Zikiwa zimesalia siku 14 kufika siku ya uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mambo si shwari katika mchakato wa kumpata mwenyekiti wake.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mjini Dodoma Januari 7, mwakani ambapo nafasi ya uenyekiti itagombewa na Janet Kahama, Sophia Simba na Joyce Masunga.
Hali hiyo, ambayo inazidi kuipaka matope CCM, imedhihirika baada ya mgombea wa nafasi ya Janeth Kahama kuwasilisha rasmi malalamiko kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akimtuhumu mpinzani wake, Sophia Simba kwamba amewahonga wajumbe wote wa Mkutano Mkuu rushwa ya Sh. 100,000 ili wampe kura.
Mbali na tuhuma za rushwa, Simba, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), anatuhumiwa pia na Kahama kuwa yeye na wapambe wake wamekuwa wakiitumia Ikulu kuwaomba kura wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Kahama, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), amewasilisha malalamiko hayo kupitia barua yake yenye kumbukumbu Na. JBK/01/08 ya Desemba 20, mwaka huu, iliyopelekwa kwa Rais Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Nakala ya barua hiyo, ambayo Nipashe inayo, imepelekwa kwa Katibu Mkuu wa UWT Taifa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Makamba alipoulizwa na Nipashe juzi jioni kama amepokea nakala ya barua hiyo, alithibitisha kuipokea.
Simba anadaiwa kutoa hongo hiyo kupitia kadi alizochapisha kwa lengo la kuwatakia heri ya Mwaka Mpya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa.
Kadi hizo, ambazo zinadaiwa kusambazwa na Diwani wa Kata ya Ilala, Moshi Kondo, zina picha, jina na saini ya Waziri Simba, kalenda ya Mwaka Mpya wa 2009 na nembo ya CCM.
Barua hiyo yenye kichwa cha habari kisemacho: `Yah: Malalamiko dhidi ya Mhe. Sophia Simba kugawa vipeperushi mikoani`, Kahama anamueleza Mwenyekiti Kikwete kama ifuatavyo:
``Kwa heshima ya pekee, nakuomba uhusike na mada ya barua hii kama inavyosomeka hapo juu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, Jumuiya yetu ya UWT hivi sasa ipo katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya taifa unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.``
``Mimi nikiwa mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, natambua kuwa wagombea wote tulizuiwa na vikao vya UWT Taifa kutoa vipeperushi vya aina yoyote kwa minajili ya kujinadi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa UWT.``
``Lakini, ajabu ni kwamba, mgombea mwenzangu, Bi Sophia Simba amechapisha kalenda na kadi za `Heri ya Mwaka Mpya` zenye picha yake na nembo ya CCM na kuzisambaza kwa wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa nchi nzima, ndani zikiwa na kitita cha Sh. 100,000 (kwa kila kadi).``
``Mheshimiwa Mwenyekiti, nalazimika kukuandikia waraka huu ili kukupa angalizo juu ya suala hilo hasa ikizingatiwa kuwa Mheshimiwa Sophia Simba ni Waziri katika ofisi yako mwenye dhamana ya Utawala Bora.``
``Hivyo hatua yake na nembo ya CCM, inakwenda kinyume na kanuni za uchaguzi za CCM, kipengele cha Miiko ya Kuzingatiwa wakati wa Shughuli za Uteuzi na Uchaguzi`, ibara ya 33 kifungu kidogo cha 14 kinachosema: `Ni mwiko kutumia makaratasi ya kampeni nje ya utaratibu wa chama au kutumia vishawishi vya aina yoyote ile kwa minajili ya kupata kura.``
``Je, hatua hii ya Mheshimiwa Simba kuchapisha nyaraka hizo zenye picha yake na nembo ya CCM na kuzitawanya nchi nzima, si uvunjaji wa makusudi wa kanuni hizo za uchaguzi za CCM tena kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa UWT?``
``Je hatuoni kwamba hatua yake hiyo ambayo haijakemewa mpaka sasa ni kielelezo kingine cha ubabe na matumizi mabaya ya madaraka yake kama Waziri tena mwenye dhamana ya Utawala Bora?
Nasisitiza hili kwa sababu Mheshimiwa Simba na wapambe wake wamekuwa wakipita mikoani na kupotosha wapigakura kuwa yeye ndiye chaguo la Ikulu.``
``Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha kwako waraka huu wenye malalamiko haya ili uweze kujua nini kinaendelea na kuchukua hatua kwani kama kitaachwa, kinaweza kujenga matabaka ndani ya UWT na mpasuko usio wa lazima ndani ya chama chetu, hasa pale hisia za mgombea mmoja kuandaliwa mazingira ya ushindi dhidi ya wenzake zinapoanza kujengwa.``
``Naambatanisha moja ya vipeperushi hivyo vya Mheshimiwa Simba vilivyosambazwa mikoani kinyume na utaratibu nilioueleza hapo juu.``
Makamba alipoulizwa na Nipashe juzi, licha ya kukiri kupokea nakala ya barua hiyo ya Kahama, alimtaka mwandishi kama ana swali lolote kuhusiana na suala hilo, akamuulize Rais Kikwete kwa vile ndiye aliyeandikiwa barua hiyo.
``Mtafute Mwenyekiti wa CCM, yeye ndiye aliyeandikiwa barua, aliyeandikiwa ndiye anayejibu. Mimi nimepewa nakala, anayepewa nakala, anaarifiwa tu,`` alisema Makamba.
Nipashe ilipowasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema kwa vile malalamiko ya Kahama yanahusiana na Chama, anayepaswa kujibu suala hilo ni Katibu Mkuu.
Baada ya Makamba kuulizwa tena, alisema: ``Mimi sina cha kusema, sijaisoma (hiyo barua), sijajua maudhui.
Nitakapoisoma na kujua maudhui, nitatoa maoni yangu.``
Kahama alipoulizwa na Nipashe jana kama barua hiyo ndiye aliyeiandika, hakukiri wala kukanusha, badala yake alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kwa vile kipindi hiki ni cha sikukuu ya Krismasi, ambayo yeye kama Mkristo anapaswa kuitukuza.
``Sina comments (maoni) kabisa kabisa, mpaka nionane na Katibu Mkuu. Pia mimi ni Mkristo na kipindi hiki ni cha Krismasi,`` alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Ilala, Moshi Kondo, alipoulizwa juzi, alikataa kuzungumzia suala hilo, badala yake alimtaka mwandishi akamuulize Simba.
``Kwani Sophia Simba mimi ni nani kwake?`` alihoji Kondo, ambaye alipojibiwa na mwandishi kuwa ``Simba anadaiwa kuwa ni mtu wake wa karibu``, alisema: ``Nenda kamuulize Simba.``
Tangu juzi hadi jana jioni Nipashe ilimtafuta Simba bila kumpata na baadaye kuelezwa na mmoja wa wanafamilia yake kuwa yuko safarini Malaysia.