16 Aug 2012


Home
TUMEROGWA na aliyeturoga naye karogwa, kisha kafariki.”
Hapana, hatujarogwa ila nadhani bongo zetu zimefungwa, na funguo zimetumbukia chooni.”
Hizo ni baadhi ya kauli zinazoanza kuzoeleka masikioni mwa Watanzania wanapojadili mustakabali wa nchi.
Ukisikia kauli hizo unaweza kuishia kucheka kwa kuzitafsiri kuwa ni utani tu. Lakini ukichukua muda kuzitafakari, unaweza kujikuta unaungana kimtizamo na watu hao.
Hivi katika mazingira ya kawaida unawezaje kuelezea ‘busara’ za Kamati ya Olimpiki kujaza viongozi wengi zaidi wa wanamichezo kwenye msafara wa wawakilishi wetu kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto yaliyomalizika juzi jijini London, hapa Uingereza?
Wakati wenzetu Wakenya wakirejea na medali kadhaa huku Waganda wakijivunia medali ya dhahabu, sisi tumeendelea kupigilia mstari ‘sifa’ yetu ya kuwa kichwa cha mwendawazimu.
Lakini ukidhani uhuni huo katika ushiriki wetu kwenye Olimpiki unachefua, basi sikiliza hii ‘kali kubwa’ kutoka kwa Bunge letu tunaloliita ‘tukufu.’ Wiki iliyopita, Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai aliwaeleza Watanzania kuwa baadhi ya wawakilishi wao bungeni (wabunge) wamekuwa wakiingia kwenye vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria wakiwa wamelewa pombe na sigara zisizo za kawaida.
Kabla hatujaenda mbali kujadili taarifa hii ya kuogofya ni vema tukakumbushana kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya hivi karibuni, waheshimiwa wabunge wanalipwa shilingi milioni 11 kwa mwezi. Ni muhimu kutaja kiwango hicho ili tunapowajadili watu hawa tuwe na uelewa kuwa pamoja na umasikini wa nchi yetu tumejikamua na kuwapatia waheshimiwa hawa maslahi manono kabisa.
Kwa namna fulani ninampongeza Naibu Spika Ndugai kwa kutufungua macho kuhusu swali ambalo ninadhani wananchi wengi wamekuwa wakijiuliza, “kwanini baadhi ya waheshimiwa huonekana wamelala bungeni huku kikao kinaendelea?”
Mitandaoni kumejaa picha za ‘wachapa usingizi bungeni’ na kuna waheshimiwa wengi tu wanaopenda kuligeuza Bunge kuwa sehemu ya kulala.
Baadhi yetu tulipoona picha za aina hiyo tulijaribu kujipa matumaini kuwa labda waheshimiwa hao wanazidiwa na usingizi kwa vile ‘wanakesha wakitafakari jinsi ya kuwatumikia wapigakura wao, na pengine nchi kwa ujumla, kwa ufanisi mkubwa zaidi.’
Kadhalika, kauli ya Ndugai imetusaidia pia kutupa mwanga kuhusu michango ya baadhi ya wabunge ambayo mwananchi hawezi kulaumiwa akihisi mchangiaji anatafuta nafasi ya ushiriki wa Bongo Star Search kwa kipaji cha mipasho. Inakera lakini ndio ukweli wenyewe, baadhi ya waheshimiwa hutumia fursa ya kuchangia hoja kuonyesha umahiri wao wa kukebehi, kudhihaki na hata kutusi.
Lakini kilichonikera katika maelezo ya Ndugai ni ‘utetezi wa kitoto’ kuwa, (ninamnukuu) “Wabunge ni watu kama watu wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine, wapo ambao kwa namna ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya kuanzia mchana wakiwa wamepiga bia.”
Kwanza, wabunge wetu si sawa na ‘watu wengine.’ Ni ‘watu wengine’ wangapi wanaitwa ‘waheshimiwa’? Na ni wangapi wanaolipwa posho kwa kutimiza wajibu wao (licha ya kulipwa mshahara kwa nyadhifa zao)? Na ni ‘watu wengine’ wangapi wanaolipwa mishahara minono japo kwa kiasi kikubwa ufanisi wao upo zaidi kwenye mipasho, kukashifiana na porojo nyingine zisizomsaidia Mtanzania?
Ndugai hayupo sahihi kudai kuwa wabunge wanaoingia bungeni wamelewa ‘wana tabia kama walivyo binadamu wengine.’ Mimi kama mwanafunzi siruhusiwi kuingia darasani nikiwa nimelewa. Hata kwenye sehemu za vinywaji ‘baamedi’ haruhusiwi kuingia kazini amelewa. Sasa hao ‘binadamu kama wengine’ anaotueleza Naibu Spika wametoka sayari gani?
Halafu cha kuchukiza zaidi ni ukweli kwamba Naibu Spika anafahamu kuwa kuna wabunge wanaingia kwenye vikao vya Bunge wakiwa wamelewa lakini hachukui hatua zozote bali anasubiri hadi apate nafasi ya kumwaga jambo hilo kwenye mahojiano na kituo cha runinga.
Huyu ni kiongozi dhaifu. Japo tunaweza kumpongeza kwa ‘kutuibia siri ya yanayojiri bungeni’ lakini dhamana aliyokabidhiwa si kunyooshea watu vidole (kwa maana ya kubainisha kuna wabunge walevi) bali kuchukua hatua stahili dhidi ya ‘wahalifu’ hao.
