haki yao.

Alisema kauli ya Waziri Chikawe imedhihirisha kuwa serikali ina wenyewe na Waislamu wamewekwa katika tabaka la pili pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuwatuliza kwa ahadi kuwa watalipatia ufumbuzi suala hilo.

Natoa wito kwa Masheikh wote nchini na Waislamu wa madhehebu yote kupinga vikali kauli iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na kwamba Waislamu waige mfano wa Waislamu wa Afrika Kusini,alisema Mufti na kuhoji:

Kwa nini iwe Afrika ya Kusini na isiwe Zanzibar, Uganda na Kenya ambazo zipo ndani ya Afrika Mashariki? Kwa niaba ya Waislamu nasema serikali haikututendea haki na imetuchukiza sana,alisema.

Alisema lengo la kuomba mahakama hiyo ni kuhakikisha Waislamu wanashughulikia masuala yao ya ndoa na mirathi na si vinginevyo, hivyo waziri asipotoshe jamii kwa kutumia mifano ambayo haiko sahihi.

Mahakama hii haitawakata wezi mikono kwa kuwa nchi hii ina katiba na sheria na sisi tutazirudisha kesi zote za jinai mikononi mwa serikali. Sifahamu hiyo kamati ambayo waziri alisema alikuwa amekaa na kutoa tamko hilo ilikuwa na watu gani,alihoji.

Aliongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo waziri arudi tena na kukutana na masheikh ili apate muongozo wa nini Waislamu wanahitaji na sio kuzungumza bila kuwa na usahihi wa kile anachosema.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya tamko la Bakwata, masheikh walikuwa na mitazamo tofauti. Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum Mussa alisema wapo baadhi ya Waislamu ambao watakubali kutokana na ufinyu wao wa elimu ya dini.

Mussa alisema haoni sababu ya serikali kufanya njia ya mkato katika suala hilo kwani Waislamu wanahitaji Mahakama ya Kadhi kama ilivyo kwa wafanyabiashara ambao wana mahakama yao.

Hukumu inayotolewa katika Mahakama ya Kadhi ni ibada kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) hivyo ni lazima kwa atakayetoa hukumu hiyo awe Muislamu na si vinginevyo,alisema.

Namshanga waziri anapotaka sheria hizi zitumiwe katika mahakama za kawaida. Aliona wapi John akawa imamu,alihoji sheikh huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Naye katibu wa Bakwata wilayani Ilala, Sheikh Issa Ausi alisema historia iko wazi. Waasisi na wanaharakati ambao waliitoa Tanganyika mikononi mwa wakoloni walikuwa Waislamu, na akahoji sababu za serikali kuwa mstari wa mbele kuwafunga midomo leo.

Bakwata imezinduka sasa Waislamu wote tumeungana katika kupigania haki zetu na kutetea maslahi yetu na serikali itambue kuwa Bakwata iko hai hao Wakristo walikuwa wapi wakati sisi tukipigania uhuru,alihoji.

Wakati huohuo, Sheikh Salum Rwambo alisema anawashangaa wabunge Waislamu ambao baadhi ni mahajat na malhaj wanakaa kimya na kushindwa kutetea hoja za msingi na kudai kuwa huo sasa ndio mwisho wao wa kuwaita masheikh na kutaka waombewe dua ili wasipate wepesi katika kampeni zao.

Sheikh Rwambo pia alimsifia mbunge wa Nzega Lucas Selelii kwamba ni miongoni mwa wabunge katika Bunge hilo wanaozungumza ukweli na kwa kujiamini tofauti na wengine ambao wanaenda kukaa bila kufanya kazi zilizowapeleka .


CHANZO: Mwananchi


KWA MWENENDO HUU SI AJABU KUSIKIA HATA WATANZANIA WALIOAHIDIWA MAISHA BORA NAO WAKAJITOKEZA KUDAI HAWAITAKI CCM....HOJA IKIWA MAISHA BORA YALIYOAHIDIWA YAMEISHIA KWA KUNDI DOGO LA MAFISADI PEKEE!