Na si kama nimetumia neno ‘wahalifu’ kwa bahati mbaya. La hasha. Mtu anayelipwa shilingi milioni 11 kama mshahara wa kumwakilisha mwananchi, kisha akaamua kufanya uwakilishi huo akiwa amepata bia kadhaa, au amevuta sigara isiyo ya kawaida (bangi?) au amelamba vitu fulani (‘unga’-madawa ya kulevya?), hana tofauti na mhalifu.
Ni jambazi anayesababisha watu waishi kwa shida ili wamudu maslahi yake kwa matarajio kuwa maslahi hayo manono yataleta ufanisi katika kazi lakini yeye anaishia kutekeleza majukumu yake akiwa na ‘faida kichwani’ (kalewa)!
Katika moja ya makala zangu huko nyuma niliweka wazi msimamo wangu kuwa mishahara mikubwa kupita kiasi ya wabunge wetu ni ujambazi wa mchana kweupe (daylight robbery) kwa sababu haiendani na hali mbaya ya uchumi watu. Na sasa ujambazi huo unajidhihirisha bayana kwa uhuni wa baadhi ya waheshimiwa wanaopuuza kanuni za Bunge na wajibu wao, na kutinga bungeni wamelewa.
Lakini kuna swali moja la msingi ambalo kila Mtanzania anapaswa kujiuliza, “IMEKUWAJE TUMEFIKA MAHALA BAADHI YA WABUNGE WANATINGA BUNGENI WAKIWA WAMELEWA?”
Msomaji mmoja wa jarida hili, Omary Abdallah, Mtanzania anayeishi nchini Ujerumani alinitumia ujumbe kupitia mtandao wa facebook akishauri kuwa badala ya kuendelea kuwalaumu viongozi wabovu inabidi sisi Watanzania wenyewe tuangalie mapungufu yetu yanayotufanya kuchagua viongozi wasiofaa (kwa mfano hao walevi).
Kwa kifupi, msomaji huyo anahitimisha kuwa Taifa limegubikwa na utapeli na uvivu. Rejea kwenye kampeni za ubunge. Utaona mgombea ‘anatoka jasho mwilini na mapovu mdomoni’ kuwahadaa wapigakura jinsi anavyowajali. Na kwa uvivu wetu wa kufikiri, wala hatuhoji iwapo ‘uchungu’ wa mgombea huyo ni kwa ajili ya maslahi yetu au ya tumbo lake (na pengine ‘nyumba ndogo’ zake). Matokeo ndio hao tunaoambiwa wanatuwakilisha wakiwa wamekunywa, kuvuta au kulamba kilevi.
Lakini pia, katika skandali hii ya ulevi wa baadhi ya wabunge, ninaona kipato cha waheshimiwa hao kuwa miongoni mwa vichocheo vya kuwasahaulisha wajibu wao.
Katika mazingira ya kawaida tu, mtu anayepewa fedha nyiiingi zaidi ya mahitaji yake anaweza kuishia kufanya mambo ya ajabu kabisa. Kwa huku Ughaibuni tunashuhudia baadhi ya wanasoka, kwa mfano, ambao wanalipwa mamilioni ya fedha, na kuna aina ya mwafaka wa kimtizamo kuwa ‘madudu’ yanayofanywa na baadhi yao yanachangiwa na wingi wa fedha usiowiana na mahitaji yao ya kawaida.
Suala la nyongeza ya mishahara ya wabunge linaonekana kama limeridhiwa na umma. Wakati madaktari na walimu wakiambiwa serikali haina fedha za kuboresha stahili na mazingira ya kazi zao, hatujapewa sababu za msingi za kuongeza mishahara ya wabunge ambao tayari walikuwa na mishahara mikubwa kabisa.
Utendaji kazi wa wengi wao hauendani na hata ‘kidogo’ walichokuwa wanapewa kabla ya mishahara mipya. Ikumbukwe kuwa mamilioni hayo kwa wabunge wetu ni fedha za walipakodi ambao wengi wao ni masikini wa kupindukia. Kuna kila sababu ya si tu kulaani ‘unyonyaji’ huu bali pia kuupinga kwa nguvu zote.
Sasa, kwa vile tumeruhusu ubunge uwe njia ya mkato ya kukwaa utajiri basi tutarajie kuona chaguzi zetu huko mbele zikiandamana na kila aina ya vituko na vioja miongoni mwa wanaotaka kuwa sehemu ya ‘mradi huu wa utajiri wa chap chap’ (get-rich-quick scheme).
Katika hali ya kawaida tu, nani asiyetaka kulipwa japo shilingi elfu kadhaa tu kwa kazi ya kulala huku una bia mbili tatu kichwani? Ni kama kwenda baa kisha unalipwa kwa kulewa.
Naomba ieleweke kuwa si kila mbunge hatimizi wajibu wake. Kuna wazalendo wachache wanaotambua majukumu yao. Baadhi yao, wameishia ‘kuumbuliwa’ na Kiti cha Spika kwa ‘kukiuka kanuni za Bunge (isomeke: kutetea maslahi ya wapigakura katika namna isiyokubalika kwa watawala).
Mashujaa hawa wachache wana ujasiri wa ziada kwani wakati wao wanatolewa nje kwa kutimiza wajibu wao, wanashuhudia baadhi ya wanaoachwa waendelee na vikao wakiwa wamelala kutokana na kinywaji, sigara zisizo za kawaida au kulamba vitu flani.
Nimalizie kwa kurejea maswali niliyoyanukuu mwanzoni mwa makala hii. Tumerogwa na aliyeturoga nae karogwa kisha kafariki, au akili zetu zimefungwa kisha ufunguo umepotea? Naomba usinijibu bali jibu lako liwe kwenye sanduku la kura katika uchaguzi ujao.
Penye nia pana njia



Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu,makala yangu katika jarida la Raia Mwema toleo la Jumatano iliyopita (Agosti 8, 2012) haikuwekwa mtandaoni japo ipo gazetini.Kwa faida ya wasomaji,nimelazimika kuiweka hapa (inaweza kuwa na tofauti chache na iliyopo gazetini ambayo imehaririwa)


MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA AGOSTI 8
Kwa zaidi ya wiki moja sasa kumekuwepo habari zisizopendeza kuhusiana na tatizo la muda mrefu la mpaka kati ya Tanzania na Malawi.

Ningependa kukiri hadharani kwamba pamoja na kiu yangu kubwa ya ufahamu wa masuala mbalimbali sikuwahi kujibidiisha kufuatilia kwa undani chanzo cha tatizo hilo. Na pengine kuliita suala hilo ‘tatizo’ ni kulipunguzia uzito kwani ukichambua kwa makini kauli mbalimbali kutoka kwa baadhi ya viongozi wetu na wenzao wa Malawi, kinachoendelea hivi sasa kinaweza kabisa kuitwa ‘mgogoro wa mpaka kati yetu na Malawi.’

Katika baadhi ya mitandao ya jamii, ambayo baadhi yetu inatusaidia sana kufuatilia mambo mbalimbali huko nyumbani kumeanza kujitokeza hofu ya vita kati ya nchi hizi ambazo licha ya ujirani zina ukaribu mkubwa kwa sababu ya mwingiliano wa makabila.

Hata hivyo, wakati hofu hiyo ya vita kati yetu na Malawi ikianza kukua, kuna mambo kadhaa yanayopaswa kujadiliwa kwa uwazi. Lakini pia ningependa kuweka wazi msimamo wangu kuwa ninaamini ufumbuzi pekee na wenye manufaa katika mgogoro huu ni kwa njia za amani.

Na moja ya sababu kubwa ya kutaka mgogoro huu utatuliwe kwa njia za amani ni kumbukumbu niliyonayo ya vita pekee nilivyowahi kushuhudia katika uhai wangu hadi sasa. Bado nina kumbukumbu nzuri ya vita ya Kagera kati yetu na Uganda, ambapo wakati huo nilikuwa mtoto mdogo ninayeishi na wazazi mkoani Kigoma.

Moja ya kumbukumbu zinazoniogofya hadi leo ni pale wakazi wa mji huo walipotakiwa kuchimba mahandaki kama hatua ya kujilinda. Kulikuwa na taarifa kwamba ‘swahiba’ wa nduli Idi Amin wa Uganda, aliyekuwa Rais wa ‘Zaire’ (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo-DRC) dikteta Mobutu, alikuwa na mpango wa kumsaidia Amin kushambulia Kigoma hasa kwa vile mkoa huo unapakana na DRC.

Ninakumbuka hofu tuliyokuwa nayo kila tuliposikia mlio wa ndege angani, tukidhani ni ndege za Mobutu zimekuja kutuangamiza. Bahati nzuri hadi vita hiyo inamalizika hakukuwa na shambulio lolote kwa mji huo.

Kwa kuzingatia kumbukumbu hizo, nisingependa kuona Watanzania wenzangu wakirejea kwenye hofu kama hiyo iliyotukumba sie wakati wa vita hiyo kati yetu na Uganda.