13 Jan 2009

Venance George, Morogoro
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kauli iliyotolewa juzi na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu kupinga oparesheni Sangara inayoendeshwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si kauli ya waislamu wote.
Akizungumza mjini Morogoro kwa niaba ya Kaimu Mufti wa Tanzania,
Shekhe Suleiman Gorogosi, mratibu wa habari wa Bakwata, ustadhi Issa Mkalinga alisema kauli hiyo ni ya waislamu wachache ambao wamekuwa wakitumiwa na viongozi wa kisiasa kwa manufaa binafsi.
Ustadhi Mkalinga pamoja na Mkurugenzi wa Utawala, ustadhi Karim Mataliwa, aakizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kaimu mufti huyo ya kutembelea mikoani kuhamasisha uhai wa baraza, alisema baraza halitambui kauli hiyo na wala halijihusishi na mambo ya siasa.
"Ujue tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu hapo mwakani, hivyo wako baadhi ya wanasiasa wanatumia mwanya wa majukwaa ya dini kupeleka ujumbe wao," alisema.
Akizungumzia ziara ya kaimu mufti mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Utawala alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu aliyojiwekea kaimu mufti ya kutembelea baraza katika mikoa yote Tanzania na kwamba kaimu mufti ametembelea Dodoma na Morogoro na atatembelea mikoa mingine.
Ustadhi Mataliwa alisema lengo la ziara hizo ni kutaka kujua uhai wa baraza na matatizo yanayolikabili baraza katika ngazi hizo ikiwa ni pamoja na kuhimiza kufanya maandalizi ya uchaguzi wa viongozi kuanzia ngazi ya msikiti hadi taifa utakaoanza kufanyika mwezi April mwaka huu.
Wakati huo huo, katika mahojiano na baadhi ya waumini wa dhehebu hilo, mkoani Morogoro wameunga mkono kauli ya Bakwata na kudai kuwa viongozi wa dini ni vema wakafanya shughuli zao za kiroho na kuwaacha wanasiasa kufanya kazi zao za siasa.
Mmoja wa waumini hao, Ismael Rashid, alisema tamko lililotolewa na waislamu katika kongamano la jijini Dar es Salaam la kudai kuwa Chadema haina manufaa na msaada wowote kwa uislamu si maneno ya kiungwaana na si vema kukipakazia chama hicho kwamba ni kikabila na cha kibinafsi.
Rashid ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Jahazi asilia mkoani Morogoro alisema hatua iliyochukuliwa na Chadema ya kuacha kuunga mkono vyama vya CUF na Sauti ya Umma (SAU) ilikuwa ni sahihi kwa sababu chadema walisimamisha mgombea ubunge katika jimbo la Mbeya vijijini lakini vyama hivyo vilimwekea pingamizi mgombea huyo na kuenguliwa.
"Pingamizi hilo lilisababisha mgombea ubunge wa Chadema akaenguliwa kugombea
nafasi hiyo, sasa iweje chadema iwaunge mkono?" alihoji Rashid .
Alisema chama cha Chadema hakiungi mkono kampeni za mgombea wa CUF kwa mdai kuwa chama hicho, mwakani inakusudia kusimamisha mgombea wake katika jimbo hilo kwa hiyo kama Chadema ikiunga mkono CUF itashindwa kusimamisha mgombea wake hapo mwakani.


CHANZO:Mwananchi

24 Oct 2008


Na Peter Edson
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imemuonya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa kauli zake kuhusu kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) zinaweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa na kumtaka aachane nazo au ajiuzulu wadhifa wake.

Tamko hilo la maaskofu wa makanisa ya Kikristo imekuja baada ya Waziri Membe kukaririwa akisema kuwa hakuna athari zozote kwa Tanzania kujiunga na taasisi hiyo, ambayo madhumuni yake ni kutetea binadamu na hasa Waislamu na sehemu takatifu.

Membe alisema hakuna haja ya kuwa na woga wa kujiunga na taasisi hiyo wakati katika mchakato wake wakristo na waislamu watanufaika na miradi itakayokuwa ikisimamiwa na OIC, na akashangaa ujasiri wa Watanzania wa kupambana na matatizo umekwenda wapi kiasi cha kuogopa nchi kujiunga na jumuiya hiyo.

Suala hilo liliwahi kuibuka mwishoni mwa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati vyombo vya habari vilipofichua kuwa serikali ilijiunga kinyemela na jumuiya hiyo. Baadaye viongozi wa serikali walikiri kufanya hivyo kabla ya kujiondoa, lakini safari hii upinzani umekuwa mkubwa zaidi.

Wakitoa tamko lao kwa waandishi wa habari jana, maaskofu hao kutokana makanisa ya kiprotestanti walisema kauli ya Waziri Membe ina lengo la kutetea maslahi ya watu wachache.

Maaskofu hao walisema kwa kuwa katiba ya OIC hiyo inaeleza bayana kuwa italinda mila, desturi na tamaduni za kiislamu, kujiunga na jumuiya hiyo itakuwa ni kukiuka katiba ya nchi inayoeleza kuwa dini ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na kwamba shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Kama serikali ikikubali, kutakuwa ni mwanzo wa kuruhusu kubomoka na kuvunjika kwa amani ya nchi kwa sababu yanagusa hisia na itikadi za wananchi," alisema Askofu Peter Kitula, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kwanza wa CCT.

Askofu Kitula, ambaye alisoma tamko hilo la maaskofu, alisema baada ya kutafakari kwa roho ya kiutume na kinabii wameamua kupinga kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi pamoja na mchakato wa kujiunga na OIC.