Lakini kuna jambo jingine linalonipa hofu zaidi. Katika moja ya shahada zangu za Uzamili nimesoma Stadi za Vita (War Studies), na katika kozi hiyo tulitumia muda mwingi mwanafilosofia mahiri wa masuala ya vita, Mchina Sun Tzu. Moja ya mambo yanayousiwa na Sun Tzu kuhusu maandalizi ya vita ni hili

Sanaa ya vita inatufundisha sio kutarajia kuwa adui hatotuvamia bali maandalizi yetu katika kukabiliana nae, na sio katika uwezekano kuwa (adui) hatoweza kutuvamia bali uimara wa nafasi yetu ‘kutohujumika’ (unassailable).”

Licha ya sote kuwa na mapenzi kwa nchi yetu, tukiangalia mwenendo wa mambo huko nyumbani kwa sasa, jambo tusilotaka kabisa kusikia kwa sasa ni vita. Mmoja wa ukweli mchungu ni kwamba hadi sasa tumeshindwa kukabiliana na maadui kadhaa wa ndani ambao hawana silaha bali fedha na porojo zao. Hapa ninawazungumzia mafisadi na maharamia wengine wanaoifanya Tanzania yetu kuwa katika umasikini tusiostahili.

Lakini pia uimara wetu kukabiliana n adui si wenye kutoa matumaini. Katika siku za karibuni tumeshuhudia migomo ya madaktari na baadaye walimu, wote wakidai kuboreshewa maslahi yao. Wakati watawala wetu wanadai serikali haina fedha za kuboresha maslahi ya watumishi wake, imemudu kupandisha mishahara ya wabunge hadi kufikia shilingi milioni 11 kwa kila mmoja wao.

Je inawezekana chokochoko kutoka Malawi zinachangiwa na uelewa wa nini kinachoendelea nchini mwetu? Lakini hata kama hiyo si sababu, je katika mazingira haya ya kuendekeza anasa kwa tabaka dogo huku wengi wa wananchi wakizidi ‘kupigika’ kutokana na uchumi dhaifu unaozidi kudhoofeshwa na majambazi wanaopora raslimali zetu kila kukicha, tunaweza kweli kukabiliana na adui huku tukiwa na uhakika wa kumshinda?

Ninatambua kuwa ninaweza kuonekana msaliti kwa nchi yangu kwa kubainisha hoja hizo hapo juu lakini kama nilivyotanabaisha hapo awali, ningependa, na ninataraji, mgogoro huu utamalizwa kwa njia za amani.

Nimeeleza hapo mwanzo kuwa sikuwahi kujishughulisha kufuatilia chanzo cha mgogoro ‘wa muda mrefu’ wa mpaka kati yetu na Malawi. Lakini jitihada kidogo tu ziliniwezesha kukutana na makala ya kitaaluma, ambayo licha ya kuwa ilichapishwa mwezi Disemba mwaka 1973, bado ina maelezo muhimu kuhusu mgogoro huo.

Katika makala hiyo, The Malawi-Tanzania Boundary Dispute (mgogoro wa mpaka wa Malawi na Tanzania) iliyoandikwa na James Mayall, na ambayo ni mapitio ya kitabu (book review) kuna taarifa ambazo kwa namna flani zinatoa taswira ya ‘msimamo wa kukanganya’ kwa baadhi ya viongozi wetu, ikiwa ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa makala hiyo, awali viongozi wetu wakiongozwa na Nyerere waliridhia kuwa Ziwa si letu bali la Malawi. Kwa kiasi kikubwa msimamo huo ulionekana kuchagizwa na dhamira ya nchi yetu katika umoja wa nchi za Afrika.

Japo sitaki kuchukulia makala hiyo kama ukweli halisi kuhusu chanzo cha mgogoro huo, mwandishi alijitahidi kwa kiasi kikubwa kubainisha jinsi suala hilo lilivyochukuliwa kuwa la kiutawala zaidi kuliko la kisheria.

Inavyoelekea, kwa mujibu wa Mayall, moja ya sababu zilizopelekea nchi yetu kubadili msimamo wake wa awali kuwa Ziwa hilo si letu ni uhusiano wa karibu kati ya aliyekuwa Rais wa Malawi, dikteta Kamuzu Banda na utawala wa makaburu. Kama ambavyo inaelezwa kuwa moja ya vipaumbele vilivyopelekea Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni sababu za kiusalama, umuhimu wa sehemu ya Ziwa hilo kumilikiwa nasi unaelekea kuchangiwa na sababu kama hizo.

Kadhalika, makala hiyo inajenga picha moja ambayo yayumkinika kuhisi kuwa inaweza kurandana na sababu za sasa za kurejea kwa mgogoro huo. Mwandishi Mayall alieleza kuwa katika wakati flani huko nyuma kulikuwa na hisia kwamba hoja ya Malawi kumiliki Ziwa lote ilihamasishwa na utawala wa Makaburu (waliokuwa wakitawala baadhi ya nchi za kusini kabisa mwa Afrika) na Wareno (waliokuwa wakitawala Msumbiji).

Kisichopendeza kwa Mtanzania yeyote kuhusu makala hiyo ni ukweli kwamba msimamo wa awali wa nchi yetu ulikuwa ni pamoja na kuwaachia Wamalawi waamue wenyewe ‘kutuachia’ sehemu ya Ziwa Nyasa na pia kauli mbalimbali zilizoonyesha kuafiki kuwa Ziwa hilo si sehemu ya nchi yetu, japo baadaye msimamo huo ulibadilika.

  Ningependa sana kuitafsiri makala hiyo nzima kwa Kiswahili lakini nafasi hairuhusu, na pengine kufanya hivyo kunaweza kuwavunja moyo baadhi ya Watanzania wenzangu na pengine kuanza kuamini kuwa sie ndio chanzo cha chokochoko zilizopelekea mgogoro huo kufikia hatua ya sasa. Hata hivyo, iwapo kuna msomaji atahitaji nimsaidie kutafsiri makala hiyo ya Kiingereza, nipo tayari kufanya hivyo.

Wakati ninajipa matumaini kuwa mgogoro huo utamalizwa kwa amani, ninajikuta nikikabiliana na maswali kadhaa ambayo ninachelea hata kudadisi majibu yake. Kwa mfano, itakuwaje iwapo Malawi watapuuza onyo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kuwa makampuni yanayojihusisha na uchimbaji raslimali katika Ziwa hilo yasitishe kazi mara moja?

Wakati viongozi kadhaa huko Malawi wametoa kauli za kuleta matumaini kuwa kilichopo si mgogoro kwa vile nchi zetu zipo katika mahusiano mazuri, takriban wote wanaonekana kuwa na msimamo unaorandana kwamba Ziwa Nyasa lote ni la nchi hiyo.
Hapo huhitaji uelewa wa mambo ya diplomasia kuhitimisha kuwa kinachoongelewa na viongozi hao ni kupunguza tu hofu kwa wananchi lakini pasipo kurudi nyuma katika msimamo kuwa Ziwa hilo ni lao lote na hawapo tayari kuliachia.

Lakini kuna swali jingine la msingi zaidi. Je jeuri ya Malawi inatoka wapi? Je inachangiwa na makampuni yanayochimba raslimali katika Ziwa hilo? Je inachangiwa na uelewa kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na ‘mizigo mikubwa’ kiasi cha kuiaminisha nchi hiyo kuwa hatuna uwezo wa kuwakabili? Na swali ambalo pengine ni gumu zaidi, je tuna uwezo wa kurejea ‘tulichomfundisha Nduli Idi Amin mwaka 1978-79?

Ili uingie vitani ni lazima uwe na taarifa sahihi dhidi ya adui yako. Je taasisi zetu zinazoonekana kama zimesalimu amri kwa mafisadi wanaotafuna nchi yetu zina uwezo wa kukusanya taarifa muhimu za kiusalama ili pindi tukiamua ‘liwalo na liwe’ dhidi ya Malawi tusiishie kujilaumu?

Vyovyote itakavyokuwa (huku tukiamini kuwa hakutokuwa na haja ya matumizi ya nguvu kutatua mgogoro huo) suala moja muhimu ni kuutumia mgogoro huu kama fursa ya kusaka suluhisho la kudumu.Kama ambavyo matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unavyoendelea kuzalisha matatizo hususan kutokana na kukosekana utashi wa kisiasa kumaliza matatizo yaliyopo, mgogoro huu kati yetu na Malawi ambao umedumu kwa takriban nusu karne sasa unahitaji kumalizwa. Lakini ili hilo liwezekane ni muhimu kwa watawala wetu kuelewa vipaumbele vya taifa letu.

Na kwa vile katika mazingira tuliyonayo tunalazimika kuwa kitu kimoja (na kuweka kando ukweli kuwa baadhi ya wenzetu wameigeuza nchi yetu kuwa kitegauchumi chao) na tunalazimika pia kuwaamini watu walewale ambao ‘wanadai hawajui chanzo cha umasikini wetu’, basi ni muhimu Tuweke kando tofauti zetu na tuwe tayari kulinda na kutetea kile tunachoamini ni halali yetu.

Nimalizie kwa kutoa wito kuwa suala hili nyeti lisigeuzwe turufu ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.Tusiruhusu wababaishaji wakurupuke na kauli za kusaka umaarufu pasipo kuwa na mikakati ya namna ya kutatua mgogoro huu kwa njia za amani.