Alisema katiba ya Tanzania ibara ya 19 kifungu cha 2 inaeleza wazi kuwa kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Ibara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kwamba mambo ya dini yanatenganishwa kabisa na shughuli za uendeshaji wa nchi," alisema.

Alisema sehemu hiyo ya katiba inapingana na ibara ya 1 kifungu cha 11 ya katiba ya OIC kinachosema kuwa jumuiya hiyo inatetea mila, tamaduni na desturi za kiislamu, kuwalinda na kuwaelimisha wananchi kuhusu uislamu nchini, jambo ambalo askofi huyo alisema linaonyesha wazi kuwa kujiunga na IOC itakuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Alisema siku za hivi karibuni Bunge la Jamuhuri ya Muungano limekuwa likijadili miswada ya sheria ya kuanzisha au kujihusisha na vyombo hivyo viwili, lakini akasema kuwa kushinikiza kukubalika kwake ndani ya bunge ni kwenda kinyume na katiba.

Naye Owdernburg Mdegela, askofu wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT), alisema kitendo cha Waziri Membe kulizungumza jambo hilo bila kulionea haya ni kutetea maslahi ya watu wachache na kuvunja katiba.

Alisema Tanzania ina rasilimali za kutosha hivyo kujiunga na umoja huo kwa lengo la kutafuta misaada ama kutafuta kula na baadaye kupoteza mwelekao wa taifa, ni kujiingiza katika mtego ambao kujinasua kwake kunahitaji gharama ambayo ni kumwaga damu.

"Sisi tunasimama kama viongozi wa kanisa tukimwambia Membe kuwa hafai wadhifa huo, hivyo ni vema akaacha mara moja kutoa kauli zake zisizo na mantiki. Lakini kama hawezi, basi inampasa ajiuzulu," alisema Askofu Mdegela.

Naye askofu wa kanisa pentekoste, Sylivester Gamanywa alisema Waziri Membe anatoa kauli ambazo zina lengo la kuweka hisia binafsi na mgawanyiko wa kitaifa pamoja na kuvunjika kwa amani.

Alisema kitendo cha waziri huyo kusema kuwa serikali inaruhusu fedha chafu na kwamba kama mtu akikuta fedha za shetani inampasa kuzichukuwa, ni kuwadhalilisha Watanzania na taifa lao kwa ujumla.

Naye askofu wa Anglikana, Dk. Stephen Munga alisema kuwa waziri Membe hafai katika kushughulikia masuala ya kitaifa kwani hakuna mamalaka yoyote iliyomuagiza aende kuzungumzia suala la kuaanzishwa kwa OIC.

"Inampasa Waziri Membe afahamu kuwa sisi ni Tanzania na tutafuata mambo yetu na si kuiga masuala ya nje. Anavyosema tuwaige Waganda si jambo sahihi," alisema Dk. Munga.

Alisema kama kanisa msimamo wao ni kuyakataa mambo hayo mawili na kuitaka Serikali na mamlaka zake zote kuacha kuendelea kukaribisha mijadala ya mambo hayo kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda wa wenye dhamana ya mamlaka ya nchi hii na rasilimali zake.

"Tunauhakika kuwa yaliyomo ndani ya OIC ni hatari kabisa, kwani endapo yakikubalika katiba ya nchi itakuwa imevunjwa na Watanzania watakuwa wameingia katika migogoro itakayoua maridhiano, mshikamano, utengemano na umoja wa kitaifa," alisema Askofu Kitula.

"Kwa kuzingatia wajibu wetu wa kinabii na kiutume, tunatoa wito kwa bunge kutoruhusu kamwe uanzishwaji wa mahakama ya kadhi kwa kupitia mchakato wa utendaji wa mamlaka ya nchi, pia kutoridhia uanachama wa Tanzania katika OIC."

Akizungumzia tamko la maaskofu, mwenyekiti wa kamati ya msikiti wa Idrissa, Sheikh Ally Basaleh alisema kuwa awali kabla ya kuanza kwa mchakato wa masuala hayo serikali ilishafanya uchambuzi wa kina na kugundua umuhimu wa kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

"Kauli za maaskofu hawa na viongozi wa kanisa zinadhihirisha kuwa wanakataa maamuzi yao ya awali kwamba Rais Jakaya Kikwete ni mteule wa Mungu, kwani ndiye anayesimamia masuala haya yote," alisema Basaleh.

Alisema waislamu ni sehemu ya jamii hivyo wao kama viongozi wa dini wanaandaa mchakato wa kutoa tamko litakalokuwa likitoa mchanganuo kuhusu uhalali wa kuanzishwa kwa vyombo vyote hivyo viwili nchini.
CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.