Kwa jirani zetu wa Malawi na hususan Rais Banda, wito wangu kwao ni huu: amani ni muhimu kwetu sote, lakini wakati mwingine inalazimu kutumia mabavu ili kuleta amani ya kudumu. Pamoja na matatizo yetu, mie na pengine kila Mtanzania anaamini kuwa kamwe hatutoruhusu Ziwa Nyasa ligeuzwe ‘uwanja wa kutupima ubavu.’ Tulimsambaratisha Nduli Amin kwa sababu nia tulikuwa nayo, sababu tulikuwa nazo, na uwezo pia tulikuwa nao. Hata kama itaonekana kwa Wamalawi kuwa nia, sababu na uwezo wetu ni hafifu kwa sasa, hakuna Mtanzania aliye tayari kuona ardhi ya nchi yake ikimegwa au mipaka yetu ikichezewa.

Mwanafalsafa Sun Tzu anaonya; “gharama ya vita ni kubwa kuliko ushindi wowote utakaopatikana”   na “wanaoingia vitani hufanya hivyo wakiongozwa na ‘miscalculations’ hasa imani kuwa watashinda...lakini vita ikimalizika hujikuta wana hasara kubwa kuliko kabla hawajaingia vitani.

Mungu Ibariki Afrika

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com   





9 Aug 2012




Picha zote mbili zinamwonyesha Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta alipotembelea maonyesho ya kilimo ya Nane Nane mkoani Morogoro.Katika picha zote,Waziri Sitta ameambatana na mlinzi (BODIGADI) kutoka Idara ya Usalama wa Taifa.Ninakumbuka,uamuzi wa kumpatia Sitta ulinzi ulifanywa na Serikali wakati waziri huyo alipokuwa Spika wa bunge lililopita,na alidai anatishiwa maisha.Je matishio hayo bado yanaendelea?Ikumbukwe,gharama za kutoa ulinzi kwa kiongozi ni kubwa sana,na kimsingi,kiprotokali,Sitta hastahili kuwa na bodyguard....unless tumembiwe kuwa tishio dhidi ya maisha yake bado lipo hai 



Picha kwa hisani ya AudifaceJackson Blog


8 Aug 2012

 


JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALI ASILI NA UTALII
 
 





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI – (PRESS RELEASE) ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. BALOZI KHAMIS .S. KAGASHEKI LIWALE
TAREHE 8/8/2012


NDUGU WAANDISHI WA VYOMBO VYA  HABARI:

1.0    SALAMU ZA JUMLA:
NACHUKUA NAFASI HII KUWAKARIBISHA NA KUWAPONGEZA KWA JINSI MNAVYOSHIRIKIANA NA WIZARA HII KUPIGA VITA UHALIFU / UJANGILI WA RASILIMALI ZA TAIFA. AIDHA NATAMBUA JINSI MLIVYOTENGA MUDA WENU  NA KUFIKA HAPA ILI TUPEANE TAARIFA ZA KIUTENDAJI HUSUSANI OPERESHENI INAYOENDELEA KATIKA WILAYA YA LIWALE MKOA WA  LINDI.

NDUGU WANAHABARI:
2.0           UTEKELEZAJI WA  OPERESHENI:
KUMEKUWA NA ONGEZEKO LA VITENDO / WIMBI LA UHALIFU / UJANGILI WA NYARA ZA SERIKALI AMBAO UNAATHIRI RASILIMALI ZA TAIFA HUSUSANI WANYAPORI TEMBO, VIBOKO, SIMBA, MAMBA, TWIGA, NYATI NA WANYAMA WENGINE PAMOJA NA UVUNAJI HARAMU WA MAZAO YA MISITU. KUTOKANA NA HALI HIYO, WIZARA YA MALI ASILI NA UTALII ILIOMBA KUSHIRIKIANA NA JESHI LA POLISI KUPITIA WIZARA YA MAMBO NDANI YA NCHI KUANDAA OPERESHENI MAALUM WILAYANI LIWALE KUDHIBITI HALI HIYO. JESHI LA POLISI LILIKIAGIZA KITENGO CHA KUPAMBANA NA UHALIFU MKUBWA NCHINI (NATIONAL AND TRANSNATIONAL SERIOUS CRIME INVESTIGATION UNIT – NATIONAL TASK FORCE) AMBACHO KINAVISHIRIKISHA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VYA (POLISI, JWTZ, TISS, MAGEREZA, UHAMIAJI NA OFISI YA DPP) KUTEKELEZA MAJUKUMU YA OPERESHENI MAALUM KAMA ILIVYOELEKEZWA. OPERESHENI HII ILIANZA TAREHE 22/07/2012  NA NI ENDELEVU. KATIKA OPERESHENI HIYO MAOFISA WAKUU WAANDAMIZI, MAOFISA WA KATI, WAKAGUZI NA ASKARI WA KAWAIDA KUTOKA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA TAJWA HAPO JUU WANASHIRIKI UTEKELEZAJI WA OPERESHENI HIYO.  

MATOKEO YA AWALI YA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI HII NI KAMA IFUATAVYO;
v WATUHUMIWA 101 NA KESI 101 ZIMEFUNGULIWA KITUO CHA POLISI LIWALE KATI YA HIZO:

i.                     KESI  15 ZIMEFIKISHWA MAHAKAMANI NA MIONGONI MWAKE KESI MOJA (1) IMETOLEWA HUKUMU NA ZILIZOBAKI ZIKO KWENYE HATUA MBALIMBALI MAHAKAMANI,

ii.                  KESI 20 ZIMESIKILIZWA NA KUPATA HUKUMU YA “BINDING OVER”, MIONGONI MWAKE KESI 7 ZIMEPATA MAAMUZI NA 13 ZINASUBIRI MAAMUZI YA MAHAKAMA. MASHARTI YA “BINDING OVER” YALIYOTOLEWA YAMETOLEWA DHIDI YA WATUHUMIWA;
a.                 KUTOTOKA NJE YA WILAYA YA LIWALE BILA KIBALI CHA HAKIMU MKAZI WA WILAYA

b.                KURIPOTI KWA OC CID KITUO CHA POLISI LIWALE  KILA MWISHO WA MWEZI

c.                 KUITWA KUHOJIWA NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA WAKATI WOWOTE KADRI ITAKAVYOONA INAFAA
d.                KUTOFANYA KOSA LOLOTE NDANI YA MIAKA MIWILI YA MATAZAMIO

e.                 KWA WALIOKUWA WAMILIKI WA SILAHA, SILAHA ZAO ZIMEHODHIWA POLISI LIWALE KWA MUDA WA MIAKA MIWILI NA MMILIKI ATAWAJIBIKA KUANZA TARATIBU ZA MAOMBI YA KUMILIKI SILAHA HIYO / HIZO UPYA PINDI UTEKELEZAJI WA HUKUMU HIYO ITAKAPOMALIZIKA

f.                  KUWEKA DHAMANA YA MALI ISIYOHAMISHIKA YENYE THAMANI YA TSH. 5,000, 000.00 NA MALI HIZO ZIWE NDANI YA WILAYA YA LIWALE


II.        KESI 66 ZINAENDELEA KUFANYIWA UCHUNGUZI ILI WAHUSIKA WAFIKISHWE MAHAKAMANI
v AIDHA KATIKA OPERESHENI HII VIJIJI 27 VYA WILAYA YA LIWALE VINGI VIKIWA VIMEPAKANA NA HIFADHI YA SELOUS VIMEHUSIKA. MATOKEO YAKE NI KUPATIKANA KWA SILAHA 80, RISASI 674 NA MAGANDA YA RISASI 289 KAMA IFUATAVYO;
v BUNDUKI 79 ZILIZOKAMATWA NI;
i.                    SAR - 1,
ii.                RIFLE - 16
iii.             SHOT GUN  - 63

v JUMLA YA RISASI 645 ZIMEKAMATWA NI;
i.                    SAR - 20,
ii.                RIFLE - 8
iii.             SHOT GUN – 647

v MAGANDA YA RISASI 289 YALIYOKAMATWA NI  ;
i.                   RIFLE - 99
ii.                 SHOT GUN – 190

v NYARA ZA SERIKALI;
SN
AINA YA NYARA ZILIZOKAMATWA
KIASI
THAMANI TSH
1
MENO YA KIBOKO,
80
18,892,500.00
3
MENO YA TEMBO
14
164,075,000.00
5
BANGILI MOJA YA USINGA WA MKIA WA TEMBO
1
23, 625, 000.00, 
6
NGOZI  ZA SIMBA,
2
15,435,000.00
7
NGOZI YA CHUI,
1
5,505,500.00
9
MIKIA MIWILI YA NGEDERE
2
378,000.00
10
KICHWA CHA NYATI CHENYE PEMBE 2,
1
2,992,500.00
11
NYAMA YA  NYATI ,
KG
2,988,700.00
12
KICHWA CHA POFU CHENYE PEMBE 2,
1
2,677,500.00
JUMLA KUU
212,944,700.00

v VIELELEZO VINGINEVYO
o       GARI NDOGO AINA YA  TOYOTA CORONA NO. T. 836 ADV 

o       PIKIPIKI MBILI ZA SANLG T. 901 BXQ NA T. 772 BSD

o       MSUMENO WA MBAO NA MBAO 149



3.0    LENGO LA OPERESHENI;
OPERESHENI HII MAALUM INALENGA KUZUIA, KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA UHALIFU / UJANGILI KATIKA MAENEO MBALIMBALI NCHINI WILAYA YA LIWALE IKIWA KAMA ‘ROLE MODEL’.

4.0           MAFANIKIO;
I.                  KWA KUWA OPERESHENI HII IMEPANGWA NA KUENDESHWA KITAALAM NA KISAYANSI (INTELLIGENCE LED OPERATIONS), MAFANIKIO YAFUATAYO YAMEJIDHIHIRISHA;

a.                 IMEUNGWA MKONO NA KUSIFIWA NA RAIA NA WANANCHI KWA UJUMLA KWA MAELEZO KUWA HAKUNA MTUHUMIWA ALIYEKAMATWA KWA KUONEWA.

b.                 KUMEKUWEPO NA MAPOKEO CHANYA (POSITIVE IMPACT) KUTOKANA NA WANANCHI KUTAMBUA KUWA MWENENDO WA OPERESHENI HII UNAIPA HESHIMA KUBWA SERIKALI

c.                 HAKUKUWA NA RAIA MWEMA ALIYEBUGHUDHIWA AU KULALAMIKIA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA OPERESHENI HII

ii.                MTANDAO WA UHALIFU WA UJANGILI UNAVUNJWA NA WAHUSIKA WOTE SASA WANAFAHAMIKA NA UCHUNGUZI MAKINI NA WA KINA UNAENDELEA DHIDI YAO NA WATAFIKISHWA MBELE YA MAHAKAMA NA SHERIA ICHUKUE MKONDO WAKE

iii.             BAADHI YA WAZEE WENYE UMRI MKUBWA NA AMBAO AFYA ZAO ZILIONEKANA KUTOMUDU MASHARTI YA KUENDELEA KUMILIKI SILAHA WALIZISALIMISHA WENYEWE NA KUOMBA ZIHIFADHIWE KATIKA KITUO CHA POLISI LIWALE MPAKA MAAMUZI YATAKAPOTOLEWA NA MAHAKAMA DHIDI YA SILAHA HIZO.

iv.             WALE AMBAO MAHAKAMA ITAONA WAMEPOTEZA SIFA ZA KUMILIKI SILAHA ZITAHODHIWA KITUO CHA POLISI KUSUBIRI UTEKELEZAJI WA MAAMUZI YA MAHAKAMA


5.0           CHANGAMOTO:
i.                   BAADHI YA WAMILIKI WA SILAHA SIO WAAMINIFU    KWA KUWA WANATUMIA SILAHA ZAO KUFANYA UJANGILI AU KUZIAZIMISHA KWA MAJANGILI. 

ii.                BAADHI YA WAMILIKI WA SILAHA WAMEPOTEZA SIFA ZA UMILIKI KUTOKANA NA MATATIZO YA KIAFYA; MFANO KUKABILIWA NA UPOFU, UGONJWA WA KIHARUSI N.K JAMBO AMBALO LINACHANGIA WAO KUSHINDWA KUZINGATIA NA KUTEKELEZA TARATIBU ZA UMILIKI WA SILAHA

6.0           MUONO WA MBELE (WAY FORWARD);
i.                   WIZARA YA MALI ASILI NA UTALII ITAENDELEA KUTOA ELIMU KWA JAMII ZINAZOISHI KANDOKANDO YA MAPORI YA AKIBA /  HIFADHI KUHUSU UMUHIMU WAO WA KUTOJIHUSISHA NA UJANGILI NA WAWE VYANZO VYA TAARIFA ZA KIINTELIJENSIA KUFUATIA MKAKATI MADHUBUTI WA KUDHIBITI MTANDAO WA UJANGILI NCHINI.

ii.                UTAKUWEPO MWENDELEZO WA KUBORESHA NA KUIMARISHA DORIA, MISAKO NA HATUA NYINGINE ZA KIOPERESHENI KWENYE MAPORI YA AKIBA NA HIFADHI ZA TAIFA MARA KWA MARA KUFUATIA MUONGOZO WA TAARIFA ZA KIINTELIJENSIA KADRI ITAKAVYOONEKANA INAFAA KATIKA KUFANYA OPERESHENI ZA PAMOJA (JOINT OPERATIONS INVESTIGATIONS & INTELIGENCE –JOII)  KWA KUTUMIA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUPITIA “TASK FORCE” YA KITAIFA .

7.0    MWISHO
NAWAPONGEZA MAOFISA WAANDAMIZI, MAOFISA WA KATI, WAKAGUZI NA ASKARI WA VYEO MBALIMBALI WANAOSHIRIKI UTEKELEZAJI WA OPERESHENI HII INAYOENDELEA. KWA UJUMLA NAMALIZIA KWA KUWASHUKURU TENA NYINYI WANAHABARI MLIOFIKA HAPA KWA USHIRIKIANO MNAOUTOA KATIKA KUPAMBANA NA UHALIFU HUU.


ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
//////////////////////////////////////////MWISHO///////////////////////////////////////

IMETOLEWA TAREHE  08/08/2012  NA

MHE. BALOZI KHAMIS .S. KAGASHEKI (MB)
WAZIRI


NAKALA KWA:
VYOMBO VYA HABARI

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.